Godbless Lema (katikati) akisindikizwa na wafuasi wake mapema leo mara baada ya kushinda kesi dhidi yake jijini Dar es Salaam. |
Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa Godbless Lema wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameshinda kesi dhidi yake na hivyo kurejeshewa rasmi kiti chake cha ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini.
Katika hukumu iliyotolewa muda mfupi uliopita na Mahakama ya Rufaa, jijini Dar es Salaam, mahakama hiyo imetupilia mbali tuhuma dhidi ya Lema ambazo zilimsababishia kuvuliwa wadhifa huo.
Hukumu ya kumvua ubunge Lema ilitolewa mwanzoni mwa Aprili mwaka huu na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika hukumu hiyo, Lema aliondolewa katika nafasi yake ya ubunge, lakini alikata rufaa.
Katika rufaa hiyo, Lema kupitia kwa mawakili wake, Method Kimomogoro akisaidiana na Tundu Lissu waliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu hiyo iliyomng’oa madarakani.
Walidai kuwa hukumu iliyotolewa haikukidhi vigezo na ushahidi uliotolewa haukuthibitisha mashitaka bila kuacha shaka. Pia walidai kuwa Jaji aliegemea ushahidi ambao haukidhi viwango.
Wakili Lissu alidai kuwa hakuna sheria ya uchaguzi inayoeleza matusi na maneno ya udhalilishaji yanaweza kuwa sababu ya kutengua matokeo ya uchaguzi.
Alifafanua katika madai hayo kuwa, katika Maadili ya Uchaguzi ndiko wanakataza maneno ya ubaguzi, udhalilishaji, maneno ya kashfa na adhabu yake ni faini ya kuanzia Sh 50,000 hadi 150,000.
Lissu alidai Sheria ya Uchaguzi haielezi kama maneno ya ubaguzi ni kosa la jinai, lakini wameeleza kuwa mtu atakayevunja maadili, ataadhibiwa kulingana na adhabu iliyotolewa kulingana na kanuni za maadili.
No comments:
Post a Comment