Monday, August 13, 2012

MWAKYEMBE AAGIZA WIZARA KUWALIPA MALIMBIKIZO WAFANYAKAZI WA TAZARA...


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kutafuta kwa udi na uvumba fedha hata ikibidi kuwakata mishahara wakurugenzi wa wizara hiyo ili kuwalipa wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) mishahara yao.
Dk Mwakyembe alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana baada ya wafanyakazi hao kufikisha kilio chao mbele yake na kudai kuwa hawajalipwa mishahara yao kwa miezi mitatu mfululizo tangu Juni.
Akizungumza na wafanyakazi hao, aliwapa pole kwa ukata unaowapata na kuwahakikishia kuwa dawa ya kinachoendelea ndani ya menejimenti ya shirika hilo inachemka.
“Kwa kweli mimi sasa si mgeni wa wizara hii na kama waziri siwezi kuvumilia nyie mkae muda wote huo bila mshahara, ndio maana naagiza fedha zitafutwe popote pale ndani ya wizara yangu na mlipwe mishahara yenu ya Juni na Julai yote kwa pamoja,” alisema Mwakyembe na kushangiliwa na wafanyakazi hao.
Alisema fedha ambayo watatakiwa kulipwa wafanyakazi hao ya mishahara ya miezi hiyo miwili, itapelekwa wizarani kwa ajili ya kurejesha fedha zilizochukuliwa kulipia mishahara hiyo.
Hata hivyo, Mwakyembe alisema aliguswa juzi alipotembelea karakana ya shirika hilo na kumkuta mfanyakazi mmoja ambaye alimueleza kuwa ingawa yupo kazini, hawajalipwa mishahara ya miezi mitatu, lakini pia hata posho hajalipwa.
“Sasa hili limenigusa sana kwani yule mama aliniambia yupo kazini, lakini hajalipwa, nikamuuliza hata posho zenu akasema hata posho, sasa sijui inakuwaje wakati tayari nimeshaidhinisha malipo ya posho, ndio maana nasema siwezi kukubali mkae bila mishahara,” alisema Dk Mwakyembe.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Erasto Kihwele aliwasilisha malalamiko ya wafanyakazi hao ambapo walitaka Serikali iwaondoe madarakani Mkurugenzi Mkuu wa Tazara na Naibu wake, kwa kuwa wameshindwa kuliendesha shirika hilo.
Kihwele alisema viongozi hao ambao ni Mkurugenzi Mkuu Kashambatwa Mbikusita Lewanika na Naibu wake, Damas Ndumbaro, wameshindwa kushughulikia maslahi ya wafanyakazi na kuendesha shirika hilo wakati uwezo wa kuliendesha upo.
“Pale Mbeya yapo magari moshi, magari ya mizigo, matangi mawili ya mafuta yenye ujazo wa lita 96 na mizigo ipo, lakini leo ni siku ya tano hayasafirishwa kwa nini? Sisi tupo hapa hata mapato ya Juni na Julai hatujui, tunaomba waondolewe, la sivyo hatufanyi kazi mpaka waondoke,” alisema Kihwele.
Akijibu ombi hilo, Mwakyembe aliwapongeza wafanyakazi wa shirika hilo kwa upande wa Tanzania kwa kuwa wavumilivu na kutogoma mara kwa mara ikilinganishwa na wenzao wa Zambia licha ya kuwa na matatizo makubwa.
Alisema kwa mwaka huu, pekee shirika hilo lilipoteza siku 60 za utendaji kutokana na migomo ya wafanyakazi, lakini kati ya siku hizo, 50 ni kutoka kwa wafanyakazi wa Zambia na 10 pekee ni kwa wafanyakazi wa Tanzania.
Hata hivyo, aliwataka wawe watulivu na kuendelea na kazi wakati suala la menejimenti likishughulikiwa kwa kuwa yeye pekee kama waziri hana mamlaka ya kutoa uamuzi hadi ashirikiane na kukubaliana na Waziri wa Uchukuzi wa Zambia.
“Naomba msigome, endeleeni kufanya kazi suala la mishahara yenu nalishughulikia, kesho (leo) ninakutana na menejimenti yenu kuzungumzia haya haya, nawaahidi kama itafikia kuwachukulia hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu na mkataba tuliojiwekea baina ya nchi mbili,” alisisitiza.

No comments: