MBUNGE LEMA SASA KUACHANA NA SIASA ZA FUJO, MAANDAMANO...

Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema.
Siku moja baada ya Mahakama ya Rufaa nchini kumrejeshea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, amempongeza mbunge huyo, lakini akimpa nasaha nzito ikiwa ni pamoja na kumtaka kuachana na uongozi wa maandamano na fujo kila kukicha.
Aidha, amemtaka yeye na chama chake kuelewa kuwa, si kila kitu kina mkono wa CCM au Serikali kama ambavyo mara kadhaa imekuwa ikitafsiriwa.
Na baada ya kurejea madarakani kuliongoza jimbo la Arusha, amemtaka kuwa kiongozi wa kupigiwa mfano katika suala la maendeleo, akiongeza kuwa, kazi ya kiongozi ni kuonesha njia.
Nape, mmoja wa vijana wanasiasa machachari nchini, aliyasema hayo jana katika taarifa yake fupi.
Katika taarifa hiyo, Nape alisema: “Nachukua nafasi hii kuwapongeza Chadema na Mheshimiwa Lema (Godbless) kwa ushindi kwenye kesi ya Ubunge wa Arusha...!
“Nilidhani na leo mtasema CCM, Nape na Ikulu wameingilia kesi.... Mkishinda haki imetendeka, mkishindwa kuna mikono ya Ikulu...!
“Ndio mnakua lakini, mkikua mtaacha… Mtajifunza majibu ya watu wazima kwenye mazingira kama hayo.
“Mdogo wangu Lema umeiona Arusha ilivyokuwa imetulia bila maandamano na kelele zisizo na msingi? Endeleza utulivu huu ambao naamini umejifunza kwa kipindi ulichokaa nje ya Bunge…! Kiongozi ni kuonesha njia, onesha njia ya maendeleo sio maandamano na fujo.”
Mahakama ya Rufaa imemrudishia Lema ubunge kwa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge huo Aprili 5, mwaka huu.
Lema alivuliwa ubunge na Jaji Gabriel Rwakibalila wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, baada ya kuridhika na ushahidi wa walalamikaji; Musa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo pamoja na mashahidi wao kuwa, mbunge huyo alitumia lugha za kashfa na matusi dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2010, Dk Batilda Burian ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya.
Juzi, pamoja na Mahakama ya Rufaa kumrudishia ubunge Lema, iliwataka pia wajibu rufaa kulipa gharama za rufaa hiyo.
Katika hukumu ya rufaa hiyo iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu, ilielezwa kuwa, wajibu rufani hawakuwa na haki ya kisheria ya kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hivyo Mahakama kutengua hukumu, tuzo na amri ya Mahakama Kuu.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya jopo la majaji wenzake wawili waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, mahakama hiyo imesema kwamba utaratibu uliotumika wa kumpa Jaji kuthibitisha kuwa wajibu rufaa walikuwa wapiga kura halali ni kinyume cha sheria kwa kuwa ushahidi kama huo ulipaswa uwasilishwe moja kwa moja mahakamani na utolewe na mmiliki wa nyaraka hizo.
“Mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambapo haki zake hazijakiukwa,” alisisitiza Jaji Luanda kwa niaba ya wenzake, Salum Massati na Nathalia Kimaro na kuongeza kuwa, katika kesi kama hiyo ilikuwa ni wajibu wa mtu yule tu ambaye au haki zake zilikiukwa ndiye afungue kesi.
Kutokana na hoja hiyo nzito kwamba wajibu rufaa hawakuwa na haki ya kufungua kesi, Mahakama haikushughulika na hoja nyingine zilizowasilishwa na warufani.
Naye Godbless Lema jana alikaribishwa rasmi kwa mbwembwe jijini Arusha.
Akihutubia wananchi, alisema yuko tayari kuwatumikia Wana-Arusha huku akiahidi kuwa hatoandamana tena, bali madai na kero zake atazielekeza kwenye vikao ndani ya Halmashauri.
Alisema akiwa madarakani, hatapenda kuona watu wakiteswa na wanamgambo wa Jiji, hasa wanawake na wafanyabiashara ndogoo na kusisitiza kuwa, hayasemi hayo kwa lengo la uchochezi, bali kama angalizo kwa kuwa siku zote yupo kwa ajili ya kupigania haki na hatarudi nyuma kwa hila yoyote.
Kabla ya kukaribishwa kuzungumza na wananchi, Katibu wa Chadema mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema chama chake kimefanya tathimini ya kesi iliyomalizika na kusema wanatarajia kudai fidia ya gharama za kesi hiyo inayofikia  Sh  milioni 253.
Golugwa pia alitumia muda huo kumkabidhi bendera ya Bunge Lema ambayo alikabidhiwa na mbunge huyo baada ya kuvuliwa nafasi hiyo Aprili mwaka huu.
Alisema alipokabidhiwa bendera hiyo alimwambia aiweke na kusubiri Mungu atende muujiza ambao kwa sasa anasema umetimia kwa Lema kurudishiwa ubunge.
Kuhusu madiwani waliofukuzwa Chadema, alisema kuwa bado anaamini walitendewa haki ya kufukuzwa sababu ya kurubuniwa na huku akiahidi kuwa, uchaguzi ukirudiwa chama chake kitaibuka na ushindi mnono.

No comments: