Mtoto mmoja anaagana na mama yake kwenye stendi ya mabasi ya mikoani Ubungo kabla ya kuanza safari ya kuelekea Tanga. Mama akaanza kumpa maagizo, "Huu ubwabwa utakula ukifika Chalinze, umenielewa?" Mtoto kwa utii akajibu, "Ndio mama." Basi bwana safari ikaanza, lakini kabla ya kufika maeneo ya Kimara mtoto akamwita kondakta kwa sauti, "Kaka tukifika Chalinze naomba uniambie." Kondakta akaitikia kwa kutikisa kichwa akiashiria kukubali ombi la yule mtoto. Basi lilipokaribia Mbezi mtoto akarejea tena ombi lake, "Kaka tukifika Chalinze naomba uniambie." Kama alivyofanya mara ya kwanza kondakta akageuka na kuitikia kwa kichwa. Maeneo ya Kibaha mtoto akarudia tena, hapo kondakta akajibu kwa ukali, "Tulia bwana, tukifika ntakwambia. Acha kunipigia kelele." Baada ya basi kuanza kuondoka Kibaha, mtoto akapitiwa na usingizi. Kondakta naye akaendelea na shughuli nyingine ya kukagua tiketi. Basi lilipokuwa likikaribia Mombo mtoto akakurupuka na kumwita kondakta, ""Kaka tukifika Chalinze naomba uniambie." Oooh abiria wote pamoja na kondakta wakafadhaika na kuanza kumshinikiza dereva ageuze basi kwakuwa yule mtoto alisisitiza vya kutosha mapema. Wengi wape bwana! Kwa shingo upande basi likageuza na kuanza kurejea Chalinze. Walipofika kondakta akamtaka mtoto ashuke, lakini badala yake mtoto akatoa ubwabwa wake na kuanza kula. Hapo ndipo ikabidi abiria waingilie kati na kumhoji mtoto kwanini hataki kushuka Chalinze kama alivyokuwa akisisitiza. Baada ya kumaliza kula mtoto akajibu, "Mama aliniambia nikifika Chalinze ndio nile ubwabwa." Duh, kaaazi kweli kweli...

No comments:
Post a Comment