Monday, December 31, 2012

MATOKEO RASMI YA SENSA YA WATU TANZANIA...


Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania iliyotangazwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete muda mfupi uliopita ni kwamba idadi ya Watanzania sasa ni 44,929,002. Zanzibar kuna watu 1,303,568 na Tanzania Bara kuna watu 43,625,434. Habari kamili zitawajia baadaye.

WAWILI MBARONI KWA KUMPIGA RISASI PAROKO Z'BAR...

Paroko Ambrose Mkenda.

Polisi Zanzibar inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumshambulia kwa risasi Paroko Amrose Mkenda (52) mwishoni mwa wiki iliyopita.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar, ACP Yusuf Ilembo, alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana kwa ushirikiano wa Polisi Zanzibar na makachero waliotoka Makao Makuu, Dar es Salaam.
Hata hivyo, alikataa kuwataja watuhumiwa hao kwa madai ya kuhofia kuingilia upelelezi wa kuwapata wengine.
Alisema watuhumiwa hao bado wanaendelea kuhojiwa  ili kuwapata washiriki wenzao waliopanga njama pamoja za kumvamia na kumjeruhi kwa risasi Paroko Mkenda wa Parokia ya Mpendae mjini Zanzibar. 
Ilembo alisema Polisi itahakikisha wale wote waliohusika na shambulio hilo wanatiwa nguvuni na kukabiliana na mkono wa Sheria.

KANISA LA KKKT SASA WAANZA KUWAJIBISHANA...

Israel ole Karyongi.

Mgogoro wa matumizi mabaya ya rasilimali za Kanisa unaofukuta ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi  ya Kaskazini Kati, sasa umeanza kushughulikiwa kwa kuwajibishana katika vikao.
Habari kutoka katika kanisa hilo zimeeleza kuwa kikao kilichohudhuriwa na viongozi wa Dayosisi, wachungaji wastaafu na wa sasa na mwanasiasa mmoja wa madhehebu hayo (jina tunalo) kimetoa maelekezo ya kukabiliana na mgogoro huo, ikiwemo baadhi ya viongozi wakuu kuachia madaraka.
Taarifa zinasema ilibainika kuwa chanzo cha mgogoro huo ni
Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Israel ole Karyongi ambaye kikao hicho kilipendekeza awajibike kwa kuandika barua ya kujiuzulu.
Kwa mujibu wa habari hizo, Karyongi alionekana kutoafiki
hatua hiyo lakini ilibidi kukubali kutokana na hali mbaya ilivyo kwa sasa.
Mtoa habari ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema kikao hicho kiliamua Katibu ajiuzulu kwa kuwa yeye ni Mtendaji Mkuu na ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Hoteli ya Corridor Springs, ambayo deni la hoteli hiyo la Sh bilioni 11, ndilo lililoanzisha mgogoro.
“Huwezi kukwepa kuwajibika kwa kuwa wewe ndio uliosababisha hasara hiyo na ni lazima uwajibike haraka iwezekanavyo bila ya masharti yoyote,” mmoja wa wajumbe alikaririwa akizungumza katika kikao hicho.
Kutokana na deni hilo lililotokana na mkopo katika benki moja jijini Arusha, waumini zaidi ya 600,000 wa kanisa hilo walitakiwa kuchangia Sh 20,000 kila mmoja ili kunusuru mali za kanisa ambazo huenda zikapigwa mnada Januari mwakani kama deni hilo halitalipwa.
Waraka huo  wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Thomas Laizer, ndio ulioamsha mgogoro ambapo baadhi ya waumini akiwemo Mchungaji Philemon Mollel walitaka waliosababisha deni hilo wawajibike kwanza.
Badala ya suala hilo kushughulikiwa, Mchungaji Philemon Mollel alivuliwa madaraka ya kuongoza ibada katika kanisa hilo na kuondolewa katika usharika aliokuwa akiuongoza wa Ngateu.
Awali katika kikao cha kutafuta suluhu, baadhi ya viongozi wa Dayosisi hiyo walimwambia mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa kiongozi wa juu wa Serikali kuwa gazeti hili linaandika uongo.
Habari zilisema kiongozi huyo aliwauliza kama taarifa za gazeti hili ni za uongo, kwa nini hawaitishi kikao cha waandishi wa habari na kukanusha taarifa hizo mpaka sasa. 
“Inaonekana hapa kuna tatizo, sasa kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa kosa alililofanya kwa maslahi ya kanisa,” alikaririwa mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Hata hivyo, jana kulisambazwa waraka maalumu na Askofu
Laizer katika baadhi ya makanisa yaliyo chini ya Dayosisi hiyo, kueleza kuwa taarifa za gazeti hili kuhusu mgogoro huo si za kweli.
“Wapendwa washarika wa sharika za KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati…napenda kuwashukuru sana kwa kujitoa kwenu kushiriki katika maendeleo ya Dayosisi yetu, hususani kwa kupokea na kutekeleza waraka wangu kwenu kumbukumbu na KKKT/DKAK 67/53/VOL .II wa tarehe 30/11/2012 kuhusu hoteli yetu ya Arusha Corridor Spring.
“Ninawashukuru sana kwa mchango mliotoa na mnaoendelea kutoa kuinusuru hoteli yetu. Wapendwa washarika wakati haya yakiendelea yapo mambo yaliyoandikwa kwenye gazeti
moja la “HabariLeo” kuhusu Dayosisi yetu yasio ya kweli.
“Ndugu zangu nawaomba msisikilize wala kuhangaika na mambo yaliyoandikwa kwenye gazeti hilo kwa sababu ni ya kupotosha ukweli. Naomba muwe na utulivu na mdumishe umoja na mshikamano wetu. Dayosisi yetu itaendelea kuwaletea taarifa na ukweli juu ya Dayosisi,” sehemu ya waraka huo ilisomeka.
Hata hivyo, taarifa tulizopata waraka huo ulisomwa katika baadhi ya sharika na nyingine ulipingwa kusomwa.
Akizungumza kwa njia ya simu, mmoja wa waumini hao, Peter Mbise alisema waraka wa Askofu hauwezi kusomwa katika usharika wa Ngateu.
“Gazeti na HabariLEO ndilo lililotushitua kuwa Mchungaji Philemoni Mollel anahukumiwa kwa kupiga vita ufisadi ndani ya Kanisa,” alisema na kupongeza kwa jinsi habari hizo zilivyofuatiliwa na kuripotiwa.
Mbise, ambaye pia ni kiongozi wa kwaya katika Usharika wa Ngateu, alisema hoja zao 10 ni lazima zitekelezwe ikiwa ni pamoja na Katibu Karyongi kuwajibika yeye pamoja na bodi
yake kwa kusababisha hasara katika hoteli hiyo na si vinginevyo.
Wakati hayo yakijiri, tayari Karyongi amefunga akaunti ya Usharika wa Ngateu iliyopo katika Benki ya NBC. 
Juzi katika usharika huo ambako Mchungaji wake, Philemon Mollel alifukuzwa kazi kutokana na mgogoro huo, Askofu Msaidizi wa Dayosisi, Solomon Masangwa na ujumbe wake walilazimika kukimbia baada ya waumini kukasirika na kutaka kuchukua sheria mkononi dhidi yao.
Kufungwa kwa akaunti hiyo kumethibitishwa na kiongozi wa usharika huo, Zafania Kwayu ambaye alisema halitasaidia kwani  wataendelea kupeleka fedha katika akaunti hiyo bila ya wasiwasi wowote.
“Sisi tutapeleka fedha katika akaunti hiyo na tukitaka za matumizi tutatafuta sehemu zingine kwa waumini kuchanga kutoka katika mifuko yao kwa maendeleo ya Kanisa.
Katibu ameona kufanya hivyo ni kutukomoa, lakini anajidanganya,” alisema Kwayu.
Wiki mbili zilizopita Bodi ya Hoteli ya Corridor Springs chini ya Uenyekiti wa Karyongi, ilimtimua kazi Meneja wa hoteli hiyo, John Njoroge kwa ubadhirifu wa fedha za hoteli hiyo.
Karyongi aliwahi kuthibitisha kutimuliwa kwa meneja huyo, akidai kuwa ni hatua ya kupisha uchunguzi ili kubaini ukweli wa ubadhirifu wa hoteli hiyo na mambo mengine.
“Ni kweli Meneja ametimuliwa ili kupisha uchunguzi wa kina ufanyike kujua ukweli wa hali halisi na sasa timu ya wakaguzi inaendelea na kazi ya kupitia hesabu za hoteli hiyo,” alithibitisha Karyongi.

MFUNGWA ATOROKA, AKIMBIA UCHI MITAANI ASITAMBULIKE...


Mfungwa aliyekuwa mikononi mwa askari Magereza, ametoroka na kulazimika kukimbia uchi wa mnyama mitaani, baada ya kuvua sare za wafungwa, ili kuficha utambulisho wake.
Mashuhuda wa tukio hilo, walilieleza gazeti hili jana kwamba mfungwa huyo baada ya kufanikiwa kuwatoroka askari Magereza na kuvua sare, alijikuta akilazimika kutafuta mahali pa kujificha.
Hata hivyo, mashuhuda walisema karibu kila nyumba alikokimbilia, wenyeji  walimfukuza kwa hofu kuwa ni mwendawazimu.   
“Bahati haikuwa yake kwa kuwa  kila nyumba alikokimbilia kujificha walimfukuza, hakuwa na la kufanya ila  kukimbia mitaani akiwa uchi.
“Lakini alipovuka tu uwanja wa ndege katika kitongoji  cha Edeni alikuwa tayari amechoka, alianguka na kuzingirwa na umati mkubwa wa wananchi hadi askari Magereza walipofika,” alisema mmoja wa mashuhuda. 
Wakati akitafuta mahali pa kujisetiri, baadhi ya watu waliomshuhudia  walidhani  ni kichaa na wengine walimpigia  yowe la mwizi huku wakimtupia mawe na fimbo  hadi walipobaini kuwa si mwizi.
Mmoja wa mashuhuda hao alidai kuwa kutokana na kipigo hicho, mfungwa huyo alilazimika kuwasihi wananchi wasimpige  wala wasimuue kwa kuwa yeye ni mfungwa  aliyekuwa akisaka fursa ya kuwa huru kwa njia  ya mkato.
“Kwanza tulidhani ni mwizi lakini alitusihi tusimuue  kwani alikuwa ni mfungwa tu  akijaribu  kutoroka  ili awe huru  ndipo tulipoacha  kumpiga…kwa kweli mtu huyu alidhamiria kutoroka lakini kwa staili  hii ya kukimbia  uchi imetustaajabisha wengi,” alisema shuhuda mwingine.
Baada ya kuacha kumpiga, wananchi hao waliendelea kumzingira mpaka askari Magereza walipofika ambapo inadaiwa baadhi  walimpiga huku wakisikika kudai kuwa
watampatia  kipigo zaidi  watakapomfikisha  gerezani huku baadhi ya wananchi wakimuonea huruma na kuomba  askari hao  wasimpige.    
Mkuu wa Gereza la Sumbawanga, SSP Mndolo  alikiri kutoroka kwa mfungwa huyo, lakini hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi.   
“Sio kweli  kuwa  askari  wetu walishiriki  kumpiga mfungwa  huyo, sio kweli kabisa,”  alikanusha na kudai kuwa  mfungwa huyo kwa sasa ni mzima wa afya.
Alipoelezwa kuhusu mashuhuda, Kamanda Mndolo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake la pili, alisema ikithibitika kuwa walimpiga watamchukulia hatua kali za kinidhamu.
“Ninavyozungumza nawe  mfungwa huyo  ni mzima wa afya  na ikithibitishwa kuwa  askari wetu walimpiga basi tunao utaratibu, kwanza  hawaruhusiwi kujichukulia sheria mikononi,  hilo ni kosa  watachukuliwa  hatua kali  za kinidhamu,” alisema Kamanda Mndolo.

HAKIKA TUMETOKA MBALI...

Hivi ndivyo Ofisi ya Posta mjini Songea, mkoani Ruvuma ilivyokuwa ikionekana mwaka 1960.

ZIRO PLUS...

**Timu nzima ya wachapakazi wa ziro99blog tunachukua nafasi hii kuwatakieni wasomaji wetu na Watanzania wote kwa ujumla heri ya Mwaka Mpya 2013. Tunawaahidi kuwaletea habari kemkem pamoja na maboresho makubwa ili muweze kufaidi uhondo ambao mmekuwa mkiupata kupitia hapa. Tunawatakia mwaka mpya wenye mafanikio tele na Mungu awabariki sana kwa ushirikiano mliotupatia kwa kipindi chote. -Mhariri

MAMA WA BINTI ALIYEBAKWA NA WAHUNI SABA AANGUKA GHAFLA...

Jeneza lenye mwili wa binti aliyebakwa na wahuni likiwa ndani ya gari mara baada ya kuwasili mjini Delhi.
Mama wa binti wa India ambaye alibakwa na kundi la wahuni amekimbizwa hospitali jana baada ya kuanguka wakati mwili wa binti yake ulipokuwa ukichomwa moto.
Pia imefahamika kwamba mwanafunzi huyo wa tiba ya viungo mwenye miaka 23 alipanga kufunga ndoa na rafiki yake wa kiume, ambaye alijeruhiwa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa majirani zake.
Mwili wa msichana huyo ulichomwa moto mapema jana baada ya ndege iliyokodiwa na Serikali ya India kurejesha mwili wake mjini Delhi kutoka hospitalini nchini Singapore ambako alifariki juzi wakati akipatiwa matibabu kufuatia majeraha makubwa aliyopata.
Mateso yake ya kutisha yamewaamsha raia wa India kutaka ulinzi mkubwa kwa wanake kutokana na vitendo vya ubakaji kupitia maandamano makubwa, uwashaji mishumaa na kupinga mitaani wakiwa na mabango na vizuizi barabarani.
Msichana huyo na rafiki yake wa kiume walikuwa wakitazama filamu ya The Life of Pi jioni katika jengo la sinema lililoko wilaya ya Saket mjini New Delhi ndipo waliposhambuliwa kwenye basi wakiwa njiani kurejea nyumbani Desemba 16, mwaka huu.
"Walishafanya maandalizi yote ya harusi na walikuwa wamepanga kufanya sherehe ya harusi mjini Delhi," jirani aliieleza NDTV.
"Tunafahamu kwamba alikuwa aolewe mwezi Februari," alisema. "Majirani wote wameshitushwa na kilichotokea."
Sherehe za siri jana zilifanyika zikiambatana huku Polisi wa kuzuia ghasia nchini India wakiweka ulinzi nje ya jengo la kuchomea miili mjini New Delhi.
Wakihofia maandamano miongoni mwa wananchi wenye hasira, eneo na muda wa kuchoma mwili haukuwekwa wazi, lakini ilifanyika mapema baada ya mwili kuwasili kutoka Singapore kwenye ndege maalumu ya Air-India.
Mama yake aliyechanganyikiwa alianguka na kupelekwa Hospitali ya Safdarjung baada ya mwili wa binti yake kuondolewa.
Waziri Mkuu Manmohan Singh na Sonia Gandhi, wakuu wa chama tawala cha Congress, walikuwa uwanja wa ndege kupokea mwili na kukutana na wanafamilia wa muathirika ambao pia waliwasili katika ndege hiyo.
Baada ya mwili kuwasili uwanja wa ndege, ulipelekwa kwenye nyumba ya binti huyo mjini New Delhi kwa taratibu za kidini kabla ya kusindikiwa na polisi hadi sehemu ya kuchomea mwili.
Ulinzi ulikuwa mkali, huku kukiwa hakuna ruhusa kwa wananchi au vyombo vya habari kuingia kwenye eneo la kuchomea mwili.
Taarifa kuhusu utambulisho wa binti huyo havikutolewa hadharani kwa usalama wa familia yake.
Wazazi wake waliuza sehemu ya ardhi jirani yao na pia ardhi kwenye kijiji chao huko wilaya ya Ballia iliyoko mashariki mwa Uttar Pradesh kugharimia elimu ya binti yao.
"Sasa kaka yake mkubwa, ambaye anajiandaa kwa mitihani ya uhandisi, hana matumaini ya kuendelea na masomo yake. Familia jiyo ilitegemea mafafikio ya binti huyo katika fani yake ili kuwanasua kutoka kwenye umaskini wao," jirani aliyejitambulisha kwa jina la Vimla aliieleza IANS.
Watuhumiwa sita waliokamatwa wanakabiliwa na adhabu ya kifo endapo watapatikana na hatia.

ZIRO PLUS...


JINSI MEDALI ZILIVYOMWOKOA MO FARAH NA UGAIDI MAREKANI...

Mwanariadha Mo Farah akionesha medali zake za Olimpiki.
Shujaa wa Olimpiki nchini Uingereza, Mo Farah amebainisha jinsi alivyohojiwa na maofisa wa mpakani nchini Marekani wakimtilia mashaka kwamba ni gaidi.
Mshindi huyo wa medali mbili za dhahabu, ambaye pia ametunukiwa tuzo ya CBE katika orodha ya watunukiwa wa Mwaka Mpya, alisema aliburutwa mbele ya walinzi wakati akiingia nchini humo kwa ajili ya mapumziko ya Krismasi mwaka huu.
Mkimbiaji huyo mwenye miaka 29 alilieleza gazeti la The Sun kwamba walinzi wa mpakani walimuuliza maswali kwa sababu ya 'asili yake kutoka Somalia'.
Mwanariadha huyo alilazimika pia kuonesha medali zake za Olimpiki katika juhudi za kuthibitisha yeye ni nani hasa.
Katika ziara yake iliyopita nchini humo, Farah alibainisha kwamba alitakiwa kuondoka kabla ya kupokea barua ikieleza kwamba 'alikuwa chini ya uchunguzi wa tishio la ugaidi'.
Farah alihamia Uingereza akiwa na baba yake mzaliwa wa Uingereza wakati alipokuwa na umri wa miaka minane tu.
Alisema kwamba alikamatwa na walinzi wa mpakani wakati akitembelea Portland, Oregon, akiwa na familia yake katika mapumziko ya Krismasi.
Mwanariadha huyo alisema: "Siwezi kuamini. Sababu ya asili yangu ya Kisomali nimekuwa nikikamatwa kila mara ninapokuja kwenye Ofisi za Forodha za Marekani."
Farah alisema alilazimika kuishia 'kuonesha medali zake' kuthibitisha yeye ni nani, ambapo mara kwa mara amekuwa akizibeba kwenye mizigo yake.
Farah, ambaye ushindi wake katika mbio za mita 5,000 na 10,000 umetoa matukio mawili ya kusisimua katika michezo iliyofanyika London mwaka 2012, amekuwa akifanya mazoezi nchini Marekani.
Baada ya kushindwa kufuzu kwa michezo ya Olimpiki mwaka 2008, alimhamishia mke wake, Tania na bintiye Rihanna mjini Portland kufanya kazi na kocha mkongwe Alberto Salazar katika makao makuu ya Nike.
Lakini mkimbiaji huyo alisema kwamba siku za nyuma alishakumbana na matatizo na maofisa wa mpakani.
Akidhani kwamba wadhamini wake Nike walishatatua viza yake ya ukaazi, Farah 'alilazimika kuondoka' Marekani huku akiwa anatumia viza ya kitalii.
Alisema: "Tulienda Toronto kukaa kwa siku chache, na kisha kurejea tena.
Lakini wakati tulipokuwa huko tulipata barua ikitueleza kwamba tuko chini ya uchunguzi kama tishio la ugaidi na tunatakiwa kuondoka kwa siku nyingine 90."
Farah amedai kwamba kocha wake Mmarekani alikuwa na 'rafiki yake anayefanya kazi FBI' ambaye alikuwa 'shabiki mkubwa'. Kwa mujibu wa mkimbiaji huyo, suala hilo 'limepatiwa ufumbuzi'.

JICHO LA TATU...


Sunday, December 30, 2012

ACHINJWA, KISA KUWAITA KWA MAJINA WEZI WAKE...

Kamanda Dhahiri Kidavashari.
Mkazi wa kitongoji cha Kapepe, tarafa ya Mwese wilayani Mpanda, Saliunga Jinane (43) ameuawa kwa kuchinjwa aliowatambua kwa sura na majina watu waliomvamia na akatishia kuwashtaki Polisi  kama wasingemrudishia fedha walizompora.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari  amethibitisha kutokea mauaji hayo, akisema yalitokea  alfajiri ya siku ya Krismasi, Kapepe.
Akielezea, Kidavashari  alisema  alfajiri ya siku ya tukio  watu watatu  wasiofahamika,  walivamia  nyumba ya  Jinane  akiwa  na mkewe, Leticia Masila (30) na kumlazimisha awape fedha alizokuwa nazo.
Inadaiwa bila ajizi aliwakubalia na kuwapa Sh 50,000 wakazipokea na kuondoka bila kuwadhuru  wanandoa hao.
“Bila shaka watu hao walikuwa na taarifa kuwa Jinane alikuwa na kiasi hicho cha fedha, wakiwa na tochi yenye mwanga mkali walivamia nyumba yake akiwa na mkewe na kumlazimisha awakabidhi fedha zote alizokuwanazo.
“Jinane hakufanya ukaidi aliwakabidhi watu hao Sh 50,000 nao wakaondoka bila kuwadhuru wanandoa hao,“ alisema.
Kwa mujibu wa Kidavashashi, baada ya watu hao kutoka nje, Jinane aliwafuata na kwa sauti akawatamkia kuwa,  anawatambua  na kuwataja kwa majinammoja baada ya mwingine huku akiwafokea na akiwataka wamrudishie fedha  zake  vinginevyo  atawashitaki Polisi.
Inadaiwa kuwa watu hao  waliingiwa na hofu  kutokana na tishio la Jinane, ndipo walirejea  nyumbani kwake wakamkamata  na  kumcharaza  viboko  na kumchinja mbele ya mkewe na kutokomea  kusikojulikama, bila kumdhuru  mkewe.
Kamanda Kidavashari alidai kuwa mke wa marehemu alikiri kumsikia  mumewe  akiwaita  ‘wauaji’ hao  kwa majina  akiwafokea na kuwasihi wamrejeshee fedha walizompora, vinginevyo  angewashitaki  Polisi  kwa kuwa anawafahamu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari  mke wa marehemu  alidai kuwa  hakuweza kukariri  majina ya ‘wauaji’ hao, kwani ilikuwa ni  mara yake ya kwanza kuwaona.
Kamanda alieleza kuwa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na walinzi wa jadi na watendaji wa vijiji, kata  na wananchi kwa ujumla, wameanza kuwasaka watu hao  ambao  wanadaiwa  kujificha  kusikojulikana.

MADEREVA WA BODABODA WATOANA ROHO KATIKA AJALI...

Madereva wawili wa pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ wamekufa papo hapo huku abiria wao  watatu  akiwamo mtoto wa miaka saba wakijeruhiwa baada ya pikipiki hizo kugongana uso kwa uso katika  barabara ya Majimoto-Mamba  wilayani Mlele.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo ilihusisha pikipiki  namba T 179 CTZ iliyokuwa ikiendeshwa na Mone Ezene (20), mkazi wa kijiji  cha Majimoto  iliyogongana uso kwa uso na  pikipiki namba T 210 VRV  iliyokuwa ikiendeshwa  na Alex Benezedi, wa kijiji cha Ntaswa, Mlele.
Alitaja  majeruhi  ambao walikuwa  wamebebwa  na  pikipiki  hizo kuwa ni Grace Masawe (24) wa Majimoto  ambaye ameumia usoni  na mwanawe, Shauri Masawe (7)  aliyeumua  kifuani. Abiria hao walikuwa wamepakiwa kama `mshikaki’.
Kwa mujibu  wa Kamanda Kidavashari,  abiria  mwingine aliyejeruhiwa katika ajali  hiyo  ametambuliwa  kuwa ni Geofrey Mkoma (32), wa  kijiji cha Kilida, ambaye amejeruhiwa begani abiria wote hao  walikimbizwa katika kituo cha afya  kwa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa  habari  hizi  kwa njia ya simu, Kamanda Kidavashari  alidai  kuwa ajali  hiyo ilitokea  juzi saa  12.30 jioni  wakati  moja  ya pikipiki  hizo ikitoka  Majimoto na nyingine Mamba.
Kwa mujibu wa Kidavashari, chanzo  cha  ajali hiyo  ni mwendo  mkali   na uzembe wa madereva  wote wawili  kwamba tukio  hilo  bado linaendelea  kuchunguzwa.

ASKOFU KKKT AJIOKOA KWA MLANGO WA NYUMA, AFICHWA...

Vurugu, mabishano na ubabe jana vilitawala katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ngateu, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha baada ya Askofu Msaidizi wa Dayosisi hiyo, Solomon Massangwa na ujumbe wake, kuwasili kujaribu kueleza hali halisi ya mgogoro unaofukuta ndani ya Kanisa hilo.
Lakini tofauti na matarajio yao, walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa waumini waliopinga kikao cha siri baina ya msaidizi wa Askofu na ujumbe wake, uliolenga kukutana na wazee wa Usharika huo.
Akifuatana na Mchungaji mstaafu Gabriel Kimelei na Katibu wa Jimbo la Arusha Magharibi la Dayosisi hiyo, Daniel Medani, Askofu huyo Msaidizi alikutana na umati wa waumini waliokuwa katika makundi kwenye viwanja vya Kanisa hilo, ndipo akaomba kuonana na wazee wa Kanisa.
Hata hivyo, wakati akiomba kukutana na wazee, waumini walicharuka na kutaka kusiwe na kikao cha siri.
Mmoja wa waumini hao ambaye ni kiongozi wa kwaya ya Usharika, Zephania Kwayu, alianzisha sakata hilo, baada ya kupaza sauti akisema: ‘’Hakuna kuzungumza na wazee wakati kila kitu kiko wazi, semeni mbele yetu na mtueleze Mchungaji Mollel (Philemon) anarudi lini kazini na waliosababisha mambo kuharibika wanawajibika vipi?’’
Kauli ya Kwayu iliwapandisha mori waumini wengine ambao nao walipiga kelele kwa sauti za juu kwamba hawataki kusikia chochote zaidi ya Mchungaji Mollel kurudishwa kazini mara moja na bila masharti.
Mollel alifukuzwa kazi Jumatatu na uongozi wa Dayosisi hiyo, akituhumiwa kuwakashifu na kuwakosea adabu viongozi waandamizi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati akiwamo Askofu Thomas Laizer, jambo ambalo linapingwa na washarika wanaoamini ametolewa kafara, kutokana na kujitoa mhanga kuhoji kinachoelezwa kuwa ni ubadhirifu mkubwa katika miradi ya Kanisa.
Wakionekana wazi kukasirika, waumini hao jana walikaribia kuchukua sheria mkononi kwa kutaka kumshambulia Askofu Massangwa ambaye alilazimika kujificha katika ofisi za Usharika huo kupitia mlango wa nyuma wa Kanisa hilo.
Huku waumini wengine wakifunga milango ya Kanisa ili Askofu huyo na ujumbe wake wasitoke, mvua kubwa ilinyesha hali iliyosaidia kuwaokoa na kipigo cha washarika wao.
"Fungeni milango yote asitoke huyo, wamezoea kulinda mafisadi na tunataka Mchungaji wetu arudishwe haraka, la sivyo tuwafundishe adabu hapa hapa kanisani,’’ washarika hao walisikika wakifoka kwa sauti za hasira huku wakiwa tayari kwa lolote.
Jitihada za baadhi ya wazee wa Usharika huo kuwatuliza waumini wao hazikuzaa matunda, huku ujumbe huo ukitoroshwa ili kuokoa maisha yao licha ya mvua kubwa kuwanyeshea.
Baada ya Askofu Msaidizi kufanikiwa kutoroka na ujumbe wake, Kwayu aliwaambia waumini kwamba wametoa hoja kumi za kutekelezwa na viongozi wa Dayosisi ili kurudisha mshikamano kanisani humo.
Moja ya hoja hizo ni pamoja na kurudishwa kazini Mchungaji Mollel, kufukuzwa kazi mara moja kwa Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Israel ole Karyongi na kujiuzulu kwa Askofu wa Dayosisi hiyo,Thomas Laizer.
Mgogoro ndani ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati uliibuka baada ya waumini kupewa waraka wa kutakiwa kila mmoja kuchangia Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya hoteli ya Corridor Springs kudaiwa Sh bilioni 11 na benki moja nchini.
Hatua hiyo inapingwa na waumini hao na baadhi ya wachungaji akiwamo Mollel anayetaka wahusika wa kadhia hiyo wachukuliwe hatua; lakini ‘aligeuziwa kibao’ na kufukuzwa na kuvuliwa madaraka ya kutoa huduma za kichungaji katika Kanisa hilo nchini.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya Kanisa hilo vilieleza kuwa hatua hiyo ilitokana na Mchungaji Mollel kushindwa kutekeleza mambo matatu aliyotakiwa na Tume maalumu ya watu watatu walioteuliwa na Menejimenti ya Dayosisi hiyo na alipewa siku tatu kuomba radhi, lakini hakufanya hivyo.
Habari zilieleza kuwa walioteuliwa Desemba 14 na kwenda kumwona Mchungaji Mollel kutekeleza hayo ni pamoja na Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Godwin Lekashu na Karyongi.
Taarifa za ndani zilisema Mchungaji Mollel aliandikiwa barua Desemba 17 na kutakiwa kufanya mambo hayo matatu kabla ya Desemba 23.
Mosi, alitakiwa kumwandikia barua Askofu  Laizer kumwomba radhi na kueleza ni kwa nini alimkashifu na kumdharau.
Pili, atoe tamko katika Mtaa wa Azimio ibadani Desemba 23, akiomba radhi kwa aliyotamka; na tatu ifikapo Desemba 23, awe amemwarifu Katibu Mkuu kwa barua kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo na kwamba yote yafanyike kabla ya Desemba 24.
Vyanzo vya habari vilisema baada ya Mchungaji Mollel kukaidi hayo, kikao cha watu watatu wakiongozwa na Karyongi kiliamua kumfukuza kazi na kumvua uchungaji.
Hata hivyo, habari za uhakika zilisema Mchungaji Mollel hakufanya hivyo kwa madai kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu aliyetukuka kufuata maadili na kamwe hawezi kufanya hivyo, kwani hakumkashifu mtu wala kiongozi yeyote, bali alieleza ukweli juu ya nani wa kuwajibika katika deni la Sh bilioni 11.
Wakati huo huo, habari zilizotufikia baadaye jana zilieleza kuwa, Askofu Laizer amelazwa katika hospitali maarufu ya Kanisa hilo ya Selian, mjini hapa.
Chanzo cha habari kilisema alilazwa tangu juzi. Juhudi za kumwona hospitalini hapo hazikuzaa matunda kutokana na kutanda kwa usiri wa kulazwa kwake. Inadaiwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.

CHEKA TARATIBU...

Jamaa wawili wamefika kwenye stesheni ya treni. Kwa bahati mbaya wakakuta treni ndio imeshaanza kuondoka, hivyo wakaanza kuifukuzia na kwa bahati mmoja akafanikiwa kudandia. Kwa mshangao yule aliyebaki akaanza kucheka sana, ndipo watu wengine pale stesheni wakahoji kulikoni kuikosa treni na kuanza kucheka. Jamaa akajibu, "Mimi ndiye ninayesafiri, yule alikuwa akinisindikiza tu!" Kasheshe...

MWANAFUNZI ALIYEBAKWA NA WAHUNI SABA AFARIKI DUNIA...

KUSHOTO: Gari maalumu likisubiri kuchukua mwili wa mwanafunzi huyo kwenye Hospitali ya Mount Elizabeth, nchini Singapore. KULIA: Madaktari wakiondoa mwili wa mwanafunzi huyo tayari kwa maandalizi ya kuusafirisha kwenda India.
Binti ambaye alibakwa na kundi la wahuni na kupigwa vibaya ndani ya basi katika tukio ambalo halikuishitua India pekee, bali dunia nzima, amefariki dunia juzi usiku katika hospitali moja nchini Singapore.
Binti huyo mwenye miaka 23 alikuwa katika hali mbaya tangu baada ya tukio hilo akisumbuliwa na viungo vyake kadhaa kushindwa kufanya kazi na mshituko wa moyo, na licha ya juhudi za madaktari bingwa katika Hospitali ya Mount Elizabeth, juzi usiku akapoteza maisha yake.
Mateso yake ya kutisha yamewaamsha Wahindi kudai ulinzi mkubwa kwa wanawake dhidi ya matukio ya ubakaji ambayo yanaathiri maelfu kati yao kila siku, huku maandamano makubwa yakiendelea kuikumba nchi hiyo.
Tofauti na mateso ya kutisha aliyopitia katika mikono ya wabakaji wake, 'alifariki bila purukushani' huku familia yake na maofisa wa Ubalozi wa India wakiwa kando yake," alisema Dk Kevin Loh, Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Mount Elizabeth ambako alikuwa akipatiwa matibabu tangu Alhamisi iliyopita.
"Timu ya madaktari wa Hospitali ya Mount Elizabeth, manesi na wafanyakazi wanaungana na familia yake katika kuomboleza kuondokewa naye," alisema katika taarifa.
Alisema mwanamke huyo aliendelea kuwa katika hali mbaya tangu Alhamisi wakati alipoletwa kwa ndege Singapore kutoka India.
Licha ya juhudi za timu ya madaktari bingwa wanane wa Hospitali ya Mount Elizabeth kuimarisha afya yake, hali yake iliendelea kuzorota katika siku hizi mbili. Alikuwa akisumbuliwa na viungo vingi kushindwa kufanya kazi kutokana na majeraha makubwa mwilini mwake na kwenye ubongo. Alikuwa na ujasiri katika kupambana na hali hiyo kwa kipindi kirefu dhidi ya mabaya yote lakini kiwewe mwilini mwake kilitawala kwa yeye kuweza kukishinda."
Balozi wa India, T.C.A. Raghanvan aliwaeleza waandishi kwamba uwiano wa majeraha aliyokuwanayo yaliashiria 'zaidi kifo' na mwishoni 'yalithibitisha hayadhibitiki.'
Alisema mipango inafanywa kuweza kurejesha mwili wake India.
Yeye na rafiki yake wa kiume walikuwa wakisafiri kwenye basi la abiria Desemba 16 jioni ndipo waliposhambuliwa na wanaume sita ambao walimbaka na kuwapiga wote wawili, kuwavua nguo wote uchi wa mnyama na kuwatupa kando ya barabara.
Tukio hilo limekuja wakati mwathirika mwingine wa ubakaji nchini India anasemekana kujiua baada ya polisi kuchukua siku 14 kufungua kesi na siku 30 zaidi kuweza kuwakamata watuhumiwa.
Mapema jana madaktari waliripoti kwamba mwanafunzi huyo mwathirika wa ubakaji alikuwa tayari 'akipambana dhidi ya mabaya kufuatia ugonjwa wa moyo, mapafu na athari za uti wa mgongo na majeraha kwenye ubongo."
Lakini Ijumaa jioni, hali ya binti huyo 'ilibadilika na kuwa mbaya' na nuru yake ikaanza kudorora kutokana na viashiria vya viungo kadhaa kushindwa kufanya kazi, alisema Dk Kevin Loh.
Hii ni licha ya madaktari kupigania maisha yake ikiwamo kumwekea vifaa bandia vya kusaidia kupumua, dawa za maumivu na pia vichocheo vya kudhibiti uwezo wa mwili wake kupambana na maambukizi," alisema, na kuongeza kwamba wanafamilia wake walikuwa kando yake.
Polisi wamewakamata watu sita kuhusiana na shambulio hilo na kwamba wako mikononi mwa polisi.
Serikali ya India imechukua hatua kufuatia siku kadhaa za ghasia kupinga shambulio hilo kwa kuahidi kuweka hadharani picha, majina na anwani za wabakaji watakaotiwa hatiani.

HAKIKA TUMETOKA MBALI...

Eneo la Posta ya Zamani, Dar es Salaam kama linavyoonekana katika miaka ya mwanzoni mwa 1980 huku basi aina ya 'Ikarus" mali ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) wakati huo likiendelea kula vichwa. Hakukuwa na daladala wakati huo.

Saturday, December 29, 2012

MSANII STEVE NYERERE ANUSURIKA KIFO AJALI YA GARI WAMI...


Msanii nyota wa filamu na mchekeshaji maarufu nchini, Steve Mangele maarufu kama Steve Nyerere, amenusurika kifo katika ajali ya gari iliyotokea juzi maeneo ya Mto Wami.
Msanii huyo pamoja na wenzake watatu akiwamo msanii mwingine wa filamu, Chikki Mchoma, walikuwa wakisafiri kwa gari dogo aina ya Toyota Verossa kutokea Arusha kuhudhuria sherehe ya mwenzao ambaye hawakumtaja, ndipo wakapatwa na masahibu hayo
Steve anasema wakiwa kwenye mwendo wa kawaida, huku Chikki ambaye ndiye alikuwa dereva, ghafla wakashitukia gari lao likipoteza mwelekeo na kujikita mtaroni ambapo gari hilo liliharibika vibaya sana.
Kwa mujibu wa Steve, wote waliokuwa kwenye gari hilo walitoka salama na kwamba gari lake hilo tayari wameshalifikisha gereji kwa ajili ya matengenezo.
Steve Nyerere amejizolea umaarufu mkubwa kwa kipindi kirefu kutokana na umahiri wake wa kuigiza kwa ustadi mkubwa sauti ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

KESI YA MSANII LULU YATINGA RASMI MAHAKAMA KUU...

Msanii Lulu akisindikizwa mahakamani kusikiliza mashitaka yake ya mauaji.
Kesi ya mauaji ya kutokukusudia inayomkabili msanii wa Filamu nchini, Elizabeth Michael `Lulu’, imepokelewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kusajiliwa kwa namba 125 ya mwaka 2012.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mahakamani hapo, kesi hiyo imepokelewa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na inasubiri kupangiwa Jaji na tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali Lulu alikuwa akikabiliwa na mashitaka ya kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba, kwa kukusudia lakini baada ya upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi alibadilishiwa mashitaka na kuwa kuua bila kukusudia.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu  Augustina Mmbando, katika hatua za awali na Lulu hakuruhusiwa kujibu mashitaka yanayomkabili kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kwa mujibu wa sheria, kutokana na Lulu kushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, anaweza kupata dhamana.
Desemba 21 mwaka huu, Lulu alisomewa maelezo ya kesi na ushahidi utakaotumika na upande wa mashitaka katika kesi hiyo, ambapo Wakili wa Serikali Shedrack Kimaro alidai kuwa watakuwa na mashahidi tisa, ushahidi wa nyaraka, ripoti ya uchunguzi wa hospitali na ramani ya eneo la tukio.
Baadhi ya mashahidi watakaotoa ushahidi ni pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, Sofia Kassim, Daktari wa marehemu aitwaye Pancras Kageigwa, Morris Semkwao na Esther Zephania ambaye ni askari Polisi wa kituo cha Oysterbay, Kinondoni.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua bila kukusudia msanii huyo nyota wa filamu nchini.

IGP MWEMA AONGEZA MAKACHERO KUSAKA WALIOMDHURU PADRI...

IGP Saidi Mwema.
Makachero kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, wamewasili Zanzibar kuungana na wenzao wengine wa Polisi Zanzibar katika Upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae, Ambrose Mkenda.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuf Ilembo, alisema kuwa timu hiyo ambayo inaongozwa na Ofisa mmoja wa ngazi ya juu (hakumtaja jina) ina jumla ya makachero watano waliobobea katika masuala ya upelelezi nchini.
Alisema kuwa nia ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuituma timu hiyo ni kutaka kuongeza nguvu katika tukio hili ambalo linatazamwa kwa aina tofauti, hasa ikizingatiwa kuwa aliyeshambuliwa ni kiongozi mkubwa wa dini na limetokea katika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi.
Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi limeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha wote waliohusika katika kumshambulia Paroko huyo wanakamatwa.
Hata hivyo, Kamanda Ilembo alisema kuwa bado polisi wanaendelea na upelelezi wa kubaini sababu za kushambuliwa kwa Paroko huyo bila ya kuibwa kwa kitu chochote kutoka kwa padre huyo aliyeshambuliwa.
Alisema kuna uwezekano kuwa watuhumiwa wameshindwa kuchukua kitu chochote baada ya kubaini kuwa eneo la tukio lisingekuwa salama kwao kwa vile kulikuwa na walinzi na ni eneo ambalo ni karibu kabisa na makazi ya viongozi wengine wa madhehebu hayo.
Padri Mkenda alipigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa katika maeneo ya Tomondo, nje kidogo ya mji wa Unguja, saa moja usiku.
Inadaiwa kuwa waliotenda uhalifu huo walikuwa wakimfuatilia wakidhani kwamba alikuwa na fedha zinazotokana na michango iliyokusanywa na waumini katika ibada ya Krismasi kanisani hapo.
Padre huyo  alivunjwa taya na uchunguzi umebaini kwamba mpaka juzi alikuwa anaishi na  risasi mbili mwilini ambazo zilitarajiwa kuondolewa  jana.
Akizungumzia Sikukuu za mwisho wa mwaka 2012 na mwanzoni mwa mwaka 2013, Kamanda Ilembo amewahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa wahalifu ili wachukuliwe hatua.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, ACP Aziz Juma Mohammed, amewatahadharisha wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wadogo kuranda barabarani ama kwenda katika fukwe za bahari kuogelea pasipo uangalizi wa watu wazima.
Kamanda Aziz amesema kuwa uzoefu unaonesha kuwa watoto wengi wamekuwa wakigongwa na magari ama kuzama na kufa maji katika siku hizi za sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kukosa uangalizi wa watu wazima.
Aidha amewataka wananchi kutoziacha nyumba zao wazi ama bila ya kuwa na uangalizi wa kutosha ili kutowapa nafasi kwa wahalifu kupata fursa ya kuwaiba.

KESI YA RAIS WA CHAMA CHA MADAKTARI YAPIGWA KALENDA...

Dk Namala Mkopi.
Kesi ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MALT), Dk. Namala Mkopi imeahirishwa hadi Januari 23 mwakani itakapoendelea kusikilizwa.
Hakimu Hellen Liwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, aliahirisha kesi hiyo hadi mwakani watakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.
Dk Mkopi anakabiliwa na mashitaka mawili ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi iliyowataka madaktari waliogoma nchi nzima wasitishe mgomo, na shitaka jingine ni kuwashawishi madaktari wagome.
Akisomewa maelezo ya awali Septemba mwaka huu ilidaiwa kuwa, Juni mwaka huu  madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za serikali waliingia kwenye mgomo dhidi ya mwajiri wao ambaye ni serikali na mgomo huo uliandaliwa na MAT ambapo madaktari waligoma kuwahudumia wagonjwa.
Wakili Tumaini Kweka alidai kuwa wakati mgomo huo ukiendelea serikali ilipeleka maombi Mahakama Kuu Diveshini ya Kazi kuomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia mgomo huo usiendelee hadi mgogoro baina ya Mat na Serikali ulifunguliwa katika Tume ya Usuluhishi wa Migogoro (CMA) utakapomalizika.
Aidha Kweka alidai kuwa Juni 22 mwaka huu, Mahakama Kuu ilitoa amri ya kuwataka madaktari waliogoma nchi nzima wasitishe mgomo na mahakama hiyo ikampa nakala ya amri hiyo Dk Mkopi  Juni 25 mwaka huu, lakini waliendeleza mgomo.
Juni 26 mwaka huu, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ilitoa amri nyingine kwa MAT iliyokuwa ikikitaka chama hicho kutekeleza kwa vitendo amri ya mahakama iliyotolewa Juni 22 mwaka huu ambayo ilimtaka Dk. Mkopi kwenda kwenye vyombo vya habari kuwatangazia madaktari wote waliogoma wasitishe mgomo huo; lakini alidharau amri hizo mbili za mahakama.
Hata hivyo, Dk Mkopi alidai kuwa madaktari hawakugoma kuwatibia wagonjwa na kwamba si kweli kuwa alidharau amri ya mahakama iliyomtaka aende kwenye vyombo vya habari kuwatangazia madaktari waache kugoma.

HAKIKA TUMETOKA MBALI...

Mji wa Singida kama unavyoonekana katika picha hii iliyopigwa katika miaka ya 1960.

KIJANA AJIUA KWA KUCHOSHWA NA MATESO YA UKIMWI...

Kijana mdogo wa miaka 18, mkazi Dar es Salaam, Abdallah Salum, amekutwa amejinyonga chumbani kwake akidai amechoshwa kusumbuliwa na ugonjwa wa Ukimwi.
Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema jana kuwa Salum, mkazi wa Charambe wilaya ya Temeke alikutwa amejinyonga juzi kwa kutumia kamba ya katani aliyoitundika kwenye kenchi.
Alisema kijana huyo aliacha ujumbe uliosema; “ugonjwa huu wa Ukimwi umenisumbua sana.”
Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Temeke na sasa unafanyiwa taratibu za mazishi.
Habari za kijana huyo kuchukua uamuzi huo zimewashangaza wengi wakihisi Salum alikuwa hafuati masharti wala kutumia dawa za kurefusha maisha kwani wanaofanya hivyo siku hizi ‘hawateswi’ na magonjwa yanayosababishwa na mtu kuishi na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi (VVU).
Wakati huo huo, mkazi mwingine wa Boko wilaya ya Kinondoni, Humphrey Stanley (35) alikutwa amekufa chumbani kwake baada ya kujinyonga kwa kutumia mkanda wa begi alioufunga kwenye kenchi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema chanzo cha mtu huyo kuamua kujinyonga hakijafahamika kwani hakuacha ujumbe na polisi wanaendelea na uchunguzi. Mwili wa Humphrey umehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala.
Katika tukio jingine, mtu aliyetambuliwa kwa jina la Andrew Charles mwenye umri kati ya miaka 25 na 30 amekutwa amekufa ndani ya gari Magomeni Makuti jijini.
Kamanda Kenyela alisema mtu huyo amekutwa amekufa ndani ya gari aina ya BMW lenye namba za usajili T 585 AFN, chanzo cha kifo chake hakijafahamika na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

WAUMINI KANISA LA KKKT WAMGEUZIA KIBAO ASKOFU LAIZER...

Askofu Thomas Laizer.
Katika hali inayoonekana Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya   Kaskazini Kati kuparanganyika, sasa waumini wa Jimbo la Arusha Magharibi ndani   ya Dayosisi hiyo wametishia kujitenga iwapo masharti yao hayatatekelezwa. 
Masharti hayo ni pamoja na kuwataka viongozi waandamizi wa Dayosisi hiyo, akiwamo   Askofu Thomas Laizer na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Israel Karyongi kujiuzulu   kutokana na tuhuma za ufisadi wanazozielekeza kwao.
Sambamba na viongozi hao kuachia nyadhifa zao, waumini hao pia wanataka Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Ngateu katika jimbo hilo, Philemon Mollel, arejeshewe   uchungaji wake mara moja bila masharti yoyote.
Mchungaji Mollel ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea na kupigania mali za Dayosisi hiyo, amefukuzwa kazi na kuvuliwa uchungaji ndani ya kanisa hilo.
Hatua  ya kuwataka viongozi hao waandamizi wa Dayosisi kujiuzulu na kurejeshewa   uchungaji wake Mchungaji Mollel ilifikiwa juzi katika kikao cha viongozi wa sharika   mbalimbali za Jimbo la Arusha Magharibi pamoja na wazee waliokutana jijini hapa kujadili mustakabali wa Dayosisi hiyo.
Mmoja wa viongozi wa jimbo hilo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alithibitisha kuwapo kwa tamko hilo akisema kuwa wachungaji waliohudhuria kikao hicho wapo tayari kujitenga na Dayosisi ya Kaskazini Kati endapo uamuzi wao hautafanyiwa kazi.
‘’Hali ni tete wala tusijidanganye, waumini hawaelewi kinachoendelea na kinachofuata ni  sisi kujitenga na Dayosisi kwa kuwa ufisadi, udikteta na ufujaji ovyo wa mali  za Dayosisi unazidi kuongezeka kila kukicha,’’ alisema na kuongeza:
‘’Watu wanapigania wahusika katika kufuja mali za kanisa wawajibishwe lakini wengine wachache wanawaunga mkono kwa maslahi yao huku wengine wakitolewa kafara... Kamwe  hatutakubali haya yafanyike kanisani.”
Juhudi za kumpata Askofu Laizer na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Karyongi hazikuzaa matunda, kwani simu zao ziliita bila kupokewa na hata walipotumiwa ujumbe wa simu uliotaka ufafanuzi juu ya hatua hiyo ya waumini, hakukuwa na majibu.
Hata hivyo, Mkuu wa  Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Godwin Lekashu, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa hatua hiyo alisema: “Mimi kama Kiongozi wa Jimbo sina taarifa rasmi ya kikao hicho, na kama kingekuwa rasmi ningekuwa na taarifa na hata maamuzi yake ningeyafahamu.”
“Kwa ufafanuzi zaidi ningekushauri uwasiliane na msaidizi wa Askofu ambaye ndiye msemaji wa Dayosisi ya Kaskazini Kati,” alisisitiza Mchungaji Lekashu ambaye inaelezwa kwamba ni mfuasi mkubwa wa Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo.
Wiki mbili zilizopita Bodi ya Dayosisi hiyo chini ya Uenyekiti wa Israel Ole   Karyongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa KKKT, ilimtimua kazi meneja wa hoteli ya   Corridor Springs inayomilikiwa na Dayosisi hiyo, John Njoroge kwa ubadhirifu wa   fedha za hoteli hiyo. 
Hata hivyo, Ole Karyongi naye katika kikao cha Desemba 15 mwaka huu  kilichohudhuriwa na wachungaji na wakuu majimbo walimtaka Mwenyekiti huyo  kuwajibika kwa kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia vizuri mali za Dayosisi  hiyo.
Kasheshe ya yote haya imetokana Dayosisi hiyo kudaiwa deni la Sh bilioni 11 na moja  ya benki kubwa hapa nchini.
Dayosisi hiyo imeshapewa muda wa kufikia Desemba 31 mwaka huu iwe imelipa deni hilo, vinginevyo mali za kanisa zitakamatwa na kupigwa mnada kufidia deni hilo, ikiwemo hoteli hiyo.
Habari zilisema kuwa uongozi wa Dayosisi uliweka hospitali ya rufaa ya Seliani  inayomilikiwa na kanisa kuwa dhamana.
Taarifa zilisema kuwa iwapo deni hilo halitalipwa ndani ya muda huo huenda hospitali  hiyo ikapigwa mnada, hatua ambayo inapingwa vikali na waumini wa kanisa hilo.

CHEKA TARATIBU...

Mshereheshaji katika harusi moja alikuwa akimsifia Bi Harusi kwa kusema, "Jamani tangu nimfahamu huyu Bi Harusi huwa havai kabisa nguo za ndani!" Ukumbi mzima ukabaki midomo wazi. Mshereheshaji akaendelea, "Narudi tena kwa msisitizo sijakosea. Bi Harusi huyu huwa havai kabisaa nguo za ndani. Yeye siku zote ni za kutoka Italia, Ujerumani, Dubai, Marekani na Uingereza!" Duh, balaa…

JICHO LA TATU...


AFARIKI BAADA YA KULA MAYAI MABICHI 28 MFULULIZO...

Mtu mmoja raia wa Tunisia amefariki baada ya kula mayai mabichi 28 katika ushindani wa kuwekeana dau.
Dhaou Fatnassi, mwenye miaka 20, anadaiwa kuwekeana dau na rafiki yake kwamba anaweza kula mayai mabichi 30 mfululizo, kwa makubaliano ya kulipwa kiasi cha fedha ambacho hakikuwekwa bayana.
Dhaou, anayetokea mji wa Kairouan ulioko kaskazini-mashariki mwa Tunisia, alifanikiwa kula mayai 28 kabla ya kuanguka huku akiugulia maumivu makali ya tumbo.
Alikimbizwa katika hospitali ya jirani lakini alitangazwa amefariki muda mfupi baada ya kufikishwa hapo, redio ya eneo hilo ya Shems FM iliripoti.
Wakati mayai yaliyopikwa vema ni chanzo kikuu cha protini na sehemu ya mlo wenye afya, mayai mabichi yanaweza kusababisha sumu na yanaweza kuwa na bakteria.
Kama unaandaa chakula kinachohitaji mayai mabichi, kama mayonizi au ashikilimu, tumia mayai yaliyochemshwa kuepuka hatari mbalimbali.

Friday, December 28, 2012

JENERALI ALIYEONGOZA VITA VYA GHUBA AFARIKI DUNIA...

  
Jenerali wa Marekani, Norman Schwarzkopf, ambaye aliongoza majeshi ya Marekani na ya ushirika yaliyoyatoa majeshi ya Iraqi kutoka Kuwait mwaka 1991 amefariki mjini Tampa, Marekani. 
Jenerali Schwarzkopf ndiye aliyeongoza vita ya Ghuba (Operation Desert Storm) ambayo ndio ilisaidia kuikomboa Kuwait kutoka kwa Dikteta wa Iraqi, Saddam Hussein mwaka 1991, amekufa akiwa na umri wa miaka 78. 
Schwarzkopf maarufu kama "Stormin' Norman," amefariki kutokana na matatizo ya nimonia akiwa Tampa, ambapo alistaafu akiwa na cheo cha Kiongozi Mkuu wa Kamandi ya Kati ya Marekani. 
Rais wa zamani wa Marekani, George H. W. Bush, ambaye naye amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa walio kwenye uangalizi maalumu mjini Texas, alikuwa wa kwanza kutoa salamu za msiba kwa kifo cha kamanda huyo ambaye ndiye alimchagua mwenyewe kuongoza vita ambayo iliwaweka kwenye chati wote wawili. 
"Barbara na mimi tunaomboleza kwa kumpoteza shujaa halisi wa Marekani na mmoja wa kiongozi mahiri wa jeshi katika kizazi chake,” alisema. 
Wakati wa vita ya kuikomboa Kuwait, Jenerali Schwarzkopf aliongoza askari 425,000 wa Marekani ambao waliungana na wanajeshi 118,000 wa ushirika kutoka mataifa mengine na kufanikiwa kuharibu mashine za vita za Saddam na kumtoa Kuwait bila kumng’oa madarakani. 
Jenerali Schwarzkopf alizaliwa Trenton, New Jersey mwaka  1934.

MWIMBAJI WA KIBAO CHA "RESCUE ME" AFARIKI DUNIA...

  
Mwimbaji Fontella Bass, aliyejizolea umaarufu mkubwa kutokana na kibao chake kilichotikisa mno mwaka 1965 cha "Rescue Me" amefariki dunia juzi Jumatano mjini Missouri. Amefariki akiwa na umri wa miaka 72.
Kwa mujibu wa familia ya Fontella, mwimbaji huyo alifariki katika Hospitali ya St. Louis kutokana na matatizo aliyokuwa akisumbuliwa nayo kufuatia ugonjwa wa moyo aliopata wiki tatu zilizopita. Bass pia amekuwa akikumbwa na maradhi ya kupooza mara kwa mara tangu mwaka 2005.
Nyota huyo wa miondoko ya R&B ametamba na vibao vyake kadhaa katika maisha yake ya muziki ikiwa ni pamoja na "You'll Miss Me (When I'm Gone)" na "Don't Mess Up a Good Thing" -- lakini hakuna kilichofikia mafanikio ya juu kama "Rescue Me."

WANAWAKE WALIOZAA NA BWANA HARUSI WATIBUA NDOA KANISANI...

Altare ya Kanisa Katoliki Parokia ya Familia Takatifu, Sumbawanga ambako ndoa hiyo ilikuwa ifungwe.
Wakati Wakristo wakiungana kusherehekea Sikukuu ya Krismasi usiku wa Desemba 24, Bwana harusi, Crispin Saadani (34) aliyekuwa akisherehekea siku hiyo kwa kufunga ndoa na mchumba wake, alijikuta akizuiwa kuweka ahadi hiyo ya maisha baada ya wanawake wawili alioishi na kuzaa nao, kuingilia kati.
Akiwa ndani ya jengo la Kanisa Katoliki, Jimbo la Sumbawanga, Parokia ya Familia Takatifu na mchumba wake aliyetambulika kwa jina moja la Elizabeth, bwana harusi huyo mtarajiwa alijikuta akizuiwa kupanda madhabahuni na wanawake wawili waliojitokeza huku wakijitambulisha kuwa ni wake zake.
Wakati Padri Boniface Nyama akijiandaa kufunga ndoa hiyo, wanawake hao, Maua Chatakwa na Mwasiti Mbegele (27) walifika kanisani hapo na kumuita mmoja wa wa  wazee wa kanisa hilo.
Akisimulia kisa hicho, Mzee huyo wa Kanisa ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Crispin na mchumba wake, siku hiyo saa sita usiku katika  mkesha  wa Krismasi walikuwa miongoni mwa  maharusi  watarajiwa 32 waliokuwa wameketi  katika  benchi  wakisubiri zamu  zao  ili  wapande madhabahuni kufungishwa ndoa  na Padri Nyama.
Alisema Mwasiti na Maua walitinga kanisani humo, wakamwita  na kumweleza kuwa wamemfuata  bwana wao ambaye wamesikia  anafunga  ndoa na mwanamke mwingine huku wakitoa ishara za kumwonesha.
Mwasiti ambaye ni mkazi  wa Bangwe mjini hapa anayejishughulisha na ufundi  wa kushona nguo za kike, alidai kuishi kinyumba na Crispin na kuzaa naye mtoto  aitwaye Henry mwenye umri wa mwaka na nusu.
Naye Maua, mkazi wa Jangwani mjini hapa, alidai aliishi kinyumba na Crispin na kuzaa naye watoto wawili.
Akisimulia hali ilivyokuwa, Mwasiti  alidai aliishi kinyumba  na mume huyo na kuzaa naye mtoto wa kiume, Henry,  lakini  walitengana  baada ya  kubaini kuwa  mumewe alikuwa  na wanawake  wengine  wawili  zaidi ambao  ni Maua  na Elizabeth.
“Nilipomtaka aachane nao alikataa  na kusema kuwa  ataishi nao kama wake zake. Alianza kutupangia zamu,  lakini  nilishindwa  pale alipoenda kulala  kwa Maua siku tatu  ya nne nilikusanya  nguo  zake  na kupeleka huko, ukawa mwisho wetu, ” alidai Mwasiti na kuongeza kuwa  kisa hicho kilitokea mwaka  huu. 
Mwasiti alikiri aliposikia Crispin anataka kumuoa Elizabeth, alimshawishi Maua wakamwekee kizuizi ili tu asifunge ndoa na Elizabeth ndipo walipokodi teksi iliyowafikisha  kanisani hapo  saa tano usiku.
Kwa mujibu wa  Mwasiti  baada ya kueleza mkasa  huo  kwa Mzee wa Kanisa, walikaribishwa katika moja ya chumba kanisani  hapo na kukutana na baadhi ya mapadre na wazee wa Kanisa na makatekista.
Alidai baada ya mjadala mrefu ilikubaliwa kuwa shauri hilo  lifikishwe  siku  inayofuata  kwa Paroko wa Kanisa hilo, Padri Leonard Teza, ambaye pia ni Mwanasheria wa Jimbo.
Mzee huyo alikiri kumfuata Crispin ambaye ni mkazi wa Utengule katika Manispaa ya Sumbawanga, alipoketi na mchumba wake akisubiri kupanda madhabahuni na kumuomba atoke nje ya Kanisa kwa dharura na wakaishia kuahirisha ndoa hiyo.   
Mwasiti  ambaye alikuwa muwazi kwa gazeti hili, alidai Crispin aliitwa na kukiri  kuwa  anawafahamu  na amezaa  nao huku wao  wakisisitiza kuwa wapo tayari  afunge ndoa  lakini  awaeleze jinsi atakavyowatunza watoto hao watatu.
“Crispin alikubali kutupatia mtaji wa Sh 100,000 kila mmoja wetu  huku mimi  akidai atanipatia fedha hizi za mtaji Aprili 25, mwaka kesho na mwenzagu Maua aliahidiwa kupewa  kiasi  hicho cha fedha.
“Pia aliahidi kutoa Sh 240,000 na seti ya TV ya inchi 9  aliyochukua kwake (Mwasiti) ifikapo Machi mwaka huu,” alisema  Mwasiti.
Kwa mujibu wa madai ya baadhi ya mashuhuda, wazazi  wa bibi harusi  walisema ndoa hiyo isifungwe tena kwa kuwa bwana harusi amewafedhehesha  huku baadhi ya wakazi  wa  mjini  hapa wakimtuhumu bwana harusi kwa kusababisha hayo yote.
“Kosa hapa  wa kulaumiwa ni huyu bwana harusi, kwa nini  asiwafahamishe  wale wake zake wengine kuwa anatarajia  kufunga  ndoa?” Alihoji mmoja wa mashuhuda.
Akizungumza  kwa njia  ya simu jana, Padri Teza alikiri kutokea  kwa  mkasa huo, lakini  hatimaye alisema baada ya kukutana  na wanawake hao walifikia makubaliano na  hatimaye ndoa hiyo ilifungwa Jumatano asubuhi.

POLISI WAKAMATWA KWA KUUA MWANAKIJIJI KIGOMA...

Kamanda Fraiser Kashai.
Jeshi la Polisi  mkoani Kigoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumpiga na kusababisha kifo cha mkazi wa kijiji cha Herushingo, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, Gasper Mussa.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Fraiser Kashai, aliwataja askari hao kwa waandishi wa habari mjini hapa kuwa ni mwenye namba NCC 8622 Koplo Peter na G.1236 Konstebo Sunday. Alisema wawili hao wanadaiwa kumpiga Mussa walipokuwa kwenye kilabu cha pombe usiku wa Sikukuu ya Krismasi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Kashai, Mussa alifariki siku moja baada ya kupata kipigo hicho alipokuwa akipelekwa hospitalini baada ya kukaa mahabusu kwa siku moja.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kashai alisema siku ya tukio, Mussa na askari hao walikuwa wakinywa pombe katika kilabu cha pombe na wakati wakinywa, ikatokea vurugu ambapo inadaiwa kusababishwa na Mussa kukataa kulipa pombe aliyokunywa.
Baada ya Mussa kukataa kulipa, Kamanda Kashai alisema askari hao ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Kasulu, walianza kumuadhibu kwa kumpiga na baadaye walienda kumlaza mahabusu.
Hata hivyo, siku iliyofuata, Kamanda Kashai alisema Mussa alizidiwa ndipo Mkuu wa Kituo cha Polisi Herushingo, alianza jitihada za kumpeleka Mussa hospitali, lakini alifariki mikononi mwa polisi kabla ya kufikishwa hospitali.
Alisema baada ya tukio hilo, alituma askari wake kufuatilia kwa undani kujua kile kilichotokea ili wachukue hatua.
Kwa sasa Kamanda Kashai alisema hatua za kijeshi kwa askari hao zinaendelea  ikiwa ni pamoja na kuwavua hadhi ya kijeshi waliyonayo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika tukio lingine Polisi mkoani Kigoma inamshikilia Hassan  Shija, mwalimu wa fani ya umeme katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) mkoani Kigoma kwa tuhuma za kumpiga mapanga na kumjeruhi mke wake sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Kashai alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Rida Mbili ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni na kwamba chanzo cha mgogoro huo ni wivu wa mapenzi.

WAUMINI KKKT WAAPA KUMTETEA MCHUNGAJI ALIYETIMULIWA...

Askofu Thomas Laizer.
Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, wamekuja juu na kuahidi kuandamana kupinga hatua ya kanisa hilo kumvua cheo na kumfukuza Mchungaji Philemon Mollel aliyekuwa Kiongozi wa Usharika wa Ngateu katika Jimbo la Arusha Magharibi.
Hatua ya waumini hao imekuja baada ya Mchungaji Mollel kutuhumiwa kushupalia suala la Kanisa hilo kuchangisha waumini wake fedha ili kulipa deni linalodaiwa na benki katika kuiokoa Hoteli ya Corridor Springs, mali ya KKKT Dayosisi ya Kati, inayoongozwa na Askofu Thomas Laizer.
Katika mazungumzo kwa simu na kwa ujumbe mfupi wa maneno waliotuma baada ya kuandikwa taarifa kuhusu mgogoro ndani ya Dayosisi hiyo, waumini hao wameapa kwamba hawatakubali Mchungaji Mollel afanywe mbuzi wa kafara.
“Mimi ni Msharika wa kawaida kabisa, muumini wa kawaida kabisa wa KKKT, nashukuru sana kwa taarifa yenu ya leo (juzi). Ni kweli mliyoandika, Mchungaji Mollel amesimamishwa na sisi hatumuoni hapa kwa sababu tumeletewa Mwinjilisti, tunashangaa Mchungaji wetu yuko wapi,” alisema muumini wa usharika huo anayeishi katika Mtaa wa Kiranyi.
Muumini huyo ambaye jina tunalo, alisema hatua hiyo imewashangaza kwa sababu Mchungaji Mollel amekuwa mkweli, kwa kuwaeleza kuhusu waraka wa kuchangia kuokoa hoteli hiyo ya KKKT, lakini jambo linalowashangaza wao (waumini) ni jinsi gani faida ya hoteli hiyo inavyotumika.
“Sisi tuliyajua haya, kwa sababu Mchungaji alitueleza akijua madhara ya kutueleza jambo hili, hawataki ukweli hawa. Sasa inakuwaje sisi tuchangishwe ili kulipia hasara, faida ya hoteli ilikwenda wapi? Tunataka maelezo ya kina, kuna matatizo KKKT, na lazima yaanikwe ili kulisaidia Kanisa,” aliongeza muumini huyo.
Alisema kutokana na hatua iliyochukuliwa dhidi ya Mchungaji wao, hawatakubali kwa sababu wanaona ametolewa kafara kwa kuwa mkweli na wataandamana kuhakikisha anarejeshwa madarakani.
“Huyu Mchungaji wetu ni mtu mkweli na mchapakazi. Amekuja hapa ametusaidia sasa tumejenga Kanisa letu na liko katika hatua ya kuweka tiles (marumaru). Na sisi tulifikiri faida ya hoteli ingetumika kutusaidia sisi tuliojenga Kanisa tulikamilishe, lakini tunashangaa tunatakiwa kulipia hasara.
“Kwa kweli hatutakubali kwa sababu kuna matatizo katika kanisa letu, hata shule tunajenga, lakini sisi watu wa kawaida, hatupeleki watoto wetu kwa sababu gharama ni kubwa. Sisi tunajenga kwa faida ya nani? Ndio maana wanaosema ukweli wanafukuzwa ili kuficha matatizo,” aliongeza muumini huyo.
Habari tulizozipata baadaye jana, zilieleza kuwa waumini wanaotoka katika Dayosisi hiyo ya Kaskazini Kati, katika Jimbo la Arusha Magharibi walikutana katika hoteli moja ya jijini Arusha (jina tunalo) jana jioni kupanga maandamano ya kupinga kufukuzwa kwa Mchungaji Mollel.
Wakati muumini huyo akisema hayo, waumini wengine waliotuma ujumbe mfupi wa maneno katika simu (sms) walidai kuwa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, imegubikwa na ufisadi na uonevu.
“Tunashukuru mnavyofuatilia hizo habari na kutupasha. Mimi niko ndani ya dayosisi hii. Mwenye msimamo ni Mchungaji Mollel. Hatua aliyochukuliwa ni kuwanyamazisha wengine kwenye hili jambo. Misaada inayotoka nje ya wafadhili ni mingi, wanaitumia huko mijini wanakotoka na haina udhibiti wala ukaguzi,” alidai muumini mwingine.
Mwingine alisema kufukuzwa kazi kwa Mchungaji Mollel siyo jambo zuri, “ila moto kwa Wakristo utawaka na bila Kanisa kuingilia kati, litashindwa kuuzuia.”
Mgogoro ndani ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati umeibuka baada ya waumini wake kupewa waraka wa kutakiwa kila mmoja kuchangia Sh 20,000 ili  kunusuru mali za kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya Hoteli ya Corridor Springs kudaiwa Sh bilioni 11 na benki moja nchini.
Hatua hiyo imepingwa na waumini hao na baadhi ya wachungaji akiwemo Mollel anayetaka wahusika wa kadhia hiyo wachukuliwe hatua; lakini akageuziwa kibao yeye na kufukuzwa na kuvuliwa madaraka ya kutoa huduma za kichungaji katika kanisa hilo nchini.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya kanisa hilo vilieleza kuwa hatua hiyo imetokana na Mchungaji Mollel kushindwa kutekeleza mambo matatu aliyotakiwa na Tume maalumu ya watu watatu walioteuliwa na Menejimenti ya Dayosisi hiyo na alipewa siku tatu kuomba radhi, lakini hakufanya hivyo.
Habari zilieleza kuwa walioteuliwa Desemba 14, mwaka huu na kwenda kumwona Mchungaji Mollel kutekeleza hayo ni pamoja na Msaidizi wa Askofu Mchungaji Solomoni Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo Arusha Magharibi, Mchungaji Godwini Lekashu na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Israel ole Karyongi.