Monday, March 19, 2012

BINTI WA WHITNEY AKATA MZIZI WA FITINA...

Ama kweli mtoto huyu 'amepinda." Bobbi Kristina akitoka kwenye duka la AT&T huku akianika pete yake ya uchumba. Kulia akiwa ameambatana na mchumba wake, Nick Gordon.
Wenyewe wanasema hawajali watu wanavyozungumzia mahusiano ya kimapenzi yaliyozusha utata.
Bobbi Kristina na 'kaka yake' Nick Gordon kana kwamba hawasikii yasemwayo wikiendi hii wameamua kukata mzizi wa fitna na kuamua kukata mitaa wakiwa wameshikana mikono katika hali inayoonyesha kuwaziba midomo wanaowasema vibaya.
Katika mizunguko hiyo, binti huyo wa Whitney Houston mwenye miaka 19 alionyesha hadharani pete yake kubwa ya uchumba kidoleni iliyotengenezwa kwa madini ya almasi.
Kristina, ambaye bado yuko kwenye maombolezo ya kifo cha mama yake, alinaswa akitoka duka la AT&T akiwa ameambatana na Gordon, ambaye alilelewa na Whitney tangu akiwa na umri wa miaka 10.
Wapenzi hao walionekana wakiwa wenye furaha na penzi lao huku wakishikana mikono wakati wakiingia na wakitoka kwenye duka hilo kwenye mji wa Atlanta yaliko makazi yao Ijumaa iliyopita.
Bobbi alikumbushia enzi za mama yake alipokuwa kwenye ziara ya kutangaza albamu yake ya "Nothing But Love" kwa kuvaa kigauni chenye mistari, kikoti cheusi na vibuti vya manyoya. Alikuwa akivuta sigara huku mkononi akiwa ameshikilia simu yake ya iPhone.
Imedaiwa kwamba Kristina anaenda kinyume na matakwa ya bibi yake kwa kuamua kutembea na Gordon.
Kristina anasemekana kutofautiana vikali na bibi yake Cissy Houston ambaye ameyaita mahusiano yao kuwa ni kama 'uchuro'.
"Ni mambo ya kusikitisha.  Ni wazi Krissy anampenda sana Nick,  lakini ametoka kupoteza mama yake na kila kitu kwake kimekwenda kinyume. Krissy anaona hawezi kungoja na amesema wazi kifo cha ghafla cha mama yake ndio sababu ya yeye kuolewa na Nick," kimeeleza chanzo kimoja cha habari.
Nick na Krissy walionekana wakila pizza kwenye duka moja mjini Atlanta Jumanne iliyopita huku wakipigana mabusu motomoto.
Kufuatia kifo cha mama yake, Bobbi na Nick wamekuwa wakimiliki kwa pamoja jumba la Whitney mjini Atlanta lenye thamani ya  zaidi ya Shilingi bilioni 1.9 za Kitanzania (Dola milioni 1.2).
Kwa mujibu wa Jarida la Star, mama yake Nick, Maxine Gordon amesema, "Nick amekuwa akiwachunga Whitney na Kristina. Amekuwa mlinzi mzuri wa Kristina."
Kwenye mfululizo wa mawasiliano yao kwenye mtandao wa Twitter, Nick amekuwa akimchukulia Bobbi kama dada na yeye amekuwa akimuita kaka.

No comments: