Thursday, October 16, 2014

WALIOKUFA LORI LA PETROLI WAFIKIA WATANO, POLISI ALIYEJARIBU KUZUIA AAMBULIA KIPIGO



Idadi ya watu waliokufa kutokana na ajali ya moto wa lori lililopinduka na kisha kulipuka baada ya watu kulivamia kwa lengo la kujipatia mafuta, imeongezeka na kufikia watano kutoka vitatu vya awali.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Alisema katika ajali hiyo iliyotokea juzi usiku eneo la Mbagala, watu 16 walijeruhiwa baada ya kuungua maeneo mbalimbali ya miili yao.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 347 BXG mali ya Moil Transporter lililokuwa likitarajiwa kusafirisha mafuta kuelekea Kampala, Uganda likiwa na kemikali aina ya petroli lita 38,000 inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola 36,000 (Sh milioni 60).
Aliwataja waliokufa kuwa ni Hassan Mohammed (25), mkazi wa Mbagala Kimbangulile, Masoud Masoud (33), Mohammed Ismail (19), Ramadhani Khalfan (36) na Maulid Rajabu, wakazi wa Mbagala Charambe.
Majeruhi waliotambuliwa ni Hamis Ally (35), mkazi wa Mbagala Kiburugwa, Rajabu Selemani (28), mkazi wa Tandika, Idd Said (28), Janney Mathayo (25), mkazi wa Mbagala Kizuiani, Mathayo Daniel (21), mkazi wa Mbagala Charambe na askari polisi, Koplo Thomas aliyejeruhiwa na jiwe kwenye paji la uso wakati akijaribu kuzuia vibaka kuchota mafuta kabla ya kulipuka.
Alisema majeruhi wengine 10 wamelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Wilaya ya Temeke wakiendelea na matibabu na wengi wao hali zao siyo za kuridhisha.
Kamanda Kova aliongeza kuwa, mbali ya kusababisha vifo na majeruhi, ajali hiyo pia ilisababisha kuungua kwa nyumba ya kulala wageni iitwayo United yenye vyumba 32, mali ya Deus Kasigwa (42), mkazi wa Mtoni Mtongani. Moto huo uliteketeza pia maduka matano yenye vitu vyenye thamani ya Sh milioni 197 na pipikipiki saba ziliteketea kabisa na moto.
Naye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya taifa ya Muhimbili, Doris Ishenda alisema majeruhi 11 wanaoendelea kutibiwa hospitalini hapo, huku akiongeza kuwa, hali zao sio nzuri kwa kuwa waliunguzwa vibaya na moto na kwamba madaktari wanaendelea kuwapatia matibabu.
‘’Majeruhi wote wamelazwa katika wadi namba 22 ya Sewa Haji wanaendelea na matibabu, lakini hali zao sio nzuri kabisa kwani waliungua sana,’’ alisema Ishenda.
Wakati huo huo, Paulo Milanzi (35), mkazi wa Chanika katika manispaa ya Ilala anayetuhumiwa kushiriki katika mauaji ya Ofisa Usalama wa Taifa, Sylvanus Mzeru, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi katika majibizano na polisi.
Kova alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu kuhusu matukio mbalimbali ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

POLISI YAZUNGUMZIA WIMBI LA UTEKAJI WATOTO DAR



Wakati hofu juu ya usalama wa watoto katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ikizidi kutanda miongoni mwa wazazi na walezi, Polisi imekanusha kuwapo kwa matukio ya utekaji nyara watoto wanaosoma shule za msingi na kufanyiwa unyama ukiwamo ulawiti, kuuawa na hata kuchunwa ngozi.
Kwa wiki kadhaa sasa, hofu juu ya matukio ya aina hiyo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na taarifa za mitandao ya kijamii, ikielezea jinsi watoto wanavyotekwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza jana, alisema hivi karibuni umezuka uvumi kutoka kwa watu mbalimbali kwamba lipo kundi la wahalifu wanaotumia gari aina ya Toyota Noah yenye rangi nyeusi kutenda uhalifu dhidi ya watoto.
Alisema Polisi imefanya uchunguzi na mpaka sasa hawana taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji nyara. Kwa mujibu wa kamanda, polisi inamshikilia mtu mmoja kwa kuhusika kusambaza uvumi huo.
“Polisi imegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo nawaomba wananchi kuachana na uvumi huo na kupuuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi na kuleta usumbufu kwa baadhi ya watu,” alisema.
Alisema Oktoba 3 mwaka huu saa 3.00 asubuhi, Vingunguti, mfanyakazi wa The Guardian Ltd, Prosper Makame (34) akiwa na mkewe MaryStella Munis (30) mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika eneo la shule ya msingi Kombo kwa ajili ya kuchukua fedha  za vyombo wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba T 252 DAY rangi nyeusi na kuvamiwa na wananchi.
“Wakati watu hao wakisubiri kuchukua fedha, ghafla walikuja zaidi ya wananchi 100 na kuzingira gari hilo huku wakipiga kelele wakidai kwamba ndilo gari linaloteka wanafunzi. Lakini polisi walipata taarifa hizo mapema na kufika eneo la tukio na kuwaokoa watu hao pamoja na gari lao,” alisema.
Kova alisema Oktoba 13 saa 10.00 katika Kituo cha Polisi Tabata katika Manispaa ya Ilala, uliibuka uvumi kuwa gari namba T 548 BUN aina ya Noah nyeusi ambayo ni mali ya askari polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani, Inspekta Esther lililokuwa kituoni hapo, ndani yake kulikuwa na vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani.
“Kutokana na uvumi huo wananchi walikusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona hivyo vichwa vitano, ndipo mkuu wa kituo hicho alipoamuru gari hilo kufunguliwa na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uongo na uvumi,” alisema.
Alisema hali hiyo ya uvumi ni ya hatari kwa sababu wananchi kila wanapoona Noah nyeusi wanaikimbilia na kuizingira kwa lengo la kufanya fujo.
“Polisi tunasisitiza kuwa uvumi huu wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu ambao wamekuwa wakiwateka watoto na wanafunzi siyo kweli hata kidogo na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema.
Alisema uchunguzi wa kubaini nani alieneza uvumi huo ulifanyika na kubaini kuwa umeenezwa na Gilbert Stanley (32), mkazi wa Tabata ambaye alikamatwa.
Alipohojiwa, kwa mujibu wa kamanda, alikiri kueneza habari hizo na kudai aliambiwa na mtu mwingine ambaye alidai hamkumbuki.

KOMBANI ANUSURU AJIRA ZA DC, DEC MAABARA ZA 'KIKWETE'



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ametoa msaada muhimu wa Sh milioni 40 na bati 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule 12 za sekondari zilizopo katika jimbo la Ulanga Mashariki wilayani humo, mkoani Morogoro.
Mbali na msaada huo pia amesaidia vifaa mbalimbali ikiwamo sare, viatu na vyakula vyenye thamani ya Sh milioni 7.2 kwa askari wa jeshi la Mgambo wa wilaya ambao wanatumika kufyatua matofali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara.
Kombani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki alikabidhi misaada hiyo kwenye ziara yake aliyoianza jimboni humo jana, ambapo alisema ameamua kusaidia ujenzi huo wa maabara ili jimbo la Ulanga Mashariki liweze kutoa wanafunzi wenye utaalamu wa masomo ya sayansi katika siku za usoni.
Kutolewa kwa msaada huo kwa wilaya hiyo kunaweza kufanikisha utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa mikoa wawe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule ya sekondari ya kata ifikapo Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa agizo la Rais, kiongozi yeyote katika ngazi za wilaya na mkoa kote nchini atakayeshindwa kutimiza wajibu kwa kutekeleza agizo hilo, atachukua maamuzi magumu dhidi yake.
Hata hivyo alisema, ili kufikia muda uliopangwa wa kukamilika kwa maabara hizo wameamua kuwatumia askari wa mgambo kwa ajili ya kutengeneza matofali na ujenzi huo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuleta maendeleo.
“Mimi nilishaanza kwa baadhi ya shule za jimboni mwangu  kujenga vyumba vya maabara kabla ya  agizo la rais, kwa hiyo huu ni mwendelezo na nia yangu ni kuhakikisha wana Ulanga wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo kwani dunia ya sasa ni sayansi na teknolojia,” alibainisha Waziri Kombani.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kwa kusema katika mafunzo yajayo ya mgambo atajitahidi  kuwapeleka  wakufunzi wa masuala ya ujasilimali ili wakati wanapata mafunzo pia wafundishwe namna ya kuendesha ujasilimali na sio ulinzi pekee ili waweze kujikwamua kwa kuongeza kipato.
Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya  hiyo, Isabela Chilumba, alisema  ujenzi wa vyumba vya maabara unaendelea na wananchi wameshahamasishwa kupitia mikutano mbalimbali kwa ajili ya kuchangia chochote ili  kukamilisha ujenzi huo.

MKUU WA WILAYA AKAANGWA KWENYE TUME YA MAADILI



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Anna Mwalende ameanika mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma ushahidi wake dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gamba na kueleza namna alivyodhalilishwa na kunyanyaswa pamoja na viongozi wengine.
Mwalende ambaye ni shahidi wa tatu katika shauri linalomkabili Gamba, alidai  amefanya kazi serikalini kwa miaka 24 katika utumishi wa umma, miaka saba katika Serikali Kuu na miaka 14 katika halmashauri, lakini miezi mitano aliyofanya katika wilaya hiyo hataisahau maisha yote.
Alikuwa akitoa ushahidi wa upande wa mashtaka ambao ni  Sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa umma,  katika  Baraza la Maadili wa viongozi wa Umma lililo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Hamisi Msumi kuhusu tuhuma zinazomkabili DC huyo za kutumia madaraka yake  vibaya alidai kudhalilishwa na Gamba.
Alidai Mkuu huyo wa wilayaamekuwa na lugha chafu kwa viongozi wenzake, ana utawala wa mabavu bila kuzingatia kanuni na sharia, jambo ambalo ni kikwazo kwa maendeleo ya wilaya hiyo. Alidai alitukanwa mbele ya Waziri wa Maji kwa kuitwa  mkurugenzi wa hovyo.
Aidha, alisema mkuu huyo wa wilaya amesababisha kukwama kwa maendeleo ya wilaya hiyo huku akiwaweka `mahabusu’ viongozi wanaofanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria kwa kutaka kufuata maamuzi yake.
Mkurugenzi huyo ambaye amesimamishwa kazi na DC huyo na kumleta mkurugenzi mwingine ameeleza kuwa halmashauri hiyo ina wakurugenzi wawili wanaolipwa mishahara hivyo, kuongezea gharama serikali.
Alidai amesimamishwa kazi na mkuu huyo wa wilaya huku tuhuma zikiwa hazijathibitika na kupelekwa mkurugenzi mwingine, hivyo kuwa wawili na wote wanalipwa sawa.
Alidai kwa wakati tofauti amekuwa akimtukana Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kuwa mwizi na mla rushwa, ikiwa ni pamoja na kuwaambia mmoja wa watendaji wa halmashauri hiyo kuwa amepata shahada kwa kutumia nguo ya ndani.
Alidai kuwa  alipotaka kutekeleza majukumu ya kumwajibisha mfanyakazi mbadhirifu  aliyekuta ripoti yake wakati anaripoti ofisini hapo baada ya tume iliyoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kumuagiza, alimwambia suala hilo litamtokea puani.
“Kuna siku alituita mimi na Ofisa Utumishi na kutaka kumrejesha kazini mwalimu aliyekuwa hajahudhuria kazini kwa miaka mitatu tukakataa ndipo akaagiza tuwekwe rumande, lakini mimi nilikataa na kupewa askari wa kike anilazimishe lakini niliwasiliana na RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) sikulala rumande,” alisema.
Alidai kuwa Ofisa Utumishi alilala ndani kwa siku kadhaa na yeye kufuatilia polisi, lakini aliambiwa hawezi kutoka mpaka kwa amri ya DC na baadaye diwani mmoja alifanikiwa kumtoa.
Alidai pia kuwa DC huyo alimweka ndani Mhandisi wa Maji wa wilaya na kutaka achukuliwe hatua na polisi hawakutaka kumtoa mpaka DC alipotoa kibali.
Mkurugenzi huyo alisema amefanya kazi serikalini kwa miaka 24 katika utumishi wa umma, miaka saba katika Serikali Kuu na miaka 14 katika halmashauri, lakini miezi mitano aliyofanya katika wilaya hiyo hataisahau maisha yote.
Baraza lilimtaka kuwasilisha vielelezo vya ushahidi wa sauti zenye maneno ya matusi na maandishi ya uongozi wa mabavu ambayo shahidi huyo alikiri kuwa navyo.
Awali, shahidi wa pili katika shauri hilo, diwani wa Kata ya Mndolwa wilaya ya Korogwe, Hillary Ngonyani ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo alidai DC huyo aliwahi kumwita `sisimizi’ wakiwa katika vikao vya halmashauri.
Pia aliunga mkono suala la DC huyo kumuita mtumishi mwenzao kuwa amepata shahada kwa kutumia nguo ya ndani na kesi ipo mahakamani huku akiwa na dharau, kiburi, kashfa na kufanya kazi kinyume cha taratibu.
“DC huyu akijua kuwa yeye ni kiongozi amekuwa na dharau na kudhalilisha viongozi wenzake kwa kuwatukana wale wote wanaofanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu na kukataa kutii maamuzi yake ambayo ni kinyume,” alisisitiza.
Kutokana na kumpa muda wa kuwasilisha vielelezo shahidi wa tatu, shauri hilo liliahirishwa mpaka kikao cha baraza kijacho ambapo vielelezo vitakuwa vimepatikana.
Wakati huo huo, baraza hilo lilisikiliza mashauri dhidi ya madiwani watano wakiwemo wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wanadaiwa kutowasilisha tamko la mali na madeni kwa mujibu wa sheria.
Waliotuhumiwa ni Diwani wa Magomeni, Julian Bujugo (CCM) aliyekiri kutowasilisha tamko hilo mwaka 2012 kutokana na kuwa mbali na mkoa yaliyosababishwa na kufiwa na mke wake, Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Uoleuole Juma (Chadema) ambaye kesi ya Uchaguzi bado iko mahakamani.
Wengine ni Diwani wa Kata ya Kunduchi, Janeth Rite (Chadema) aliyedai kupeleka fomu hizo, lakini akashangaa kuambiwa hazijafika, Diwani wa kata ya Sinza Renatus Pamba ambaye alisema amewasilisha tamko na nakala anazo, lakini shauri lake halikukamilika baada ya Mwenyekiti kubaini wanaapa bila kutumia vitabu vya dini.
Jaji Msumi alilalamika kutopelekwa kwa Biblia na Kurani kwa ajili ya kuapa na kusema viapo vyote havikuwa halali na kuahirisha mashauri yaliyobaki hadi leo.