Friday, August 17, 2012

AMGONGA NA KUMUUA MSTAAFU MIEZI MIWILI BAADA YA KUPATA LESENI...

KUSHOTO: Mtaa ambako ajali hiyo ilitokea. KULIA: Abbey Frost anayetuhumiwa kumgonga mstaafu na kumuua.
Dereva kijana amepatikana na hatia ya kumgonga na kumuua mstaafu wakati akikatisha mtaa wenye pilika nyingi, miezi miwili tu baada ya kupata leseni ya udereva.
Abbey Frost, ambaye alikuwa na miaka 18 wakati huo, alikuwa katika ziara ya manunuzi na rafiki zake soko la mjini la Guildford ndipo alipomgonga William Etherington mwenye miaka 85, mpiganaji wa zamani wa Vita ya Pili ya Dunia katika kikosi cha Mizinga.
Alikuwa tayari ameshavuka barabara moja na alibakisha inchi kadhaa kufikia sehemu ya watembea kwa miguu ndipo alipogongwa na Frost, ambaye alikuwa akiendesha gari la bibi yake.
Athari zake zilisababisha kujibamiza kwenye kioo cha mbele cha gari hilo kabla ya kutupwa chini mtaani.
Alifariki siku sita baadaye katika Hospitali ya St. George iliyoko Tooting, huko South London, Mei 19, 2011.
Frost sasa ana miaka 19, alidai mstaafu huyo alisimama barabarani kwa nia ya kumpisha gari lipite, kabla ya kuamua kukatisha ghafla barabara ya North Street.
Baraza la Mahakama lilioneshwa picha za CCTV kuhusu athari ya ajali hiyo, ikifuatiwa na mashuhuda wakikimbilia kwenda kutoa msaada.
Mwendesha Mashitaka Ruby Selva alieleza jinsi William alivyopanda basi huko Guildford, mjini Surrey, Mei mwaka jana.
"Hali ilikuwa nzuri. Ilikuwa siku yenye jua. North Street ilikuwa na pilika nyingi za waenda kwa miguu kutokana na kuwa siku hiyo kuwa ni ya gulio," alisema.
"Picha hizo za CCTV zinaonesha William akivuka kutoka upande wa soko, akikatiza barabara ya kwanza na wakati akivuka barabara ya pili na kukaribia njia ya waenda kwa miguu, aligongwa.
"Shuhuda wa ajali hiyo alielezea kuwa alikuwa inchi kadhaa kutoka njia ya waenda kwa miguu."
Selva aliongeza: "Frost alifaulu mtihani wa kupatiwa leseni Februari mwaka huo na kutunukiwa leseni kamili ya Uingereza Machi, 2011, miezi kama miwili iliyokuwa imepita.
"Mahakama inasema uendeshaji wake ulikuwa wa kizembe."

No comments: