JK AKEMEA WENYE USONGO NA UJUMBE WA KAMATI KUU CCM...

Dk Jakaya Kikwete.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Rais Jakaya Kikwete, amezima ubashiri juu ya watakaoteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu, ambao majina yao yanatarajiwa kuwekwa hadharani leo.
Akizungumza wakati akifungua semina kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM,  Rais Kikwete alisema hadi jana hapakuwa na orodha yoyote iliyokuwa imeandaliwa ya wajumbe hao. 
Alihoji mantiki ya kauli za ‘kampeni’ kwamba baadhi ya watu wanafaa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM na wengine ni hatari na kutaka mambo hayo yaachwe mara moja. 
“Nimesikia (wanaosema) hawa ni ndiyo wanaofaa sana, hawa ni hatari sana, imekuwaje wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wawe hatari kwa chama chetu? Jamani acheni,” alisema na kushangiliwa. 
Alikemea ‘magenge’ hususani wanaotaka watu wengine waharibikiwe na kusema wanajipa kihoro, hasa pale watakapokuta hawakuharibikiwa. 
Katika semina hiyo ambayo mada mbalimbali zitatolewa na makada na viongozi wa ngazi ya juu ya chama, Kikwete alisisitiza kwamba watakaowaambia wanayo orodha ya majina,  wanawapotezea wakati. 
“Napenda niwatahadharishe, asiwadanganyeni mtu kwamba orodha ndiyo hii; hawa ndio watakaochaguliwa, anapoteza wakati,” alisema Kikwete.
Kikwete ambaye kauli zake ziliendelea kusababisha vicheko na kushangiliwa, alisema yeye na Makamu wake wanakaa leo kwa ajili ya maandalizi hayo. “Tutakaa kesho (leo) wala msiamke usiku huu (jana) mkasema nimekaa na orodha,” alisema. 
Msisumbuke kufanya mikutano, kwamba lazima tumuunge mkono fulani, orodha hiyo haina fulani kwa sababu orodha yenyewe haipo,” alisema. 
Aliwataka wajumbe wa NEC walioingia kwa mara ya kwanza kujihadhari na magenge. Aliwataka wajishirikishe kwenye mambo ya kujenga na wasikubali  kushirikishwa kwenye mambo ya kubomoa. 
“Kutengeneza magenge mahali fulani huyu aharibikiwe, ni jambo ambalo halina tija. Unajipa kihoro hasa pale inapofikia kwamba uliyetaka aharibikiwe hakuharibikiwa.
“Kwa nini ufanye biashara isiyo na  maana?  Wekeza kwenye kitu chenye maana badala ya kuwekeza kwenye magenge…Lakini akili ni nywele kila mtu ana zake,” alisema.
Katika taarifa yake, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema yatatangazwa majina 28 na wajumbe wanaopaswa kuchaguliwa ni 14. 
Kati ya hao 14, saba watatoka Zanzibar na mengine saba  watatoka Tanzania Bara. Alisema watazingatia pia jinsia katika uchaguzi wa wajumbe hao. 
Miongoni mwa mada zilizotolewa jana katika semina hiyo ni suala zima la maadili, ambalo Kikwete alisema kiongozi anapaswa kuwa na maadili mema kwa kuwa ndiyo taswira ya chama. 
Alitoa mfano kwamba ikitokea mjumbe wa NEC akawa mlevi, chama pia kitaonekana ni cha walevi. 
“Mjumbe wa NEC unalewa, wewe ndiye wa mwisho kuondoka baa, unamalizia kwa kusema kidumu Chama Cha Mapinduzi, watu wataona chama cha walevi,” alisema. 
Alisema haiwezekani mjumbe wa NEC akawa mtu wa kukopa mara kwa mara kiasi cha kusababisha anapopigia watu simu wanaikataa wakijua atakopa. 
Alisema ajira ni tatizo lakini haitoshi kuzungumzia bila kutoa jawabu lake. Alisema haipaswi mtu kulaumu bila kutoa njia mbadala ya kumaliza tatizo. 
Aliongeza kuwa ingawa suala la kutoa ajira siyo la moja kwa moja ndani ya CCM, wameamua lijadiliwe kwa kuzingatia  ndicho chama tawala kinachoweza kuelekeza Serikali nini kifanyike. 
Hata hivyo, alisisitiza kwamba suala la ajira si la Serikali pekee bali pia la sekta binafsi. Alisema katika Serikali wigo wa  nafasi za ajira ni ndogo, ikilinganishwa na sekta binafsi. 
Hata hivyo alihoji: “Ni namna gani sekta binafsi itatoa ajira wakati wawekezaji wakiendelea kuitwa wezi na wakati huo huo wanaowekeza wakifanyiwa fujo wasiwekeze?”  
Akielezea mkakati wa kutekeleza maazimio ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Novemba mwaka jana, Kikwete alisisitiza  lazima yatekelezwe kwa kuwa heshima ipo kwenye kutekeleza wanayotamka. Alisema watajipanga vizuri namna ya kuyafanikisha. 

No comments: