WATATU WAFA BAADA YA BASI KUGONGANA USO KWA USO NA BODABODA...

Watu watatu akiwemo dereva wa basi, mali ya Kampuni ya Jai, Sindi Salumu (48), lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Tanga, wamekufa papo hapo baada ya basi hilo  kupata ajali.
Katika ajali hiyo, basi hilo liligongana uso kwa uso na pikipiki na kuserereka kwenda kugonga mti.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo iliyotokea eneo la Kihangaiko, Msata mkoani Pwani, chanzo chake ni mwendokasi wa basi hilo wakati dereva akijaribu kupita basi lingine lililokuwa mbele yake.
Mbali na dereva wa basi hilo, wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na mwendesha pikipiki iliyogongana na basi hilo Mangula Idd (48) pamoja na abiria aliyekuwa amempakia, Sharifa Shomari (26).
Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla ya ajali hiyo dereva wa basi hilo alikuwa akijaribu kulipita basi jingine katika eneo ambalo kulikuwa na kilima.
Mashuhuda hao walidai kuwa kabla hawajamaliza kupita basi hilo, mbele yake ilitokeza pikipiki hiyo na kugongana uso kwa uso hali iliyolifanya basi kupoteza mwelekeo na kupinduka.
Alisema baada ya basi hilo kupinduka, liliserereka moja kwa moja hadi upande wa kulia mwa barabara na kugonga mti wa mwembe hali iliyomfanya dereva wake kukandamizwa katika mti  huo na kupoteza maisha.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Uric Mtei alisema watu 11 walijeruhiwa  na kukimbizwa katika Hospitali ya Chalinze kwa ajili ya matibabu na marehemu wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitalini hapo.

No comments: