![]() |
| Spika Anne Makinda. |
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema Bunge sasa linatia aibu kwa ‘utoro’.
Alisema hivyo jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, alipokuwa akizungumza tukio la juzi la kushindikana kupitishwa maazimio ya Bunge, kutokana na idadi ya wabunge kuwa pungufu ukumbini.
“Jana (juzi) tulihesabiwa, tulikuwa wachache…ilikuwa ni aibu kweli,” alisema Spika.
Makinda alisema wabunge wanapokuja bungeni, haimaanishi kwamba wako likizo kiasi cha kuondoka na kwenda kufanya shughuli zao.
Makinda alionya kitendo cha wabunge kutoonekana katika ukumbi na kusema ufike wakati, wabunge wasianze kuchungana.
Juzi Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu, alilazimika kuahirisha kikao baada ya idadi ya wabunge inayoruhusu kufanya uamuzi kutotimia.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, ili uamuzi ufanyike akidi kwa kila kikao cha Bunge lazima iwe nusu ya wabunge wote.
Ingawa Mwenyekiti alizingatia kanuni kwa kusimamisha shughuli za Bunge na kumwagiza Katibu kupiga kengele kuwaita, idadi ya wabunge haikufikia akidi inayohitajika, hivyo akaamua kuahirisha shughuli hizo hadi jana.
Maazimio yaliyoshindikana kuridhiwa juzi na hivyo kufanyika jana ni Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Vitendo vya Ugaidi wa kutumia nyuklia.
Azimio lingine ni la kujiunga na Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu dhidi ya Watu wenye Kinga ya Kimataifa pamoja na Wakala wa Diplomasia.
Hali hiyo ilitokea licha ya Spika karibu katika kila mkutano kuhimiza wabunge kuwa ukumbini wakati wote Bunge likiendelea na vikao.
Mwaka jana alifikia hatua ya kutaka kuchukua hatua kali dhidi ya wabunge wanaokosekana wakati wa vikao ikiwa ni pamoja na kuorodheshana majina wanapoingia, lakini pia kukatana posho.
Pengine kutokana na ahadi ya Spika kutotekelezwa ndivyo pia wabunge hao ambao hivi sasa wamekithiri katika utovu wa nidhamu kutojali na hivyo kujiondokea wanapotaka.
Hali hiyo inasababisha hata waliowatuma kuwawakilisha bungeni kukosa imani na uwakilishi wao.

No comments:
Post a Comment