Sunday, May 6, 2012

MTALII CHUPUCHUPU KUUAWA NA DUMA...


Akilazimika kulala ardhini huku damu ikibubujika kichwani, huyu ni mtalii wa Uingereza ambaye ameepuka kifo kimiujiza baada ya kushambuliwa na duma wenye hasira.
Violet D'Mello alikuwa akitembelea hifadhi ya wanyama akiwa na mumewe, Archie wakati wa ziara yao nchini Afrika Kusini kusherehekea kutimiza miaka 60 ya kuzaliwa.
Lakini siku yao iliisha vibaya kwa balaa wakati duma wawili walipomrudi na kumtupa chini kisha kuanza kumng'ata miguuni na kichwani katika tukio la kutisha mno.
Watalii wengine walijaribu kuwatisha duma hao wamwachie wakati askari wa hifadhi hiyo akipambana huku na kule kuwasambaratisha mbali na mwanamke huyo aliyejeruhiwa.
Na mumewe? Yeye alikuwa akiendelea kuchukua picha akidai hakugundua kabisa kilichokuwa kikitokea.
Shambulio hilo lilitokea kwenye hifadhi ambayo watalii hulipia Pauni za Uingereza 4.50 kuwashika-shika duma hao Mark na Monty ambao wote wamefungiwa kwenye uzio.
Ndani ya Hifadhi binafsi ya wanyama ya Kragga Kamma jirani na mji wa Port Elizabeth, Bibi D'Mello alipiga picha na duma akiwakwaruza kichwani huku akiwafagilia, "wanyama wazuri walaini."
Hatahivyo, mambo yakabadilika ghafla baada ya duma mmoja kumnyakua binti wa miaka minane, Camryn Malan, mmoja kati ya watalii wengine waliokuwa jirani, na kuanza kumng'ata mguu wake.
Bibi D'Mello akamuwahi kaka wa binti huyo mwenye miaka saba, Calum, akimwambia asikimbie kusudi aepushe wanyama hao kumdhuru zaidi, lakini wakati akifanya hivyo duma hao wakamgeukia yeye.
Mama huyo wa watoto wawili amesema: "Sikutegemea kama wangenishambulia kwa sababu ni mtu mzima. Lakini kitu kingine nilichobaini nilikuwa kwenye sakafu na duma hao walikuwa juu yangu kidogo.
"Alianza kunikwaruza vibaya sana na kisha nikahisi mwingine akinifuata pia na mmojawapo akakita mdomo wake shingoni mwangu.
"Nilikuwa nikipiga mayowe na kujaribu kujishika shingoni kujikinga, lakini niling'atwa miguu yangu yote na chini ubavuni karibu na mapavu yangu.
"Watu wote eneo lile walikuwa wakipiga mayowe, na sikujua jinsi nilivyookoka. Nilisikia sauti ndani yangu iliniambia, "Usikimbie. Usikimbie kabisaa. Usijitikise, jifanye tu umekufa."
"Hatimaye mtu mmoja akaja na kuwatimua mbali nami na mume wangu akaniinua kutoka sakafuni."
Mke huyo kutoka Aberdeen, alikuwa akibubujikwa damu kwenye majeraha yake miguuni, kichwani na tumboni na akalazimika kushonwa nyuzi hospitalini.
Alisema: "Madaktari hospitalini walisema duma kwa kawaida wanalenga maeneo ya tumboni na kuwamaliza adui zao, hivyo nilikuwa na bahati kuwa hai."
Bwana D'Mello mwenye miaka 64, rubani wa helikopta ambaye aliandaa safari ya mwezi mzima kama zawadi ya bethdei kwa mke wake, alisema aliendelea kuchukua picha hadi pale alipogundua kuwa duma walikuwa wakimng'ata mkewe.
Aliongeza: "Sikufanya chochote na askari hakuwa na fimbo kuweza kumkinga mkewe.
Mwishoni mwanamke kutoka mapokezi akaja na fimbo ambayo askari akaitumia kuwatishia duma na kukimbia. Shambulio hilo linaweza kuwa lilidumu kwa dakika tatu hadi pale walipoingilia kati.
Alisema: "Tuliingia kwenye hifadhi na kulikuwa na duma wawili wakirandaranda ndani. Kulikuwa na bango lililoruhusu kusogelea duma hao na kuwashika-shika huku ukiwa sambamba na askari.
"Tuliamua kuwaendea kwa kuwa ilionekana kuna usalama, na mwanzoni duma walikuwa watulivu. Tulikuwa pale pamoja na familia moja waliokuja na watoto wadogo.
"Askari alikuwa msichana, aliyesema tunaweza kwenda pale na kuwashika-shika duma. Lakini mke wangu alipowafuata kufanya hivyo, wanyama waliinuka na kuanza kuondoka.
"Askari akatuambia kuwa kwa wakati ule wa mchana huwa hawapendi bugudha. Tukawafuata na kadri tulivyowakaribia mmoja wa duma akageuka na kumnasa binti aliyeingia mle ndani.
"Alipiga kelele kubwa na tukageuka kujua kinachoendelea. Alimlalia binti tumboni huku mnyama yule akimng'ata."
Wanandoa hao walilazimika kusitisha mipango yao kwa siku kadhaa kabla ya tukio hilo la Jumamosi lakini wakaendelea na mapumziko yao katika hifadhi nyingine karibu na Port Elizabeth.
Huku akitetemeka, Bibi D'Mello alikimbizwa hospitali kwa matibabu baada ya tukio hilo.
Alifungwa bendeji katika majeraha yake kichwani, tumboni na miguuni na akapewa dozi ya dawa za kupunguza maumivu na dawa za kuua bakteria.

No comments: