MHITIMU ALIYEPATA KAZI NZURI AFA KATIKA AJALI YA NDEGE NEPAL...

KUSHOTO: Watu wakishuhudia ndege hiyo ikiteketea moto. JUU: Ben Ogden enzi za uhai wake kabla ya ajali. CHINI: Ben siku alipohitimu masomo yake Oxford.
Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Oxford mwenye miaka 27 ambaye anafanyakazi kwenye kampuni moja kubwa ya kimataifa ya sheria ni miongoni mwa Waingereza saba waliokufa katika ajali ya ndege nchini Nepal, imefahamika.
Ben Ogden, ambaye ameelezewa na wenzake kama 'mwanasheria bora', alikuwa akiishi na rafiki yake wa kike mjini London na kufanya kazi katika kampuni ya sheria ya Allen & Overy Solicitors.
Hivi karibuni alifuzu na kwenda mapumziko ya safari ndefu huko Nepal ikiwa ni kujiweka sawa kabla ya kuanza kazi yake mpya kama mshirika katika kampuni hiyo.
Ndege yenye injini mbili, inayofanya safari zake za ndani ya Sita Air, ilikuwa imebeba watalii kuelekea eneo la Everest ndipo ilipoanguka dakika chache baada ya kuruka karibu na Mto Manohara ulioko ncha ya kusini-magharibi ya mji mkuu wa Kathmandu mwishoni mwa wiki iliyopita. Watu wote 19 waliokuwamo walifariki dunia.
Janga hilo limetokea wakati wa kumbukumbu ya ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1992 mjini Kathmand ambayo iliua watu wote 167 wakiwamo Waingereza 36 wakati ndege hiyo ikikaribia uwanja wa ndege wa mji huo.
Waingereza wengine waliokufa wametajwa jana na kampuni binafsi ya usafiri ya Sherpa Adventures kuwa ni Raymond Eagle, 58, Christopher Davey, 51, ndugu wawili Vincent Kelly, 50, na Darren Kelly, 45, Timothy Oakes, 57, na Stephen Holding, 60, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Press Association.
Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola (FCO) imesema kwamba familia za waathirika wote zimeshataarifiwa.
Miili kadhaa iliyoteketea kwa moto ilikuwa imezagaa mita kadhaa kutoka ndege hiyo ilipokuwa ikiendelea kuteketea, mashuhuda wameelezea jinsi walivyosikia abiria 'wakipungia na kulia' wakati moto ulipolipuka katika ndege hiyo mara ilipoanguka majira ya saa 12:30 asubuhi baada ya kuwa imegonga ndege mkubwa angani.
Ilifahamika kwamba rubani wa ndege hiyo iliyoangamia aliamriwa kugeuza ndege hiyo mwelekeo na kutua kwa dharura baada ya kueleza maofisa wa uwanja wa ndege kwamba ndege amegonga injini yake ya mbele, kuharibu pangaboi na kuzimika.
Maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga walisema athari hiyo ilimfanya rubani 'kuchanganyikiwa' na kuelezwa awashe injini ya pili lakini injini iliyoharibika ikashika moto, kwa mujibu wa gazeti la Daily Telegraph. Rubani kisha akajaribu kutua ndege hiyo kwenye mto katika harakati za kuzima moto lakini badala yake pua ya ndege ikajikita kwenye uwanja wa soka ulio karibu.
Mama mmoja wa nyumbani, Tulasa Pokharel mwenye miaka 26, ambaye nyumba yake iko mita chache kutoka ilipoanguka ndege hiyo, amekumbushia pale ndege ilipojikita ardhini. Alisema: "Wakati ule niliweza kusikia watu kadhaa ndani ya ndege wakilia. Tulipokwenda kuwataarifu polisi na mamlaka nyingine kuhusu tukio hilo na kurejea, palikuwa kimya. Tuliona ndege ikiteketea moto na wote kufariki."
Aliongeza: "Tuliweza kusikia watu ndani ya ndege wakilia, lakini hatukuweza kurusha maji kwenye ndege ile kuzima moto sababu tulikuwa tukiogopa kwamba injini zilikuwa zikikaribia kulipuka."
Alisema pia aliona mikono ikipungia madirishani mwa ndege hiyo wakati ikikaribia kujikita ardhini na kusema kwamba kikosi cha moto kiliwasili ndani ya dakika kumi kuzima moto huo.
Waingereza wote saba walikuwa wakitarajiwa kuanza safari yao ndefu katika milima ya Himalaya, wakianzia kambi ya Everest Base, kupitia kampuni ya usafiri ya Explode Worldwide yenye makazi yake Hampshire, mwishoni mwa wiki iliyopita.

No comments: