Monday, November 19, 2012

HOFU YATANDA TANZANIA KUIBIWA GESI ASILIA...

Hofu ya matarajio ya maisha bora kwa kila Mtanzania kutokana na kugundulika kwa gesi asili futi za ujazo trilioni tatu katika eneo la nchi kavu na majini la Tanzania, imewakumba wananchi waliojitokeza kutoa maoni ya sera ya gesi.
Wakitoa maoni juzi kuhusu sera ya gesi, baadhi ya wananchi mbali na kuhofia wachache kunufaika na gesi hiyo huku wengi wakiendelea na umasikini, wengine wameelezea hofu ya kutokuwa na wataalamu wazalendo na Serikali kuzungukwa.
Mkazi wa Dodoma anayejishughulisha na kilimo, Erick Sese alitaka Serikali ijifunze yaliyotokea katika uchimbaji wa madini mbalimbali na kuhakikisha hayajitokezi katika gesi.
Sese alisema kama hakuna wataalamu wa kutosha hapa nchini wa gesi, ni vyema gesi hiyo iachwe kuchimbwa kwani haiozi lasivyo inaweza kunufaisha watu wachache ambao ni wajanja.
"Tunaona kwenye madini wanabeba tani nyingi za mchanga kwa madai wanakwenda kufanyia utafiti, huo utafiti unafanyika wapi kama sio kutuibia Watanzania kila siku, nina mashaka hata kwenye gesi.
“Tunaona hata tanzanite inachimbwa Tanzania lakini inauzwa nje kwa nembo ya Kenya, hata sangara wa Mwanza wanauzwa kwa nembo ya Kenya na Watanzania hatufuatilii vitu kama hivi vinavyoua uchumi wa nchi yetu," alisema.
Kwa upande wake, Agustino Ndejembi ambaye ni mfanyabiashara wa nafaka, alisema kuwa suala kubwa la gesi ambalo linabeba uchumi wa nchi si la kuchukulia mzaha .
"Naona ninyi mliokuja kukusanya maoni kama vibaraka wa kampuni za uwekezaji wa gesi maana haiwezekani mwisho wa kuwasilisha maoni ni mwezi huu, muache kutania Watanzania suala la gesi litabadilisha maisha ya Watanzania lazima mjipange ili mpitishe jambo litakalowanufaisha  Watanzania," alisema Ndejembi.
Naye Juma Nduguye wa Chuo Kikuu cha St John, alisema tatizo la Watanzania ni mimi kwanza Tanzania baadaye na kupendekeza  kuundwe bodi ya gesi itakayojumuisha wataalamu mbalimbali na viongozi wa vyama vya siasa kwani kuna watu wenye kawaida ya kuzunguka Serikali.
Awali mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Maseke Mabiki alisema hadi Juni mwaka huu, mikataba 26  ya uzalishaji na mgawanyo wa mapato ilikuwa imesainiwa kati ya Serikali na kampuni 18 za utafutaji wa mafuta.
Naye Elias Kilembe kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) alisema kuwa hakuna mfumo wa kusimamia gesi ndio maana Serikali inawekwa  sera ili  kuweka mfumo mzuri na baada ya sera wataandaa sheria na kanuni kwani gesi ni rasilimali ya Tanzania lazima isimamiwe vizuri.

No comments: