Kumezuka
mapigano baina ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha Jiungeni Lolokai, kata
ya Ruvu wilayani Same na tayari wakulima wanne wamejeruhiwa vibaya na silaha za
jadi, na mmoja kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi.
Jeshi la Polisi
mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba askari wake
wamepelekwa eneo la tukio kudhibiti vurugu.
Awali, Diwani wa
Kata ya Hedaru, Gerald Mgwena jana alikieleza kikao cha Baraza la Madiwani cha
Halmashauri ya wilaya hiyo kwamba hali ni tete katika kata yake na kata ya Ruvu
wanakoishi wafugaji wa jamii ya Kimasai.
"Mheshimiwa
mwenyekiti ni siku ya pili mfululizo kuna mapigano, watu waliojeruhiwa ni Juma
Julius, Haruna Mashaka na mwingine aliyetambuliwa kwa jina mola la
Hamisi...kuna mwanamke naye amepigwa na haijulikani alipo hadi sasa, ninaomba
tamko katika hili," alisema.
Hata hivyo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo ambaye pia ni Mkuu wa
Wilaya, Herman Kapufi, alithibitisha kuwapo kwa mapigano hayo na kuongeza kuwa,
tayari ametuma askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa ajili ya
kudhibiti hali hiyo.
Aidha mkuu huyo
wa wilaya alisema lengo la kupeleka askari ni kuhakikisha wakulima wenye
vibanda vyao katika kata ya Ruvu kwa ajili ya kusimamia kilimo wasidhurike
wakati kesi ya msingi kuhusu umiliki halali wa eneo hilo itakapoamuliwa na
mahakama ya ardhi.
Akizungumzia
mgogoro huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Same, Christopher Irira
alisema baraza linakemea kuwapo kwa mapigano hayo na kutaka wenyeviti wa
vijiji, watendaji na madiwani wa kata hizo mbili kuwatuliza wananchi wao
kuepuka mapigano.
No comments:
Post a Comment