ASKARI AJIFUNGUA MTOTO KATIKA MAPAMBANO AFGHANISTAN...

Askari wa Uingereza ambaye hakufahamu kama ni mjamzito amejifungua akiwa katika mstari wa mbele katika mapambano.
Mwanamke huyo alipata mtoto wa kiume katika Kambi ya Bastion Jumanne iliyopita - ikiwa ni siku chache baada ya Taliban kufanya shambulio kubwa zaidi kwenye kambi kuu ya vikosi vya Uingereza huko Helmand.
Mtoto huyo alizaliwa wiki tano kabla ya muda wake wa kawaida. Usiku mmoja kabla, mama na mtoto huyo walisemekana kuwa wanaendelea vizuri.
Timu ya madaktari wa magonjwa ya watoto kutoka Hospitali ya John Radcliffe mjini Oxford itakwenda nchini Afghanistan katika siku chache zijazo kumhudumia askari huyo na mtoto wake kabla ya kurejeshwa nyumbani kwa ndege.
Kuzaliwa kwa mtoto huyo kumewapiga bumbuwazi wakuu wa jeshi na kulazimika kuitisha ukaguzi wa ziada wa afya kwa askari wanawake ambao wamepelekwa katika ukanda wa mapambano.
Takribani askari 200 wamegundulika walikuwa wajawazito katika vita tangu mwaka 2003 - na kulazimisha makamanda kuwarejesha mara moja nchini Uingereza. Lakini hii ni mara ya kwanza kwa askari wa Uingereza kujifungua mtoto nchini Afghanistan.
Askari huyo, mpiganaji katika kikosi cha mizinga ambaye aliwasaidia askari waliokuwa wakipambana na waasi, hakufahamu kama alikuwa amebeba mtoto tumboni.
Alikuwa alikuwa amepangiwa kufanyakazi katika Brigedi ya 12 ya Mizinga tangu Machi, lakini siku mbili zilizopita alikuwa akilalamika maumivu makali ya tumbo.
Katika kustaajabisha kwake, madaktari walimtaarifu kwamba alikuwa akikaribia kabisa kujifungua.
Alikuwa katika wiki ya 34 ya ujauzito wake, ikimaanisha alipata ujauzito huo kabla ya kwenda Afghanistan kwa ziara yake ya kikazi ya miezi sita.
Alipelekwa hospitali ya Kambi ya Bastion iliyogharimu Pauni za Uingereza milioni 10 kukamilika ambako madaktari - ambao wanauzoefu mkubwa wa kuhudumia ukataji viungo vya mwili na kutibu majeraha ya risasi, wakamzalisha mtoto huyo wa kiume.
Licha ya sehemu ilipo, hospitali hiyo ni moja kati ya hospitali zenye vifaa bora duniani na yenye mashine za X-ray zinazohamishika, chumba cha upasuaji, CAT scanner na chumba cha uangalizi maalumu chenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 20 mahututi.
Vyanzo vya habari za kijeshi vilisema: "Tukio hili limetuacha tukiwa tumezibwa domo. Unajiandaa kukabiliana na majeraha ya vita katika Bastion - na sio mama anayejifungua mtoto. Ni gumzo la kambi hii.
"Hili ni tukio lisilo la kawaida. Mama aliyepangiwa majukumu hafahamu kwamba alikuwa mjamzito na hakujua kabisa kama ni mjamzito hadi alipojifungua. Hakufanya kitu chochote kibaya."
Luteni Kanali Andrea Lewis, ofisa mkuu wa hospitali hiyo, alisema: "Hili ni tukio la kipekee, lakini timu yangu imejipanga vema kwa matukio yasiyotarajiwa na wameshiriki kikamilifu katika kushughulikia suala hili.
"Napenda kuripoti kwamba mama na mtoto wanaendelea vizuri na wote tumefurahishwa na matokeo."
Askari huyo mwenye asili ya Fiji alifaulu mafunzo magumu kujiandaa kwa majukumu hayo, ambayo yalihusisha kutembea umbali wa maili nane na kukumbia maili tano, bila kuwa na fununu ni mjamzito.
Takribani wanawake 500 wa Uingereza kwa sasa wako kikazi nchini Afghanistan. Wanaweza kuhudumia kitengo chochote isipokuwa wale wote ambao majukumu yao ni 'kukaribia na kuua' - wanaojihusisha na kuwakabili maadui ana kwa ana.
Wanawake nane wamekufa nchini Irak na Afghanistan, asilimia mbili ya jumla ya vifo vya vita. Hao ni pamoja na Koplo Sarah Bryant mwenye miaka 26 anayetokea Carlisle, ambaye aliuawa katika mlipuko nchini Afghanistan mwaka 2008, na mwingine ni Luteni Joanna Dyer mwenye miaka 24 anayetokea Yeovil, rafiki wa Prince William. Aliuawa kwa bomu lililotegwa kando ya barabara nchini Irak mwaka 2007.

No comments: