Friday, August 31, 2012

SUMATRA YATANGAZA VITUO VYA 'KUCHIMBA DAWA' NJIANI...

Abiria wa mabasi yaendayo mikoani kuanzia kesho watalazimika kuwa na fedha za ziada mifukoni kwa ajili ya kulipia huduma ya choo.
Fedha hizo zitatumiwa kulipia huduma hiyo baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), kutangaza rasmi kwamba utaratibu wa abiria kushuka maporini na kujisaidia imepigwa marufuku.
Katika Mkutano wa Nane wa Bunge la Jamhuri uliomalizika hivi karibuni Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kukataza ‘uchimbaji dawa’ porini ifikapo leo.
Baada ya agizo hilo, Mamlaka hiyo ilifanya kikao na wasafirishaji ili kuweka mikakati kwa pamoja juu ya utekelezaji wake ambapo maeneo ya kujisaidia yalibainishwa ili abiria wajulishwe.
Hivyo kwa mujibu wa tangazo la Sumatra kwenye vyombo vya habari jana, vitu kadhaa viliainishwa katika barabara tano kuu ambazo kwa upande wa barabara ya Dar es Salaam – Mbeya, vituo vilivyoainishwa ni vya mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na Njombe.
Vituo hivyo ni Ruvu iliko hoteli inayotoa huduma hiyo bure, Chalinze kuna hoteli inahudumia kwa Sh 200; stendi kuu ya mabasi ya Msamvu huduma inatolewa kwa Sh 200 na Ruaha Mbuyuni hoteli ya Al Jazeera inatoa huduma bure.
Kitonga, hoteli ya Comfort inahudumia bure, stendi ya Ipogoro malipo ni kati ya Sh 100 na 200, Mafinga abiria watalazimika kulipia kiasi kama hicho na Makambako malipo yatakuwa kati ya Sh 200 na 300.
Katika njia ya Dar es Salaam - Mwanza; ambapo magari yanapitia mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga, ‘dawa itachimbwa’ Msamvu, Gairo kuna hoteli ambayo inahudumia bure, Badueli umbali wa kilometa tatu kutoka Dodoma mjini pia huduma ni ya bure.
Singida mjini iliko stendi ya mabasi huduma hiyo pia itapatikana kwa malipo ya Sh 200, kituo cha mabasi Nzega mjini huduma italipiwa Sh 200 na katika stendi kuu mjini Tabora malipo ni Sh 200 pia.
Katika stendi kuu ya mabasi Shinyanga mjini, huduma hiyo italipiwa Sh 200 na kwa waendao Kagera kupitia Kahama huduma itapatiokana stendi kuu ya mabasi kwa kati ya Sh 200 na 300 huku Mwanza mjini katika stendi kuu ya mabasi pia huduma italipiwa Sh 200.
Kwa waendao Kagera baada ya kutoka Kahama, huduma zitapatikana Ushirombo kwa Sh 100 na Sh 500 ambapo pia watapata fursa ya kuoga, Chato Sh 200, Muleba Sh 200 na Bukoba Sh 200.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa abiria watokao Kigoma kabla ya kufika Kahama watahudumiwa Kasulu kwa Sh 200, Kibondo kwa Sh 200 na Runzewe kwa Sh 200 pia.
Upande wa njia ya Dar es Salaam -Tanga, abiria watahudumiwa katika kituo cha mizani Msata bila gharama yoyote sawa na Segera.
Kwa njia ya Dar es Salaam - Moshi, Arusha na Manyara, huduma zitapatikana Korogwe katika hoteli mbili bila malipo na Mombo ambako pia kuna hoteli isiyotoza malipo.
Lakini Same, Mwanga, Himo, Moshi Mjini na Boma Ng’ombe, huduma itatolewa kwa Sh 200 na Arusha huduma itapatikana stendi kuu kwa Sh 200 sawa na ilivyo kwa Manyara.
Njia ya Dar es Salaam-Lindi-Mtwara, eneo la Nangurukuru kuna hoteli iitwayo StarCom ambayo itatoa huduma bila malipo, ambapo Lindi huduma hiyo haitalipiwa huku Mtwara ikilipiwa Sh 200 ingawa haitoshelezi mahitaji.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema lolote kuhusu watoto na wale ambao wana matatizo ya kupata haja ndogo kila baada ya muda mfupi.

WAGOMBEA 'WALIOBEBWA' NA MAKUNDI CCM WATOSWA...

Mary Chatanda
Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Arusha, imepinga uteuzi wa wagombea uongozi wa jumuiya za chama hicho kwa madai ya ‘kubebwa’ na kundi lililopo ndani ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alisema jana kwamba katika wilaya ya Monduli, Halmashauri hiyo imekataa uteuzi wa wagombea wa Umoja wa Vijana (UVCCM) kutokana na uteuzi huo kuwa wa kundi fulani ambalo hakulitaja.
Mbali na Monduli, Chatanda alisema katika wilaya za Longido na Karatu, halmashauri hiyo ilikataa uteuzi wa wagombea katika Jumuiya ya Wazazi kutokana na sababu hizo hizo.
Alifafanua kuwa katika wilaya hizo mbili, majina ya baadhi ya wagombea ambao walionekana kutounga mkono kundi fulani ambalo pia hakuwa tayari kulitaja, yalikatwa.
Katibu huyo ambaye ana msimamo wa kutaka viongozi ndani ya chama kufuata utaratibu na kuacha makundi, alisema baada ya kugundua kasoro hizo, kikao cha Halmashauri kiliagiza vikao husika vya uteuzi katika wilaya hizo kupitia upya na kurekebisha kasoro hizo ndani ya wiki moja.
Alisema baada ya kasoro hizo kurekebishwa, viongozi husika wanapaswa kakabidhi mapendekezo hayo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa iliyokasimiwa madaraka ya kuthibitisha uteuzi huo.
Chatanda alisema katika wilaya tatu zilizobakia, Arusha, Arumeru na Meru, uteuzi wake umekubalika na zitaendelea na uchaguzi wake kuanzia Septemba mosi hadi 5 mwaka huu ili kuwapata viongozi katika nafasi hizo.
Katika nafasi ya uenyekiti wa Mkoa, kikao hicho kilipitisha majina ya wagombea watano ambao walijitokeza kuwania nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa CCM anayetetea nafasi yake Onesmo ole Nangole amejitosa tena kutetea nafasi hiyo na atachuana na Mganga Mkuu mstaafu wa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Dk Salash Toure.
Wengine wanaowania nafasi hiyo ni Hamis Shaaban, mfanyabiashara Onesmo Metili na aliyepata kuwa Shekhe wa Mkoa wa Arusha, Adam Chora.
Katika nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi, Lootha Sanare anatetea nafasi hiyo na atachuana na Anna Msuya, Gasper Kishumbua, Isack Capriano na Hagai Kissali.
Nafasi ya Katibu wa Fedha na Uchumi kikao hicho kiliwapitisha Juma Losini, anayetetea nafasi hiyo, Violeth Mfuko, Julius Mungure, Hilal Sood, Metili, Victor Mollel, Julius Laizer na Kissali.
Kikao hicho pia kilibariki wagombea uenyekiti wa wilaya sita za mkoa ambapo katika wilaya ya Arusha kuna wagombea saba na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na katika wilaya zingine, wapo 18.
Katika wilaya ya Arumeru, wagombea uenyekiti wako tisa na NEC wanne; Meru uenyekiti kuna wagombea wanane na NEC watano; Monduli uenyekiti wako sita, NEC watatu; Longido uenyekiti watatu, NEC sita; Karatu uenyekiti sita, NEC tisa na Ngorongoro uenyekiti wawili, NEC saba huku mgombea ujumbe wa NEC Taifa wa mkoa kwenda kapu ni mmoja Sylvester Meda.
Chatanda alisema kikao hicho pia kilipitisha uteuzi wa wagombea wa nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya na nafasi za ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya za Arusha, Arumeru, Meru, Karatu, Longido na Monduli.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kilipitisha majina mawili ya kuwania nafasi za udiwani katika uchaguzi mdogo kwa kata mbili za Daraja Mbili, Arusha na Bangata, Arumeru baada ya madiwani wao kufariki dunia.
Katika kata ya Daraja Mbili, kikao hicho kilimpitisha Phillip Mushi kugombea, baada ya kupita bila kupingwa wakati kwa kata ya Bangata, kilimbariki Olais Mfere, baada ya kupata kura 977 kati ya 1,158 sawa na asilimia 84.4.
Mfere aliwashinda David Mollel aliyepata kura 154 na Ezekiel Lameck aliyepata kura 27.
Naye Namsembaeli Mduma anaripoti kuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan ‘Zungu’, ameshindwa kurejesha fomu za kugombea uenyekiti wa Taifa katika Umoja wa Wazazi wa Jumuiya ya CCM.
Kutokana na hatua hiyo, Mbunge huyo ameondolewa kwenye orodha ya watakaoshiriki uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba.
Ingawa Zungu alilieleza gazeti hili kuwa hagombei tena, lakini Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Khamis Dadi alidai mbunge huyo hakutoa sababu wala kuwasiliana na uongozi wa Jumuiya hiyo kuhusu uamuzi wake, hadi muda wa kurejesha fomu ulipokwisha saa 10 jioni ya juzi.
Pamoja na Zungu, watu wengine 15 wakiwamo wabunge na wafanyabiashara, walichukua fomu hizo zilizoanza kutolewa Agosti 24, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, akiwamo mwanamke mmoja tu, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata.
Wengine waliochukua fomu ya kugombea nafasi hiyo na kuzirejesha kwa muda uliopangwa ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza na Mbunge wa Chalinze, Said Bwanamdogo.
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kuanzia mwaka 1989 hadi 2006, Abiud Maregesi, John Machemba, Mosha Konrad, William Bocco, Maseke Muhono, Manley Mgata, Dk Muzamil Kalokola, Alfred Mwambeleko, Alphonce Siwale, Salim Chicago na Abdalla Bulembo.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo wa masuala ya siasa na oganaizesheni, Ali Haji alisema licha ya muda wa kurejesha fomu katika maeneo yote nchini kumalizika, wanaendelea kupokea taarifa za mikoani kwa nafasi mbalimbali kujua idadi ya watakaochuana katika uchaguzi huo.
"Hao 15 waliozungumziwa ni wa Dar es Salaam pekee kwa sababu taarifa za waliochukua fomu mikoani bado tunazipokea kutoka kwa wenzetu wa huko. Kwa ufupi, wanatupa taarifa za waliorudisha, hakuna anayepokea fomu tena kwa sasa," alisema.

KATIBU KATA CHADEMA ATAPELI KWA JINA LA KAGASHEKI...

Kamanda Liberatus Sabas
Tuhuma za ufisadi katika siasa zimeendelea kukisakama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo jana Katibu wa Kata ya Endulen wilayani Ngorongoro, Denis Paulo (33) alikamatwa na Polisi kwa madai ya kutaka kufanya utapeli.
Paulo ambaye ni mtumishi wa chama hicho kinachojinasibu kwa kupiga vita ufisadi, alikamatwa na Polisi Arusha kwa tuhuma za kutaka kutapeli wafanyakazi wawili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Sh milioni 16.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kukamatwa kwa Katibu huyo na kusema Paulo aliwapigia simu wafanyakazi wawili wa NCAA Agosti 27 saa 6 mchana kwa nia ya kuwatapeli.
Alidai kwamba baada ya kupiga simu kwa wafanyakazi hao, Paulo ambaye chama chake kimekuwa kikiituhumu Serikali kwa ufisadi, alijitambulisha kwa jina la David Kagasheki na kudai kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii bila kujua kwamba Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ni Maimuna Tarishi.
Katika kujitambulisha huko kwa mujibu wa madai ya Kamanda Sabas, Paulo alidai kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameunda Tume ya kuchunguza tuhuma zilizofikishwa wizarani dhidi ya Menejimenti ya NCAA na yeye ndiye Mwenyekiti.
Ilidaiwa kuwa Paulo alisema yeye na wajumbe wengine sita wa Tume hiyo wako Arusha na jana wangefika ofisi za Mamlaka hiyo kwa mahojiano zaidi.
Kutokana na umuhimu wake katika Tume hiyo, Kamanda Sabas alidai Paulo aliomba fedha kwa wafanyakazi hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa upelelezi zaidi.
Inadaiwa Paulo aliomba kila mfanyakazi atoe Sh milioni 6 na mwingine Sh milioni 10 ili awasaidie kuzima sakata hilo. Alisema wafanyakazi hao walitoa taarifa Polisi wakaweka mtego na kumkamata Paulo kati ya saa 8 na saa 9 alasiri jijini Arusha na hadi sasa inaendelea kumshikilia kwa mahojiano zaidi.
Katibu wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alithibitisha kuwapo tuhuma hizo dhidi ya Paulo na kuelezea kushangazwa na madai hayo, huku akidai kuwa hizo ni mbinu za kukichafua chama na kuahidi kulifuatilia suala hilo kwa kina.
Hivi karibuni bungeni Dodoma, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema baadhi ya wabunge, wakiwamo wa Chadema walihongwa na kampuni za mafuta ili kuhujumu uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hujuma hizo, zilidaiwa kumlenga Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliackim Maswi ili waondolewe katika nafasi zao.
Viongozi hao walidaiwa kukiuka Sheria ya Ununuzi kwa kuzinyima baadhi ya kampuni fedha za zabuni ya kununua mafuta kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kufua umeme, ingawa katika uamuzi huo waliokoa zaidi ya Sh bilioni 6 kila mwezi.
Wakati hali ikiwa hivyo Arusha, jijini Dar es Salaam Jumuiya ya Wazazi ya CCM imeelezea kuchukizwa na mwenendo unaofanywa na Chadema kwa madai kuwa imekuwa ikisababisha uvunjifu wa amani na machafuko ya kisiasa nchini.
Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la CCM kupitia Jumuiya ya Wazazi, Dk Salim Chicago alisema hayo jana wakati akitoa tamko la Jumuiya hiyo kuhusu machafuko yaliyotokea Morogoro juzi.
Alisema Jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es Salaam inalaani mauaji yaliyotokea Morogoro baada ya Chadema kukiuka agizo la Jeshi la Polisi kuwataka wasiandamane.

CHEKA TARATIBU...

Mlevi mmoja katika kubatizwa akazamishwa kwenye maji na kisha Mchungaji akamwambia, "Kuanzia sasa wewe sio Rashid, sasa ni Yohana!" Kesho yake jamaa akiwa nyumbani akabanwa sana na kiu ya pombe. Moja kwa moja akaenda kwenye jokofu na kuchukua bia moja na kuizamisha kwenye ndoo ya maji na kuitoa kisha akasema, "Kuanzia sasa wewe sio Bia, sasa ni Soda!" Akaifungua na kuanza kunywa taratibu..! Ama kweli walevi noma...

ZIRO PLUS...

MAPACHA WASIOPENDA KULA WAFARIKI DUNIA...

Mapacha wawili wanaofanana mno, ambao wamekuwa maarufu kupitia mapambano yao makali dhidi ya ugonjwa wa kukosa hamu ya kula, wamekufa kwa ajali ya moto ulioteketeza nyumba yao.
Clare na Rachel Wallmeyer wenye miaka 42, walikuwa baada ya moto kulipuka nyumbani kwao huko Geelong, karibu na Melbourne, mmoja akiteketea kwa moto, mwingine akipata majeraha makubwa ya moto na kufariki muda mfupi baadaye akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Lilikuwa ni janga lililokatisha maisha ya ghasia, kwa madada walioonekana kwenye Televisheni ya Australia mara kadhaa kuzungumzia kuhusu ugonjwa wao wa kukosa hamu ya kula ambao uliwafanya wote wawili kukonda na kuishi kama wakiwa kama mifupa mitupu na kuwa tatizo pia kwa wazazi wao, wafanyakazi wa jamii na polisi.
Katika mapitio ya kutia uchungu ya maisha yao walisema katika miaka ya hivi karibuni kwamba hawakuwahi kuwa katika mapenzi, hawakuwahi kupata kazi na wanaamini kwamba ilikuwa wakisubiri tu muda kabla hawajafa, na kwamba watakufa pamoja.
Vifo vyao kwenye moto inaaminika kuwa ni ajali ya kawaida, kwa mujibu wa wapelelezi kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Jinai cha Geelong ambao walisema kwamba uchunguzi wa awali haukubainisha matukio yoyote yenye kutia mashaka.
Hatahivyo kumekuwepo na taarifa kwa miaka kadhaa kuhusu wanawake hao kila moja ikidai kwamba wamekuwa wakijaribu kuuana.
Rachel alishitakiwa kwa kujaribu kumuua Clare baada ya polisi, ambao waliitwa nyumbani kwao kudai walishuhudia Rachel kwa mikono yake akiwa kamkaba dada yake kooni.
Mashitaka hayo baadaye yalifutwa.
Uwepo wao, uliwiana kati ya maisha na kifo, ndio ukapelekea kampuni za Televisheni kuwatafuta kwa ajili ya mahojiano baada ya mamlaka husika kufikiria kuwafungia katika harakati za kuwakinga wanawake hao wasijiue kwa njaa na 'kubadili kabisa maisha yao.'
Claire baadaye alifungwa na Mahakama ya Geelong kwa marukio kadhaa ya wizi, lakini pale Hakimu Ian von Einem kusema hakuwa na jinsi ila kumpeleka jela ili kumuepusha na vitendo vya kutaka kujiangamiza mwenyewe.
Dada yake pia alizipasua vichwa mamlaka pale alipokamatwa kwa kosa la kuendesha gari huku akiwa kalewa dawa za kulevya na alituhumiwa kumsukumia mtu mmoja kwenye njia ya treni.
Alihukumiwa kifungo cha miezi 21 jela.
Lakini pale walipoanza kupungua uzito katika kipindi cha miaka 20, uzito wa kila mmoja uliporomoka kwa kilo zisizopungua nne. Madaktari walisema walikuwa na mifupa kama ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 70 na 100.
Wazazi wao, Bob na Moya walikiri kwamba mapacha hao walipokuwa chini ya miaka 20 walihofia wangeweza kuwakuta wamefia kitandani kutokana na matatizo yao hayo.
Katika mahojiano kwenye kipindi cha Dakika 60 mapacha walitoa uzoefu wao wa kushitusha kuhusu tabia zao za kula.

ZIRO PLUS...

ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA MBARALI AFARIKI DUNIA...

Hawa Ngulume
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Hawa Ngulume amefariki dunia jana asubuhi katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu kwa muda mrefu.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alithibitisha kutokea kwa msiba huo ambapo alifafanua kuwa msiba uko nyumbani kwa marehemu Goba jijini Dar es Salaam.
"Ni kweli tumepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa mheshimiwa Ngulume ila bado hatujajua sababu ya kifo hicho tunasubiri taarifa ya madaktari wa Lugalo ambako alilazwa kwa muda wa wiki nzima," alisema Rugimbana.
Hata hivyo kwa mujibu wa Msemaji wa familia hiyo, Alhaji Mwenza, alisema Ngulume alifariki jana majira ya saa 4.25 asubuhi ambako alikuwa akitibiwa ugonjwa wa saratani ya mapafu.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali alizokuwa nazo marehemu ilikuwa azikwe leo saa saba mara baada ya sala ya Ijumaa nyumbani kwake Goba, lakini baadaye ratiba ilibadilika na leo anatarajiwa kusafirishwa kijijini kwao Kintiko mkoani Singida.
"Kwa mujibu wa watoto wake, kesho (leo) atasafirishwa kupelekwa Singida katika tarafa ya Kintiko ambako anatarajiwa kuzikwa keshokutwa (kesho) kama mambo yote yataenda sawa," alisema Mwenza.
Ngulume wakati wa uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ukuu wa wilaya katika wilaya za Kinondoni, Bagamoyo na Mbarali ambako ndiko alikostaafu wadhifa huo.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Ngulume.
Rais Kikwete alisema jana kuwa marehemu Ngulume, enzi za uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia uamuzi wake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuletea wananchi maendeleo sehemu zote alizotumikia.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana ilisema alipopewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya za Singida Mjini mkoani Singida, Kinondoni, Dar es Salaam na mara ya mwisho katika wilaya ya Mbarali, Mbeya.
"Nilimfahamu marehemu, enzi za uhai wake, akiwa kiongozi mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu uamuzi wake na hivyo kuthibitisha ukweli, kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza," alisema Rais Kikwete.
"Kutokana na msiba huo mkubwa, natuma salamu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu, Hawa Ngulume kwa kuondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia.
"Natambua machungu mliyonayo hivi sasa kwa kumpoteza mama wa familia, lakini nawahakikishieni kuwa niko pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa," aliongeza Rais Kikwete katika salamu zake.
Rais aliwataka wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu wanapoomboleza msiba wa mpendwa wao kwani yote ni mapenzi yake Mola. Alisema anamwomba Mwenyezi Mungu, aipokee na kuilaza mahali pema peponi roho ya marehemu.
Marehemu ameacha watoto wawili pamoja na wajukuu watano.

JICHO LA TATU...

Thursday, August 30, 2012

CHADEMA YAIKALIA KOONI POLISI MAUAJI YA MOROGORO...

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakina imani na Tume iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuchunguza mauaji yanayodaiwa kufanywa na Polisi mkoani Morogoro wakati wa maandamano ya chama hicho.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa taarifa juu ya tukio la mauaji ya muuza magazeti wa eneo la Msamvu, Ally Zona (38).
Alisema kuna mgongano wa taarifa kuhusu tukio hilo kutoka kwa mashahidi na Polisi, akidai kuwa kifo hicho kina utata na hakiwezi kuchunguzwa na Polisi.
"Kiundwe chombo kingine huru cha uchunguzi au Rais Kikwete (Jakaya) aingilie kati iundwe Tume huru kuchunguza kifo hiki, kwani hii ya sasa haiwezi kuchunguzwa na polisi kwani wao ni watuhumiwa," alisema Mnyika na kuongeza kuwa hata baadhi ya viongozi wa chama chake ni mashahidi.
Aidha, alisema chama hicho kwa kuheshimu sheria, kimeamua kusitisha operesheni ya vuguvugu ya mabadiliko iliyokuwa iendelee Iringa, na kuomba maelezo kutoka kwa Serikali na Polisi kuwa ni kwa nini vyama vingine vinaendeleza matukio ya kisiasa yenye halaiki ya wananchi huku Polisi wakiinyima Chadema ruhusa ya kufanya hivyo.
"Kwa mfano, Lindi Mjini kuna maandamano ya wafuasi wa CCM wanarudisha fomu kuwania nafasi za uchaguzi, huku polisi mikoani wakisema mikutano inayofanyika sasa inaingilia ratiba ya sensa," alihoji Mnyika.
Alisema kutokana na tukio la Morogoro ipo haja ya sheria ya vifo vyenye utata ianze kutumika sasa ili kupata Tume huru ambayo itashughulikia mgogoro wa Morogoro na kuupatia suluhu stahiki.
Kuhusu kusaidia matibabu ya majeruhi wa tukio hilo, Mnyika alisema chama hicho kitahakikisha kinatoa matibabu yao na kuwezesha maziko ya marehemu huyo.
Hata hivyo, hakuzungumzia sababu ya kufanya maandamano juzi huku sensa ikiendelea na kuja kushituka baadaye na kusitisha operesheni yao.

MZUNGU ANASWA NA KILO 4 ZA COCAINE KILIMANJARO...

Polisi nchini inamshikilia raia wa Lithuania kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya kokeni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Polisi Viwanja vya Ndege Dar es Salaam jana, anayeshikiliwa ni Christina Biskasevskaja (20) ambaye ni mwanafunzi, mwenye pasipoti namba LTY 231302121 iliyotolewa Lithuania Agosti 7.
Mshukiwa huyo alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) juzi saa 9.20 alasiri, wakati mzigo wake ukipita katika mashine ya ukaguzi uwanjani hapo.
Taarifa hiyo fupi ilisema Biskasevskaja alikutwa na mzigo wa kilo 4.4 akiwa njiani kwenda Ubelgiji kupitia Addis Ababa, Ethiopia na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopian.
Jeshi la Polisi halikutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo ambalo ni la aina yake kuhusisha raia wa kigeni ambaye ni mwanafunzi.
Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja, kuwa mwanafunzi huyo anasoma shule au chuo gani na wapi; na alikuwa nchini kwa madhumuni yapi.
Hata hivyo, inatia udadisi kuona kwamba pasipoti yake haina umri mkubwa, kiasi cha kutilia shaka kuwa huenda aliipata kwa ajili ya kuja nchini kuchukua ‘mzigo’ huo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza katika Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya hivi karibuni, alisema wakati mwingine hata viongozi wa kisiasa hujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuchangia kuendeleza vitendo hivyo katika jamii.
Pinda, ambaye hakufafanua kuhusu kuhusishwa kwa viongozi wa kisiasa katika dawa hizo, alitoa mfano wa Rais wa zamani wa Panama, Manuel Noriega aliyekamatwa na majeshi ya Marekani na kupelekwa nchini humo na kushitakiwa mwaka 1986.
Akizungumzia zaidi kuhusu biashara hiyo, Pinda alisema nchi inapokuwa kitovu cha dawa za kulevya, inajivunjia hadhi kimataifa na wananchi wake hushukiwa kila wanaposafiri nje ya nchi na hupata tabu katika viwanja vya ndege vya kigeni kwa kupekuliwa sana.
Alisema tatizo la dawa za kulevya bado lipo nchini na linazidi kukua kila mwaka ambapo Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama inajitahidi kupambana nalo.

MKONO MREFU WA SERIKALI: 'BAO' MPAKA PORINI...

Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro ambaye jina lake halikufahamika mara moja akisimamisha gari lililosheheni mizigo na abiria katika barabara ya Ifakara - Mlimba katika Kijiji cha Ihanga kilicho umbali wa kilometa 150 kutoka Tarafa ya Mlimba, kama alivyokutwa juzi.

CHEKA TARATIBU...

Polisi kamsimamisha dereva aliyekuwa akiendesha kwa kasi katika barabara moja mjini Iringa na mahojiano yaka kama hivi:
Dereva akaanza kujitetea, "Lakini afande, naweza kuelezea."
Afande akajibu kwa ukali: "Nyamaza, utakaa kwanza ndani hadi bosi wangu atakaporudi."
Dereva akaendelea kumsihi: "Lakini afande nilikuwa nataka kusema..."
Afande akadakia kwa ukali: "Kelele, unakwenda ndani!"
Baada ya masaa kadhaa Afande akamtazama yule Dereva na kusema huku akitabasamu: "Una bahati sana Bosi yuko kwenye harusi ya binti yake kipenzi...atakaporudi atakuwa mwenye furaha."
Dereva akasema kwa msisitizo: "Usijipe uhakika huo Afande, mimi ndio bwana harusi mwenyewe!" Duh...

KOMANDOO AFICHUA SIRI ALIVYOUAWA OSAMA, TUKIO KUTENGENEZEWA FILAMU...

Taarifa za askari aliyeshiriki kwenye shambulio la ghafla lililofanya na makomandoo wa SEAL Team Six kummaliza Osama bin Laden zimebainisha kwamba kiongozi huyo wa kundi la al-Qaeda alikutwa tayari ameshakufa wakati makomandoo hao wa Marekani wakivamia chumbani kwake katika himaya yake nchini Pakistan.
Kitabu cha 'No Easy Day: The Firsthand Account of the Mission That Killed Osama bin Laden, kiliandikwa bila kufahamika na mtu aliyetumia jina la Mark Owen, ambaye alikuwa mmoja wa timu ya makomandoo sita wa SEAL katika oparesheni hiyo ambaye alishuhudia kiongozi huyo wa ugaidi akikata roho Mei, 2011.
Nakala ya kitabu hicho iliyopatikana, inasema kwamba mpango haukuwa maarufu kwa kile kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba hiyo iliyoko Abbottabad.
Owen aliandika kwamba mfuasi huyo wa kikosi kidogo alishuhudia kiongozi huyo wa ugaidi alivyovamiwa kwenye chumba chake, na wapiganaji, waliokuwa wakipandisha ngazi kwa kasi kuelekea ghorofa ya tatu, wakifuatiliwa.
Alisema: "Tulikuwa umbali wa hatua zisizozidi tano kufika juu ndipo tuliposikia vishindo vikubwa vya milipuko ya bunduki. Siwezi kusema kutokana na sehemu nilipokuwa kama milipuko hiyo ililenga shabaha au la. Mtu huyo alitokomea kwenye chumba chenye giza."
Wakati vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kwamba Osama aliuawa katika shambulio na kutoonesha nia ya kunyamaza, askari huyo aliandika kwamba kiongozi huyo wa ugaidi alikuwa tayari akikaribia kukata roho.
Owen aliandika kwamba wakati Osama akiwa anakufa sakafuni, yeye na komandoo mwingine "tulielekeza silaha zetu kifuani mwake na kumimina risasi kadhaa. Risasi hizo zilimchana-chana na kuangusha mwili wake kwa kishindo sakafuni hadi alipotulia kabisa."
Kitabu hicho kilimuelezea Osama wakati huo alikuwa kavalia fulana yake nyeupe.
Wakati wa kupiga picha mwili wa kiongozi huyo wa ugaidi, bunduki mbili zilikutwa kwenye chumba hicho, lakini hakuna yoyote iliyokuwa na risasi.
'Owen" aliandika: "Hakuwa hata kajiandaa kwa ulinzi. Hakuna na nia yoyote ya kupambana. Kwa miaka kadhaa aliweza kuwaamuru wafuasi wake kuvaa fulana za kujitoa mhanga kugonga majengo kwa kutumia ndege, lakini hata hakunyanyua silaha yake.
Kitabu hicho mwanzoni kilipangwa kuwa kwenye mbao za maduka ya vitabu Septemba 11 lakini sasa kitakuwa mitaani siku saba kabla.
Kumeshazuka umkanganyiko mkubwa baada ya kubainika kwamba Pentagon, CIA, Ofisi ya Mkurugenzi wa Intelijensia, na hata Ikulu inaonekana hawakuwa na taarifa zozote kwamba kitabu hicho kilikuwa kikiandikwa.
Tawasifu yake inaweza kwenda kwenye filamu, baada ya kubainika Jumapili iliyopita kwamba Mwongoza filamu Steven Spielberg alikutana na Komandoo huyo mstaafu kujadili uwezekano wa kutengeneza filamu kuhusu alichokiona katika Oparesheni hiyo.
Zaidi ya Spielberg, ambaye aliongoza filamu ya 'War Horse' na 'Saving Private Ryan', Richard Plepler kupitia kampuni yake ya Dreamworks and HBO ameshakutana na mwandishi huyo.
"Bado yuko kwenye mazungumzo na Dreamworks na Spielberg," chanzo kimoja cha habari kimelieleza gazeti la The New York Post.
Hii itakuwa filamu ya tatu kuelezea habari ya shambulio la ghafla ambalo limeua mwanzilishi mwamba aliyepanga mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11.
'Zero Dark Thirty,' iliyoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Oscar, Kathryn Bigelow itazinduliwa Desemba 19. Kampuni ya Sony imerudisha nyuma tarehe ya uzinduzi kufuatia uchaguzi wa rais baada ya kufahamika kwamba Bigelow ilipewa ruhusa maalumu kuigiza filamu hiyo ndani ya Pentagon na katika ofisi za CIA.
Kampuni ya Weinstein imependekeza itatoa filamu yake kuhusu shambulio la ghafla la makomandoo nchini Pakistan lililofanyika Mei 2011 iliyopewa jina, 'Code Name Geronimo' kabla ya uchaguzi.
"Kama ilivyo kwa wafuasi wetu wa sasa au wastaafu wa jamii ya oparesheni maalumu, waandishi wana matakwa yao, na majukumu ya kisheria, kukabidhi kazi zao kwa ajali ya mapitio ya kiusalama kabla ya kuchapishwa," mkuu wa jeshi la wanamaji ameandika.
Muda si mrefu baada ya kutangazwa kitabu hicho, mtandao wa FoxNews.com ulimtaja askari huyo kuwa ni Matt Bissonnette mwenye miaka 36, ambaye amestaafu kazi hiyo mara tu baada ya shambulio hilo la ghafla la Osama.
Hadi Ijumaa, jina la mtu huyo, picha na umei wake ulipostiwa kwenye mtandao wa kijamii wa 'the Al-Fidaa Islamic Network', moja kati ya mitandao rasmi inayotumiwa na kundi la al-Qaeda, kwa mujibu wa Evan Kohlmann, muasisi wa kampuni ya usalama ya Flashpoint Global Partners yenye makazi yake mjini New York.
Ilifuatiwa na maoni ambayo yaliita kifo cha mtu huyo, ukiwamo mmoja uliosema, "O" Mungu, ua kila mmojawao," na mwingine ukisema kwamba, "O" Mungu, fanya mfano wake kwa dunia nzima na mpe siku za giza mbeleni."
Mchapishaji Dutton, kutoka kampuni ya Penguin Group, alizitaka taasisi za habari Alhamisi kuficha jina lake.
Lakini hiyo haikuzuia Shirika la Associated Press, ambalo baadaye lilithibitisha taarifa ya FoxNews.com kupitia vyanzo vyao wenyewe, na kusambaza taarifa kupitia kwa wasomaji wake.
Kubainishwa huko kumeamsha tahadhari katika anga za kijeshi.
Msemaji wa Pentagon, Luteni Kanali James Gregory amesema kwamba kutajwa kwa jina la askari huyo wa zamani kunaweza kuzusha hofu.
Alisema: "Tunalinda majina ya watu wetu wanaoshiriki oparesheni maalumu kwa sababu za kiusalama. Wakati wowote majina yanapobainika, ni jambo linalotuhusu."
Orodha ya vitabu kwenye mtandao wa Amazon.com inasema kwamba mojawapo kati ya mamia ya Oparesheni alizoshiriki Owen duniani kote kama mshirika wa makomandoo wa SEAL Team Six ilikuwa ni kumwokoa Kapteni Richard Phillips kutoka kwa maharamia wa Somalia mwaka 2009.

JICHO LA TATU...

Wednesday, August 29, 2012

KUENDESHA MABASI SASA NI KWA KIBALI MAALUMU CHA SUMATRA...

Ili kukabiliana na wimbi la ajali za barabarani kanuni mpya za Leseni ya Usafirishaji Magari ya Usafiri wa Umma zimeandaliwa.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, madereva wataruhusiwa kuendesha magari hayo tu kwa kibali maalumu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Sumatra itatoa cheti au kibali kinachomwidhinisha dereva kuendesha gari la usafiri wa umma na asiyekuwa nacho hataruhusiwa kuendesha.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Barabarani wa Sumatra, Aron Kisaka alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akiwasilisha mada katika Mkutano wa Kukusanya Maoni kuhusu Kanuni za Leseni za Usafirishaji.
Katika mada hiyo, Kisaka alisema utafiti umebaini kuwa asilimia 76 ya ajali nchini, hutokana na makosa ya binadamu ambayo dereva huchangia kwa kiasi kikubwa.
Kisaka alisema baada ya kupata cheti hicho, dereva anatakiwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukomo wa mwendo kama ilivyoainishwa katika cheti hicho.
Mambo hayo ya kuzingatia ni pamoja na kutoruhusiwa kuendesha kwa fujo, kunyanyasa abiria, kuzuia wanafunzi, kuongea na simu, kupakia wanyama au vitu hatarishi na kuendesha gari katika njia ambayo haikuidhinishwa kwenye leseni.
Kisaka alisema dereva atakayekwenda kinyume na matakwa ya kanuni hizo, atakuwa ametenda kosa na akibainika, atatozwa faini isiyopungua Sh 100,000 na kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka miwili au vyote pamoja.
"Sumatra inaweza kusitisha kwa muda au kumfutia dereva cheti iwapo atafanya makosa yanayofanana zaidi ya mara mbili au kukataa kufuata maelekezo yaliyotolewa na Ofisa wa Mamlaka kwa mujibu wa sheria," alisema Kisaka.
Mbali na hayo, alifafanua kuwa Sumatra pia inaweza kusitisha kwa muda au kufuta cheti hicho kama dereva amesababisha ajali iliyosababisha vifo au majeraha makubwa kwa abiria, au amekutwa akiendesha akiwa amelewa kwa kiwango chochote.
Alisema dereva ambaye cheti chake kimesitishwa kwa muda au kufutwa, hataruhusiwa kuendesha gari lolote linalotoa huduma ya usafiri kwa umma.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabruk alipongeza hatua hiyo lakini akadai kuwa faini kwa madereva ni ndogo, kwani wanahatarisha maisha na kutaka ibaki Sh 500,000 kama awali.
Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva na Makondakta Dar es Salaam (Uwamada), Shukuru Mlawa alipendekeza itafutwe namna ya wamiliki kuwajibishwa kwa kuwalazimisha kufanya makosa ili wapate hesabu ya siku.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamata), Salum Abdallah alipendekeza umri wa kupewa leseni madereva uwe miaka 25 badala ya 30 kama ilivyoidhinishwa katika kanuni kwani miaka 30 itakuwa imebana vijana kupata ajira.
Wakati huo huo, Mshauri wa Idara ya Huduma ya Maoni kutoka Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Wilson Mashaka alipongeza mabadiliko hayo na kutaka kiingizwe kipengele cha mabasi yanayosafiri kimataifa yanapopata matatizo, maofisa ubalozi wahudumie abiria.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmadi Kilima alisema wakati wa kufanyia mapitio ya kanuni hiyo, suala la kudhibiti mwenendo wa madereva lilizingatiwa na kubainisha kuwa baada ya kupokea maoni ya wadau watayapeleka Wizara ya Uchukuzi na yatapitiwa na mwanasheria na kufuata taratibu zote hadi kupitishwa.

DUNIANI KUNA MAMBO! TAZAMA PAKA HUYU WA AJABU...


TUME YAUNDWA KUCHUNGUZA KIFO MAANDAMANO YA CHADEMA MORO...

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi amesema Mkuu wa Polisi (IGP), Saidi Mwema ameunda timu ya kuchunguza mauaji ya mtu mmoja yaliyofanywa na Polisi Morogoro, wakati wa maandamano ya Chadema.
Akizungumza jana Dar es Salaam Nchimbi alisema maofisa walioko kwenye tume hiyo waliondoka jana makao makuu ya Polisi kwenda Morogoro kwa kazi hiyo.
Nchimbi alikiri polisi kupewa taarifa za kuuawa kwa mtu huyo aliyekutwa akiwa na majeraha meta 300 kutoka maandamano yalikofanyikia.
"Polisi walikwenda eneo hilo na kukuta mwili umeondolewa," alisema Nchimbi na kusisitiza kuwa polisi walipiga marufuku maandamano ya Chadema kutokana na kuendelea kwa Sensa ya Watu na Makazi.
Alitoa sababu nyingine ya kutoruhusu maandamano hayo kuwa muda walioomba ulikuwa wa kazi jambo ambalo alisema si busara kuandamana muda huo kwani kungevuruga shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na watu mbalimbali katika barabara sita walizoomba kupita.
Waziri pia aliitaka Chadema kutii na kuheshimu sheria za nchi, kwani bila kufanya hivyo, Taifa litasambaratika.
Alisema hata kama chama hicho hakiridhiki na uamuzi unaofanywa na ngazi moja ni vema kikafuata utaratibu wa kukata rufaa badala ya kulazimisha kama ilivyotokea Morogoro.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umelaani vurugu na mauaji hayo na kuomba uchunguzi huru ufanyike haraka kubaini waliohusika na mauaji hayo.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo yaliyodaiwa kumkumba kijana muuza magazeti wa eneo la Msamvu, aliyefahamika kama Ally Zona (38).
Shigela alisema ni vema vyombo vinavyohusika vifanye uchunguzi huru utakaobaini wahusika wa mauaji hayo na aina ya silaha iliyotumika.
Aliitupia lawama Chadema kwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba kama kuna kiongozi anayemiliki silaha atakuwa amekosa sifa ya umiliki.
"Mkakati wote wa vurugu hizo ulifanywa na Chadema, wana tabia ya kutumia vijana katika matukio mbalimbali yakiwamo maandamano haramu kama hayo yaliyosababisha kushambulia wananchi," alisema Shigella na kuongeza kuwa wana ushahidi kuwa hata Igunga walifanya maandamano wakiwa na silaha.
Alidai wanasikitika kwa Chadema kusema waliohusika na tukio hilo ni polisi, kwani ni jambo la kushangaza kwa askari kuacha kuua wananchi walio kwenye msafara na kukimbilia kuua muuza magazeti ambaye hakuwa kwenye maandamano.
Uongozi wa Chadema umesitisha mikutano yake ya M4C mkoani Iringa kwa siku tano ili kupisha siku saba za sensa iliyoanza Agosti 26.
Kusitishwa kwa mikutano hiyo ambayo ilipangwa kuhamia Iringa baada ya kumalizika Morogoro, kulikubaliwa baada ya mazungumzo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mwema na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya hitimisho la mikutano hiyo ya siku 18 Morogoro.

Polisi mkoani Iringa imepiga marufuku mikutano yote ya Chadema iliyokuwa ianze jana.  
Pamoja na mikutano ya Chadema, Jeshi hilo pia limepiga marufuku mikutano ya vyama vingine vya siasa ikiwamo CCM ambayo iko kwenye uchaguzi wa ndani ili kutekeleza maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa. 
Chadema walipanga kufanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Mwembetogwa, lakini pamoja na baadhi ya wabunge wa chama hicho kusisitiza kuwa wana kibali cha kufanya mkutano huo, walishindwa kupenya kwenye uwanja huo. 
Ilikuwa saa sita mchana wakati Kikosi cha Polisi wa Kuzuia Ghasia (FFU) kilipofika uwanjani hapo na kuamuru watu wote wakiwamo wafanyabiashara ndogo kuondoka eneo hilo. 
Wakiwa na mabomu ya machozi na silaha nyingine za kujihami, FFU na makachero wengine wa Polisi, waliimarisha ulinzi uwanjani na kuhakikisha hakuna mkutano unaofanyika nje ya ofisi ya chama hicho ya Mshindo. 
Katibu wa Chadema Iringa Mjini, Suzan Mgonakulima aliwaambia waandishi wa habari kwa kifupi kwamba mkutano huo na mingine iliyokuwa imepangwa kufanywa wiki hii haitafanyika licha ya kuwa na vibali.  
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema Polisi ilipokea maelekezo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kuzuia mikutano ya kisiasa mpaka sensa itakapokamilika.

MKE ASHUSHIWA KIPIGO NA MUMWE KWA KUSHIRIKI SENSA...

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala
Mkazi wa Ndembezi mjini Shinyanga amepigwa na mumewe hadi kuzirai na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu baada ya kutoa ushirikiano kwa karani wa Sensa ya Watu na Makazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Evarist Mangala, alisema jana kuwa mwanamke huyo, Esther Zablon (40) alipigwa juzi saa mbili asubuhi baada ya mumewe, Ismail Yahya kupata taarifa kuwa karani wa sensa alifika nyumbani kwao na mkewe kukubali kuhesabiwa na kutoa takwimu za familia yao.
Akisimulia, Kamanda Mangala alisema karani huyo alipokwenda nyumbani hapo, mume hakuwapo na kama mkuu wa kaya, Esther akazungumza na kutoa taarifa.
Alisema baada ya mume kurudi nyumbani na kugundua kuwa mkewe alikubali kuhesabiwa, alimshambulia kwa ngumi na mateke na kusababisha mke huyo kupoteza fahamu.
Kutokana na kipigo hicho, kwa mujibu wa Kamanda Mangala, Esther alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi na matibabu.
"Wakati mwanamke huyo akichukua fomu namba tatu ya Polisi (PF3) kituoni kabla ya kufikishwa hospitalini, huku akilia kuwa sababu ya kipigo ni yeye kukubali kuhesabiwa, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa dini ya mumewe (Uislamu)," alisema Kamanda Mangala.
Hata hivyo, Kamanda alisema Esther alitoroka wodini kwa kuhofia mumewe kukamatwa na hatimaye kufungwa.
Kamanda Mangala alisema Polisi wanaendelea kumtafuta Yahya na akipatikana atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
Katika tukio lingine Polisi mkoani humo inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumwua na kumpora mali karani wa sensa, Stanley Mahene (34) baada ya kupokea
malipo yake ya semina ya sensa na kurejea nyumbani katika Kijiji cha Kawe Kata ya Iyenze wilayani Kahama.
Kamanda Mangala alisema Mahene alivamiwa Jumapili saa tatu usiku na watu wasiojulikana wakiwa na silaha za jadi na kumshambulia kwa kumkata mapanga.
Mbali na kumkata mapanga, Kamanda Mangala alisema watuhumiwa hao pia walimchoma mshale shingoni na kusababisha kifo chake.
Katika uvamizi huo, walipora Sh 200,000 alizolipwa posho kwenye semina, simu mbili za mkononi, redio, spika mbili na jenereta.
Alisema baada ya mauaji hayo wananchi kwa kushirikiana na Polisi, walianza msako na kuwakamata watu wawili wakiwa na baiskeli tatu zilizokuwa na mali ya karani huyo ambaye pia ni Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kawe.
Kwa mujibu wa Kamanda Mangala, mmoja wa watu waliokuwa na baiskeli hizo alitoroka lakini wawili, Juma Mayala (38) na Idd Lubala (29), wakazi wa Kawe, walikamatwa na baada ya uchunguzi wa Polisi kukamilika, watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, karani wa sensa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kliniki eneo la Mazwi mjini humo, walikurupushwa na mapanga wakizuiwa kuendesha sensa.
Akizungumza jana, Mwenyekiti huyo, Michael Mwampulo ‘Kambwa’, alidai kuitwa na karani aliyemkumbuka kwa jina moja la Maembe, akielezea kuzuiwa kufanya kazi katika nyumba ya Muislamu.
Baada ya kufika, Kambwa alidai mkuu wa kaya alisisitiza kuwa hahesabiwi yeye na familia yake, kwa kuwa walitangaziwa na viongozi wao hivyo na baada ya kuendelea kumshawishi, mkuu huyo wa kaya aliingia ndani na kutoka na panga.
Alidai alipotoka nje aliwafukuza kwa silaha hiyo huku akitoa lugha ya matusi hali iliyowalazimu nao kukimbia wakihofia usalama wao na kwenda kutoa taarifa Polisi.
Wakati hilo likijiri, zipo taarifa kwamba baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu waliandamana jana hadi Polisi Mkoa wakishinikiza kuachiwa huru kwa watu watano wanaodaiwa kuwa viongozi wao waliokuwa wakihojiwa kwa kuhamasisha Waislamu wenzao kukataa kuhesabiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema kikundi hicho kiliondoka baadaye baada ya watu hao (majina yanahifadhiwa) kuhojiwa na Polisi kisha kuachiwa.
Wilayani Longido, baadhi ya makarani walikabiliwa na changamoto kadhaa katika sensa baada ya kutembea umbali mrefu kutoka boma moja hadi lingine huku wakinusurika kudhuriwa na wanyama wakali wakiwamo simba.
Simba hao wanadaiwa kuzagaa kwenye baadhi ya vijiji ambavyo vimepakana na Hifadhi ya Amboseli katika nchi jirani ya Kenya.
Msimamizi wa Sensa wa Kijiji cha Sinya, wilayani humo, Herman Kipuyo alisema tangu kuanza kwa sensa, wamekuwa na wakati mgumu kutokana na hali ya kijiografia
katika baadhi ya vijiji.
Herman alisema kwa sasa hofu kwao ni tishio la simba wanaotoka Kenya kwenda Mlima Kilimanjaro kutafuta malisho.
Mkoani Dodoma wananchi wa Bahi Sokoni wilayani Bahi wameandamana hadi kituo cha Polisi kutoa taarifa kuwa makarani wa sensa hawajapita kuwahesabu.
Walichukua hatua hiyo jana baada ya kauli za viongozi wa wilaya na mkoa kutaka kila mmoja ahesabiwe na atakayeshindwa kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Habari kutoka eneo la tukio zilisema baada ya kuona maandamano mmoja wa viongozi wa halmashauri hiyo aliwasiliana na Mkuu wa Wilaya, Betty Mkwasa ambaye alitafuta watu kwenda kuzungumza na wananchi hao na kuwaelimisha kuwa kazi hiyo inaendelea kwa siku saba na kila mmoja atahesabiwa.

ZIRO PLUS...

MAPATO YA OPRAH WINFREY YAPOROMOKA KWA KASI...

KUSHOTO: Oprah Winfrey. KULIA: Nyota anayelipwa zaidi, Oprah akiwa na Mwigizajiwa Kiume anayelipwa zaidi, Tom Cruise.
Mapato ya mwanamama Oprah Winfrey kwa mwaka yameporomoka kwa Dola za Marekani milioni 125 kulinganisha na mwaka jana, lakini bado amebakia kileleni katika orodha ya nyota wanaolipwa zaidi duniani.
Mkali huyo wa kwenye runinga amefanikiwa kuvuna kiasi cha Dola za Marekani milioni 165 ikiwa pungufu kutoka milioni 290 alizopata mwanzoni mwa mwaka jana, kwa mujibu wa Jarida la Forbes.
Hii inamaanisha anaongoza kwenye orodha ya vipato vya nyota inayochapishwa na Jarida hilo kwa mara ya nne mfululizo, lakini pengo kileleni linaelekea kuzibwa kwa kasi mno.
Kipindi cha mahojiano cha Oprah kilifunga milango yake mwaka 2011 baada ya kuwa hewani kwa miaka 25 lakini umiliki wake kwenye vipindi kama 'Dr. Phil,' 'Rachael Ray,' ;The Dr. Oz Show' umemuweka kileleni mwa ligi hiyo.
Lakini utawala wake kileleni unatishiwa amani na Mwongozaji wa filamu ya Transformers, Michael Bay ambaye yuko nyuma ya Oprah kwa tofauti ya Dola za Marekani milioni 5 akiwa amevuna Dola za Marekani milioni 160.
Mtengenezaji filamu amefikia hapo kutokana na kufanya vema kwa sehemu ya pili ya Transformers: Dark of the Moon na mkataba ambao unamaanisha amevuna kiasi fulani cha faida kutokana na mauzo ya midoli ya kuchezea watoto.
Na mwaka ujao, Forbes haitajumuisha mapato yoyote ya Oprah kutokana na kushiriki kwake kwenye vipindi, ikiwa na maana anaelekea zaidi kupoteza nafasi yake kileleni.
Steven Spielberg alikuwa wa tatu akiwa amevuna Dola za Marekani milioni 130 kutokana na kuchapisha katalogi ya filamu zake zilizotamba.
Pia amefaidika kutokana na mauzo ya tiketi kwenye bustani ya Studio za Universal, mapato ya DreamWorks na mshahara wake uongozaji filamu.
Jerry Bruckheimer, anayefahamika kwa filamu zake za mikiki kama ile ya mwaka jana ya Pirates of the Caribbean: On Stranger Tides ambayo iliingiza Dola za Marekani bilioni 1 duniani, anashika nafasi ya nne akiwa amevuna Dola za Marekani milioni 115.
Anayehitimisha tano bora ni rapa aliyegeuka maarufu kwa spika zake za kichwani Dr. Dre ambaye amevuna Dola za Marekani milioni 110.
Nyota huyo wa zamani wa NWA alilipwa Dola za Marekani milioni 300 na kampuni kubwa ya vifaa vya umeme ya HTC kutokana na hisa kupitia kampuni yake ya Beats by Dr Dre ambayo aliianzisha mwaka 2006.
Nafasi ya kwanza ya Orodha ya Forbes kwa Nyota wa Mitandao ya Kijamii imekwenda kwa Rihanna wakati Kristen Stewart alitajwa na Forbes kuwa Mwigizaji wa Kike anayelipwa zaidi akivuna Dola za Marekani milioni 34.5.
Tom Cruise ameibuka kidedea kama Mwigizaji wa Kiume anayelipwa zaidi akichuma Dola za Marekani milioni 75 katika kipindi cha kati ya Mei 2011 na Mei 2012.

ZIRO PLUS...

CHEKA TARATIBU...

Jamaa watatu wamevamia supamaketi moja kwa nia ya kupora. Lakini kabla ya kuanza kupora wakaingia polisi waliopewa taarifa kuhusu tukio hilo. Jamaa wakajificha kwenye maboksi matatu tofauti yaliyokuwa jirani. Moja kwa moja polisi wakaanza kuwasaka jamaa kwa kucheki kwenye maboksi. Polisi akagonga gonga boksi la kwanza kwa kirungu chake na jamaa akaitikia, "Nyaaaaauuuu!" Polisi akasema, "Ah, humu kuna paka." Akaendelea la pili na jamaa akaitikia, "Wow, wow, wow!" Polisi akasema, "Huku kuna mbwa." Akaenda boksi la tatu na jamaa akaitikia, "Nyanya!" Duh...

JICHO LA TATU...

Tuesday, August 28, 2012

HUKUMU YA MCHUNGAJI MTIKILA KUTOLEWA WIKI IJAYO...

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kutoa hukumu ya kesi ya kusambaza waraka wa uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Rais Jakaya Kikwete hadi Septemba 6 mwaka huu.
Kesi hiyo imeahirishwa jana mbele ya Hakimu Frank Moshi baada ya hakimu anayeisikiliza, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mgeta kutokuwepo mahakamani.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, Moshi alisema kuwa Hakimu Mgeta yuko katika majukumu mengine na amepanga siku ya kutoa hukumu hiyo iwe Septemba 6 mwaka huu.
Hakimu Mgeta alipanga jana kutoa hukumu ya kesi hiyo baada ya Mchungaji Mtikila kufunga ushahidi kwa upande wake ambapo alikuwa na shahidi mwingine ambaye ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Mpoki Bukuku.
Hakimu Mugeta alisema anakubaliana na ushauri wa Mtikila uliosema ameamua kufunga ushahidi wake licha ya awali kuahidi kuleta mashahidi 10 ili wamtetee kwa sababu endapo mashahidi hao angewaleta wangezungumza mambo aliyozungumza yeye na hivyo asingependa kutumia fedha ya umma bure.
Mtikila katika ushahidi wake alikiri kuandaa na kusambaza waraka huo, wenye kichwa cha habari ‘Kikwete kuungamiza kabisa Ukristo!’ ulisababisha ashitakiwe si uchochezi bali maneno ya Mungu.
Kwa upande wake shahidi Bukuku alidai gazeti la Mwananchi liliandika habari zinazohusu waraka unaodaiwa kuwa wa uchochezi ila hadi sasa si Jeshi la Polisi au Mtikila waliofika ofisini kwao kuilalamikia habari hiyo kuwa imepotoshwa.
Mtikila anadaiwa kati ya Januari, 2009 na Aprili 17, 2010 jijini Dar es Salaam kwa nia ya uchochezi alisambaza kwa umma nyaraka hizo za uchochezi. Shitaka la pili, anadaiwa Aprili 16, 2010 eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka huo wa uchochezi kwa jamii.

WALIOGOMEA SENSA SASA KUKIONA CHAMOTO...

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki (pichani) amesema wanaogomea Sensa ya Watu na Makazi, watatambulika kwa namba za nyumba zao na baada ya siku saba baada ya sensa, watachukuliwa hatua za kisheria kwa kutenda kosa la jinai.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sadiki alisema wapo baadhi ya watu mitaani wamegoma kuhesabiwa na kufafanua kuwa watatambuliwa kwa nyumba zao kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa wanaofuatana na makarani wa sensa.
"Makarani wetu wana ramani zinazowaonesha nyumba wanazotakiwa kuhesabu zikiwa na namba, pia wanafuatana na viongozi wa mitaa, hawa ndio watatusaidia kutambua waliogoma kuhesabiwa ili tuwachukulie hatua," alisisitiza.
Alisema kwa sasa hawatawachukulia hatua waliovunja sheria, kwa kuwa wanaweza kudai kuwa bado watu wanaendelea kuhesabiwa, lakini wataanza kuwachukulia hatua baada ya siku za sensa kumalizika.
Akielezea hali ya sensa ilivyo, Sadiki alisema baadhi ya matukio yaliyojitokeza ni pamoja na watu wanane kushikiliwa kwa kushawishi mgomo wa sensa, ikiwa ni pamoja na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa simu.
Alisema kati yao, yumo aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) akafukuzwa, aliyekamatwa Mbagala, Yusuph Ernest ambaye na wenzake watatu wanaendelea kushikiliwa na Polisi kwa mahojiano.
Alisema wengine waliogoma kuhesabiwa walikutwa Magomeni Kagera, wakihamasisha watu kugoma, lakini baadaye walidhibitiwa na kuacha uhamasishaji.
Aliwataka watu kutoa ushirikiano kwa kuwaripoti wanaokataa kuhesabiwa au kukwamisha sensa, ili sheria ichukue mkondo wake.
Mkoani Kigoma, kulikuwa na changamoto kadhaa baada ya baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu kukimbilia misikitini ili wasifikiwe na makarani.
Mkuu wa Wilaya Kigoma, Ramadhani Maneno alisema jana kuwa katika pitapita yao kufanya tathmini, walikutana na changamoto hiyo na wameanza kuifanyia kazi.

Alitaja maeneo waliyogundua tatizo hilo ni Mwandiga na Katonga, ambapo licha ya kutaka kuzungumza na viongozi wao, alikosa ushirikiano.
Kutokana na ukaidi huo, Maneno alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama inatarajia kujadili kuhusu hatua za kuchukua.
Mkuu wa Wilaya alisema katika baadhi ya misikiti, waumini walijichimbia huko wakifanya ibada na kulala ili kuhakikisha makarani hao hawawafikii.
Mbali na hao waliolala msikitini, Maneno alisema katika kijiji cha Bubango kata ya Bitale wilayani Kigoma, familia 40 kati ya 64 za eneo hilo zilikataa kuhesabiwa.

Alisema makarani walipokwenda kwenye familia hizo, wenyeji walieleza kuwa wakuu wa kaya hawapo na hawajui kutoa maelezo ya chochote hadi viongozi hao wa kaya wawepo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai alisema watu 11 walitiwa mbaroni katika maeneo kadhaa ya mkoa huo wakihusishwa na kuchochea wananchi kususia sensa akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji wilayani Kibondo.
Kamanda Kashai alitaja watu hao kuwa ni Juma Hussein, Shuri Hamad, Hadija Siajari na Yapemacho Hussein ambao walikamatwa Mwandiga.

Wengine ni Nkatula Issa, mkazi wa Uvinza ambaye alikamatwa akisambaza vipeperushi vya kuhamasisha watu kususia sensa.
Pia Mussa Sadick, Japhari Abdallah, Husein Hassan na Halfani Rashidi ambao walilala msikitini na kuhamasisha watu kukataa kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kalunde B, Kibondo ambaye alikataa kutoa msaada kwa makarani na kuhamasisha jamii kutoshiriki sensa, alikamatwa pamoja na Idrisa Ibrahimu ambaye ni mvuvi wa Katonga aliyekuwa akichochea watu kugomea sensa.

POLISI WALIPUA MABOMU YA MACHOZI MORO, WAWILI WADAIWA KUUAWA...

Polisi mkoani hapa imelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuvunja maandamano ya Chadema na kutawanya wafuasi na wanachama wa chama hicho waliokaidi amri ya polisi ya kuacha kuandamana.
Katika purukushani hizo, taarifa zilizotufikia ambazo hata hivyo hazikupata uthibitisho wa Polisi, zilieleza kuwa mtu mmoja alifariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa.
Vurugu hizo zilianza saa tano asubuhi jana katika maeneo ya Msamvu, baada ya wafuasi hao kukaidi amri ya Polisi Mkoa juzi jioni kupitia Kamanda wa Mkoa, Faustine Shilogile.
Hata hivyo, eneo la Msamvu na barabara ya kwenda Iringa na katikati ya mji kulikuwa na magari ya doria ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia ( FFU), askari wa kawaida na kanzu.
Wakati ulinzi wa Polisi ukiimarishwa, wafuasi wa Chadema walijiandaa na kuandamana kwa pikipiki na magari machache.
Sakata hilo la Msamvu lilisababisha baadhi ya wenye maduka na wafanyabiashara kufunga biashara zao wakihofia kuingiliwa na watu waliokuwa wakikimbia ovyo kukwepa moshi wa mabomu na kukamatwa na polisi.
Hali ilirejea kuwa ya utulivu saa saba mchana, baada ya baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema kwenda kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Kiwanja cha Ndege, ambako walifanya mkutano wa hadhara.
Baadhi ya mashuhuda wa vurugu hizo, walidai kuwa polisi waliwafyatulia mabomu wafuasi hao wa Chadema, baada ya kuona wanajikusanya na kukaidi amri halali ya kutawanyika katika eneo la Lupila.
Eneo hilo lilipangwa maalumu kupokea viongozi wao wa kitaifa na kuanza maandamano hadi uwanjani hapo.
Habari ambazo hazijathibitishwa zimedai kwamba watu wawili wanaomaminika kuwa ni wafuasi wa Chadema wameuawa katika ghasia hizo.