Monday, August 4, 2014

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na michezo, Said Ali Mbarouk akizungumza na wamiliki wa mahoteli pamoja na wenye kusambaza bidhaa katika mahoteli ili kutatua matatizo yao huko kwenye Ukumbi wa Wizara ya Habari Zanzibar.

Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samwel Sitta akiongoza kikao cha Kamati ya uongozi cha Bunge hilo kilichokaa leo kupanga ratiba ya bunge hilo linaloanza kesho Agosti 5, 2014 baada ya kuahirishwa Aprili 25, 2014 kupisha Bunge la Bajeti.

Washiriki wa Shindano la Redd's Miss Kinondoni 2014 wakiwa katika picha ya pamoja kwenye mazoezi yanayofanyika kwenye Hoteli ya Piccolo jijini Dar es Salaam. Jumla ya warembo 20 wapo kwenye mazoezi kujiwinda kwa shindano hilo litakalofanyika Ijumaa ya Agosti 15, 2014 kwenye fukwe za Escape One kwa kiingilio cha Shilingi 10,000 na 30,000 kwa VIP.

AJIFUNGUA WATOTO WANNE, HOSPITALI 2 NA SIKU MBILI TOFAUTI

Mkazi wa Kijiji cha Lupili wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, Tecla Kazimili (24), amejifungua watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume kwa njia ya kawaida katika hospitali mbili tofauti na siku mbili tofauti. 
Katika hospitali ya kwanza, ambayo ni zahanati ya Kijiji cha Lupili Agosti mosi mwaka huu, Tecla alionekana ana ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja ambapo wakati wa kujifungua, alizaliwa wa kiume akiwa na kilo 1.6, lakini kwa bahati mbaya alikufa. 
Hata hivyo, wakunga walishuhudia mzazi huyo akiendelea kuwa na dalili ya kujifungua mtoto mwingine, lakini akawa amegoma kupita katika njia.  
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Marko Mwita, alisema baada ya kutokea kwa hali hiyo, alipigiwa simu kuombwa msaada.  
“Baada ya kupokea taarifa hiyo majira ya usiku, nilituma gari la wagonjwa kukimbilia kwenye zahanati hiyo iliyopo umbali wa kilometa 60 na kumleta mama huyo katika Hospitali ya Wilaya kwa huduma zaidi,” alisema.  
Alisema alipofikishwa hospitalini hapo, Tecla aliendelea kujifungua mpaka kesho yake hatimaye idadi ya watoto ikafikia wanne. 
“Hili ni tukio la kwanza katika hospitali hii ya Wilaya, mtu kujifungua watoto wanne, ni matukio yanayotokea mara chache, lakini tunamshukuru Mungu mzazi anaendelea vizuri huku watoto wake watatu, wote wa kike kila mmoja akiwa na uzito wa kilo mbili,” alisema.  
Dk Mwita alisema watoto hao wanahitaji uangalizi na msaada wa hali ya juu, kwani ni rahisi kupata maambukizi. 
Alitoa mwito kwa jamii kumsaidia mama huyo, kwani watoto hao wanahitaji msaada wa hali na mali kwa kuwa maziwa ya mama pekee hayatawatosheleza.  
Akizungumzia historia yake ya uzazi, Tecla alisema watoto hao ni uzazi wake wa nne na katika ule uliopita, watoto wote aliowazaa walifariki dunia katika umri tofauti, lakini wa utoto. 
“Kitendo cha watoto kufa baada ya kufikisha umri fulani, kilimfanya mume wangu anifukuze, nikalazimika kurejea nyumbani kwetu ambapo nilipewa ujauzito na kijana mwingine,” alisema. 
Alisema wakati anahudhuria kliniki, alielezwa kwamba alikuwa na zaidi ya mtoto mmoja baada ya kutoa taarifa kuwa anaona  tabia ya ujauzito huo ni tofauti na uzazi wake uliopita.   “Namshukuru Mungu kwa kunipatia watoto hawa na naiomba Serikali inisaidie kuwatunza ili wakue vizuri kwani peke yangu siwezi,” alisema. 
Kwa mujibu wa Tecla, aliumwa uchungu kwa siku tatu na alimaliza kujifungua Agosti 2. 

BUNGE LA KATIBA KUANZA BILA WAJUMBE WA UKAWA

Bunge Maalumu la Katiba litaendelea na vikao bila kujali uwepo au kutokuwapo kwa baadhi ya wajumbe waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),  William Lukuvi, ambaye ndiye Mratibu wa Bunge hilo, alitoa kauli hiyo jana wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa).
Alikuwa akijibu hoja iliyowasilishwa wa wachangia mada mbalimbali, kuhusu kusitishwa kwa Bunge hilo kupisha Uchaguzi Mkuu ufanyike, kisha mchakato uanze upya katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Hoja nyingine kama hiyo ambayo Lukuvi aliitolea jibu hilo, ni ya kusogezwa mbele kwa Bunge Maalumu la Katiba, ili kutoa muda kama wa wiki moja wa kushawishi zaidi wajumbe wa Ukawa, kurejea katika Bunge hilo.
“Ukawa wasipofika bungeni hatutasitisha Bunge, tuliopo tunatosha, tutajadilina na kufikia makubaliano na kuja kuwaeleza wananchi ingawa haitakuwa na afya sana,” alisema Lukuvi katika mdahalo huo ambao mada ilikuwa  ‘Nini kifanyike Bunge Maalumu la Katiba liendelee’.
Lukuvi alirejea kauli ya mtoa mada, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kuwa mjadala wa Bunge hilo litakaloanza kesho, utahusu mahitaji ya maisha ya Watanzania na sio idadi ya Serikali, wala mgawanyo wa madaraka.
Alifafanua kuwa mjadala utahusu kama watoto wa Watanzania wapewe elimu bure au la, namna ya kugawana kwa haki rasilimali za Taifa, maji, afya na masuala kama ya ardhi na uchumi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, haoni sababu wala mantiki ya wajumbe wa Ukawa, kususa kujadili mambo yanayohusu wananchi kwa kuwa suala la idadi ya Serikali, halitakuwepo.
Wasira alisema mjadala wa kipengele cha muundo wa serikali ulishafungwa na kuwa Bunge Maalumu litajadili sura 15 za Rasimu ya Katiba zilizobakia, zinazohusu maisha ya Watanzania.
“Suala la Serikali tatu au mbili tulishamaliza, tunakwenda kuzungumza mambo ya msingi yanayohusu jamii, tunakwenda kuzungumzia haki za wanawake, uchumi wa nchi unavyoendeshwa, hivyo Ukawa waje tujadili vifungu vilivyobaki," alisema Wasira.
Wasira alimshukuru Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwa mwepesi wa kubadilika na kuwa msuluhishi na msikivu wa hoja tangu mchakato wa Katiba ulipoanza.
Katika hatua nyingine, mtoa mada, Dk Kitila Mkumbo, alikiri kuwa hatua ya Rais Kikwete kukubali kuanzisha mchakato huo, ni ya mafanikio makubwa na ameingia katika historia, kwa kuwa hakuna Rais wa Tanzania aliyemtangulia, aliyewahi kuchukua hatua hiyo kubwa.
Hata hivyo, Dk Kitila alitaka Rais Kikwete ashawishiwe kusitisha mchakato huo, kutokana na hali iliyofikiwa, ili pamoja na mambo mengine, atoe nafasi ya kufanyika kwa  Uchaguzi Mkuu ujao, kisha Rais ajaye auendeleze.
Mchangiaji, Profesa Anna Tibaijuka, alisema Rais Kikwete ameibuka mshindi katika mchakato huo, kwa kutimiza matakwa ya demokrasia ya kusikiliza wachache, kwa kuwa alianzisha mchakato huo, ingawa haukuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010.
Alisema kama Rais asingechukua uamuzi huo, elimu kuhusu mchakato wa Katiba iliyopatikana mpaka sasa, isingepatikana.
Mtoa mada, Tundu Lissu, ambaye ndiye Msemaji wa Ukawa, alisisitiza nia ya wajumbe wa kundi hilo ya siku nyingi ya kususa Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema hawataingia bungeni na kuwa endapo Bunge litapitisha Katiba inayopendekezwa, wao wataendelea na mapambano ya kutaka Katiba mpya wakiwa nje ya Bunge.
“ Posho hizo hatutaki, mtakayoyajadili na kuyapitisha, kesho yake tutaendeleza mapambano ya kutaka Katiba mpya, hoja yetu ni kupata Katiba mpya na sio kalamu ya chama,” alisema.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema utafiti uliofanywa, ulibaini chanzo cha kuvurugika kwa mchakato wa Katiba, ni kutozingatia misingi ya rasimu ya Katiba iliyowasilishwa.
Sababu zingine alitaja kuwa ni hali ya kubeza na kuiponda rasimu na mazingira ya ufunguzi wa Bunge na mjadala kugubikwa na lugha za matusi, kebehi, kubaguana na lugha za kukashifiana.
Akizungumzia ufumbuzi wa tatizo hilo, Profesa Mpangala alitaka mjadala uzingatie maoni ya wananchi, wabunge kuwa na mtazamo wa kitaifa na kwa manufaa ya vyama vyao.
Aliwataka Ukawa kurejea bungeni. Alisema endapo Ukawa wataendelea na msimamo wa kutorejea bungeni, basi wanasheria waangalie mwanya wa kanuni wa kusitisha vikao vya Bunge hadi baada ya uchaguzi mkuu 2015.
Wakati limesitishwa, Profesa Mpangala alitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano, lirekebishe sheria kadhaa, zitakazotumika katika uchaguzi ujao na Bunge la Katiba, liundwe upya kwa kurekebisha kasoro zilizopo, ikiwamo kupunguza idadi ya wanasiasa, iwe theluthi moja ya wajumbe.
Dk Mkumbo katika mada yake, alisema mchakato wa Katiba mpya ni kama umeshindwa, kutokana na pande mbili za Ukawa na CCM kushindwa kufikia maridhiano na kila upande kusimamia msimamo wake.
Alisema mchakato huo, pia umeshindwa kuendelea, kutokana na wajumbe wa Bunge Maalumu, kutokuwa na  weledi na umakini wa kuandika Katiba mpya, hasa kutokana na mwenendo ulionekana katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo.
“Hawana weledi wa kuandika Katiba na wamekosa weledi ambao uko katika kushindwa kukabiliana na hoja kinzani, kwani kila mtu anataka kusikia hoja yake na kuisikia sauti yake,” alisema.
Alitaka mchakato huo, uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu ili Bunge Maalumu liundwe upya, kwa kuwa na theluthi moja ya wajumbe ambao ni wanasiasa.
Katika Bunge hilo jipya, Dk Mkumbo pia alipendekeza kuwa wajumbe wake watakiwe wasigombee uchaguzi ujao, kwani baadhi ya wajumbe wa sasa, wamekuwa wakitumia mjadala huo kujipatia umaarufu.
Pia, alitaka Wazanzibari waulizwe kama wanataka Muungano au la, kwani nchi inapokubali Muungano ni lazima wajue kuwa kuna haki, ambazo inapoteza kwa kuwapo katika Muungano.
Alisema haiwezekani nchi ikawa huru ndani ya Muungano, au ikawa na Mkataba katika Muungano na kuendelea kuwa huru.
Wasira katika mada aliyotoa, alisema: “Tatizo la wenzetu (Ukawa) ni serikali tatu au mbili, lakini kwa sababu Katiba ni zaidi ya tatu na mbili, kuna mambo ya msingi tunarudi Dodoma kuyashughulikia na kuyazugumza.
“ Suala la serikali tatu au mbili tulishamaliza, tunakwenda kuzungumza mambo ya msingi yanayohusu jamii, tunakwenda kuzungumzia haki za wanawake, uchumi wa nchi unavyoendeshwa, hivyo Ukawa waje tujadili vifungu vilivyobaki."
Akifunga kongamano hilo,  Lukuvi alisema mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Ukawa, ni Lissu na kumuomba alegeze msimamo ili warejee bungeni.
 “Ninakuomba Lissu maana wewe ni mzizi wa Ukawa… unaweza kujifungia saa sita mpaka 24 bila kula kwa ajili ya kujenga hoja, sasa nakuomba kawashawishi warejee bungeni,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, alisema sababu ya kukwama kwa Bunge la Maalum la Katiba, ni kutawaliwa na dhambi ya ubinafsi kwa vyama, kutumia wananchi kama kichaka cha kupitisha mambo binafsi.
“Tumefanya dhambi ya ubinafsi na hili limefanywa na vyama vyote na tulianza kwa kuwa na vikao vya kivyama ambako tulikwenda kuweka misimamo ya vyama, tumeshinda hata kutumia viongozi wetu kutushauri pale tulipokwama na hatuwezi kusubiri tukodi watu kutoka nje ili watupatanishe.
“ Pia kuna dhambi ya kuwageuza wananchi kuwa kichaka cha kupitisha mambo yao, hivi kweli wananchi walitaka tulipwe Sh 300,000?.
“ Ukawa warudi na tufike mahali tujifungie na kukubaliana, kama ni serikali tatu au tukubaliane kurudisha kodi ya mbwa ili tupate fedha za kuendesha serikali tatu, lakini tupitishe mambo kwa umoja na tusiwapeleke Watanzania kama nyumbu,” alisema Mwigulu.
Akijibu swali la kwanini CCM haitaki kukubaliana na hoja ya kuwa na serikali tatu, Mwigulu alisema chama chake hakijaona sababu za msingi za kuvunja muundo ulioafikiwa na waasisi wa Taifa.
“ Ukawa, hii ni aibu Bunge kuendelea bila kuwapo au livunjike kwa sababu yenu, tumekomboa nchi nyingi na tumekuwa wasuluhishi, leo hii tukashindwa kwenye jambo hili,” alisema.
***************************

DEREVA WA BASI LILILOUA ABIRIA AJISALIMISHA POLISI

Dereva wa basi lililotumbukia katika korongo  na  kuua watu sita na  kujeruhi vibaya wengine 18, waliokuwa wakisafiri kutoka Mbinga mjini kwenda Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, amejisalimisha polisi akiwa katika hali mbaya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amemtaja dereva huyo ni Paul Nchimbi (31), mkazi wa kijiji cha Liparamba wilayani Nyasa.
Kamanda alisema mwili wa dereva huyo, umejaa majeraha na kwa kuwa amepatikana kwa hiari yake na kuripoti katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga, alisema dereva huyo amepelekwa kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo, akiwa chini ya ulinzi mkali.
 Alisema  baada ya matibabu na kupona, polisi itamhoji kufahamu chanzo cha ajali hiyo, iliyosababisha vifo na majeruhi.
Basi alilokuwa akiendesha ni lenye namba za usajili T 759 BVR, aina ya Nissan Civillian, mali ya Dismas Ndomba, mkazi wa kijiji cha Kingirikiti wilayani wilayani humo. Basi hilo lilipata ajali katika kijiji cha Burma  saa 10:30 jioni Agosti mosi mwaka huu.   
 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbinga,  Elisha Robert, alimwambia mwandishi,  majeruhi wote ambao wamelazwa katika hospitali hiyo wanaendelea vizuri, isipokuwa  wanne waliosafirishwa kwenda Hospitali ya Peramiho iliyopo Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kutokana na kuwa katika hali mbaya.
“Vile vile tumesafirisha wagonjwa wengine wawili wameenda kupatiwa matibabu Hospitali ya Misheni Litembo iliyopo huku Mbinga, hali zao sio nzuri wamevunjika nyonga, tukaona ni vyema wapelekwe kwanza huko kwa uchunguzi zaidi wa afya zao,” alisema Dk Elisha.
Awali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,  Mihayo alifafanua kwamba  ajali hiyo ilisababishwa na mwendo kasi wa gari hilo.
Inadaiwa dereva wa gari hilo, alishindwa kulimudu kwenye kona kali na hatimaye lilitumbukia katika shimo kubwa  na kusababisha mauaji na majeruhi hao.
Watu sita waliokufa ni Esther Kumburu ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Kilimani wilayani Mbinga. Mwingine ni Efigenia Kayombe, ambaye ni mwalimu wa shule ya Linda iliyopo Mbambabay wilayani Nyasa.
 Wengine ni Ernest Ndunguru, mkazi wa kijiji cha Mikalanga wilayani Mbinga, Anna Chitete kijiji cha Kilosa wilayani Nyasa na  mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mbunda, mkazi wa kitongoji cha Lusonga Mbinga mjini na maiti ya mwanaume ambayo haikutambulika.

WATOTO 100 KUFANYIWA UPASUAJI WA MOYO INDIA

Watoto 100  wenye maradhi ya moyo, wanatarajiwa kwenda India kwa matibabu ya moyo, ukiwemo upasuaji baada ya kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Regency  jijini Dar es Salaam.
Kambi ya uchunguzi itafanyika mwezi huu. Imeandaliwa kwa pamoja na Hospitali ya Regency Klabu ya  Lions ya Dar es Salaam (HOST) and Fortis Escorts Heart Institute ya India.
Taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Regency, ilisema kambi hiyo itakayofanyika katika hospitali hiyo kuanzia Agosti  11 na 12 mwezi huu, itaendeshwa na mtaalamu bingwa wa maradhi ya moyo kutoka Fortis Escorts Heart Institute ya India, Dk Ashutosh Marwah
“Uchunguzi utakaofanywa na mtaalamu huyo, utaangalia watoto wote wenye matatizo ya moyo, yakiwemo matundu na valvu na uchunguzi utafanyika katika hospitali ya Regency Upanga hivyo ni fursa kwa wenye matatizo ya moyo waje kuchunguzwa na mtaalamu kutoka India,” ilisema taarifa iliyotolewa na Mratibu wa maradhi ya moyo katika Klabu ya Lions, Dk Rajni Kanabar.
Dk Kanabar alisema uchunguzi wa moyo, pia utafanyika Zanzibar kuanzia Agosti 13 na 14. Aliomba Watanzania wote kuchangamkia fursa hiyo ili wajue matatizo yanayowakabili, watakapokutana na wataalamu.
Alisema wagonjwa 100 watachaguliwa kwenye kambi hiyo kwa ajili ya kwenda kufanyiwa matibabu na upasuaji nchini India kwa punguzo kubwa la gharama, wakati wengine watafanyiwa bure.
Alisema watoto wote watakaochaguliwa kwenda kwa matibabu nchini India, watasafiri kwa pamoja kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kati ya  Novemba na Desemba mwaka huu, kwenda kutibiwa katika hospitali kubwa na za kisasa nchini India.
”Katika kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, watoto 50 watachaguliwa kutoka Tanzania Bara na watoto 50 kutoka Tanzania Visiwani wakiwa na wasaidizi wao watasafiri na wanachama wachache wa Lions na wauguzi kutoka Regency Medical Center kwenye ndege ya matumaini,” alisema Dk Kanabar.
Kwa upande wake, Shiraz Rashid ambaye anasimamia michango ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi, alisema mwezi Oktoba watafanya harambee kubwa kwa ajili ya kupata fedha za kuwapeleka watoto 100 India kwa ajili ya upasuaji.

HATARI!! HOMA YA INI INAUA ZAIDI KULIKO UKIMWI

Idara ya afya mkoani hapa imehadharisha jamii dhidi ya ugonjwa wa ini, ikisema ni mbaya zaidi ya virusi vya Ukimwi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Emmanuel Mtika alitoa hadhari hiyo kwenye kikao cha 27  cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Alikuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya upatikanaji wa  damu salama  katika  vituo,  vinavyotoa  huduma ya afya mkoani humo.
Alisema virusi vya  homa ya ini viligunduliwa kwenye damu, iliyokusanywa  kutoka kwa watu wanaochangia damu kwa  hiari yao, kuokoa maisha  ya wahitaji  wakiwemo wajawazito na watoto.
“Idara ya Afya imekumbana na  changamoto  kubwa  ya magonjwa  yanayoambukizwa  kwa njia  ya  damu  hususani homa ya ini,  kama iliyogunduliwa  kutoka  kwenye damu iliyokusanywa  kutoka kwa wateja,” alisema.
Alisema magonjwa  yanayoambukizwa kwa njia ya damu yaliyogundulika kwenye damu iliyokusanywa ni  homa ya ini aina  ya HBV.
Kwa mujibu wake,   asilimia 10.3  ya  watu 206   waliopimwa walikutwa na maambukizi  ya aina hiyo HBV, wakati aina  nyingine  ya homa ya ini ya HCV ambapo  ni asilimia  1.5 ya watu 30 walikutwa  na maambukizi ya ugonjwa huo.
Kwa upande  wa maambukizi  ya virusi vya Ukimwi,  ni asilimia 1.2 ya watu 28 waliopimwa na kukutwa na maambukizi hayo.
Akitoa mfano wa  upatikanaji hafifu  wa damu salama katika vituo vinavyotoa  huduma ya afya  mkoani humo,  alisema mahitaji ni chupa za damu  4,350 kwa mwaka. Lakini,  ni chupa 2,003 tu zilizokusanywa mwaka jana,  ambazo ni sawa na asilimia 53 ya mahitaji halisi.
“Hata  hivyo  ni  chupa za damu zipatazo 1,665 tu  zilizosambazwa  katika  vituo  vitano vinavyotoa huduma  ya afya  mkoani kwetu…hiki ni kiwango kidogo sana  ikilinganishwa na mahitaji  halisi,” alisema.

ARUMERU WATAKA SERIKALI IWALIPE SHILINGI BILIONI 3.7

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, limemwagiza Mbunge wa Arumeru Magharibi, kufuatilia malipo yao ya Sh bilioni 3.7 kutoka serikali kuu baada ya serikali kuchukua viwanja katika halmashauri hiyo.
Limemtaka Mbunge huyo, Goodluck ole Medeye kuhakikisha anafuatilia fedha hizo kwa ukaribu zaidi na kuwa na majibu ya uhakika katika kikao kijacho cha baraza la madiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Saimoni Saning’o  alisema halmashauri ina changamoto nyingi zinazohitaji fedha.
Alisema baraza liliamua kuuza viwanja hivyo kwa watu binafsi ili waweze kutumia fedha hizo katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kutokana na ucheleweshwaji huo, unaofanywa na serikali kuu wa malipo hayo ya Sh  bilioni 3.7,  inakuwa vigumu halmashauri kujiendesha kikamilifu.
"Halmashauri ina matatizo mengi kama vile barabara mbovu, maji, zahanati hazina dawa na baadhi ya shule madawati ni shida sasa nakuagiza Mbunge fuatilia hili, kwani wewe ndio uko karibu na wahusika  na kikao kijacho uje na hundi,’’ alisema.
Mbunge wa Jimbo hilo alikubali kubeba jukumu hilo. Alisema hata yeye suala hilo halimpi usingizi kwa kuwa fedha hizo zikipatikana, zitatatua changamoto nyingi za maendeleo zilizoko katika jimbo lake, ikiwa ni pamoja na ahadi alizoahidi katika kampeni ya mwaka 2010.
"Ninakwenda katika Bunge la Katiba na wahusika wote watakuwa huko na nitakuja na majibu mazuri, ama nitakuja na hundi ya kiasi kilichobaki," alisema.
Hata hivyo, aliwataka madiwani kuamini serikali yao juu ya deni hilo. Alisema Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia aliahidi  kulipa deni hilo haraka, lakini majukumu yamekuwa yakiingiliana. Inadaiwa kati ya Sh bilioni 5.7, serikali imeshalipa Sh bilioni mbili kwa halmashauri hiyo.

WANAFUNZI WATUMIA VISODA NA MABUA DARASANI

Upungufu wa vitabu, vifaa vya kufundishia na kuhesabia kwa watoto wa darasa la awali kwa baadhi ya shule za msingi katika Halmashauri ya Iramba, mkoani Singida unasababisha wanafunzi kutumia mabua, visoda na vijiti kwa ajili ya kuhesabia.
Aidha, walimu wakuu wa shule mbalimbali za msingi wilayani hapa wanaiomba serikali kutoa ruzuku kwa watoto wa darasa la awali kwa kuwa huduma zao haziwezi kutenganishwa na  madarasa mengine.
Akizungumza na gazeti hili, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kizega, Elisante Gyuzi alisema sehemu kubwa, shule yake imekuwa ikipata vifaa mbalimbali kutoka kwa wahisani. 
Alisema kulingana na sera ya elimu ni lazima madarasa ya awali yawe maalumu, yawe na vyoo na madarasa ya kujitegemea kwa ajili ya watoto hao wadogo.  
“Kwa mfano, hapa shuleni kwangu lipo darasa ambalo lilikarabatiwa na wahisani na pia kutupatia vifaa mbalimbali ambapo imepunguza ile hali ya watoto kubeba vijiti ama mabua kwa ajili ya kuhesabia,” alisema. 
Shule ya msingi Kizega ni maalumu kutokana na kuwa na wanafunzi wenye mahitaji muhimu.
“Nawashukuru wakazi wa eneo hili ambao kwa nguvu moja wameelimishwa na kufahamu umuhimu wa elimu ambapo katika kuonesha jitihada zao wanafyatua tofali ili kujenga darasa la watoto wa awali,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tutu, Rebecca Pyuza alisema elimu ya awali shuleni hapo ni changamoto kubwa kwani hata mwalimu anayefundisha watoto hao ni wa kujitolea ambaye awali alikuwa mwalimu lakini baadaye alipumzishwa kabla ya shule kuamua kumtumia. 
Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kisiriri, Gerson Mkoma alisema shuleni hapo watoto wa awali hutumia visoda, mabua na vijiti kwa ajili ya kuhesabia huku michoro  mingine wakisaidiwa na walimu wao.
Alisema shule hiyo haijawahi kuwa na vifaa maalumu kwa ajili ya mafunzo shuleni hapo na kuiomba serikali kuzikumbuka hasa shule ambazo ziko pembezoni ama vijijini zaidi.

KIKWETE, MARAIS 46 AFRIKA WAKUTANA NA OBAMA

Rais Jakaya Kikwete yuko Marekani kwa ziara ya siku tisa nchini humo ambako miongoni mwa mambo mengine, atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Kihistoria wa Viongozi wa Bara la Afrika na Marekani ulioitishwa na Rais Barack Obama. 
Mkutano huo wa siku mbili unafanyika kuanzia leo ukianza na mkutano wa biashara kati ya Afrika na Marekani.  Unafuatiwa na mkutano wenyewe wa Marekani na Afrika utakaofanyika kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.  
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles mjini Washington, Rais Kikwete alipokewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. 
Kwenye ziara hiyo, Rais Kikwete ameongozana na mkewe, Mama Salma Kikwete ambaye naye atakuwa na programu tofauti wakati wa ziara hiyo, kama watakavyokuwa wake wa viongozi wengine wa Afrika wanaohudhuria mkutano huo. 
Mkutano huo wa kwanza wa aina yake kati ya kiongozi wa Marekani na viongozi wa Afrika umepangwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi 47 ambazo zote zimealikwa na Rais Obama kushiriki mkutano huo. 
Mbali na shughuli zake nyingi za mjini Washington, Rais Kikwete atasafiri kwenda Dallas, Jimbo la Texas, ambako atakutana na Rais wa 43 wa Marekani, George W. Bush, kabla ya kuendelea na safari katika mji mwingine mkubwa wa jimbo hilo wa Houston. 
Mjini Houston, Rais Kikwete atafanya mkutano wa kimkakati wa kibiashara na wafanyabiashara maarufu mbalimbali hasa wa sekta ya gesi na mafuta kabla ya kumaliza ziara yake. 
Miongoni mwa shughuli zake, Mama Salma Kikwete atahudhuria mkutano wa wake wa marais wa Afrika na mke wa Rais wa Marekani, Michelle Obama utakaofanyika kwenye Kituo cha John F Kennedy.
Mkutano huo utahudhuriwa pia na mke wa Rais George W. Bush, Mama Laura Bush.

SUMAYE ATAJA SIFA ZA VIONGOZI WAZURI

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema Watanzania wanatamani kupata viongozi wazuri na wanamwomba Mungu awasikilize na awasaidie katika hilo, huku akitaja baadhi ya sifa ambazo wangependa viongozi wao wawe nazo. 
Aidha, amesema Tanzania hivi sasa inapita katika wakati wenye changamoto nyingi  na wakati huu kuna mambo makubwa na mazito, ambayo yanahitaji kuombewa kwa Mungu, ambayo ni amani na utulivu na kupata viongozi wazuri.
Sumaye alisema hayo jana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa albamu ya Kamata Pindo la Yesu ya mwanamuziki nyota wa injili nchini, Rose Muhando.
Alitaja sifa ambazo  Watanzania wanatamani viongozi wao wawe nazo kuwa ni kutambua na kuthamini umoja, kiongozi bora anayejiamini, uadilifu, kupiga vita rushwa na maovu mengine kama ufisadi, matumizi ya dawa za kulevya, mauaji, ujambazi na mengineyo, kupiga vita umasikini
Sifa nyingine ni kuboresha huduma za jamii, nidhamu na utendaji kazi, kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma, kukuza uchumi imara na mzalendo.
“Tunahitaji kuwa na amani na utulivu wakati wa uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la wapiga kura, wakati wa kampeni zetu, wakati wa upigaji kura na hatimaye wakati wa kutangaza matokeo. Maeneo haya manne ni muhinmu sana yakatekelezwa kwa umakini na kwa haki na uwazi kadri inavyowezekana,” alisema Sumaye aliyedumu katika nafasi yake kwa miaka 10.
Aidha, alisema wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia uandikishaji, wakati wa kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo na kukubali matokeo, ni lazima kila mhusika ahakikishe anatimiza wajibu wake ili kutoleta vurugu na kuharibu amani ya nchi.
Kuhusu kupata viongozi wazuri,  Sumaye alisema: “Hivi sasa taifa letu linapita kwenye mchakato wa Katiba mpya, ni vema kuhakikisha kuwa mchakato huu hautupeleki kwenye kudhoofisha Muungano wetu na mshikamano wetu kama taifa.
“Watanzania tumekaa kwenye Muungano wetu kwa miaka 50 sasa kwa amani na mshikamano na hatutarajii kiongozi atakayetuingiza katika majaribio. Tuna mafunzo ya kutosha kwa baadhi ya nchi ambazo zimejigawanya jinsi ambavyo zimepoteza amani waliyokuwa nayo.”
Aliongeza: “Hizi ni baadhi tu ya sifa ambazo Watanzania wa wangependa kiongozi wao awe nazo. Katika sala zao wanapomwomba Mungu kila moja kwa namna yake wanatamani Mungu awapatie kiongozi wa sifa hizo na zingine nzuri ambazo mimi sikuzitaja. Wakina Rose Muhando na wenzake ndiyo sala zao na sisi ndiyo sala zetu.”
Sumaye alisema pamoja na kumwomba Mungu atuvushe salama kama taifa, kama vyama vya siasa na kama mtu mmoja mmoja, lazima tutekeleze wajibu wetu.
“Hatuwezi kumwomba Mungu atuvushe salama huku sisi wenyewe kwa makusudi tunakoroga misingi ya amani na utulivu wetu,” alisema.

PINDA AAGIZA JIJI LA MBEYA KUONGEZA MAPATO

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya, kuongeza mapato yake ya ndani kwa kuweka mifumo ya kisasa ya ukusanyaji mapato.
Alitoa agizo hilo juzi wakati akizindua stendi ya kisasa ya mabasi katika eneo la Nanenane, nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
“Nikuombe Meya Kapunga, wewe na watu wako ongezeni mapato ya ndani ya Jiji la Mbeya. Wekeni mifumo ya kisasa ya makusanyo inayotumia teknolojia ya habari na mawasiliano, acheni kutumia risiti za kuandika wa mikono,” alisema.
Akizungumzia mradi wa stendi mpya ya mabasi, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa stendi hiyo ni miongoni mwa kazi zilizo kwenye mradi mkubwa, unaohusisha uboreshaji wa huduma na miundombinu kwenye miji na majiji saba hapa nchini.
Alisema mradi huo uliibuliwa na Serikali mwaka 2006 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Miji na majiji mengine yanayotekeleza mradi kama huo ni Mwanza, Arusha, Tanga, Kigoma, Mtwara na Dodoma.
 “Utekelezaji wa miradi katika miji na majiji haya saba, umetuwezesha kupata ufadhili katika awamu ya pili ya mradi huu ambayo itajumuisha miji 17. Tusingekubaliwa kuingia awamu ya pili kama ninyi madiwani msingesimamia vizuri miradi hii,” alisema.
 Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza alisema ujenzi wa stendi hiyo yenye ukubwa wa meta za mraba 30,000 utasaidia kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara kuu ya Tanzam, ambako mabasi ya mikoani yalikuwa yakisimama na kupakia ama kushusha abiria.
 Alisema mradi huo wa stendi ya Nanenane, uliogharimu Sh bilioni 2.9 ni sehemu tu ya mradi mzima ambao thamani yake ni Sh bilioni 31.4, ambazo zimetumika kujenga barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 23.1, daraja moja na dampo la kisasa la kutupia taka (sanitary land fill) katika kata ya Nsalaga.
 Hata hivyo, mradi huo uko chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi Desemba 4, 2014 utakapokabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Jiji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha unatengeneza kwanza miundombinu ya maji na vyoo katika eneo jipya lililopo jirani na stendi mpya ya Nanenane ambalo limetengwa mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama ‘wamachinga’.

NBC YATOA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 100 KWA STAR OILS

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetia saini makubaliano ya mkopo wa Sh bilioni 100 na kampuni ya kusambaza mafuta ya jijini Dar es Salaam ya Star Oils katika mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya mafuta nchini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Mizinga Melu alisema  hiyo inahitimisha safari ya majadiliano na kampuni mama ya Star Oils, Mohammed Entrepries Tanzania Limited (METL) ya mkopo wa Sh bilioni 100.
"Star Oils ni kampuni dada ya METL ni moja ya kampuni zinazokwenda kasi katika biashara ya ushindani katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara na rekodi yao ya mauzo na biashara ni ya kuridhisha," alisema.
Alisema METL ni moja ya kampuni zenye rekodi nzuri katika biashara ya viwanda, nguo, vinywaji, bima na mafuta na wanastahili kuwezeshwa kwa kupata mikopo mikubwa na ya muda mrefu kupitia taasisi za kifedha nchini na nje ya nchi.
"Sisi Benki ya NBC tunayo furaha kubwa kwa kupata nafasi ya kufanya biashara na moja ya kampuni zinazokuja kwa kasi katika bara la Afrika na vile vile NBC ni benki ambayo ipo tayari kusaidia wateja wake,” aliongeza.
Melu alisisitiza baada ya NBC kujiridhisha na shughuli za kibiashara na mzunguko wa fedha wa METL, wameamua kutoa mkopo huo wapanue biashara yao katika masoko ya kimataifa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa METL, Mohammed Dewji  alisema hatua ambayo kampuni hiyo imefikia ni kubwa kwa kuonesha dhamira ya kuwekeza na kufanya biashara ya mafuta Afrika Mashariki na kusini mwa Jangwa la Sahara.
"Sisi tuna mipango ya kuanza kusambaza mafuta na bidhaa za petroli katika nchini za Kusini mwa Afrika kama sehemu ya jitihada za kampuni za kupanua biashara zake katika soko la Afrika," alisema.
Star Oils kwa sasa inatekeleza awamu ya pili ya mradi mkubwa wa kuhifadhi mafuta ya petroli na baadaye kujenga usambazaji wa mafuta nchi nzima kwa njia ya mlolongo wa vituo vya karibu 200 ya petroli nchini.

JICHO LA TATU


YASEMAVYO MAGAZETI LA YA LEO JUMATATU - AGOSTI 04

Saturday, August 2, 2014

UKAWA PASUA KICHWA, KIKAO CHAFANYIKA MASAA 10 BILA MAFANIKIO

Licha ya agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwataka viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao, wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya wananchi (UKAWA), kuacha kususa na kurejea katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ili kuendelea na mchakato huo, kufikia jana hakukuwa na mwelekeo wa kulegeza msimamo wao.
Hali hiyo inajitokeza, licha ya jana kuwapo kwa kikao kirefu cha maridhiano baina ya pande zinazovutana, Ukawa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mchakato huo, unaotarajiwa kuendelea tena kwa siku 60 kuanzia Jumanne ijayo mjini Dodoma.
Katika nasaha zake kwa Ukawa juzi, wakati akihutubia taifa kupitia utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na wananchi kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete aliahidi kuwa tayari kusaidia kwa lolote pale atakapohitaji. Alisisitiza kuwa lengo lake ni kuona Watanzania wanapata Katiba bora, wanayoihitaji.
Hata hivyo, katika kikao cha maridhiano jana, kilichokuwa cha nne na kilichotarajiwa kuwa cha mwisho ili kupata mwafaka kamili, wajumbe waliokutana kwa zaidi ya saa 10 katika hoteli ya Sea Cliff, Masaki jijini Dar es Salaam chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, msimamo wa Ukawa ulibaki kutorejea bungeni.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho, kilichokuwa na ajenda moja tu ya kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni, kuendelea na mchakato wa Katiba mpya, zinasema hatua hiyo imemkatisha tamaa na kumvunja moyo Jaji Mutungi, huku wajumbe wa CCM wakiwaangushia lawama wenzao kuwa hawaoneshi uzalendo na nia ya kuwapa Watanzania Katiba mpya.
Mmoja wa maofisa kutoka Ofisi Msajili aliyekuwa eneo hilo la hoteli hiyo, lakini alisisitiza kutotajwa jina, alielezea kushangazwa na uamuzi wa Ukawa, akisema kila mara wanapoitwa kwa ajili ya kikao cha kumaliza mvutano baina ya pande mbili, wamekuwa na madai mapya, hali inayochangia ugumu wa kufikia mwafaka.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)  ya CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akizungumza jana kwa njia ya simu, alisema anasikitishwa na kile alichokiita unafiki wa Ukawa katika kufikia mwafaka chini ya upatanishi wa msajili wa vyama nchini.
“Ni aina ya unafiki na nadhani wana kitu cha ziada zaidi ya Katiba, haiwezekani kila siku zitafutwe sababu za kukwepesha mwafaka.  Inaonesha kuwa watu hawana nia njema na dhamira ya Rais Jakaya Kikwete na Watanzania ya kuwa na Katiba mpya…mambo ya ajabu kabisa,” alisema Nnauye.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya ofisi ya Msajili, kikao cha jana kilitarajiwa kuwa kikao cha mwisho cha maridhiano katika juhudi hizo za kukwamua mchakato huo ili kuwapa wajumbe wa Ukawa, ambao pia ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, nafasi ya kujiandaa na safari ya kuelekea Dodoma kwenye vikao vya Bunge hilo vinavyotarajiwa kuanza rasmi Agosti 5, mwaka huu.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni jana, kulikuwa na taarifa za ndani ya kikao hicho, zinazoeleza wazi kwamba hakukuwa na uwezekano wowote wa pande mbili hizo kufikia maridhiano baada ya Ukawa kuwasilisha hoja zao tisa mpya.
Waliwasilisha hoja hizo mpya, badala ya hoja mbili ambazo ziliridhiwa na pande mbili hizo katika kikao kilichopita, ambacho kilikuwa ni cha tatu, kwamba zingejadiliwa katika kikao jana na kufikia hitimisho la majadiliano hayo.
Kwa mujibu wa habari hizo, hoja tisa hizo zilizowasilishwa na Ukawa katika kikao hicho cha jana, zilishajadiliwa na kufikiwa muafaka na pande mbili hizo katika kikao kilichopita, zikawekwa kiporo hoja mbili, ambazo ndizo zilipaswa kujadiliwa jana kabla ya kufikia hitimisho.
“Hawa Ukawa wanamvuruga tu Msajili kwa sababu hawaeleweki ni kitu gani hasa wanachokitaka…kwa kweli wamem-put off (kuvunja moyo, kuvunja nguvu) Msajili wa vyama vya siasa, uwezekano wa kufikia maafikiano na maridhiano ili tuweze kurejea bungeni kuendelea na mchakato wa kutafuta Katiba mpya ni mdogo sana,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kikao kwa sharti la kutotajwa.
Nje ya kikao hicho, baadhi ya maofisa wa Ofisi ya Msajili, walionesha kushangazwa na hali hiyo ya kutofikia muafaka, wakisema kwa vikao vinne tu hivyo, Ofisi ya Msajili imeingia gharama kubwa kuliko ilivyofikiriwa awali, wakati Jaji Mutungi anapanga mipango ya kuzikutanisha pande mbili hizo.
Kwa mujibu wa maofisa hao, kikao cha kwanza cha pande mbili hizo za Ukawa na CCM, kilichofanyika chini ya upatanishi wa Jaji Mutungi, kiliwakutanisha wenyeviti na makatibu wakuu wa vyama vinne vya siasa vya CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na hivyo kikao hicho kuwa na wajumbe tisa akiwemo mpatanishi, Msajili wa vyama.
Katika kikao hicho cha kwanza, habari zinasema Ukawa waliomba kupanua wigo kwa kuongeza idadi ya wajumbe zaidi ili kila upande uwe na wawakilishi 20, kwa maana ya Ukawa wawe na wajumbe 20 na CCM wawe na wajumbe 20.
Habari zinasema, busara ya Msajili wa vyama na wajumbe wengine wa kikao hicho, wazo hilo la Ukawa lilikubalika na hivyo kikao cha pili, cha tatu na hicho cha jana vikawa vinahudhuriwa na wajumbe 41, kwa maana ya Ukawa 20, CCM 20 na Msajili wa vyama.
Idadi hiyo ya wajumbe na mahali vinavyofanyikia vikao hivyo, hoteli ya Sea Cliff, kuanzia ukumbi na huduma nyingine za hoteli, ikiwemo chakula na vinywaji ndivyo vinavyodaiwa kuongeza gharama ambayo awali Ofisi ya Msajili haikuwa imezifikiria.
Kutokana na kuwepo kwa dalili za kukosekana kwa mwafaka baina ya pande hizo, jana gazeti hili lilifanya juhudi za kuwasiliana kwa nyakati tofauti na viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR), lakini kwa muda mrefu siku zao za viganjani ziliita bila kupokelewa.
Hata hivyo, juzi viongozi wa Ukawa walikutana katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la kutorejea kwenye Bunge Maalum la Katiba kuendelea na vikao, wakisema ni muujiza tu ndio unaoweza kuwafanya warejee.
Wajumbe wa Ukawa walisusia vikao vya Bunge Maalumu katika siku za mwisho za awamu ya kwanza ya bunge hilo lililoketi kwa siku 70 kuanzia Februari 11 mwaka huu, kwa kile alichodaiwa wanaburuzwa na wenzao wa CCM, ambao kimsingi ndio wengi, kutokana na uwakilishi wao katika Bunge la Muungano, ambalo wajumbe wake wameunganisha na wengine 201 walioteuliwa na Rais hivyo kuunda Bunge Maalumu la Katiba.

MAMA WA MTOTO WA MIEZI 10 NAYE KORTINI KWA MABOMU ARUSHA

Watuhumiwa 19 wa ulipuaji mabomu mkoani Arusha, jana walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Walisomewa mashtaka yanayowakabili chini ya ulinzi mkali ndani na nje ya viwanja vya mahakama.
Wakati hayo yakitokea mjini Arusha, jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, Shekhe Farid Hadi Ahmed (45) na mwenzake, Jamal Swaleh wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
Mjini Arusha, ulinzi uliimarishwa kwa kila aliyeonekana maeneo hayo kuanzia mapema asubuhi.
Walioingia mahakamani walikaguliwa kwa vifaa maalumu vya ukaguzi pamoja na  askari polisi wenye silaha na mbwa.
Ilipotimu saa 5:00 asubuhi, pikipiki ya polisi iliyokuwa ikipiga king’ora, iliongoza msafara wa magari matatu, yaliyobeba washitakiwa.
Baada ya saa mbili baadaye, watuhumiwa hao akiwemo Sumaiya Ally (19), mama mwenye mtoto mwenye umri wa miezi 10, walishushwa ndani ya magari na kuingizwa chumba cha mahabusu, kusubiri kusomewa kesi yao.
Waliingizwa chumba cha mahakama saa 8.00 mchana na kusomewa mashitaka yanayowakabili mbele ya mawakili wa Serikali, Augustino Kombe, Felix Kwetukia na Marceline Mwamunyange.
Wakili Kwetukia alisoma shitaka la kwanza  kwa kudai linawahusu watuhumiwa Yahaya Mpemba (37), Yusuph Huta (30), Kassim Ramadhan (34), Jafari Lema (38), Abdul Humud `Wagoba’ (30), Said Temba (42), Idd Yusuph (23), Hassan Mfinanga (57), Anwar Hayel (29), Nabian Mswahili na Yusuph Ramadhan (23).
Alidai washitakiwa hao kwa pamoja, kati ya Januari na Februari mwaka huu Jijini Arusha, walikula njama ya kufanya vitendo vya ugaidi nyumbani kwa Shekhe Sudi Ally Sudi.
Pia, alidai shitaka la pili linahusu watuhumiwa wote hao,  kwamba Julai 3 mwaka huu, eneo la Majengo Chini walifanya kitendo cha kigaidi na kurusha bomu nyumbani kwa Shekhe Sudi na kumsababishia majeraha.
Alidai shitaka la tatu, linawahusu washtakiwa hao  la kufanya vitendo vya kigaidi kwa kurusha bomu la kutupwa kwa mkono na kusababisha kifo.
Shitaka lingine linawakabili washtakiwa Yahaya Twahir (37), Lema  na Humud ambao ilidaiwa kuwa  kati ya Juni na Julai mwaka huu, katika siku tofauti kwa pamoja walitoa fedha kwa ajili ya kufanya tukio la ugaidi. Hawakutakiwa kujibu lolote.
Katika kesi nyingine inawakabili Huta, Lema, Ramadhan, Humud, Abashar Omar (24), Morris Muzi (44), Niganya Niganya(28), Baraka Bilango (40), Abdulrahman Hassan (41), Said Temba (42) ambao kwa pamoja walisomewa shtaka la mauaji. Walidaiwa kuwa Juni 5 2013 katika Viwanja vya Soweto, walimuua Ramadhan Juma na kuwajeruhi wengine. Tuhuma nyingine inamkabili Huta na wenzake tisa, wanaotuhumiwa kukusanya zana kwa ajili ya ugaidi.
Wakili Kombe alidai  kuwa Lema, Abdul Mohamed, Abdulrahman Hassan, Morris Muzi, Niganya Niganya na Baraka Bilango  kwa pamoja kati ya Juni 23 na Julai 21 eneo la Ngusero, walikusanya mabomu mawili ya kurusha  kwa mkono kwa lengo la kufanya ugaidi.
Shitaka la pili ni kwa washitakiwa hao hao, kati ya Juni 23 na Julai 22 mwaka huu, wanadaiwa kukusanya mabomu matano kwa nia ya kufanya matukio maovu.
La tatu ni kwa washitakiwa hao kwa pamoja kuwa kati ya Juni 23 na Julai 22 mwaka huu maeneo ya Ngusero, walikusanya risasi sita aina ya Shortgun kwa lengo la kufanya ugaidi.
Shitaka la nne ni kwa mshitakiwa Bilango, Niganya na Muzi ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kusambaza mabomu matano mkoani Kigoma  kwa lengo la kufanya ugaidi.
Shitaka lingine ni kwa washtakiwa Huta, Lema na Ramadhan, ambapo wakili Mwamunyange alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya ugaidi. Ilidaiwa kuwa  Februari 26 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha, kwa pamoja walifanya njama ya kufanya ugaidi msikiti mkuu wa Ijumaa.
Aidha, ilidaiwa watuhumiwa hao kwa pamoja Februari 28 mwaka huu wakiwa katika msikiti wa Ijumaa, walimmwagia usoni tindikali Shekhe Mustapha Kiago na kumsababishia majeraha.
Kosa jingine linahusisha watuhumiwa hao kummwagia tindikali usoni Khalid Mustafa katika msikiti huo Februari 28, mwaka huu. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 15 mwaka huu
Shitaka lingine linamhusu Huta, Lema, Ramadhan Waziri (28), Ramadhan (34) kwa pamoja  Julai 2009 hadi 2013 walifanya njama ya kufanya ugaidi, Kombe alidai  washtakiwa hao Julai 11 mwaka maeneo ya Kwamrombo, walimwagia tindikali Shekhe Said Makamba. Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilka na Hakimu Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15 mwaka huu.
Shitaka lingine linamhusu Huta, Mustapha Kiago (49) Ramadhan na Abdul-Aziz Mkindi (49). Walidaiwa kuwa kati ya  Oktoba mosi na 25 mwaka 2012 ndani ya Jiji la Arusha,   walifanya njama ya kumdhuru Shekhe Abdulkarim Jonjo
Katika shitaka jingine, Oktoba 25 mwaka huo wa 2012 eneo la Sokoni 1 jijini Arusha, wanatuhumiwa walirusha bomu lililotengenezwa kienyeji na kulipuka kisha kumsababisha majeraha Shekhe Jonjo.
Shitaka la tatu ni kwa washtakiwa hao Huta, Kiago, Ramadhan, Mkindi kwa pamoja wanatuhumiwa kutoa ufadhili ili kufanya matukio ya kigaidi. Uchunguzi wa kesi hiyo, bado unaendelea na kesi imepangwa Agosti 15 mwaka huu.
Shitaka lingine linawahusu Ibrahim Leonard (37), Anwar Hayel (29), Yassin Shaaban (20) ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa kosa la kushawishi na kutoa ufadhili ili kufanikisha matendo ya kigaidi. Wanashitakiwa pia kwa kushawishi watu 10 kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Alshabab Islamic maarufu Alshab .
Kwa mujibu wakili Mwamnyange,  vijana walioshawishiwa kujiunga na kikundi hicho ni Abuu Harris, Abuu Shafy, Mwinyi Mwinyi, Abuu Mujahd, Soud Kabaju, Ahmed Ismail, Omary Mohamed, Issa Mkombo, Qassim Salaf na Rashid Salaf
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na baada ya kusomewa mashtaka saba yanayowakabili, walitolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi na askari Magereza kwenda mahabusu ya gereza la Kisongo hadi Agosti 15 mwaka huu, watakapofikishwa tena mahakamani hapo.
Kiongozi wa Uamsho Zanzibar, Shekhe Farid Hadi Ahmed jana alipandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi sambamba na mwenzake, Jamal Swaleh.
Walisomewa mashitaka manne na mawakili waandamizi wa Serikali, Bernald Kongola, Peter Njike na George Barasa mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema.
Ilidaiwa kati ya Januari mwaka jana na Juni mwaka huu katika maeneo tofauti nchini, washitakiwa hao walikula njama za kuingiza watu nchini kufanya vitendo vya ugaidi.
Wakili Kongola alidai kuwa katika tarehe tofauti nchini, washitakiwa walikubali kuwaingiza nchini watu waliokuwa na lengo la kufanya vitendo vya ugaidi.
Katika mashitaka mengine yanayomkabili kiongozi huyo wa uamsho, ilidaiwa aliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omar kushiriki katika  vitendo vya kigaidi.
Aidha, anadaiwa katika kipindi hicho, alishiriki na kusaidia kutendeka kwa vitendo vya ugaidi. Washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na kuomba itajwe Agosti 6 mwaka huu, ambapo watakuwa na ombi.
Hakimu Lema alikubali ombi hilo. Aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6 mwaka huu itakapotajwa tena. Washitakiwa walirudishwa rumande, kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana.

ATUPA MTOTO WA SIKU MOJA KUNUSURU NDOA YAKE

Mtoto wa kike mwenye umri wa siku moja amenusurika kufa baada ya kuokolewa na wasamaria kutoka katika shimo alimotupwa na mama yake mzazi.
Imeelezwa kuwa mwanamke huyo alifanya hivyo ili kulinda ndoa yake changa, kwa kuwa mumewe hakuwa mhusika wa ujauzito huo.
Taarifa za tukio hilo zimethibitishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Rwabigaga, Fron Nestory.
Alisema  tukio hilo ni la usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita katika kijiji cha Rwabigaga kata ya Kamuli wilayani Kyerwa.
Alidai siku hiyo ya tukio, mwanamke huyo, Jane Leonard alijifungua salama mtoto wa kike, lakini baadaye akamwambia mama mkwe wake, kuwa mtoto amepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Nestory alisema kutokana na taarifa hizo, juhudi za kumsaka mtoto zilianza na ilipofika asubuhi wamlikuta mtoto huyo kwenye shimo, akiwa amefunikwa kwa maganda ya maharage na tayari siafu na wadudu wengine, walikuwa wameanza kumshambulia.
Alisema jitihada za kumuokoa mtoto huyo zilifanyika, ambapo baada ya kumuosha alipelekwa katika Kituo cha Afya Kamuli na kupatiwa huduma. Kwa sasa anaendelea vizuri na tayari amekabidhiwa kwa mama yake mzazi.
Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto huyo alisema alifanya hivyo, kutokana na hofu ya kuvunjika kwa ndoa yake changa, kwani imepita miezi miwili tu tangu aolewe.
Ingawa hakutaka kuingia kwa undani, imeelezwa hofu yake imetokana na ukweli kwamba, ameingia katika ndoa mpya akiwa mjamzito, ilhali mumewe wa sasa si mhusika.
Hata hivyo, Nestory aliwataka wananchi kuwa na hofu ya Mungu na kuacha  vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa watoto, kwani mtoto ni tegemeo la taifa kwa ujamla.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo hajalipata;na alisema ameagiza polisi wilayani Kyerwa, kufuatilia zaidi na kumpa taarifa juu hilo.

PINDA ACHARUKA, ATAKA MAJIBU YA UZEMBE NDANI YA SAA 30

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa saa 30 na kutaka kupatiwa majibu, ni kwa nini maelekezo aliyotoa kuhusu kiwanda cha kusindika nyama cha Mbeya, hayajafanyiwa kazi.
Alitoa kauli hiyo jana mchana wakati akizindua Kongamano la siku tatu la Uwekezaji la Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya la mwaka 2014. Kongamano hilo lilianza kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Mbeya.
“Mbeya inaweza kuwa na fursa kubwa ya viwanda vya usindikaji nyama, unga wa mahindi ili kuongeza thamani ya mazao mnayozalisha katika mkoa wenu. Nilipokuwa hapa ziara yangu ya mwisho 2012, niliagiza kiwanda hiki kitafutiwe mwekezaji ili kianze uzalishaji. Jana nimeuliza kiwanda cha nyama kimefikia wapi, naambiwa watu bado wanaongea. Wanaongea nini?,” alihoji.
“Mtu akija kusikia habari ya kiwanda hiki, atatuona ni wajinga tena ni wajinga wa kujitakia, kisa watu bado wanazungumza…hiki kiwanda cha nyama ni cha Mbeya na manufaa yake ni kwa ajili ya wana Mbeya. Hivi wahusika kwani hamuioni hiyo fursa?” alisema.
“Dk Mary Nagu watafute watu wa CHC, waje hapa kujieleza ni kwa nini suala hili limechukua muda mrefu. Kabla sijaondoka hapa Mbeya kesho (leo) nataka nipate majibu kuhusu jambo hili,” aliagiza.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu alisisitiza suala la watendaji wa mikoa na wilaya, kuchukulia kwa umakini suala la uwekezaji, kwani wasipofanya hivyo wao ndiyo watageuka kikwazo na kukwamisha maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.
“Ndugu zangu wa Serikali za mitaa msiwe vikwazo, kuweni wawezeshaji. Ninyi si watawala, bali ni waleta maendeleo kwa jamii. Natoa wito mshirikiane na wafanyabiashara kuharakisha maendeleo ya wananchi mliokabidhiwa kuwaongoza. Acheni kudai hongo, kwani badala ya kuwasadia jamii, mtajikuta ninyi ndo mnakuwa vikwazo vya maendeleo,” alionya.
Alisema Serikali za Mitaa zinapaswa kuwa wawezeshaji na siyo wakwamishaji wa masuala ya maendeleo.
Ili kufanikisha hilo, aliwataka wakuu wa mikoa waanzishe eneo moja la biashara katika ngazi ya mkoa na halmashauri ili wawekezaji wanapofika katika mikoa yao, wasizungushwe na kukatishwa tamaa kwa sababu ya mlolongo wa taasisi zilizopo.
Alisema kila mmoja, hana budi kudumisha amani na utulivu wa nchi ili uwekezaji uweze kufanikiwa na kushamiri.
 “Hakuna uwekezaji endelevu na wenye tija katikati ya fujo na migogoro, na uwekezaji utashamiri pale tu penye amani na utulivu,” alisisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk Mary Nagu alisema ili uwekezaji uweze kuwanufaisha wananchi ni lazima rasilimali za nchi zigeuzwe kuwa bidhaa.

OFISA WANYAMAPORI MBARONI KWA UWINDAJI HARAMU

Ofisa Uhifadhi wa wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Rashid Ndimbe amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  akikabiliwa na mashitaka ya kuwinda bila kibali na kukutwa na nyama ya nyati.
Ndimbe, ambaye alirudishwa rumande baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana, alikana mashitaka yanayomkabili.
Alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka matatu na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bernald Kongola mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka.
Wakili Kongola alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari na Septemba mwaka jana, katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Ndimbe alikamatwa akisafirisha nyara za serikali ambazo ni nyama ya nyati yenye thamani ya Sh 200,000, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.
Alidai kuwa Septemba 21 mwaka jana katika maeneo hayo, Ndimbe alikutwa akiwa na nyara hizo. Pia anadaiwa katika eneo la hifadhi la Kilwa alikamatwa akiwinda nyati bila ya kuwa na kibali.
Mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo. Upande wa jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu Kisoka aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14 mwaka huu, itakapotajwa tena na mshitakiwa alirudishwa rumande baada ya DPP kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana yake.

SHIRIKA KUFADHILI WAUGUZI 20 KUSOMA MAREKANI

Shirika la Colom Faundation Inc (CFI) la Marekani limetoa ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi kwa wauguzi 20 nchini, watakaokwenda nchini humo kujifunza zaidi masuala ya afya ya uzazi na mtoto kwa lengo la kuboresha huduma hiyo nchini.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa Chama cha Taifa cha Wauguzi nchini (TANNA), Paulo Magesa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Magesa alisema makubaliano hayo, yamefanywa baina yao na CFI. Alisema katika mpango huo wa mafunzo, awamu ya kwanza wauguzi 10, kati ya 20 watakwenda nchini Marekani majira ya joto katika Chuo Kikuu cha Dixie kwa ajili ya mafunzo ya wiki nane.
Alifafanua jinsi ya kuwapata wauguzi hao, kwamba watatangaza nafasi hizo za mafunzo kwenye vyombo vya habari ili kutoa fursa kwa wauguzi nchini, kuomba na kwamba wenye sifa watafanyiwa usaili na watakaoshinda ndio watakaokwenda.
Magesa alisema gharama zote za mafunzo hayo, zitagharamiwa na shirika hilo na kwamba kwa wale watakaopata nafasi za mafunzo, watakaporudi watatakiwa kutoa mafunzo kwa wengine ambao hawakupata fursa hiyo.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuboresha huduma za afya nchini, hasa kwa afya ya mama na mtoto.
Alisema kwamba fursa hiyo, itakuwa endelevu ili kutoa nafasi zaidi kwa wengine kushiriki na kurudi kusaidia huduma za afya ya uzazi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa CFI ambaye pia ni mwekezaji  nchini wa Hoteli za Nashera, Wilbur Colom alisema wameingia kwenye mkataba huo, ikiwa ni sehemu ya kusaidia jamii ya Tanzania kutokana na wao kuwekeza hapa nchini.
“Tumeamua kuwa na makubaliano ya ushirikiano na TANNA, tumewekeza nchini, na tuna wajibu wa kusaidia jamii tuliyomo, ili tuendeleza undugu na kusaidiana ili afya ya mama na mtoto iboreke”,alisema Colom.
TANNA ilianzishwa nchini mwaka 1979, ikiwa ni chama cha wauguzi wenye taaluma ambao wamesajiliwa katika baraza ya wauguzi na ina matawi 29 nchini, yenye zaidi ya wanachama 3,500 ambao wanafanya kazi kwenye taasisi mbalimbali nchini.

WAVUVI 9 WAFARIKI DUNIA ZIWA TANGANYIKA

Wavuvi tisa wakazi wa kijiji cha uvuvi cha Mpasa wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa, wamekufa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Tanganyika.
Habari kutoka eneo la tukio,  ambazo pia zimethibitishwa na jeshi la polisi, zinasema wavuvi  hao walikuwa  wakisafiri kwenda  katika Mji wa Mpulungu, mwambao mwa Ziwa  Tanganyika katika nchi jirani ya Zanmbia. Walikuwa  wakitokea kijiji cha uvuvi  cha Mpasa  wilayani Nkasi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Ferdinand  Rwegasira,  alithibitisha kutokea  kwa ajali hiyo. Alisema  miili  yote  tisa  ya waliokuwa wakisafiri ndani ya boti  hiyo, haijapatikana  hadi sasa.
Alitaja wanaosadikiwa  kufa ni Fadhili Nkambi (30), Shaaban Kasokota ((33) Audifas Miele (43), Linus Maliyatabu (38), Kashindi Tantika (25), Venus Albeto (35), Geofrey Kazumba (24), Mwambe Ntapantapa (21) na Mathias Ulaya (20) .
Kamanda Rwegasira  alisema uchunguzi  wa ajali hiyo  ya majini,  bado unaendelea na  pia wanaendelea kutafuta miili  hiyo.
Akizungumza na mwandishi kwa simu kutokea  eneo la tukio, Ofisa Mtendaji  wa Kata ya Kasanga  mwambao  mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Kalambo, Francis Simfukwe  alisema wavuvi  hao  walianza safari  yao kuelekea Zambia Julai 28 mwaka huu  sasa 11:00 alfajiri .
Alisema  wavuvi hao  walikuwa  wakisafiri kwenda mji wa Mpulungu, Zambia  kuuza samaki  wao,  waliowavua  kwa ndoano na kuwahifadhi katika  makasha  27, ambapo  kila mvuvi alikuwa na makasha  matatu .
“Sasa kwa kuwa walikuwa wakikwepa kupitia  kijijini  Kasanga  ili wasiweze kulipa  ushuru wa samaki hao,  waliokuwa wakisafirishwa  kwenda  nchi jirani ya Zambia,    walipita  nchi jirani ya  Kongo ( DRC)  katika  Ziwa,  hivyo kufanikiwa  kukwepa  kupita  katika kijiji cha Kasanga  ambayo ni bandari  ya mwisho  katika Ziwa Tanganyika  kwa upande wa Tanzania  kabla ya  kuingia  nchini  Zambia,”  alidai Simfukwe.
Kwa mujibu  wa Simfukwe,  wavuvi  hao  walipofika  vijiji vya uvuvi  vya Kilewani na Kipwa  mwambao  mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Kalambo,  ghafla  upepo mkali ulivuma  ndipo walipoamua  kuanza kurejea ufukweni  mwa  kijiji cha uvuvi  cha Kipwa. Lakini,  boti yao  ilipigwa na dhoruba kali na kuzama.
“Siku iliyofuata  makasha  manne yakiwa na samaki  wabichi,  huku yakiwa  yameandikwa  majina,  yalionekana  yakielea ziwani  katika kijiji cha Kipwa…ndipo tulipohisi kuwa  kuna ajali  imetokea  ziwani," alieleza Simfukwe.
Simfukwe alisema wakazi wa kijiji  cha  uvuvi  cha Nsumba mwambao mwa Ziwa Tanganyika  nchini Zambia,  walitoa  taarifa kuwa wameona mtumbwi  ukielea  ziwani, karibu na kijijini chao ukiwa  hauna wala mashine ya  kuendeshea.
Baadhi ya  wavuvi  wa kijiji cha Mpasa,  walimweleza mwandishi wa habari  hizi  kwa njia ya simu,  kwa masharti ya kutoandikwa  majina yao, kuwa  baada ya  kukatika kwa mawasiliano ya  simu  baina  yao  na wavuvi wenzao, waliokuwa  wakisafiri  kwa boti kuelekea  nchini Zambia kuuza  samaki wabichi,  walianza  kuwatafuta .

SERIKALI YAMWAGA WATAALAMU KILA KONA KUKABILI EBOLA

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesambaza wataalamu wa afya katika mipaka yote nchini, ikiwa ni tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa wa ebola.
Kusambazwa kwa wataalamu hao wa afya ni sehemu ya mikakati iliyowekwa na serikali kupitia wizara hiyo ya kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo na kuhakikisha unadhibitiwa.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema, wataalamu hao mbali na kusambazwa katika mipaka yote nchini lakini pia katika viwanja vya ndege vya kimataifa ili kuhakikisha watu wenye virusi vya ugonjwa huo wanajulikana kabla ya kuingia nchini.
Mwamwaja alisema mikakati mingine iliyopo ni kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC) katika kukabiliana na ugonjwa huo.
"Pia kusimamia mpango mkakati wa kupambana na ebola ambao upo, maandalizi ya kudhibiti ugonjwa huu tulishayafanya mwaka 2012 wakati nchi jirani ya Uganda ilipopata wagonjwa wa ebola," alisema Mwamwaja.
Alisema wataalamu wa afya wataendelea kutoa elimu ya afya juu ya ugonjwa huo ambao alisema hauna chanjo wala tiba. Aidha, alisema mpaka sasa kwa hapa nchini hakuna mgonjwa aliyedhaniwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo.
Mwamwaja alisema wizara inawasihi na kuwaomba wananchi kutokuwa na hofu bali wachukue tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo. Alisema wizara itaendelea kutoa taarifa juu ya ugonjwa na mikakati iliyopo ya kukabiliana nayo.
Ugonjwa huo wa ebola uliibuka hivi karibuni katika nchi ya Guinea na kusambaa katika nchi za  Sierra Leone, Liberia kati ya Julai 18 na 20, mwaka huu.
Tayari katika nchi hizo wagonjwa 1,323 wameripotiwa kukumbwa na ugonjwa huo huku vifo 729 vikiripotiwa.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa damu ya mtu mwenye ugonjwa huo au maji maji ya mwilini mwake, kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo zimeelezwa kuwa ni kupatwa na homa kali ya ghafla, kulegea kwa mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa pamoja na kutokwa na vidonda kooni.
Aidha, dalili hizo hufuatiwa na kutapita, kuharisha, kutokwa na vipele, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu ndani na nje ya mwili.

CHANA: TOENI TAARIFA ZA UKATILI WA KIJINSIA

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana ameitaka jamii kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia, badala ya kuona kama ni mila na desturi.
Chana alisema hayo jijini Dar es Salaam jana baada ya kutembelea kituo cha "One Stop", kinachohudumia watu waliofanyiwa ukatili kilichopo katika hospitali ya Amana pamoja na makao ya watoto Kurasini.
Alisema kuwa wapo watu wengi wanafanyiwa ukatili na jamii inafahamu lakini wanakaa kimya hawatoi taarifa kutokana na tamaduni mbalimbali.
"Matukio ya ukatili ni mengi katika jamii ila wakati umefika sasa wa kusema matukio hayo sasa basi. Tutumie vituo kama hivyo kutoa taarifa za ukatili ili na muathirika apatiwe huduma," alisema.
Alisema pia yapo madawati ya jinsia katika vituo vya polisi, hivyo jamii ihakikishe inavitumia ipasavyo na kuripoti matukio yote ya ukatili. Aidha, alisema jukumu la kuwatunza watoto ni la wote ili wasiishi mitaani, hivyo ukatili unatakiwa kukomeshwa.
Kituo cha One stop kilianzishwa Desemba mwaka jana. Hadi sasa kimewahudumia wahanga 293, ambao ni waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto chini ya miaka 18.
Mbali na kutembelea vituo hivyo,  pia Chana alitembelea Manispaa ya Temeke na kuzungumza na viongozi wake pamoja na kupokea taarifa ya Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na vijana.

ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI

Mkazi wa Kata ya Busi Tarafa ya Pahi Wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Bakari Hussein (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo  lilitokea Julai 31, mwaka huu.
Alisema mtuhumiwa alimuua Rukia Juvency (50) kwa kumpiga mtama na alipoanguka alimpiga na tofali la saruji kichwani upande wa kushoto na kumsababishia kifo muda mfupi baada ya kufikishwa katika Kituo cha Afya cha Kijiji cha Busi.
Kamanda Misime alisema chanzo cha mauaji hayo kinachunguzwa, ingawa mtuhumiwa anadai siku ya Idd el Fitr alitukanwa na mwanamke huyo.
Aidha,  Kamanda Misime alisema mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika. Alitoa mwito kwa wananchi, kuacha kujichukulia sheria mkononi.
“Kama umetukanwa ufumbuzi wake ni kwenda kushitaki katika idara zilizowekwa kisheria ili walifanyie kazi tatizo hilo,” alisema.

WATENDAJI WAWILI WILAYA YA BAHI MATATANI

Maofisa watendaji wa vijiji viwili katika Wilaya ya Bahi, wameingia matatani baada ya kutafuna fedha za michango ya wananchi zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa maabara za shule za sekondari.
Watendaji hao ni Killian Makota wa Kijiji Nhinyila Kata ya Mwitikila na  Issa Rashid wa  Kijiji cha Msisi Kata ya Msisi.
Hali hiyo ilitokana na madiwani wa Kata hizo, kutoa malalamiko juu ya watendaji hao katika kikao cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika wilayani humo jana.
Akitoa malalamiko hayo, Diwani wa Kata ya Mwitikila, Jamal Shabiby alidai kutokana na Makota kula fedha za michango ya wananchi, wananchi wamegoma kuchangia tena kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa maabara.
“Mimi ninaomba kabla ya kuendelea kuwahimiza wananchi kuendelea kuchangia ujenzi wa maabara, kwanza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mtendaji wa Kijiji cha Nhinyila kutokana na kula fedha za michango ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Msisi, Chuga Mgaliwa alidai mtendaji wake ametafuna zaidi ya Sh. milioni moja, ambazo ni michango ya wananchi.
Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa alisema Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Msisi, tayari ameshachukuliwa hatua, ikiwemo kuwekwa mahabusu.
Alisema baada ya Mtendaji huyo, kuwekwa mahabusu  aliamriwa kulipa fedha zote anazodaiwa Sh 800,000 ndipo atolewe. Hata hivyo, alilipa Sh 600,000 na akaomba aachiwe ili fedha nyingine akakope benki.
Mkwasa alisema mtendaji huyo, tayari ameanza utaratibu wa kukopa fedha benki ili amalizie Sh 200,000 zilizobaki.
Kuhusu Ofisa Mtendaji wa Nhinyila, Ofisa Utumishi wa Wilaya  ya Bahi, Fredrick Kayombo alisema wameshaanza kushughulikia tuhuma hizo, ikiwemo kumchukulia hatua za kisheria. Alisema katika mahojiano ya awali, mtendaji huyo alidai alivamiwa na kuibiwa fedha hizo.

HALMASHAURI 41 KUSHIRIKI NANENANE MWANZA

Halmashauri 41 za Kanda ya Ziwa na wadau 15 wa maonesho nya kilimo, wamethibitisha ushiriki wao kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa, yaliyoanza jana.
Maonesho hayo yanafanyika katika viwanja vya Nyamhong’olo, nje kidogo ya jiji la Mwanza. Yatafunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi, Celina Kombani.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Nanenane Kanda ya Ziwa, Pascal Mabiti, uzinduzi rasmi utafanyika Agosti 3, mwaka huu.
Aliwataja wadau waliothibitisha kushiriki katika maonesho hayo kuwa ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Victoria Polybags & Moulders, Nyanza Bottling Ltd, SBC Tanzania, Yara Mila Co. Ltd na Star Times. Wengine ni Sahara Media Group, Taasisi ya Utafiti-Ukiriguru, Umwagiliaji Kanda, Tigo, Meru Agro Consultant, Bodi ya Pamba Tanzania, SIDO Mwanza, Mabatini Moulders na TCRA.
Alisema maonesho hayo ya wakulima, yatatoa fursa washiriki kupata elimu kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa, zikiwemo za ugonjwa mpya wa mahindi, magonjwa ya mazao ya mihogo na migomba na udhibiti wake.
Pia, mada za matumizi sahihi ya mbolea na stakabadhi ya mazao ghalani, zitatolewa katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Alisema asilimia 80 ya maandalizi, yamekamilika, hivyo kutoa fursa kwa mgeni rasmi kufungua maonesho hayo, yatakayokuwa na kaulimbiu inayosema “Matokeo Makubwa Sasa - Kilimo na Biashara”’.
Katika maadhimisho kama hayo mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo aliwatahadharisha wakulima na wafugaji juu ya fedha bandia, zinazotumiwa na watu wasio waaminifu kununua bidhaa kwenye maonesho hayo.

Friday, August 1, 2014

JICHO LA TATU


YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO IJUMAA - AGOSTI 01