KUSHOTO: Mzee Alan Smith enzi za uhai wake. JUU: Mama wa Matthew (kushoto) na mpenzi wa Matthew. CHINI: Mgahawa wa BB ambako ugomvi ulianzia.
Baba aliyekuwa ametoka kwenda kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa binti yake ameshambuliwa vibaya kwa kuchomwa visu hadi kufa mbele ya familia yake sababu tu ya kuuliza kilichokuwa kikimliza mtoto mmoja kwenye mgahawa waliokuwamo, mahakama imeelezwa jana.Alan Smith mwenye miaka 63, alichomwa visu zaidi ya mara tano akiwa ameketi na mpenzi wake, bintiye na mkwewe katika mgahawa mmojamashariki mwa jiji la London.
Mtuhumiwa wa mauaji hayo, Matthew Quesada, aligeuka mbogo pale Alan alipoinuka na kumfuata mtuhumiwa kwenye mgahawa wa BB kumuuliza kuhusu binti yake aliyekuwa akilia kama yuko salama, wazee wa baraza walielezwa.
Matthew akamjibu, "Inakuhusu nini?" kabla ya kuanza kumshambulia na kumtoa nje ya mgahawa.
Akiwa amekasirika mno, Matthew ambaye wakati huo alikuwa na miaka 25, akamchukua mchumba wake na kwenda kumuanza nyumbani na kubeba silaha.
Akiwa amebeba kisu, alirudi tena kwa kasi na kuivamia familia ya Alan waliokuwa wakiingia katika mgahawa mwingine wa Roma walipokwenda kupata chakula cha jioni kwa mara ya pili kuepusha matatizo zaidi.
Ni hapo inapodaiwa Matthew alianzisha mashambulio ya kimyakimya, akimchoma visu Alan kwenye kichwa na mwilini.
Wakati Estelle Jenkins akijaribu kuingilia kati ya baba yake na adui yake, Alan alijaribu kujinasua kwa kujilaza kwenye meza kabla ya kuanguka sakafuni ambapo alijaribu bila mafanikio kumzuia muuaji huyo, mahakama imeelezwa.
Matthew alimwachia pale tu mkwe wa Alan, Mark Jenkins aliporusha kiti na kusitisha shambulio hilo, huku mpenzi wa Alan, Denise Facey akishuhudia, mahakama imeelezwa.
Baada ya kisu kuchomolewa, walipiga simu kuita madaktari ambao walifika na kulazimika kumfanyia upasuaji wa dharura wa moyo kwenye moja ya meza za mgahawa huo.
Baadaye alipandishwa ndege kupelekwa hospitalini ambako alifariki dunia kutokana na majeraha kadhaa, matatu kati ya hao yakiwa mabaya sana.
Matthew ambaye sasa ana miaka 26 amekanusha kumuua Alan Machi 26, mwaka jana.
Mwendesha mahitaka, Roger Smart amelieleza baraza la mahakama la Old Bailey kuwa Matthew amekiri kumchoma visu Alan na kwamba ilisababishwa na akili yake ilivyomtuma wakati ule.
Mahakama imeelezwa kuwa kabla ya tukio hilo, Alan alikuwa akiisubiria familia yake ifike kwenye mgahawa huo wa BB uliopo Leyton mjini London, ndipo Matthew alipoingia na binti yake aliyekuwa akilia.
Baada ya dakika chache wakati kilio kikiendelea, na wakati Matthew akimnawisha binti yake mikono kwenye karo, Alan alimfuata kumuuliza kama kuna tatizo lolote kwa binti yake, imedaiwa.
Hatahivyo, baba huyo wa watoto wawili aligeuka mbogo na kumsukuma mhudumu kwa hasira akijaribu kutaka kuingia jikoni lakini akadhibitiwa.
Baada ya hapo akajaribu kutumia simu ya kwenye mgahawa, lakini akazuiwa kwa maelezo kuwa haruhusiwi.
Baraza hilo la Mahakama la Old Bailey limeelezwa kwamba wakati Matthew akielekea mgahawa wa jirani kuazima simu akiwa na binti yake huyo, familia ya Alan ikawasili.
Wakati Alan akiwataarifu kwamba watakula chakula sehemu nyingine alisikika Matthew akisema kwenye simu, "Nahitaji kipande" huku alan na familia yake wakitoka kwenye mgahawa.
Wakiwa wanaondoka Matthew alisikika akiwapigia kelele akiwaambia, "Unaona. Wewe? Nitakukamata tu."
Kesi hiyo inayotarajiwa kusikilizwa kwa wiki tatu, inaendelea.

No comments:
Post a Comment