Monday, November 12, 2012

WAZAZI WAKABIDHI BINTI WA MIAKA 13 KWA 'MBAKAJI' MKOA WA KATAVI...

Imani ya wazazi kwa dereva wa basi kuwa angemfikisha mtoto wao wa kike wa miaka 13 katika kituo husika apokewe na ndugu zake, imeharibu maisha ya mtoto huyo baada ya kupitishwa kituo husika na kuishia kunajisiwa
Akisimulia mkasa huo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Joseph Myovela amedai kuwa mtoto huyo alisema wazazi wake, wakazi wa Kijiji cha Tutuo mkoani Tabora, juzi kwa imani walimkabidhi kwa dereva wa kampuni ya mabasi ya Air Bus, Nasibu Ramadhani (33) ili amfikishe anapokwenda.
Kamanda Myovela alidai kuwa mtoto huyo (jina limehifadhiwa), alipandishwa katika basi hilo na wazazi wake na kukabidhiwa kwa Ramadhani ili amshushe katika Kijiji cha Inyonga, wilayani Mlele ambako angepokewa na ndugu zake.
Alidai kuwa dereva huyo alipofika katika Kijiji cha Inyonga, hakusimamisha gari hadi alipofika mjini Mpanda na kumpeleka mtoto huyo moja kwa moja  kwenye  nyumba  ya kulala wageni ya Miami iliyoko katika Mtaa wa Majengo.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Myovela, mtoto huyo wa kike katika mahojiano yake na Polisi alisema dereva huyo alilipa gharama za chumba katika nyumba hiyo na kuondoka.
Msichana huyo katika maelezo hayo Polisi, alisema baadaye dereva huyo alirejea katika chumba hicho na kumlazimisha afanye naye mapenzi kwa  nguvu  lakini hakuwa tayari ndipo alipompiga makofi  na kumtisha kwa maneno makali na kumuingilia kwa nguvu.
Kutokana na vurugu hizo, inadaiwa mhudumu wa nyumba hiyo alisikia na kutoa taarifa Polisi.
“Baada ya askari Polisi na mhudumu kuingia chumbani  humo walipigwa na  butwaa kumkuta  msichana huyo mwenye umri mdogo akiwa amelala  kitandani chumbani mwa mtuhumiwa, askari wetu walipomhoji  msichana huyo  alieleza kuwa yeye ni mkazi  wa Kijiji cha Tutuo mkoani Tabora ambako anaishi na wazazi wake,” alieleza Kamanda.
Kamanda Myovela alisema mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa Polisi na atafikishwa mahakamani  mara baada ya uchunguzi dhidi yake kukamilika.

No comments: