Tuesday, August 21, 2012

SIRI ZA MWANARIADHA MO FARAH NA PACHA WAKE WA SOMALIA HIZI HAPA...

KUSHOTO: Dada mkubwa wa Mo Farah, Ifrah akiwa na wanawe katika mazingira magumu nchini Somalia. JUU: Hassan Farah. CHINI: Mo Farah akiwa na medali zake mbili za dhahabu alizotwaa kwenye Michezo ya Olimpiki iliyomalizika hivi karibuni mjini London.
Pacha wa shujaa wa Uingereza aliyetwaa medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki, Mo Farah amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu namna walivyotenganishwa wakati wakiwa watoto katikati ya ghasia za vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.
Katika simulizi ya kuhuzunisha ya maisha ya utotoni iliyofuatiwa na vurugu na mauaji, Hassan Farah amebainisha yeye na Mo kwamba walikuwa karibu kiasi cha kulala katika kitanda kimoja na mara nyingine kuchangia hata sahani wakati wa chakula.
Wawili hao wamefanana kiasi cha walimu na hata marafiki kuwachanganya mmoja na mwingine.
Lakini vijana hao walilazimika kuagana wakiwa na umri wa miaka minane pale wazazi wao walipofanya uamuzi mgumu kuwapeleka watoto wao watatu kati ya sita, akiwamo Mo, nchini Uingereza kujaribu kupata maisha mazuri. Ni tukio ambalo hakuna yeyote kati yao atalisahau na ilidumu hivyo kwa miaka 12 hadi mapacha hao walipoonana tena.
Hassan alikulia katikati ya vumbi na umaskini uliokithiri barani Afrika katika nchi ya Djibouti ambayo inapakana na Somalia, wakati kaka yake, ambaye alijikita katika viwanja vya michezo nchini Uingereza, akaja kuwa mwanariadha wa daraja la juu duniani.
Mo amekuwa akiongelea maisha yake ya zamani Afrika mara chache mno. Lakini gazeti la The Mail lilifanikiwa kumnasa Hassan nyumbani kwake huko Hargeisa, kaskazini mwa Somalia, wiki iliyopita.
Ni hapa, nusu ya dunia kutoka Uwanja vya Olimpiki huko London, kwamba Hassan alikuwa akifuatilia kwa njia ya televisheni akiwa na fahari kubwa na furaha wakati kaka yake akifanikiwa kunyakua medali mbili za dhahabu.
Ilikuwa usiku wa manane kabla ya waliokuwa wakienda kumpongeza kuacha kufika nyumbani hapo kwa Hassan kushiriki furaha aliyowaletea kijana huyo wa mjini mwao.
Juzi, bado akiwa anasherehekea na akiwa bado kavalia jezi ya timu ya Olimpiki ya Uingereza, Hassa alizungumzia matukio yasiyokuwa ya kawaida ambayo yaliwasambaratisha na kaka yake.
"Tulikuwa pamoja kwa kila kitu, tulikuwa hatutenganishiki," alisema. "Tulichangia chakula kwenye sahani moja, tulilala pamoja na tulicheza na kusoma pamoja. Kulikuwa na penzi maalumu kati ya mapacha ambao ni tofauti kutoka mapenzi ya ndugu wengine.
"Pale Mo alipopelekwa mbali nami nilibaki na pengo kwenye moyo wangu. Pengo hilo halikuweza kuzibika, lakini bado yuko mahali kwenye moyo wangu na nafahamu nipo kwenye moyo wake pia.
"Kama familia nyingi za Wasomali tulisambaratishwa na vita. Kwangu lilikuwa janga kubwa kuliko chochote. Ninahisi nimepoteza nusu ya mwili wangu, pacha mwenzangu.
"Siku hizi wote tuko pamoja karibu, licha ya ugumu wa usafiri na mawasiliano katika nchi hii."
Hassan anaamini hawawezi kubadilisha miaka iliyopita wakiwa mbalimbali, lakini ilijieleza hivyo pale Mo aliposhinda dhahabu kwenye mbio za mita 10,000, kaka yake alikuwa ni mtu wa kwanza kumpigia simu.
Hassan alisema: |"Aliniambia, "Niombee, ndugu yangu. Nina matumaini makubwa kwamba naweza kushinda dhahabu ya pili. Ndicho nilichokuwa nikisubiri kwa muda wote huu".
Baba wa mapacha hao ni Muktar Farah. Aliondoka Somalia akiwa kijana na kuweka makazi yake mjini London ambako alifanya kazi kama Mshauri wa Mifumo ya Kompyuta.
Wakati wa likizo alikwenda kutembelea kwao ambako alimuoa Amran na kuamua kuishi huko. Waliishi pamoja mjini Mogadishu na tayari walikuwa na watoto wawili wa kiume na msichana mmoja kabla ya kuwazaa mapacha hawa.
Mohammed na Hassan walizaliwa mjini Mogadishu Machi 1983, wakati wa vuguvugu la ghasia na machafuko katika mji mkuu huo wa Somalia. Mapigano kati ya makundi hasimu ya kikabila yalikuwa kitu cha kawaida kila siku mjini humo. Rais Dikteta Siad Barre ambaye alitwaa madaraka mwaka 1969, alikuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa wapiganaji ambao waliunganisha vikosi vyao dhidi yake. Mwishowe Barre akang'olewa na kuuawa mwaka 1990, na hapo vita vya kikabila vikashika nafasi katika nchi hivyo na kuathiri hatima yake kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Matumaini pekee kwa usalama na uimara kwa sasa umeelekezwa kwenye uchaguzi wa kidemokrasia uliopangwa kufanyika mwezi ujao.
Kwa wazazi wa Mo na Hassan uchangukaji wa nchi yao baada ya 1990 unamaanisha maamuzi makali na ya kuumiza mno. Hassan alikumbuka: "Tulikuwa wadogo na kulikuwa na ufyatuliwaji risasi na mauaji kila siku karibu na nyumbani kwetu. Tulijua baba yetu anarejea Uingereza kujaribu kuandaa makazi kwa ajili ya familia yetu, na mama yetu aliwarejesha kaka zetu kijijini kwao maeneo ya kaskazini.
"Familia ya kila mmoja ilikuwa kwenye machafuko wakati huo. Kulikuwa na kambi za wakimbizo nje ya jiji, watu waliishi kwenye mahema. Wengine walikuwa wakitaka kutoka na ingawa tulikuwa vijana tulifahamu uliwakuwa wakati ambapo familia zetu zilikuwa zikifanya maamuzi yenye kuumiza.
"Walitupeleka, na dada yetu mkubwa Ifrah, kuishi nchini Djibouti pamoja na bibi yetu ili tuweze kupata amani katika maisha yetu ya utotoni. Kwa Mo na mimi, ilitosha kwamba tulikuwa tukikaa pamoja."
Bibi wa vijana hao kwa upande wa mama alikuwa akiishi katika moja ya vitongoji maskini sana kwenye Jiji la Djibouti. Kutoka Oktoba hadi Aprili wastani wa joto ni nyuzijoto 37.
Hassan alisema: "Mimi na Mo ni watoto wanamichezo. Lakini ilikuwa joto sana, joto mno kiasi cha kushindwa kufanya chochote. Tulicheza soka mitaani na kukimbia sana eneo hilo, tulicheza chesi na kila mara tuliwashinda vijana wengine.
"Lakini pale hapakuwa na vifaa, ni mitaa pekee. Tulipendelea mno soka na Mo na mimi tulicheza upande mmoja, hakuna aliyeweza kutushinda. Huko tulikuwa wakimbizi wa kivita, tukiishi bila wazazi wetu, na ninakumbuka maisha ya furaha ya utotoni. Nilichohitaji wakati huo kwa ulinzi na uimara wangu alikuwa ni kaka yangu.
"Tulifanya kila kitu pamoja, tulikuwa marafiki wakubwa. Mara chache kulikuwa na mapigano kati yetu na yalidumu kwa dakika moja, wote tuliangua kicheko."
"Hakuna aliyeweza kushawishi mapacha watengane.
"Tulibadilishana nguo wakati wa mchana kuwachanganya watu.
Hassa anakumbuka siku moja alimchokoza binti mmoja akiwa mbele ya nyumba ya bibi yake. Binti yule alipirudi na kaka zake wakamkuta Mo ameketi pale. Ilibaki kidogo ashushiwe kipigo lakini hakuacha hilo litokee na kuamua kujitokeza na kubeba msalaba wake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kati yangu na Mo."

No comments: