Thursday, September 18, 2014

MABINTI PACHA WALIOUNGANA KUHITIMU KIDATO CHA NNE MAKETE


Hatua ya kwanza ya ndoto ya kuzama katika elimu ya mabinti pacha walioungana kiwiliwili, Consolata na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete  mkoa mpya wa Njombe, inatarajiwa kutimia Novemba mwaka huu, wakati mabinti hao watakapofanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.
Itakumbukwa kwamba walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao Ikonda, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema wanataka kuwa wasomi waliobobea katika utaalamu wa kompyuta. Lakini, kwa sasa, wanasema wanatamani kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi.
Wanafunzi hao ambao mwaka 2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar es Salaam.
Kwa sasa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Shule hiyo inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari Wakatoliki wa Italia, kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii shuleni hapo hivi karibuni, walisema wanafurahi kuwa miongoni mwa watahiniwa watakaofanya mtihani huo wa kidato cha nne mwaka huu.
"Tunafurahi, tunajiandaa tunasoma kwa bidii, mtihani uko karibu tunataka tufaulu vizuri masomo yetu, ili ile ndoto yetu ya kuwa Makatibu Muhtasi itimie," walisema Maria na Consolata, ambao wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani, ambako pia wana kiti maalumu.
Pacha hao wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana madaftari yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
"Wala hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia," anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Ilianzishwa mwaka 2006 na hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 183. Wote wanaishi kituoni hapo na wote wanatoka kwenye mazingira magumu.
Changamoto kubwa iliyokuwa shuleni hapo ni ukosefu wa nishati ya umeme, ambapo uongozi wa shule na kituo hicho unalazimika kutumia jenereta na umemejua, jambo ambalo mapema wiki hii Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa kuwapelekea umeme.
Pacha hao walizaliwa mwaka 1996 wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Iringa.
Walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010, ambapo kila mmoja alipata alama 151, ingawa walitofautiana ufaulu  kwenye masomo yao.
Katika somo la Maarifa ya Jamii, Consolata alipata alama 29 na Maria alama 25, kwenye somo la Kiingereza, Maria alipata alama 36 na kumzidi Consolata aliyepata alama 34, wakati kwenye somo la Sayansi, Maria alimzidi Consolata kwa kupata alama 31 dhidi ya 29.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliwapanga pacha hao kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo hawakujiunga na sekondari hiyo, kutokana na hali yao na pia umbali kutoka Iringa hadi Dar es Salaam. Ndipo Wamisionari hao wakawachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza.
Walizaliwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996. Lakini, taarifa zao hazikufahamika hadi pale walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa bado wadogo.

MAANDAMANO YA CHADEMA MARUFUKU, VYUO VIKUU 14 VYAYALAANI


Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), yaliyotarajiwa kuanza kufanyika leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Jeshi hilo limeonya kuwa maandamano hayo ni batili na ni kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana makao makuu ya jeshi la Polisi Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja alisema jeshi hilo limeanza kupokea taarifa ya chama hicho, kikitaka kufanya maandamano kuanzia leo. Lakini, alisisitiza kuwa maandamano hayo hayataruhusiwa.
“Septemba 15 jeshi lilitoa taarifa kuhusu kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwahimiza wafuasi wa chama chake kufanya maandamano na migomo isiyokoma pote nchini ili kusitishwa kwa Bunge la Katiba na hivi sasa tumeanza kupokea taarifa ya chama hicho kufanya maandamano,” alisema.
Alisema maandamano hayo ni batili, kwa sababu Bunge la Katiba linaloendelea hivi sasa, linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hakuna sheria iliyokiukwa, hivyo kitendo cha kufanya maandamano, kushinikiza kuvunjwa kwa Bunge hilo ni kinyume cha sheria, jambo ambalo jeshi la polisi haliwezi kuruhusu.
Aidha, alisema kuwa ieleweke wazi kwamba Bunge la Katiba, lipo kisheria na kila jambo linalofanyika bungeni ni kwa mujibu wa sheria.
Chagonja alisema jeshi la polisi lina jukumu la kulinda watu wote, wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
“Hata hivyo, hivi sasa kuna kesi inayoendelea Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayohoji uhalali wa kuendelea kwa Bunge hilo na kesi hiyo haijafikia mwisho na uamuzi kutolewa, hivyo maandamano hayo yaliyopangwa na Chadema yanaingilia uhuru wa Mahakama, jambo ambalo siyo sahihi. Mahakama kama chombo cha kutoa haki, kiachwe  kifanye kazi yake,” alisema.
Chagonja alitoa mwito kwa wananchi wote, kuendelea na shughuli zao na yeyote atakayekiuka katazo hilo, jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Wakati Chagonja akiyasema hayo, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, amewaonya wafuasi wa Chadema wanaodaiwa kutaka kuandamana hadi Viwanja vya Bunge
kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo, uongozi wa Chadema mkoani humo, umedaiwa kusisitiza maandamano yako palepale.
Akizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula alisema maandamano hayo, pia yamepangwa kufanyika katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma.
Alisema juzi walipokea taarifa kutoka kwa Uongozi wa Chadema Mkoa wa Dodoma, juu ya kufanya maandamano ya amani kuanzia viwanja vya Nyerere Square hadi viwanja vya Bunge kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana.
Alisema taarifa ya maandamano kama hayo, yanayotarajia kufanyika katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma, ilitolewa jana ambapo ni muda ulio kinyume na sheria ya kutoa taarifa za maandamano ndani ya saa 48.
Alisema katika barua ya chama hicho kwenda kwa Jeshi la Polisi, viongozi wa Chadema  wa Mkoa huo, walisema wanapinga Bunge la Katiba  na wanataka kupaza sauti zao, zisikike dunia nzima na walisisitiza kufanya maandamano hayo leo.
“Walikuja hapa viongozi wa Chadema Mkoa, tulikaa nao kwenye mazungumzo zaidi ya saa mbili, tuliwaambia Bunge lipo kwa mujibu wa sheria za nchi na hakuna mahakama iliyotamka Bunge lisitishwe, lakini walisisitiza kuwa maandamano yako pale pale,” alisema.
“Maandamano hayo ni batili yanapinga chombo ambacho kipo kwa mujibu wa sheria, tunasisitiza wananchi wa Dodoma wasishiriki maandamano hayo, hayana tija hata kidogo na wananchi wasijitokeze waendelee na shughuli zao,” alisema.
Alisema maandamano ni haki ya kikatiba, lakini wanatakiwa kufuata sheria. Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kudhibiti maandamano hayo katika wilaya zote, kutokana na viongozi wa Chadema kukaidi amri ya kutaka kusitisha maandamano hayo.
Wakati jeshi la Polisi likichukua hatua hiyo, Umoja wa Vijana Wazalendo wa Vyuo vya Elimu ya Juu Dar es Salaam, nao umejitokeza na kulaani kauli zilizotolewa na Mbowe za kuhamasisha maandamano na migomo nchi nzima, hata kama jeshi la Polisi halitabariki kufanyika kwa mambo hayo.
Mwenyekiti wa Umoja huo, Mussa Omar anayesoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), alisema umoja huo ni Muungano wa vyuo 14 vya elimu  ya juu vilivyopo Dar es Salaam.
Alisema Watanzania wengi wamekerwa na kusononeshwa na kauli ya kiongozi huyo ya kuhamasisha maandamano, alizozitoa wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chadema, mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Tumemsikia akiahidi maandamano bila kikomo kwa kibali cha polisi au bila kibali cha polisi mbele ya wajumbe na wageni ambao wengine sio Watanzania,” alisema Omar.
Aliongeza kuwa kauli kama hiyo, haiwezi kusemwa hata na Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.
Alimtaka Mbowe afahamu dhamana kubwa ya uongozi aliyonayo kwa wafuasi wake na Watanzania kwa ujumla, wakimtaka afuate misingi ya sheria za nchi, katiba na utawala bora.
Pia, alisema kauli zilizotolewa na Mbowe, hazibebeki na mtu yeyote katika taifa hili, kwani alitoa kauli mbaya kuliko zote kisiasa, ambazo zimewahi kusemwa majukwaani.
“Watanzania tukikaa bila kuzilaani na kuzikemea kauli zake tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe na pia hatuvitendei haki vizazi vijzvyo vya nchi yetu,” aliongeza.
Alihoji uhalali wa kutoa amri hizo kwa wafuasi wake, ilhali ni kiongozi tu wa chama, tena ambacho hakiko madarakani.
Alisema Watanzania wanapaswa kuwakataa viongozi wenye jazba na kutumia mabavu katika kutimiza majukumu yao, kwani wanaweza kuiingiza nchi katika vurugu zisizo na ulazima.
Pia alivitaka vyombo vya dola, visizivumilie kauli kama hizo, zilizotolewa na Mbowe, kwani vyombo vya dola vina dhamana ya kulinda, kutunza na kuendeleza amani na utulivu wa nchini, wachukue hatua kali za kisheria kwa kauli ya kutishia uvunjifu wa amani kabla hajaingiza nchi kwenye machafuko ya kisiasa.
Wakati huo huo, viongozi wa juu wa chama hicho, leo wamepanga kumsindikiza Mbowe kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini, ambako ameitwa kwa barua.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema Mbowe alipokea barua, ikimtaka afike Makako Makuu ya jeshi hilo leo saa 5:00 asubuhi.
“Mwenyekiti wetu ameitwa Makao Makuu ya Polisi leo na hatujui kaitiwa nini, huenda anakwenda kuhojiwa na huenda mwito huo umetokana na kauli  alizotoa awali katika mkutano mkuu, ambazo zililenga kuhamasisha maandamano ya nchi nzima kupinga Bunge la Katiba linaloendelea”, alisema Dk Slaa.
Alitaja watakaoongoza msafara wa amani wa kumsindikiza Mbowe kuwa ni  mwanasheria wao, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Profesa Abdallah Safari na Mwanasheria Peter
Kibatala.
Hata hivyo, alisema pamoja na kiongozi huyo kuitwa na polisi, bado jeshi hilo haliwezi kuvunja ajenda ya kuandamana, kwa kuwa ilipitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, na kwamba polisi wao wanapaswa kutoa kibali cha kuruhusu maandamano hayo.
Awali, alisema maazimio yaliyopitishwa na  Kamati Kuu ya chama hicho ni kuunganisha nguvu ya pamoja na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) .
Alisema maazimio hayo, yataanza Desemba 14, mwaka huu, siku ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa unaanza.
Alieleza kwamba chama hicho kimeunda kamati ya watu watano, itakayoangalia jinsi ushirikiano wa Ukawa utakavyokuwa kwenye uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutoka kwao nje bungeni, kulikuwa sahihi. Alisema katiba mpya, haiwezi kupatikana leo au kesho.

ASKARI WA DORIA WASHAMBULIWA KWA BOMU SONGEA


Siku chache baada ya majambazi kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Bukombe mkoani Geita, kuua askari wawili na kuiba silaha za moto, watu wasiofahamika wamewajeruhi askari watatu waliokuwa doria kwa kuwarushia kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu.
Askari hao kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea wakitibiwa majeraha.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa moja na nusu jioni katika kata ya Msufini karibu na daraja la Matarawe, wilayani Songea.
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa tukio hilo, ingawa alishindwa kuingia kwa undani akisema alikuwa njiani kwenda eneo la tukio akitokea mkoani Mbeya.
Hata hivyo, mwandishi ameweza kubaini waliojeruhiwa kuwa ni WP. 10399 PC Felista aliyejeruhiwa mguu wa kulia  kwenye unyayo na pajani, G 7351 PC Ramadhani aliyejeruhiwa mguu wa kulia karibu na goti na tumboni upande wa kulia na G. 5515 PC John aliyepata majeraha katika mguu wa kulia chini ya goti na jeraha dogo tumboni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Daniel Malekela, akizungumzia tukio hilo alikiri kupokea majeruhi na kueleza kuwa ametoa vipande vya bati na misumari katika majeraha ya askari hao na mpaka sasa wanaendelea na matibabu.
Habari zaidi zinasema jeshi la polisi mkoani humo kwa kushirikiana na maofisa wengine kutoka makao makuu ya jeshi, wanaendelea na uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kujua chanzo cha tukio hilo. Bomu hilo la kutupwa kwa mkono inasadikiwa limetengenezwa kienyeji.
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho cha wahalifu kujeruhi askari kwa makusudi na amesema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama itahakikisha wanawasaka na kuwakamata.

WAFA KATIKA AJALI WAKITOKA KUZIKA MWENZAO MUSOMA


Watu wawili wamekufa na wengine watano kujeruhiwa baada ya magari mawili, likiwamo basi dogo la abiria walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la mafuta.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Athuman Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilihusisha gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa linatokea kwenye msiba Musoma mkoani Mara kwenda Dar es Salaam na kugongana na lori la mafuta.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi maeneo ya Ubena Senge katika barabara ya Morogoro, chanzo kikitajwa kuwa ni uzembe wa gari dogo aliyehama upande wake kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni uchovu wa safari ndefu.
Alisema basi dogo lenye namba za usajili namba T 663 BKP lililokuwa likiendeshwa na Ally Abdul (34), likiwa na abiria 20 liligongana na lori la mafuta aina ya Leyland Daf lenye namba za usajili T 858 CLK na tela namba T 421 CKY, mali ya kampuni ya Ramader ya Dar es Salaam ambalo dereva wake ametajwa kwa jina moja la Rashid.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni Neema Mile (39) na Jane Mtani (38) ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi ambako pia majeruhi wamelazwa.

MTUHUMIWA KESI YA UGAIDI ALALAMIKIA POLISI


Mtuhumiwa katika kesi ya ugaidi, Abdallah Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kumruhusu kutohudhuria siku za kesi na abaki magereza, kutokana na maumivu makali anayodai anayapata sehemu za siri alikominywa na polisi na kuingiziwa mti kwenye haja kubwa.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata maumivu makali sana sehemu za siri kunauma kwa sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,” alisema.
Alisema mbele ya Wakili wa Serikali, Rose Sulle kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri, pia mguu wake uliokatwa hospitalini, bado unamsumbua kutokana na maumivu.
Maginga pia aliomba iagize Magereza wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5 mwaka huu, ila alizuiwa hadi sasa.
Akijibu hoja hizo, Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devotha Msofe, alisema  suala la kuja mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia, alimshauri mshitakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi, amweleze hakimu anayesikiliza kesi yake, Mustapher Siyani ambaye kwa siku hiyo hakuwepo.
“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza ndio mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa  hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi, ambapo Sheria Namba 22  ya Mwaka 2002 inasema upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo, pia wanahusishwa na  tukio la  mlipuko wa bomu lilitokea baa ya  Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.
Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajab Hemedi, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yassin Sanga, Shaaban Wawa, Swaleh Hamisi, Abdallah Yassin, Abdallah Maginga na Sudi Nassib Lusuma. Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaaban Mussa, Athuman Hussein, Mohammed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohammed na Said Michael Temba.

MWANAFUNZI AJIUA KWA KULAZWA HOSPITALINI


Katika hali isiyotarajiwa, mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Ezra Gerald (19), amejinyonga hadi kufa kwa kutumia shuka ya hospitali, alikokuwa amelazwa kwa kile kinachoeleza alikuwa anasumbuliwa na homa ya matumbo.
Hata hivyo, ujumbe ulioachwa na marehemu huyo unaonesha alichukua uamuzi huo, kutokana na kuchukizwa na uamuzi wa daktari aliyemhudumia wa kumlaza ili atibiwe ugonjwa ambao hakuwa anaumwa.
Aidha, katika ujumbe huo imeelezwa alichukizwa na kitendo cha kupotezewa muda hospitalini wakati wenzake wakiendelea na masomo.
Tukio hilo limethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Gilles Muroto aliyesema mwanafunzi huo alijinyonga Septemba 16 mwaka huu saa moja asubuhi.
Alisema mwili wake uligundulika ukining’inia kwenye mti uliopo maeneo ya hospitali hiyo na alipopekuliwa katika mifuko ya suruali yake, zilionekana karatasi mbili, moja ikiwa na ujumbe uliosomeka; “Haiwezekani binadamu kuhudumiwa kama mbwa, yaani nafika hospitali najieleza hali yangu halafu daktari ananiandikia kulazwa bila kupima, sasa sijui wanatibu nini?
“Kwa kweli siwezi kuvumilia wenzangu wanasoma halafu mimi nimekalishwa tu hapa hospitali bila kujua wananitibu nini, inaniuma sana mpaka nafikia hatua hii ya kujiondoa duniani kwa sababu naona watu wanachezea ndoto zangu, mimi siwezi kuona ndoto yangu inazimwa wakati natakiwa niwepo shuleni nikamilishe ndoto zangu “mjitahidi tukutane mbinguni “Respect My Family and Brother Henry.”
Kamanda Muroto amesema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, lakini polisi wanaendelea na uchunguzi.
Inaelezwa mwanafunzi huyo aliyetajwa kuwa ni mwenyeji wa mkoa wa Tabora, alilazwa hospitalini hapo tangu Septemba 11 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera, Benges Justus, tukio hilo lilitokea Septemba 16, mwaka huu, siku moja baada ya mgonjwa huyo kulazwa.
Alisema baada ya mwanafunzi huyo kupokelewa hospitalini hapo, alifanyiwa vipimo vyote vya kitabibu na kugundulika anasumbuliwa na malaria, ndipo akaanzishiwa tiba ya ugonjwa huo.

PINGAMIZI LA MWANASHERIA MKUU DHIDI YA TLS LATUPILIWA MBALI

Pingamizi la Mwanasheria Mkuu (AG) dhidi ya ombi la kibali cha kufungua kesi ya kupinga vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mkoani Dodoma limetupiliwa mbali katika
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Pingamizi hilo lilikuwa la kupinga ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) waliofungua kesi ya kikatiba wakiomba mahakama itoe zuio la kuendelea kwa vikao vya Bunge maalumu la katiba hadi kesi hiyo itakapokwisha.
Aidha, wanaomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) awasilishe bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 8 ya mwaka 2011 na namba 2 ya
mwaka 2012, sura ya 83 na ifafanue kifungu cha 25 cha sheria hiyo. 
 Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la majaji watatu wanaosikiliza ombi hilo wakiongozwa na Jaji Augustine Mwarija, Dk Fauz Twaib na Aloyisius Mujulizi.
Wakati huo huo, kesi nyingine ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Saidi Kubenea akihoji mamlaka ya Bunge hilo inaanza kusikilizwa leo ambapo ilitakiwa ianze kusikilizwa jana lakini AG aliwasilisha pingamizi ambalo pia litaendelea kusikilizwa leo.
Katika kesi hiyo, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba, kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Mbadiliko ya Katiba namba 83 ya mwaka 2011.
Aidha, anaiomba mahakama itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.

YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO ALHAMISI - SEPTEMBA 18

WATAKA MFUKO WA NHIF UGHARIMIE NAULI ZA WAGONJWA


Baadhi ya wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wametaka kuongezwa kwa huduma za malipo ya nauli na posho kwa wanachama wanaokwenda kwenye matibabu ya rufaa nje ya vituo vyao, sambamba na kugharamia upimaji wa vinasaba (DNA).
Walisema hayo walipozungumza wakati wa kikao cha pamoja baina ya wanachama wa mfuko huo katika kijiji cha Mwamgongo, Kigoma Vijijini mkoani hapa na viongozi wa mkoa wa mfuko huo.
Walisema kuwa ni vizuri wanachama wanaokwenda kupata matibabu ya rufaa,  wagharamiwe nauli na posho na mfuko huo.
Nassib Ally, mtumishi katika Kituo cha Afya cha Mwamgongo, alisema licha ya sasa malipo ya nauli na posho za safari kulipwa na mwajiri, lakini wakati mwingine malipo hayo hayalipwi kwa wakati.
Alisema hali hiyo huwafanya wanachama kuhangaika kufuatilia matibabu ya rufaa nje ya vituo vyao vya kazi.
Mussa Boniface, mwalimu wa Shule ya Msingi Mwamgongo, alitaka mfuko kugharamia huduma za upimaji wa DNA na kugharamia huduma za matibabu ya nje ya nchi kwa wanachama wake.
Akizungumzia maombi hayo, Meneja wa NHIF mkoa wa Kigoma, Elius Odhiambo alisema kwa sasa mfuko haugharamii malipo ya posho na nauli kwa wanachama wake, wanaokwenda rufaa nje ya vituo vya kazi. Alieleza kwamba suala hilo litabaki kuwa juu ya mwajiri.
Odhiambo alisema kitendo cha kugharamia posho na nauli kwa wanachama, itawalazimu wanachama hao kuchangia zaidi.
Alieleza kwamba suala hilo linahitaji mjadala mrefu ambao utaridhiwa na wanachama wote kuweza kutekeleza hilo.
Meneja huyo pia alisema suala la maombi ya mfuko kugharamia matibabu ya nje ya nchi, litabaki chini ya wizara ya afya huku upimaji wa vinasaba ukiendelea kuwa gharama za mtu binafsi.

MBIO ZA MWENGE KUZINDUA MIRADI 72 MKOANI MWANZA


Miradi 72 ya maendeleo ya Sh bil. 23 inatarajiwa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru, utakaokimbizwa kwa siku nane mkoani hapa, ambao utapokelewa leo kutoka mkoa wa Simiyu.
Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo wakati akitoa taarifa ya mwenge huo, iliyosomwa kwa niaba yake na Mratibu wa Mbio za mwenge mkoani hapa, Diana Rwechungura.
Alisema thamani hiyo inatokana na michango ya wananchi inayofikia zaidi ya Sh bil. 2.9, Serikali Kuu Sh bil. 9.5, michango ya halmashauri Sh bil. 2.3 na michango ya wahisani Sh bil. 8.1.
Alisema miradi itakayozinduliwa katika mbio za Mwenge ni ya sekta za afya, kilimo, ufugaji, maji na hifadhi ya mazingira.
Alisema ujumbe wa mwaka huu wa Mwenge huo unasema ‘Katiba ni sheria kuu ya nchi, jitokeze kupiga kura ya maoni tupate Katiba mpya’, ambao utaandamana na kaulimbiu za kudumu za mapambano dhidi ya Ukimwi, rushwa, malaria na vita dhidi ya dawa za kulevya.

UTALII WACHANGIA SHILINGI TRILIONI 3 KWENYE PATO LA TAIFA


Sekta ya Utalii nchini imekuwa ikichangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa mwaka jana ilichangia dola bilioni 1.8 (Sh trilioni 3) katika pato hilo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Onesho la Kimataifa la Utalii (SITE).
Alisema sekta hiyo imekuwa na mchango mkubwa. Alisema kutokana na ukuaji wake, wameamua kuanzisha onesho hilo, ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka.
“Kwa mwaka huu maonesho hilo kubwa la kimataifa litafanyika kuanzia Oktoba mosi hadi nne ambapo watakuwepo wageni kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kutangaza utalii,” alisema.
Alisema katika kufanikisha maonesho hayo, wamewashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo TANAPA, Hifadhi ya Ngorongoro, Kampuni ya ndege ya Ethiopia, makampuni na mashirika mengine, ambapo TTB imechangia Sh milioni 500 katika maandalizi hayo.
Alitoa mwito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza utalii wa ndani na kujivunia vivutio vilivyopo na kutafuta soko kupitia wadau  walioalikwa katika maonesho hayo.
Mratibu Mkuu wa maonesho hayo, Philip Chitaunga alisema lengo la maonesho hayo ni kuwakutanisha watanzania na masoko ya nje na pia watawaleta wadau mbalimbali wanaoandika habari za utalii na wadau wenye makampuni ya watalii.
Wageni hao pia watapata fursa ya kufanya ziara kwenye vivutio mbalimbali, ikiwemo Zanzibar na Ngorongoro, ambapo kwa watanzania itakuwa ni fursa kwa wenye makampuni ya watalii kujitangaza na kutafuta soko.

WABUNIFU WA MAJENGO KUKUTANA LEO DAR


Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,  Ali Hassan Mwinyi, leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 22 wa wataalamu wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi utakaofanyika kwa siku moja jijini Dar es Salaam.
Mbali na Mwinyi, alisema pia atakuwemo Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msajili wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Jehad Abdallah Jehad, alisema mkutano huo utakaohudhuriwa na washiriki wapatao 400, mada kuu itakuwa sheria ya manunuzi namba 7 ya mwaka 2011 na athari zake katika mazingira ya ujenzi.
Mwenyekiti wa AQRB, Ambwene Mwakyusa alisema mategemeo yao ya baadaye katika mashindano hayo ni kuendelea kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi hususani taaluma za ubunifu na ukadiriaji majenzi ili kukidhi pengo la upungufu uliopo ambapo hadi kufika mwaka 2025 wanataka kuwa na wataalamu wa aina hiyo walau 6,500 kutoka 1,000 waliopo sasa.

HAWA NDIO WATAKAOCHEZESHA MECHI ZA LIGI KUU YA VODACOM


Ikiwa imebaki siku moja kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014-15, mambo tayari yamenoga baada ya kukamilika kwa safu ya waamuzi watakaochezesha mechi za ufunguzi wiki hii.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Silas Mwakibinga aliliambia gazeti hili jana, orodha ya waamuzi iko tayari na kuwataka watakaochezesha katika michezo hiyo kutenda haki.
Katika mchezo wa Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar ya Mvomero, Morogoro, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri itachezeshwa na mwamuzi Dominick Nyamisano kutoka Dodoma.
Wakati huo, mabingwa watetezi, Azam FC itakuwa mwenyeji wa Polisi ya Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo utakaochezeshwa na mwamuzi Abdallah Kambuzi kutoka Shinyanga.
Mwamuzi wa Dar es Salaam, Hashim Abdallah atakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga kuziamua timu mbili ngeni katika ligi msimu huu, wenyeji Stand United na Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Mgambo JKT ya Tanga dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Kennedy Mapunda wa Dar es Salaam.
Aidha, Ruvu Shooting ya Pwani itacheza na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi na kuchezeshwa na mwamuzi David Paulo wa Mtwara.
Washindi wa tatu wa ligi hiyo msimu uliopita, Mbeya City itawakaribisha JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika mchezo utakaochezeshwa na Mohamed Theophil wa Morogoro.
Baada ya michezo hiyo ya Jumamosi katika mchezo wa Jumapili, Simba watakuwa ni wenyeji wa Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na mwamuzi Jacob Adongo wa Mara atachezesha.
Kwa mujibu wa Mwakibinga, waamuzi hao wa kati ni miongoni mwa waamuzi wa kati 21 watakaochezesha ligi hiyo iliyopangwa kufikia tamati Aprili 18, mwakani. Kutakuwa na waamuzi wasaidizi 46.
Mwakibinga alisema anategemea waamuzi hao watachezesha mchezo huo kwa kufuata sheria 17 za soka bila kupendelea na kwa haki.
“Hiyo ndio orodha ya kwanza, kuna nyingine itatoka kwani wapo wengi, na wasaidizi wao tayari, tuna imani watazingatia maadili ya kazi yao,” alisema Mwakibinga.

Thursday, September 11, 2014

RASIMU YA KATIBA MPYA KUPIGIWA KURA SEPTEMBA 21

Wakati kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) likishinikiza Bunge Maalumu la Katiba lisitishwe haraka iwezekanavyo, Bunge hilo limejiandaa kuwasilisha Katiba inayopendekezwa Septemba 21.
Hatua hiyo ya Bunge Maalumu, inalenga kuwapa fursa wajumbe wa bunge hilo, kuipigia kura Katiba hiyo. 
Spika wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema hayo jana. Aliongeza kuwa hatua hiyo itadhihirisha kuwa kazi waliyopewa na taifa ya kuandika Katiba mpya, itakuwa imekamilika.
Hatua hiyo ya Bunge kufupisha ratiba zake, inatokana na uamuzi wa Serikali kuwa shughuli zote za bunge hilo, ziwe zimekoma ifikapo Oktoba 4 mwaka huu na sio Oktoba 31. 
Sitta abainisha kuwa majadiliano ndani ya Bunge hilo yatakamilika kesho kutwa Jumamosi na kuanzia Jumatatu ijayo kamati ya uandishi wa katiba, itaendelea na kazi yake ambayo wataifanya kwa wiki moja na baada ya  hapo watawasilisha rasimu  Septemba 21.
Ratiba inafafanua kuwa baada ya katiba inayopendekezwa kuwasilishwa, wabunge wataipitia kabla ya kuanza kupiga kura Septemba 26 mwaka huu.
 “Nafurahi kuwaambia kwamba jana katika kikao cha kamati ya uongozi, tumedhihirisha kwamba tunakwenda vizuri na kamati ya uandishi, ambayo imekuwa ikitazama mambo yanavyokwenda na mjadala ulivyoanza jana, tumejipanga kutupa rasimu ya mwisho tarehe 21 mwezi huu.
“Kwa hiyo ni dhahiri kabisa kwamba lengo tulilopewa na taifa la kutoa katiba inayopendekezwa tutalimudu ndani ya wakati huo,” alisema Sitta. 
Sitta alisema kwa sasa uongozi wa Bunge hilo, unaangalia utaratibu wa kupiga kura  kwa wale ambao wako nje ya Bunge kwa sababu mbalimbali ukiacha wale ambao walisusa hasa wale ambao wako hospitali, ambao kanuni zinawaongoza utakapofika wakati wa kupiga kura, waandaliwe utaratibu wa kufanya hivyo.
Alisema wanafanya hivyo, kwa sababu akidi inahusu wabunge wote, ambao waliteuliwa na  rais kuwa wajumbe wa Bunge hilo na wajumbe wengine ambao wameingia kwa nyadhifa zao.
Upigaji kura huo, pia utawahusisha wajumbe wa Bunge hilo ambao watakuwa safari nje ya nchi. Baadhi ya wajumbe wanaenda Hijja huko Mecca, Saudi Arabia.
Katika kuhakikisha kuwa wajumbe wengi wanachangia ndani ya muda ambao wamepewa, uongozi wa Bunge hilo ulitoa mwongozo wa namna ya kuchangia na Sitta aliwataka wajumbe kuhakikisha wanafuata muongozo huo ili kuokoa wakati.
“Jana kidogo tuliongelea lakini leo mtaona kuna muongozo tumeugawa, kila mmoja ahakikishe anao kwa sababu kiti kitaangalia tunakaa ndani ya muongozo huo, kwa leo nadhani na kesho kwa sababu  mjadala tuukamilishe kufikia siku ya Jumamosi hii inayokuja, kwa hiyo tutakuwa tunagawa miongozo hii kuwawezesha waheshimiwa wajumbe kujua tunalenga wapi,” alisema Sitta.
Mwongozo alioutoa jana ulihusu Sura ya 2,3,4,5  ambao uliandaliwa na sekretarieti. Alisema mwongozo huo ni  muhtsari wa maoni, ambayo yalitoka ndani ya kamati zote 12. Alisema kwa hali hiyo mwenendo huo, hautaruhusu kuibua upya mjadala uliokuwapo ndani ya kamati.
Sitta alifafanua kuwa kuna masuala mbalimbali ambayo rasimu ilisema na muhtasari kamati zilijielekeza na kufikia muafaka na sehemu hawakufikia muafaka. Aliwakumbusha wajumbe hao kuwa ni kazi yao sasa kuboresha yale yaliyopo  kwenye mwongozo huo.
Sitta alisema kuhusu mambo ya imani ya dini, kamati kadhaa zilisema ibara hiyo ibaki kama ilivyo kwenye rasimu ya katiba  na nyingine zikaongezea  kwamba uwepo utaratibu wa kutambua na kuruhusu sheria na vyombo vya dini, kutambuliwa kisheria.
“Sasa mjadala wa jana ulifikia mahali kwamba kidogo uharibu mambo kwa sababu tumerejea tena kuidai mahakama ya kadhi ndani ya katiba na wengine wanasema ndivyo ilivyo Uganda wakati sio kweli, Zanzibar sio kweli mahakama kama hiyo inatambuliwa ndani ya sheria, sio lazima ndani ya katiba.
 “Tunachotunga hapa ni kuandika katiba, sio sheria na kwa suala hili  hapa kwa Tanzania Bara Kamati ya Pamoja ambayo inasimamiwa na waziri mkuu imekuwa ikilishughulikia ili lifike mwisho wake, kwa hiyo kulirejea  tena na kusema kwamba ni jambo ambalo linazungumzwa ndani ya katiba sio sahihi,” alisema Sitta.
Kwa hali hiyo aliwaomba wajumbe, kuhakikisha kuwa hawarudii tena yale waliyoyajadili kwenye kamati. Alisema kama hoja ilishindikana na ikawekwa pembeni, kutokana na wajumbe kutofikia muafaka fulani; sio wakati wa kurejesha jambo hilo ndani ya Bunge, kwani kufanya hivyo ni kuanzisha upya mjadala  wakati kazi yao kwa sasa ni kuboresha kile ambacho kinaweza kuleta muafaka.
Kutokana na msimamo huo wa Sitta, baadhi ya wajumbe walimpinga na mjumbe wa kwanza kufanya hivyo, alikuwa ni Ezekiah Oluoch aliyetaka apewe mwongozo, kwa sababu kuna kifungu cha kanuni  kinachotoa fursa kwa mjumbe yeyote wakati wa mjadala, kuwasilisha marekebisho na maboresho au mabadiliko, ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo hayabadilishi msingi au maana.
“Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti tukiendelea tu na haya ambayo yamewekwa na kamati na tusiongezee vingine, tutakuwa na shida kwa sababu tayari ulishapokea malalamiko kwamba baadhi ya kamati hawakuweka hata vile  vifungu, ambavyo vilikuwa vimekubalika, kwa hiyo nilikuwa naomba nipate muongozo kwamba kwa nini hiyo haki mjumbe asiitumie iliyopo kwenye rasimu na badala yake tutumie muongozo tuliogaiwa  asubuhi ya leo?” alihoji Oluoch.
Akijibu hoja hiyo, Sitta alisema hilo ni jambo ambalo lipo wazi. Alionya kuwa taratibu wa kuleta mabadiliko ni kitu kimoja, ambacho kitafumbua mjadala upya.
Alisema mjadala huo ni kitu kingine na mambo yaliyokuwa ndani ya kamati ni kitu kingine. Alisema yeye anajielekeza kwenye hilo la pili kuanzisha mjadala,  ambao tayari kwenye kamati walishazungumza.
Mwenyekiti huyo alisema fursa za kuleta mabadiliko kwa maandishi, zinabaki palepale na hata hatua ya kusoma ile rasimu kamili kuanzia ibara ya kwanza hadi ya mwisho, ipo pale pale kwa mjumbe kuweza kupeleka pendekezo la mabadiliko ambalo linaweza kupigiwa  kura. 
“Kwa hiyo mimi sioni kama hayo mambo mawili yanapishana, hata kidogo, kuna kanuni za mjadala ambazo lazima tuzizingatie, hatuwezi kurudia kazi tulizofanya kwenye kamati kwa takribani wiki tatu tukairejesha kwenye mjadala, lakini kuleta mapendekezo ya mabadiliko inaruhusiwa,” alisema.
Waziri katika ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya alionya kuwa wajumbe walioko nje ya Bunge, ambao wanatarajia kuwa kuna katiba nyingine itaandikwa baada ya mwaka 2015, wamechelewa.
Alisema propaganda wanayoiendesha nje ya Bunge hilo  kuwa mchakato huo utaanza upya, hauna tija. Aliwahakikishia wananchi kuwa wajumbe wa bunge hilo, wamefanya kazi kwa weledi mkubwa na watawapatia wananchi katiba mpya.
Wakati huo huo,  viongozi wa Ukawa waliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam  jana na kuendelea kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete, atoe agizo mara moja la kusitishwa kwa vikao vinavyoendelea vya Bunge Maalum la Katiba.
Aidha umoja huo umependekeza katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, ifanyiwe marekebisho na kuwekwa kipengele kitakachotoa amri kwa utawala ujao, kuhakikisha unamalizia mchakato wa Katiba uliositishwa kwa kuendelea na hatua ya Bunge la Katiba.
Mwenyekiti Mwenza wa umoja huo, James Mbatia alisema katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni kati yao na Rais Kikwete, walikubaliana mchakato huo wa Katiba kwa sasa usitishwe.
“Tumeshakubaliana kimsingi kwamba mchakato huu wa Katiba hautaweza kufikia hatua ya mwisho kwa wakati huu ya uchaguzi, muda umekwenda sana na makubaliano hayo tumetiliana saini wote hadi wenzetu wa CCM, ila tunashangaa kwanini Bunge hilo hadi sasa linaendelea tena hadi Oktoba 4, haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma,” alisisitiza Mbatia.
Alisema katika makubaliano waliyoyafikia kwenye vikao hivyo, vilivyofanyika Agosti 31 na Septemba 8, mwaka huu, yalizingatia maoni ya wadau na kukubaliana kwa pamoja kuahirisha mchakato wa katiba ili kupisha maandalizi ya Bunge la kawaida.
“Hata hivyo, pamoja na makubaliano haya, sisi kama Ukawa msimamo wetu ni Bunge linaloendelea la Katiba lisitishwe ili tuanze kufanyia marekebisho Katiba ya sasa tuweze kufanya uchaguzi kwa maridhiano na amani,” alisema.
Alimpongeza Rais Kikwete kwa kuchukua uamuzi wa kukubali kukutana na umoja huo kwa mashauriano  hadi kufanikisha, hatua hiyo aliyoiita nzuri ya kuwezesha kupata muafaka wenye maslahi mapana kwa taifa, kuhusu suala la katiba na uchaguzi.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alimtaka Sitta kuacha kutumia vibaya fedha za umma na kusitisha mara moja Bunge hilo, vinginevyo kukitokea machafuko au vurugu zinazotokana na mchakato huo wa Katiba atalaumiwa yeye.
Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo kutoka CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema katika marekebisho ya 15 ya Katiba ya sasa, walichopendekeza ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, kuweka mgombea huru, Rais kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 50 na matokeo ya Urais kuhojiwa mahakamani.
Mwenyekiti wa Chadema na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, wakati akifungua uchaguzi wa Baraza la Vijana wa chama hicho Dar es Salaam jana, alisisitiza juu ya Bunge hilo kusitishwa mara moja kabla ya Oktoba 4, mwaka huu, vinginevyo wataingia barabarani.