Monday, April 30, 2012

ASIMAMISHA SHUGHULI ZOTE MTAANI BAADA YA KUTISHIA KULIPUA JENGO...


Jamaa huyo mara baada ya kutiwa nguvuni huku akiwa tumbo wazi.
Huyu ndiye mtu anayedaiwa kusimamisha shughuli zote katikati ya Jiji la London jana baada ya kutishia kulipua jengo na tuhuma za kuwashikilia mateka wanaume wanne huku akidai kubeba mabomu.
Mtu huyo alikamatwa majira ya saa 9 alasiri na kukokotwa bila shati hadi kwenye gari la polisi kabla ya polisi kuanza kuchunguza kwa umakini jengo hilo lililoko Barabara ya Tottenham Court.
Maelfu ya watu waliondolewa maeneo yanalolizunguka jengo hilo majira ya mchana baada ya ripoti kuzagaa kuwa mwanaume mmoja amebeba mitungi ya gesi na kiberiti cha kuwashia, akitishia kulipua ofisi za kampuni inayotoa mafunzo ya udereva na kisha kutishia kujilipua mwenyewe.
Inaaminika alikuwa na chuki na kampuni hiyo baada ya kufeli mara mbili mtihani wa udereva.
Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mak Chishty alisema mtuhumiwa ni mwananchi wa kawaida tu.
Alithibitisha kuwa hakuna mateka aliyebaki kwenye jengo baada ya mtuhumiwa kuondolewa kwenye jengo kufuatia wapatanishi kupelekwa eneo la tukio.
Ofisa huyo alisema mwanzoni polisi waliamini mtuhumiwa alikuwa na mabomu ama vifaa vya milipuko lakini uchunguzi eneo la tukio umebaini hakuwa na chochote kati ya hivyo.
Mtuhumiwa bado anashikiliwa na polisi.
Mwanaume huyo alikuwa akiwashikilia mateka wanne baada ya kuingia kwenye ofisi za kampuni hiyo ya mafunzo.
Alidai amefeli mara mbili mitihani ya udereva na kwamba anataka kurejeshewa fedha zake, huku akipiga kelele: "Sina sababu za kuendelea kuishi."
Maofisa, wakiwamo walinzi, wataalamu wa mabomu na wapatanishi wa polisi walikimbilia eneo la tukio muda mfupi baada ya mchana.
Waliamuru kuondolewa zaidi ya wafanyakazi 1,000 wa jengo hilo na watu waliokuwa wakifanya manunuzi madukani pamoja na watalii katika eneo hilo.
Abby Baafi mwenye miaka 27, Mkuu wa Mafunzo na Uendeshaji wa Advantage, kampuni inayotoa kozi za udereva, alisema mwanaume huyo alizilenga ofisi zake na alikuwa akiwashikilia mateka wanaume wanne. Alisema mwanaume huyo alifeli mara mbili kozi ya udereva.
Mateka hao inaaminika kuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa kampuni hiyo pamoja na maofisa mauzo watatu.
Abby aliliambia gazeti la Huffington Post: "Tulikuwa ofisini na mtu mmoja akaingia ndani. Nilimtambua kwa kuwa aliwahi kuwa mmoja wa wateja wetu.
"Alikuja namtungi mkubwa wa gesi akiwa ameubana kwapani na kutishia kulipua ofisi.
"Alisema hahofii maisha yake, hahofii chochote, anachotaka yeye ni kulipua ofisi.
"Ni dhahiri alikuwa akinitafuta mimi lakini sikuthubutu kujitambulisha jina langu na akaniruhusu kuondoka sababu nilikuwa na mimba ya miezi mitatu."
Aliongeza, mwanaume huyo akachukua simu zote za mikononi za mateka wake hao.
Mfanyakazi wa mgahawa wa KFC, Arti Pal mwenye miaka 23 alisema: "Sakata zima lilianza majira ya saa 6:30. Polisi walifika na kuwaagiza wateja wasiendelee kuagiza chakula na kwamba wanatakiwa kutoka nje.
"Dakika 15 baadaye walikuja na kutuamuru kutoka nje mapema iwezekanavyo. Vitu vyetu vyote bado viko ndani."
Haikufahamika mara moja mtuhumiwa alifikaje eneo la tukio, ikiwa ni kwa gari ama kwa miguu.
Polisi hawakueleza kiundani zaidi kama kuna mashuhuda wowote waliomwona mtuhumiwa akiingia ama kuona gari lolote linalohusiana na mtuhumiwa.
Edwards, Meneja wa Shirika la Outside alisema: "Kuna mtu alikuwa akitupa vitu dirishani - zilionekana kompyuta na samani mbalimbali kisha makaratasi.
Polisi walifika ofisi ya mapokezi na kutuambia tunatakiwa kutoka kwenye jengo mara moja.
Richard Webb mwenye miaka 26 anayefanya kazi kwenye eneo hilo anasema: "Niliona polisi wakiingia kwenye jengo hilo na mara kutoka nje na watu wanne huku mikono yao ikiwa kichwani.
"Watu walikuwa wakikimbia huku na huko mtaani na polisi walikuwa wakiwashusha watu kutoka kwenye magari yao ambayo hadi sasa yametelekezwa kwenye mtaa."

No comments: