BEI YA PETROLI YASHUKA, SASA LITA NI SH. 1,994...

Bei kikomo ya mafuta kwa mwezi huu imetangazwa ambapo petroli imeshuka kwa Sh 306, dizeli kwa Sh 192 huku mafuta ya taa yakibakia katika bei ya awali.
Taarifa iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo, ilieleza kuwa kutokana na bei mpya, kwa sasa mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam yatauzwa Sh 1,994 au chini ya hapo kutoka Sh 2,300 iliyokuwepo mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa Kaguo, bei ya dizeli kwa Dar es Salaam imeshuka hadi kufikia Sh 1,950 au chini ya hapo kutoka Sh 2,142, huku mafuta ya taa yakibakia Sh 1,993 kutokana na kutoingia meli yoyote ya mafuta hayo.
Taarifa hiyo, ilieleza kuwa bei hizo zitaendelea kuongezeka kutokana na gharama za usafirishaji kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, ingawa kwa ujumla katika kila eneo punguzo litakuwa ni shilingi 306 na shilingi 192 kwa petroli na dizeli kwa lita moja.
"Kampuni za mafuta zipo huru kuuza kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo na kama mfanyabiashara atakiuka, atapewa adhabu ya kulipa Sh milioni tatu," alisema Kaguo.
Pia alivitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei zao katika mabango yanayoonekana bayana, ili kumfanya mteja afanye uchaguzi wa kununua mafuta akiwa anajua bei halisi ya mafuta katika kituo husika.
"Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
"Stakabadhi hiyo o itatumika kama kidhibiti cha ununuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama kuuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa," alisema Kaguo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaguo, bei ya juu kabisa ya mafuta hayo nchini itakuwa mkoani Kigoma na wilayani Karagwe ambapo petroli lita moja itauzwa kwa Sh 2,225, dizeli Sh 2,181 na mafuta ya taa Sh 2,224.

No comments: