Friday, October 19, 2012

WAATHIRIKA MABOMU YA GONGO LA MBOTO KUPEWA NYUMBA KABLA YA MASIKA...

Misururu mirefu ya watu na magari waliokuwa wakikimbia makazi yao kujinusuru na milipuko ya mabomu katika eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Nyumba za waathirika wa mabomu wa Gongo la Mboto mkoani Dar es Salaam zilizopo katika eneo la Msongola lililotengwa na Serikali kwa ajili ya makazi mapya ya watu hao, zimekamilika kwa asilimia 95 na watakabidhiwa kabla ya kuanza kwa mvua za masika.
Nyumba hizo 36 zilijengwa na Kikosi cha Shirika la Uchumi na Maendeleo la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT), licha ya kukamilika, bado zinakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alibainisha hayo hivi karibuni katika kikao kilichowajumuisha wabunge, madiwani pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na kuomba wizara hiyo kufikisha umeme maeneo hayo ili wakazi hao wahamie kwa muda uliopangwa.
Akijibu suala hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alisema gharama za kufikisha umeme katika makazi hayo mapya zinagharimu Sh milioni 400.
Alimshauri Mkuu wa Mkoa kuiandikia wizara kuomba kupelekwa kwa umeme katika maeneo hayo na kumhakikishia kuwa umeme huo utafika kwa muda muafaka isipokuwa lazima wapate taarifa hiyo.
Milipuko ya mabomu ilitokea Februari 15, mwaka jana katika Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Gongo la Mboto na kusababisha vifo vya watu takriban 20 na majeruhi 400. Pia  nyumba na mali mbalimbali za wananchi ziliharibiwa na nyingine kupotea kabisa.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ilifanya tathimini ya uhakiki kwa uharibifu huo na kubaini nyumba 75 ndizo zinazotakiwa kujengwa upya kutokana na kuwa na uharibifu mkubwa.
Hata hivyo, baadaye Serikali ilipunguza idadi ya nyumba zilizotakiwa kujengwa upya hadi kufikia 36 baada ya uhakiki mwingine kufanyika na kuonekana ndizo zilizopata athari kubwa.

No comments: