ALIYETHIBITISHWA KUFA NA KUZIKWA AIBUKA AKIWA HAI SIKU 13 BAADAYE...

KUSHOTO: Sharolyn Jackson. KULIA: Mahali ambako mwili uliodhaniwa ni wake ulipozikwa.
Mwanamke mmoja wa Philadelphia amejitokeza akiwa hai siku 13 baada ya familia yake kumzika kwenye mazishi yaliyovuta hisia kali.

Sharolyn Jackson, miaka 50, alizikwa kwenye makaburi ya Colonial Memorial Park na familia yake iliyopagawa Agosti 3, kufuatia Daktari Mkaguzi wa Philadelphia kusaini hati ya kifo na kukabidhi mwili uliosadikika kuwa ni wa mwanamke huyo.
"Nilimpigia simu mke wangu na kumpa habari za kuhuzunisha kwenye simu unayoifahamu, kwamba wamemkuta binti yangu akiwa amefariki," alisema baba yake, Dave Minnie.
Lakini Ijumaa iliyopita, Sharolyn alijitokeza akiwa hai kwenye hospitali ya watu wenye matatizo ya akili huko katikati ya Philadelphia.
Mtoto wake wa kiume, alisambaza habari hizo njema kwa baba yake, ambaye alifurahi kupita kiasi.
"Unajua unahisi karibu kumsahau, kwamba amefariki, kisha Travis anakuja hapa na habari njema kwamba yu hai," alieleza huku akicheka.
Sharolyn aliripotiwa kupotea kutoka nyumbani kwake West Philadelphia mnamo Julai 18.
Pale mwili wa mwanamke uliofanana na taarifa zake ulipopatikana Julai 20 kwenye mtaa mmoja wa West Philadelphia, maofisa walidhani utakuwa wake.
Mfanyakazi mmoja wa jamii ambaye anamfahamu Sharolyn, na Travis, wote walitambua picha za mwanamke aliyekufa kuwa ni Sharolyn aliyekuwa amepotea.
Ofisi ya Daktari wa Uchunguzi kisha ikasaini cheti cha kifo, ambacho kiliruhusu mwangalizi kuutoa mwili huo kwa ajili ya shughuli ya mazishi.
"Walimwonesha (Travis) picha zisizokuwa za rangi. Zilionekana kama yeye," alisema Minnie.
Idara ya Afya ya Philadelphia inasisitiza taratibu zote zinazotakiwa zilifuatwa na, watu wawili, akiwamo mwanafamilia, walimtambua, ilikuwa kufuata taratibu ili kukabidhi mwili huo.
Uchunguzi sasa umeanza kujua ni mwili wa nani uliozikwa kwenye kaburi hilo lililodhaniwa kuwa ni la Sharolyn.
Maofisa wanajua mwanamke huyo alikufa kifo cha kawaida na mwili wake ulikutwa kwenye mtaa Julai 20.
Wanasubiri amri ili kuweza kufukua mwili huo katika jaribio la kumtambua mwanamke huyo.
Minnie alisema kwamba wakati akisubiria kurejeshwa nyumbani kwa binti yake, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mwanamke huyo aliyezikwa kwenye makaburi hayo.

No comments: