MTOTO WA MIAKA SITA ADONDOKA DIRISHANI NA KUFA AKIMUIGA SPIDERMAN...

Dirisha alilodondoka Kevin lililoko katika ghorofa ya tatu nyumbani kwao huko Southall.
Mtoto wa kiume mwenye miaka sita amedondoka na kufa kupitia dirishani akidhania alikuwa 'asiyeshindika' kama alivyo shujaa wake Spiderman.
Kevin Morais alikuwa amekwea kando ya dirisha la chumbani kwake katika ghorofa ya tatu ndipo alipoteleza na kuangukia kwenye bustani ya nyuma ya jengo hilo.
Mama yake, nesi Maria Morais alisikia kishindo hicho na kukuta 'kijana wake mtundu' akiwa amelala katika dimbwi la damu.
Huku akibubujika machozi, aliieleza mahakama ya West London: "Nilikwenda kufungua mlango kuona nini kimeanguka na alikuwa mtoto wangu."
Mama huyo wa watoto wawili, ambaye ni nesi mtaalamu, alisema aliita gari la wagonjwa, lakini Kevin tayari alikuwa ameshafariki.
"Nilisema 'Nafahamu mwanangu amefariki'. 'Amefariki'," alisema kwa huzuni.
Aliwaeleza wachunguzi rasmi kuwa mtoto wake alikuwa amemaliza tu kupanga chumbani kwake, na kufanya kazi zake za shule, ndipo alipopanda ghorofani kwenda kucheza.
Aliongeza: "Kevin alikuwa aina hiyo ya mtoto, alizoea kujihisi mpweke haraka sana, hivyo alitokomea ghorofani na nilidhani, ilikuwa sawa, baba yake alikuwa huko kwenye chumba cha kupumzikia na dada yake pia alikuwa huko.
"Baada ya dakika chache, dakika kumi hadi kumi na tano baada ya kutoweka kutoka machoni kwangu, nikasikia kishindo kikubwa kwenye bustani na kisha kilichonijia haraka kichwani mwangu, ni kitu gani ambacho mume wangu amekiacha bila kukifunga hadi kikaanguka.
"Sikusikia mayowe yoyote au kelele ila tu kishindo kikubwa kwenye sakafu.
"Nilikwenda kufungua mlango kuangalia nini kimeanguka sababu sikuweza kusikia na nilimwona mtoto wangu pale, na alikuwa pale kwenye sakafu akiwa kazingirwa na damu.
"Nilipiga kelele na mayowe, mume wangu alishuka chini na binti yangu pia. Hawakuweza kuamini kilichokuwa kimetokea.
"Walinieleza endelea kuongea naye, nilikuwa nikimwita, hakukuwa na majibu yoyote, nikasema najua mwanangu amefariki. Amefariki."
Kevin alikuwa tayari ameanguka kutoka ghorofa ya tatu ya nyumba yao huko Southall, masharibi mwa London mwaka mmoja uliopita.
Timu ya uchunguzi ilielezwa alikuwa akijidhania 'asiyeshindika' na kwamba angeweza kunusurika katika kuanguka huko.
Baba wa Kevin, John Morais, ambaye ni fundi ujenzi, aliieleza timu ya uchunguzi kwamba anafikiri madirisha hayo yanafunguka kwa urahisi mno baada ya kuyakagua kufuatia kifo cha Kevin.
"Baada ya mkasa ule nilipoenda kwenye dirisha lile nilikuta kwa kulisukuma lilifunguka kwa urahisi mno," alisema.
"Sitaki kutengeneza hisia zozote zile zilizo nje ya uelewa wangu, lakini kitu kimoja ambacho ni hakika sababu ya moja ya dirisha ambalo lilitakiwa kuwa limefungwa nimepoteza kijana wangu. Natumaini haitatokea kwa familia nyingine yoyote."
Mtafiti wa Vifo amesema chanzo cha kifo hicho ni ajali ya kawaida.

No comments: