Sunday, October 21, 2012

MALI ZA NABII MWINGIRA WA EFATHA ZACHOMWA MOTO...

Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira.
Wananchi  wenye  hasira  ambao  wanadaiwa kuwa wakazi wa   kijiji  cha Sikaunga  wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa  wamevamia  moja ya kambi iliyomo kwenye  shamba  lililonunuliwa na Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha Tanzania na kusababisha  hasara ya zaidi ya  Sh milioni 228.
Wakazi hao  walifanya uharibifu  mkubwa  ambapo  inadaiwa  kuwa  wameyateketeza kwa moto matrekta mawili makubwa aina ya New Holland  pia nyumba  kadhaa  zilidaiwa kubomolewa na shehena ya mahindi  kuchomwa moto  wakimtaka  mwekezaji huyo  kuwaachia  ardhi  yao  ambayo wanadai  amewapora.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa  wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amekiri kutokea kwa  tukio hilo hivi karibuni ambapo watu 11 wanaotuhumiwa kuongoza wenzao kufanya  uvamizi  huo  wamekamatwa  na juzi walifikishwa  mahakamani.
Inadaiwa kuwa, tangu Nabii Mwingira auziwe shamba hilo lililokuwa shamba la taifa la mifugo  la DAFCO–Malonje lenye ukubwa ekari 10,000 na uongozi wa Halmashauri ya  Manispaa miaka zaidi ya mitano iliyopita kwa bei ya Sh milioni 600  huku mwekezaji wake  akituhumiwa  kukiuka mkataba  wa mauziano  ya  shamba hilo.
Hivyo, Serikali  baada ya kupokea taarifa kuwa mwekezaji aliyenunua shamba   hilo  ameanza kulima mazao mbalimbali tofauti  na  mkataba  wa ununuzi ambao  unamtaka kufuga, iliuagiza  uongozi wa  mkoa  wa Rukwa  kuupitia upya mkataba huo ambapo  tume  tayari  imeundwa  pia imeshamaliza  kazi yake.
Licha ya  kukiukwa  kwa mkataba huo, lakini  pia  watumishi wa  shamba  hilo  wamekuwa  wakituhumiwa  kukamata na kutesa wananchi wanaishi pembeni mwa shamba hilo huku  baadhi yao  wakilalamika kukatwa masikio na wanawake kubakwa.
Kutokana na kadhia hiyo, kumeibuka uhasama baina ya watumishi wa Efatha waliomo ndani ya shamba hilo na wananchi wa  vijiji jirani na shamba  hilo.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi kijijini humo ambao hawakuwa tayari majina yao  kuandikwa gazetini wamedai kuwa wamevumilia kiasi cha kutosha, ndiyo maana wameamua kuchukua sheria mkononi, ikiwa ni jitihada za kumlazimisha mwekezaji huyo  kuwaachia ardhi hiyo ambayo  wanadai ni mali yao.
Akizungumzia  sakata hilo la  uvamizi   uliofanywa katika kambi hiyo ya Sikaunga  ndani ya shamba hilo  Mchungaji Kiongozi Michael Meela wa Kanisa hilo la Efatha mkoani Rukwa alikiri  kuwa  mmiliki wa shamba hilo amepata  hasara  ya zaidi ya Sh milioni 228 kufuatia uharibifu huo  uliofanywa na wananchi hao  wenye  hasira.
Akifafanua alisema kuwa uvamizi huo ulitokea mara tu baada ya Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha kuhutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo na kuwahamasisha wananchi watumie nguvu ya umma kuyakomboa mashamba yao yaliyochukuliwa na mwekezaji huyo.
Hata hivyo, alikiri kuwa katika risala  yao   iliyoandaliwa  na Mtendaji wa kijiji  cha Sikaunga, R. Mkangwa  kwa niaba ya Serikali ya kijiji  hicho  na kusomwa mbele yake  pamoja kueleza changamoto  kadhaa  zinazowakabili, lakini pia wakazi wa kijiji hicho  walitaka kujua  hatima  ya shamba hilo la  Efatha  kama watarudishiwa  wao  kwa sababu  mwekezaji huyo  amekuwa  akiwatishia maisha  yao.
Hata hivyo  Mbunge  Malocha amekanusha kuhusika na suala hilo, akisema taarifa hizo zimepikwa ili kumchafulia jina, akisisitiza hazina msingi  wowote na kuongeza alikwenda hapo kufanya  mikutano  ya hadhara ili  kuwahamasisha  wananchi  kujitokeza kutoa maoni  ya Katiba mpya  mbele ya  tume  ya kuratibu  maoni hayo  ambayo kwa  sasa  inafanya mikutano   wilayani  Sumbawanga.
Hata  hivyo  Kamanda Mwaruanda alipohojiwa na  gazeti hili  alikanusha  na kueleza kuwa  hakuna ushahidi  wa kutosha  kuwa mbunge huyo alihamasisha wakazi wa Sikaunga  kutumia nguvu  ya umma  kuyakomboa  mashamba hayo  yaliyochukuliwa na  mwekezaji Nabii Mwingira. Juhudi za kumpata Nabii Mwingira hazikufanikiwa.

No comments: