BARAZA LA WAZEE KKKT LAACHIA NGAZI...

Baraza la Wazee na Kamati ya Maendeleo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Engarenarok, mtaa wa Bethania katika Dayosisi ya Kaskazini Kati Arusha wametangaza kuwajibika kwa kujiuzulu.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni kuashiria hali ya kuchoshwa na ufisadi ndani ya KKKT.
Kuwajibika kwa Baraza la Wazee na Kamati ya Maendeleo ya Usharika huo ni mfululizo wa hatua za waumini wa Dayosisi hiyo wanaokadiriwa kufikia 600,000 kupinga kinachoelezwa kuwa ufisadi wa wazi wa viongozi waandamizi wa Dayosisi hiyo wakishirikiana na wafuasi wao wachache.
Katika barua ya kujiuzulu kwenda kwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, iliyoandikwa Januari 11 na kutolewa jana, Baraza hilo na Kamati ya Maendeleo ilisema wamechoshwa na kukwazwa na uamuzi unaowagusa moja kwa moja kiutendaji kuchukuliwa bila kuwashirikisha.
Wazee hao na Kamati hiyo walimnyooshea wazi wazi kidole cha lawama Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Mathias Mushi  kuwa amekuwa akichukua uamuzi na kutekeleza bila kujali uwepo wa vyombo hivyo kikatiba na kwamba hatua hiyo imekuwa ikiwakwaza kwa muda mrefu.
“Mwaka 2009 yalifanyika mabadiliko katika mtaa lakini kamati husika hazikushirikishwa na wana mtaa walikaa kimya, ingawa walikwazika.
“Kama vile haitoshi, pamoja na jitihada zote tunazofanya za maendeleo ya mtaa na usharika kwa ujumla yamefanyika tena mabadiliko ya uongozi wa mtaa bila kushirikisha kamati husika na hili limetukwaza tena,” lilisema Baraza hilo katika barua yake ya kujiuzulu.
Tuhuma nyingine za waumini hao ni pamoja na kile walichodai kuwa ni Usharika kuendeshwa kidikteta na kikabila na Mchungaji Mushi ambaye amekuwa usharikani hapo kwa miaka 12 kinyume na Katiba  ya Dayosisi
hiyo inayotaka kila Mchungaji akae katika usharika mmoja kwa miaka minane tu.
Alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya madai ya waumini hao, Mchungaji Mushi, kwanza alidai hajui barua hiyo na yeye si msemaji wa Dayosisi lakini alipobanwa zaidi alisema: “Nikwambie kitu, si kwamba nakudharau, ila naona unanisumbua,” alisema Mchungaji na kukata simu. Alipopigiwa tena simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na wajumbe 13 wa Baraza la Wazee na wengine 15 wa Kamati ya Maendeleo, walidai kuwa uongozi wa usharika umeshindwa kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ya mtaa na hivyo kutowatendea haki na kuona bora wajiuzulu ili wawakilishi wengine wachaguliwe.
Pamoja na kujifanya kuwa hajui barua hiyo, Mchungaji Mushi alielezwa kuhaha kubembeleza baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo na Kamati hiyo kwa kuwatumia Wainjilisti na waumini wengine wenye ushawishi ili wabatilishe uamuzi huo na kulegeza msimamo bila mafanikio.
Mchungaji Mushi inasemekana kuwa mshirika wa karibu wa viongozi waandamizi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati hasa Katibu Mkuu aliye matatani na kwamba amekuwa akisikiliza na kutekeleza maagizo ya mabosi wake hao badala ya waumini anaotakiwa kuwatumikia kwa nguvu zake zote.

No comments: