HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
MHESHIMIWA BALOZI KHAMIS SUEDI KAGASHEKI (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki akiwasilisha bungeni jana. |
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wake Mhe. James Daudi Lembeli (Mb.), Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kwa mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuniwezesha kuiongoza Wizara hii yenye dhamana ya kusimamia Rasilimali za Maliasili na Malikale na kuendeleza Utalii. Nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu, nikishirikiana na viongozi wenzangu ndani ya Wizara na wadau wote wa sekta hii kuhakikisha kuwa ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali hizo ni kwa manufaa ya Watanzania na dunia nzima.
Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kuchambua na kujadili Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka 2012/13 na Mpango wa Bajeti wa Wizara yangu kwa mwaka 2013/14. Nalihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ushauri wa Kamati umezingatiwa.
Mheshimiwa Spika, napenda kuungana na wenzangu kutoa pole kwako Mheshimiwa Spika na kwa waheshimiwa Wabunge kutokana na kuondokewa na aliyekuwa mbunge mwenzetu Mhe. Salim Hemed Khamis Mbunge wa Chambani - CUF. Vilevile, natoa pole kwa familia za marehemu na watanzania wote kwa ujumla kutokana na majanga mbalimbali yaliyotokea nchini. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika, Hotuba yangu imegawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza ni Utangulizi; Sehemu ya pili inazungumzia Utekelezaji wa Mpango wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010 - 2015; Sehemu ya tatu ni Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka 2012/2013 ambao umezingatia utekelezaji wa ahadi pamoja na maelekezo yaliyotolewa Bungeni na maagizo mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa Serikali. Sehemu hii inazungumzia pia changamoto ambazo Wizara ilikabiliana nazo katika utekelezaji. Sehemu ya nne ni Mpango wa Utekelezaji na Malengo ya Wizara kwa mwaka 2013/2014, na sehemu ya tano ni hitimisho ambapo bajeti inayoombwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa mwaka 2013/2014 inawasilishwa.