Sunday, December 9, 2012

BEKI DALLAS COWBOYS AFARIKI AJALINI, MWENZAKE MBARONI KWA MAUAJI...

Josh Brent.
Jerry Brown, mchezaji katika safu ya ulinzi kwenye kikosi cha timu ya Dallas Cowboys, amefariki dunia jana kwa ajali ya gari -- na mchezaji mwenzake, Josh Brent alikamatwa kwa mashitaka ya kusababisha kifo kutokana na ulevi.
Kwa mujibu wa polisi, Brent alikuwa akiendesha gari kwa mwendo mkali majira ya Saa 8:20 usiku wa manane ndipo gari lake lilipoginga kingo za barabara, kupinduka na kuangukia upande mwingine katikati ya barabara.
Wakati polisi walipofika eneo la tukio, Brent alikuwa akimkokota Brown kutoka kwenye gari hilo ... ambalo lilikuwa limepinduka juu-chini huku likiwa linawaka moto. Brown alikuwa hajitambui na baadaye akatangazwa kuwa amefariki dunia katika hospitali ya jirani.
Maofisa wa polisi katika eneo la tukio wanahisi pombe kuwa ni chanzo cha ajali, hivyo walimfanyia kipimo Brent kutambua kama alikuwa amelewa, ambacho kilibaini kwamba ni kweli. Damu yake baadaye ilipelekwa katika hospitali hiyo ili kuweza kubaini kiasi cha kilevi ndani yake. Majibu hayo bado hayajafahamika.
Brent alikamatwa na Idara ya Polisi ya Irving na kufunguliwa mashitaka Saa 10:14 alfajiri na bado yuko ndani baada ya kunyimwa dhamana.
Mmiliki wa Dallas Cowboys, Jerry Jones ametoa taarifa jana akisema: "Tumepokea kwa masikitiko makubwa habari za ajali hii na kifo cha Jerry Brown. Kwa wakati huu, mioyo yenu na sala na rambirambi za dhati tunazipeleka kwa familia ya Jerry na wote ambao waliomfahamu na kumpenda."
Tukio hili limekuja wiki moja tu baada ya mchezaji katika safu ya ulinzi ya Kansas City Chiefs, Jovan Belcher kumuua rafiki yake wa kike kabla ya kujiua mwenyewe.

No comments: