Saturday, May 31, 2014

BREAKING NEWS!! GEORGE TYSON AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI



Mwongozaji filamu wa siku nyingi nchini na Prodyuza wa kipindi cha runinga cha The Mboni Show, George Tyson (39) amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea jana jioni wakati yeye na wenzake wengine saba wakitokea mjini Dodoma kikazi.
 Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, SACP David Misime, ajali hiyo ilitokea kwenye Kijiji cha Silwa, katika Barabara ya Dodoma – Morogoro majira ya Saa 12:45 jioni ambapo chanzo cha ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda huyo ni mwendo kazi wa gari hilo.
Marehemu Tyson na wenzake walikuwa wakisafiri kwenye gari namba T150 CWA aina ya Toyota Granvia Station Wagon kutoka Dodoma walikokwenda kwa ajili ya shughuli ya kukabidhi madawati kwa shule ya Msingi Chaula ya mjini Dodoma.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Mgeni Shemakame (29) mkazi wa Mburahati, Dar es Salaam ambaye amejeruhiwa, lilipata ajali hiyo iliyokatisha maisha ya Tyson ikiwa ni masaa manne tu tangu waanze safari ya kurejea jijini Dar es Salaam.
Marehemu George Tyson alitamba sana kwenye ulimwengu wa filamu akiwa na kikundi cha Mambo Hayo ambapo alishiriki kikamilifu kwenye uaandaji wa michezo ya kuigiza ya kwenye runinga iliyokuwa ikirushwa na kituo cha televisheni cha ITV.
Marehemu aliwahi kufunga ndoa na mwigizaji maarufu wa kike nchini, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ kabla ya kutengana miaka kadhaa iliyopita.
Baadaye, Tyson akajiunga na mwanadada Mboni Masimba katika kuandaa kipindi cha runinga cha Mboni Talk Show ambacho amekitumikia mpaka mauti yalipomfika.
Mungu ailaze roho ya marehemu George Tyson mahali pema peponi, Amina.

YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI - MEI 31

Dokta Mwaka Juma akisamiliana na Samia Othman na Zainab Aziz wakati alipotembelea ofisi za Makao Makuu ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) jijini Bonn, Ujerumani jana. Dk Mwaka ambaye ni mtaalamu wa tiba asilia kutoka Tanzania yuko nchini humo kwa ziara ya mafunzo kwenye taasisi mbalimbali za tiba yenye lengo la kustawisha tiba mbadala kwa afya.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akizungumza na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara jana jioni wakati wa ziara yake kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akirejesha fomu za kugombea tena nafasi hiyo kwa Katibu wa CUF Wilaya ya Magharibi, Juma Rajab, katika ofisi za chama hicho Wilaya ya Magharibi, Kilimahewa mjini Unguja.

Baadhi ya wasanii watakaotoa burudani katika Tamasha ya Kili Music Tour litakalofanyika leo jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Tamasha hilo ni moja kati ya kumi yanayotarajiwa kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini chini ya udhamini wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager.

'MTOTO WA BOKSI' BADO APUMUA KWA MSAADA WA MASHINE MUHIMBILI


Mtoto wa miaka minne aliyekuwa amefichwa kwenye boksi mkoani Morogoro, bado anaendelea kutumia mashine ya kupumua baada ya kushindwa kupumua vizuri. 
Hali hiyo imesababishwa na maradhi ya kichomi yanayomsumbua.
Akizungumza na mwandishi, jana jijini Dar es Salaam, mama mlezi aliyekabidhiwa jukumu hilo Josephina Joel alisema, hali ya mtoto huyo ilibadilika Mei 21 jioni, hali iliyowafanya madaktari waliokuwa zamu kumsaidia kwa kumuwekea mashine ili aweze kupumua.
Alisema hali yake hivi sasa sio mbaya, ingawa anatumia mashine kumsaidia kupumua, lakini pia bado anaendelea na tiba ya awali ya lishe ambayo anaipata katika wodi aliyolazwa ya Makuti B, ya watoto wenye utapiamlo.
“Tulihamishiwa hapa juzi jioni, baada ya baadhi ya majibu ya vipimo vya awali kutoka ambapo yanaonesha mtoto hali yake kilishe ni  duni, hivyo tukaletwa hapa ili apatiwe lishe na wataalamu, na ameshaanza kupewa,” alisema Josephina.
Hivi sasa mtoto huyo ameanzishiwa lishe ya maziwa peke yake ambapo kila baada ya saa mbili hupewa maziwa hayo na kwamba hicho kwa sasa ndicho chakula chake hadi wataalamu hao watakavyoelekeza vingine.

Josephina aliongeza, maziwa hayo kwa mujibu wa wataalamu wa afya na lishe yana virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika kutibu tatizo la utapiamlo mkali unaomkabili mtoto huyo.
Akizungumzia hatua walizofanya hadi sasa, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto hospitalimi hapo, Dk Mwajuma Ahmada alisema walichofanywa kwanza ni kumhamishia kwenye wodi hiyo ya watoto wenye utapiamlo, ambapo wapo wataalamu wa lishe wanamhudumia.
Kuhusu majibu ya awali ya damu, mama mlezi  wa mtoto huyo alisema majibu ni mazuri na kwamba jana , watamfanyia kipimo cha kumulikwa mwili wote na mashine kwa uchunguzi zaidi.
Mtoto huyo aliibuliwa na majirani waliotoa taarifa katika ofisi ya serikali ya mtaa eneo la Azimio, Morogoro baada ya kuhisi kwamba kuna sauti ya mtoto ndani ambaye hawajawahi kumuona katika familia ya mpangaji  Mariam Saidi na mumewe, Mtonga Ramadhan.
Baada ya mtoto huyo kuibuliwa akiwa katika hali ya uchafu alipelekwa hospitali ya mkoa ya Morogoro kwa ajili ya uchugnuzi wa afya yake, huyo watuhumiwa wa ukatili dhidi ya mtoto huyo, akiwemo baba mzazi Rashidi Mvungi, na  walezi hao, wakishikiliwa na hatimaye kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu mashtaka yanayowakabili ya ukatili.
Imadaiwa mama  mzazi wa mtoto huyo alifariki mtoto akiwa na umri wa miezi tisa na hivyo dada wa marehemu akakubali jukumu la kumlea mtoto huyo.

WAZIRI ASEMA BAJETI NISHATI NA MADINI NI YA UPENDO NA UPOLE


Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini imetajwa kuwa ya upendo na ya masikini, huku ikionesha mafanikio makubwa ikiwamo kuvuka lengo la kuwapatia umeme Watanzania wengi kabla ya muda uliowekwa na kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo. 
Aidha, Waziri Profesa Sospeter Muhongo amesema hakuna kushindwa wala kukata tamaa na hawatarudi nyuma katika kutafuta ufumbuzi na changamoto mbalimbali zinazoikabili wizara hiyo. 
Akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2014/15 juzi usiku bungeni, Profesa Muhongo pia amebainisha kuwa Watanzania wanamiliki asilimia 70 ya leseni za madini wakati wageni wakimiliki asilimia 25. 
Kuhusu umeme, alisema kiwango cha uunganishaji umeme mijini kimeongezeka na kufikia asilimia 24, Machi mwaka huu, baada ya uwezeshwaji wa Mfuko wa Umeme Vijijini (REA). 
Aidha alisema katika mwaka 2013/14, hali ya upatikanaji wa umeme ulikuwa ya kuridhisha ambapo hapakuwa na mgawo wowote kama alivyoahidi mwaka 2012/13. 
“Hadi mwishoni mwa mwezi Aprili 2014, uwezo wa mitambo yote ya kufua umeme (total installed capacity) ulifikia megawati 1,583. 
“Uwezo huu mpya ni sawa na ongezeko la asilimia 78 ikilinganishwa na megawati 891 zilizokuwepo mwaka 2005 wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani. Hili ni jambo la kujivunia kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi,” alieleza. 
Alisema mbali ya kutekeleza miradi mikubwa ya kufua umeme, Serikali imeanza kutekeleza miradi mikubwa yenye uwezo wa kusafirisha umeme mwingi kwenye umbali mrefu. 
Aliitaja ni Mradi wa Iringa – Shinyanga (kv 400), Mradi wa Makambako – Songea (kv 220), Mradi wa North East Grid (kv 400), Mradi wa North West Grid (kv 400), Mradi wa Singida – Arusha – Namanga (kv 440). 
Mengine ni Bulyanhulu – Geita (kv 220), Mradi wa Electricity V, Mradi wa Kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam, Mradi wa ufuaji na Usambazaji Umeme – Biharamulo, Mpanda na Ngara. 
Kuhusu miradi ya REA, alisema kwa miradi hiyo awamu ya pili, gharama za kuunganisha umeme ni Sh 27,000 tu, na kwamba kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, gharama ya kuunganisha itaendelea kuwa Sh 99,000 hadi Juni mwakani. 
Akizungumzia miundombinu ya gesi, alisema hadi kufikia Mei mwaka huu, ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Songo Songo kupitia baharini hadi Somanga Fungu lenye urefu wa kilometa 25.6, umekamilika kwa asilimia 100. Kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia na mafuta, alisema Serikali iliidhinisha Sera ya Gesi Asilia, Oktoba mwaka jana na kuwa Muswada wa Sheria ya Gesi Asilia utapelekwa bungeni Novemba mwaka huu. 
“Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa (Local Content Policy) itakamilika ifikapo Desemba 2014. Lengo kuu la sera ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki ipasavyo katika shughuli zote za rasilimali za gesi asilia na mafuta kwa manufaa ya Watanzania wote bila upendeleo au ubaguzi wa aina yoyote,” alisema waziri huyo. 
Akizungumzia uchimbaji mdogo wa madini, alisema Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu alikabidhi hundi zenye thamani ya Sh milioni 88 kwa miradi 11 ya wachimbaji wadogo iliyokidhi vigezo vya kupata ruzuku. 
“Ili kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa mitaji na mikopo, Wizara imetenga shilingi bilioni 2.50 katika mwaka wa 2014/15 kwa ajili ya mikopo yao,” alifafanua. 
Alisema kumejengeka dhana kwamba wawekezaji wageni wanamiliki maeneo mengi na makubwa kuliko Watanzania, na Serikali haijachukua hatua ya kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu. 
“Ukweli ni kwamba, Watanzania wanamiliki asilimia 70 ya leseni za madini, wageni asilimia 25 na asilimia tano ya leseni hizo zinamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni,” alibainisha Profesa Muhongo na kuongeza kuwa yeye na “timu yake ya ushindi, hakuna kushindwa, hakuna kukata tamaa.”