TAARIFA KAMILI YA USHINDI WA GODBLESS LEMA MAHAKAMANI...

Godbless Lema akishangilia ushindi wake na wafuasi wa chama hicho.
Mahakama ya Rufaa jana imemtangaza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa Mbunge halali wa jimbo hilo baada ya kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha uliomvua wadhifa huo.
Hatua hiyo inatokana na Lema kushinda katika rufaa ya kupinga kuvuliwa wadhifa huo aliyoifungua katika Mahakama hiyo. Ifuatayo ni taarifa kamili...
Akisoma hukumu hiyo jana, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu, alisema Mahakama imethibitisha kuwa Lema ni Mbunge halali wa Arusha Mjini na kuwataka wajibu rufaa kumlipa gharama za rufaa hiyo.
Alisema kuwa wajibu rufani hawakuwa na haki ya kisheria ya kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi, hivyo Mahakama imetengua hukumu, tuzo na amri ya Mahakama Kuu.
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini Mahakama ya Rufaa imetoa hukumu kwa kutumia hoja moja ambayo haijawahi kutolewa na upande wowote katika Mahakama Kuu.
Hoja hiyo ilitolewa wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ambapo mawakili wa Lema, Tundu Lisu na Method Kimomogoro walihoji kama wajibu rufaa walikuwa ni wapiga kura halali waliojiandikisha.
Katika uamuzi, Mahakama ilisema kuwa wajibu rufaa hao hawakuwa wapiga kura kwa kuwa katika kumbukumbu za Mahakama hakuna ushahidi unaoonesha kuwa ni wapiga kura waliosajiliwa.
Awali wakati wa usikilizwaji rufaa hiyo, Wakili wa wajibu rufaa, Alute Mughway, alidai kwamba  wajibu rufaa ni wapiga kura halali waliosajiliwa na hata Mahakama ilijiridhisha kwa kuwa waliwasilisha kadi zao katika Mahakama Kuu na Mahakama ilinakili majina na namba zao na kisha kuzirejesha.
Hata hivyo, Wakili Lisu alidai kuwa kama walifanya hivyo ni utaratibu ambao haukuwa wa kisheria, bali walipaswa waziwasilishe kama vielelezo vya ushahidi na si Jaji kuziangalia na kisha kuzirejesha kwa wahusika.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya jopo la majaji wenzake wawili waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, Mahakama hiyo imesema kwamba utaratibu uliotumika wa kumpa Jaji kuthibitisha kuwa wajibu rufaa walikuwa wapiga kura halali ni kinyume cha sheria kwa kuwa ushahidi kama huo ulipaswa uwasilishwe moja kwa moja mahakamani na utolewe na mmiliki wa nyaraka hizo.
Alisema katika kumbukumbu za Mahakama kuna kiambatisho na maelezo tu kuwa wajibu rufaa ni wapiga kura waliosajiliwa, lakini hakuna kielelezo kuwa waliwasilisha kadi kama ushahidi  na badala yake wakili wao ndiye aliyejaribu kuthibitisha hilo kwa maelezo, badala ya vielelezo.
Alisema hata kama ingethibitika kuwa wajibu rufaa walikuwa wapiga kura waliosajiliwa, bado hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi, kwa madai kwamba Lema katumia lugha za matusi kwenye kampeni zake.
“Mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambapo haki zake hazijakiukwa,” alisisitiza Jaji Luanda kwa niaba ya wenzake na kuongeza kuwa, katika kesi kama hiyo ilikuwa ni wajibu wa mtu yule tu ambaye au haki zake zilikiukwa ndiye afungue kesi.
Kutokana na hoja hiyo nzito kwamba wajibu rufaa hawakuwa na haki ya kufungua kesi, Mahakama haikushughulika na hoja nyingine zilizowasilishwa na warufani.
Baada ya kusomwa kwa uamuzi huo, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika ndani hadi nje ya Mahakama walianza kupiga kelele kusherehekea hata kabla Msajili hajatoka katika chumba cha Mahakama.
Walitoka nje ya Mahakama huku wakiimba kaulimbiu yao ya “People’s Power”, na wengine wakiitikia “Lema, Lema, Lema” na  kusukumana kwenda kumkumbatia Lema, huku wengine wakipanda kwenye viti vya mahakamani.
Akizungumza nje ya Mahakama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wamepokea kwa heshima uamuzi huo kwa kuwa walilalamika sana lakini hatimaye haki imetendeka.
Hata hivyo, Lema aliyekuwa amebebwa hadi kwenye gari alishindwa kuzungumza maneno mengi, zaidi ya kusema “tumeshinda, tumeshinda”.
Wakati hayo yakitokea Dar es Salaam, miji ya Moshi na Arusha ililipuka kwa milio ya honi za magari na pikipiki pamoja na miluzi mara baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo wa Mahakama. Baadhi ya watu waliingia mtaani kushangilia kwa kupeperusha bendera za Chadema.
Wakati nderemo hizo zikiendelea, magari ya doria ya Jeshi la Polisi yalionekana kupita mitaani ili kulinda usalama.
Katika maeneo mengine wananchi walikuwa na furaha, wengi wakielezea kufurahishwa na jinsi haki ilivyotendeka na hatimaye kumrudishia ubunge mwakilishi wao huyo wa Jimbo la Arusha Mjini.
Wakili wa Kujitegemea, Emmanuel Saringe, aliipongeza Mahakama ya Rufani kwa hukumu hiyo akielezea kuwa imetenda haki kwa kuridhia kwamba ushahidi uliotolewa kwenye kesi ya awali haukutosha kumvua Lema ubunge.
Lema alivuliwa ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Mahakama Kuu Aprili 5, mwaka huu na Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibalila.

No comments: