Saturday, June 30, 2012

OFA YA SERIKALI KUMTIBIA DK ULIMBOKA INDIA YATUPWA...


Hali  ya afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka imeendelea kuwa siri,  huku mipango ya haraka ya kumpeleka nchini India kwa matibabu zaidi ikifanywa na madaktari wenyewe wanaodaiwa kukataa msaada wa Serikali.
Inaelezwa hisia za madaktari dhidi ya Serikali kuwa huenda ina mkono katika kutekwa na kuteswa kwa kiongozi huyo wa mgomo wa madaktari, ndizo zinazowasukuma kuizuia Serikali kushiriki katika kumpatia tiba Ulimboka ambaye kufikia leo asubuhi alikuwa anatibiwa na jopo la madaktari katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Kuzuiwa kwa Serikali kuchangia tiba za Ulimboka kulithibitishwa leo na Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja aliyesema kuwa, Serikali ilikuwa tayari kutoa msaada wa kumsafirisha Dk Ulimboka kwenda India kwa matibabu zaidi, lakini madaktari wamegomea msaada huo wa Serikali.
Alisema wizara  hiyo ilipata taarifa kwamba Dk Ulimboka alikuwa anahitajika kupata matibabu zaidi nchini India au Nairobi, Kenya na hivyo iliamua kutoa msaada wa usafiri na matibabu kwa daktari huyo, lakini madaktari wenzake wamegoma Serikali kushiriki katika suala hilo.
Habari kutoka Muhimbili zilisema zilikuwa zinahitajika Dola za Marekani 40,000 (zaidi ya Sh milioni 60) kumwezesha Dk Ulimboka kusafirishwa nje kwa matibabu zaidi, na mwito ulitolewa kwa wahisani na wasamaria  kujitolea kusaidia mpango huo.
Na kufikia leo mchana, habari zilizonaswa zinasema madaktari na baadhi ya makundi ya watu, wamekuwa wakikamuana kuhakikisha wanapata fedha za kumsafirisha Dk Ulimboka.
Huku mgomo ukiendelea na kuwaumiza wagonjwa katika taasisi ya MOI na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, madaktari wameunda Jopo la Madaktari sita wakiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kumtibu na kumlinda Dk Ulimboka hospitalini hapo.
Wakati mipango ya safari ikikamilishwa leo, milango ya MOI iliendelea kuwa chini ya ulinzi wa madaktari wenyewe, huku wageni wachache wakiruhusiwa kuingia ndani, huku wageni wengine wakiwemo waandishi wa habari na wapigapicha wakiagizwa kusubiri maelekezo zaidi.
Hali ya ulinzi ilionekana pia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) huku shughuli zikionekana kusimama, ikiwa pamoja na kutoonekana kwa pilika za wauguzi na ndugu wa wagonjwa. 
Aidha, kutokana na mazingira yaliyowekwa na madaktari, ilikuwa ni vigumu kwa watu wa nje kuweza kuingia MOI ambalo Dk Ulimboka anapatiwa matibabu.
Wagonjwa waliokuwa wamekusanyika nje ya hospitali hiyo wakisubiri huduma walilaani kuendelea kwa mgomo huo huku wakiziomba pande hizo mbili zinazovutana kumaliza mgogoro uliopo ili kuwezesha huduma kurejea katika hali ya kawaida.
Wakati mgomo ukiendelea kutesa wananchi, Serikali imechukua hatua kadhaa za kunusuru maisha ya wagonjwa ikiwa pamoja na kuingia makubaliano ya kushirikiana na  hospitali binafsi kadhaa zikiwemo TMJ, Regency, Aga Khan, Hindu Mandal, CCBRT za jijini Dar es Salaam na ile ya Jeshi iliyopo Lugalo.
Alisema hatua hiyo ilifikiwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu,  Mizengo Pinda, ambaye alisema Hospitali ya Lugalo ambayo ni ya Jeshi itatumika kama Hospitali ya Rufaa.
"Serikali itaelekeza nguvu zake moja kwa moja katika  Hospitali za  Mwananyamala, Amana na Temeke ambako hakuna mgomo, ili kuhakikisha kwamba hazilemewi na mzigo wa wagonjwa,” alisema.
Utafiti umebaini huduma kuendelea bila matatizo katika hospitali hizo za Amana, Temeke na Mwananyamala.

HATIMAYE SERIKALI YAKUBALI RASMI MAHAKAMA YA KADHI...


Serikali imekubaliana na Waislamu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi itakayokuwa nje ya Mfumo wa Serikali na itagharimiwa na kuendeshwa na waumini wa dini hiyo wenyewe.
Kwa kuanzia mahakama hizo zitakuwepo katika maeneo machache kwa lengo la kuufanya umma kuielewa vizuri tofauti na hisia potofu zilizokuwepo kuwa zitahusisha makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa msimamo huo wa Serikali uliokubaliana na Waislamu jana wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa kuipitisha bajeti ya ofisi yake. 
“Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Kamati Kuu inayojumuisha Viongozi wa Waumini wa Dini ya Kiislamu na Serikali chini ya Uenyekiti wangu, kimsingi imekubaliana kwa kauli moja Uanzishwaji wa Mahakama hiyo Nchini itakayokuwa nje ya Mfumo wa Serikali.
“Mahakama hiyo itagharamiwa na kuendeshwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wenyewe. Serikali kwa upande wake hususan katika hatua hizi za awali za kuanzishwa kwa Mahakama hii itaendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa azma hii inafanikiwa,” alisema Pinda.
Pinda alikuwa akijibu hoja za wabunge waliotaka kufahamu maendeleo ya Mahakama hiyo huku wakitaka Serikali itimize ahadi yake hiyo ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Hamad Rashid Mohammed (Wawi); Rashid Ali Abdallah (Tumbe); Ahmed Juma Ngwali (Ziwani) na Hussein Nassor Amar ( Nyang’hwale).    
Pinda alisema; “Katika kikao cha mwisho cha pamoja kati ya Serikali na ujumbe wa Wawakilishi wa Waumini wa Kiislamu kilichofanyika Machi mwaka huu, tumekubaliana katika kuwezesha suala hilo liende kwa haraka, kwa kuanzia, ni vyema zikaanzishwa Mahakama za Kadhi katika baadhi ya maeneo machache nchini. Lengo ni kuwezesha umma kulielewa vizuri suala hili kinyume na hisia potofu zilizopo sasa zikihusisha Mahakama ya Kadhi na Sharia (inayohusisha masuala ya jinai) chini ya Dini ya Kiislamu”.
Pinda alitaja masuala yatakayoshughulikiwa katika Mahakama hiyo kuwa ni pamoja na Ndoa na Talaka, Mirathi, Wosia, Hiba/Zawadi/Tunu, Wakfu; Malezi ya Watoto na Usuluhishi wa Migogoro ya Kiislamu. Mahakama hiyo haitahusika na Mashauri ya Jinai.
Alisema katika kikao cha mwisho cha Kamati Kuu inayosimamia suala hilo iliamuliwa na pande zote kuwa baadhi ya wajumbe kutoka upande Waislamu na Serikali wakafanye ziara ya mafunzo katika nchi za India, Uingereza, Kenya na baadaye Zanzibar ili wakajifunze namna ya kuratibu na kuendesha Mahakama za Kadhi katika nchi hizo ambazo zina Mahakama za Kadhi kwa muda mrefu. 
“Lengo ni kupata uzoefu na kujua njia bora ya kutuwezesha kuanzisha Mahakama hiyo nchini. Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni na kugharimiwa na Serikali,” alisema.
Akizungumzia chenji ya Rada, alisisitiza kuwa itatumika kama ilivyokusudiwa kwani Tanzania na Uingereza zilikubaliana  asilimia 75 ya fedha hizo kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada, viongozi vya walimu, mihtasari na miongozo ya mihtasari na asilimia 25 ya fedha hizo kununulia madawati.
Kwa sasa kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi 10, lakini baada ya kununuliwa kwa vitabu hivyo wanafunzi kati ya wawili na watatu wa shule za msingi watatumia kitabu kimoja. 
Alisema vitabu hivyo vitanunuliwa kutoka katika kampuni 13 na kati yake kampuni mbili ndio za nje, lakini zina matawi nchini. Kampuni hizo ni Ben; Best Deal Publisher; E & D Vision; Education Books Publisher; Jadida; LongHorn; Longman; Macmillan; Mkuki na Nyota; Mture; Oxford; Tanzania Institute of Education (TIE) na Ujuzi Book.
Alisema fedha hizo za madawati Sh bilioni 18.1 zitaweza kununua madawati 400,000 kwa ajili ya wanafunzi  milioni 1.2. Kwa sasa wanafunzi wenye uhaba wa madawati ni 8,000,000.
Alisema ununuzi wa rada ulifanywa na Wizara ya Miundombinu ambayo sio Muungano hivyo Zanzibar haitapata mgawo huo.
Akizungumzia juu ya uvunjwaji wa Jiji la Dar es Salaam lililoanzishwa mwaka 1999, Pinda alisema mapendekezo ya kulivunja jiji hilo na kubakishwa manispaa zake tatu ili ziratibiwe na sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam yalitolewa  Novemba mwaka 2010, lakini baada ya kuonekana lina kasoro tangazo hilo lilibatilishwa Februari mwaka huu.
“Kutokana na Tangazo la Serikali la Juni 15 mwaka huu, kwa sasa, kisheria Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, bado ina hadhi kamili ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Aidha, halmashauri hiyo ina nguvu ya kisheria kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria,” alisema.
Kuhusu zaidi ya Sh bilioni 300 zilizowekwa na Watanzania sita katika benki ya Uswisi zilizotokana na gesi ya nchini, alisema; “Serikali kupitia vyombo vyake vya Takukuru, Financial Intelligency Unit (FIU) wameanza kufanya uchunguzi wa taarifa hizo kwa kuzingatia taratibu za kisheria. Uchunguzi huo utakapokamilika matokeo yake yatatangazwa,” alisema.

SERIKALI YAINGILIA KATI KUOKOA MAISHA YA WAGONJWA...


Juhudi zaidi zimechukuliwa na serikali ambapo sasa itatumia pia hospitali binafsi za TMJ, Regency, Aga Khan, Hindu Mandal, CCBRT na Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Aidha, nguvu zimeongezwa katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke za Dar es Salaam kunakodaiwa hakuna mgomo, ili kutotoa rufaa nyingi kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kunakodaiwa kuwa na mgomo. 
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alilsema ofisini kwake kuwa, utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu kutumia hospitali za Jeshi na madaktari wastaafu limeanza na sasa nguvu imeongezwa kwa kuhusisha hospitali binafsi.
“Pamoja na Lugalo kuwa tayari, tulikuwa katika mazungumzo na hospitali za binafsi ikiwa ni juhudi hizo hizo za Serikali, hospitali kadhaa zimeshakubali ambazo ni CCBRT, Aga Khan, Hindu Mandal, Regency na TMJ na tunaendelea kuzungumza na nyingine,” alisema Mwamwaja.
Pamoja na hilo, Mwamwaja alisema nguvu kubwa pia imeelekezwa katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana kuhakikisha kuwa wagonjwa wanatibiwa kikamilifu.
Akifafanua kuhusu namna ya wagonjwa watakavyotibiwa katika hospitali hizo za binafsi, Mwamwaja alisema;” Kutakuwa na fomu maalumu ambayo daktari wa Amana, Mwananyamala au Temeke atakayeona mgonjwa anahitaji tiba zaidi, atamjazia ili apokewe ama kupelekwa katika hospitali hizo”.
Pia alisema wagonjwa watakaohitaji rufaa, kwa utaratibu huo huo, watatibiwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo ambayo imekuwa tayari muda mrefu ikishirikiana na hospitali nyingine chini yake. 
Alisema mgomo wa awali madaktari walipelekwa Muhimbili kutoa huduma, lakini baadhi ya madaktari wenyeji mgomo wa awali walidaiwa kuwakwamisha makusudi kufanya huduma na Serikali ililiona hivyo na kuona ni bora wagonjwa wapelekwe huko ili kupata tiba vizuri zaidi.
Alisema madaktari wastaafu na wa Wizara kama alivyosema Waziri Mkuu Pinda, ndio watakaohusika Muhimbili. Pinda alieleza hayo bungeni akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kujua hatua za Serikali kukabili mgomo huo.
Mlinzi wa MOI ambaye hakufahamika jina, aliwaeleza waandishi kuwa, amepewa agizo kuwa mwandishi yeyote asiingie kupata taarifa za mgomo au za Dk Steven Ulimboka.
Mmoja wa wagonjwa Lydia Rwechungura kutoka Chamwino, Dodoma, akiwa nje ya lango la MOI alisema, alifika hospitalini hapo Juni 25 mwaka huu baada ya kupewa rufaa ya Hospitali ya Mkoa Dodoma na sasa hajui afanyeje.
“Pingili za uti wa mgongo zinasigana, nilikuja wakaniambia nije ili nianze mazoezi, nimeingia humo ndani, mapokezi wameniambia niondoke maana hakuna huduma. Eti niangalie vyombo vya habari mgomo ukiisha ndio nije, sijui niende wapi, kwa nini madaktari hawana huruma jamani,” alisema Rwechungura huku akilia.
Eneo la Hospitali ya Muhimbili tofauti na siku nyingine,  lilikuwa kimya, hakukuwa na pilikapilika za wagonjwa wala wahudumu na baadhi ya wagonjwa walionekana kuingia na kutoka huku wengine wakisikitika kwa kuelezwa kuwa hakuna huduma.
Simu za Jumaa Almasi, Ofisa Uhusiano wa MOI ziliita bila majibu na Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaeshi alikataa kuzungumza na waandishi akidai hajui kama mgomo upo au haupo. Alipotafutwa simu haikuwa hewani.
Wakati hali ya huduma ikizorota Muhimbili, Mkoa Mwanza madaktari 63 waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo kazini katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na ya Sekou Toure wametimuliwa kutokana na mgomo na kurejeshwa wizarani.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk. Charles Majinge alisema inawarejesha wizarani madaktari 47 baada ya kukataa kurejea kazini.
“Hospitali ya Bugando ina jumla ya madaktari 47 walio katika mafunzo kazini ambao tumewarudisha wizarani wamegoma kurejea katika mafunzo kazini, na sasa kwa kuwa walitoka wizarani kuja hapa kwetu kwenye mafunzo, basi tunawarejesha huko walikotoka,” alisema Dk. Majinge.
Alisema kuwa kuondoka kwa madaktari hao, waliokuwa katika mgomo kutaathiri utendaji wa utoaji huduma, kwa muda mpaka baadaye watakapojipanga na kupata ufumbuzi wa kudumu. 
Kwa upande wa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, madaktari 16 waliopo kwenye mafunzo kazini wamesimamishwa pia kwa agizo la Wizara ambao waliamuliwa kuchukua barua zao na kuondoka katika eneo la Hospitali ya Sekou Toure.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Valentine Bhangi akielezea kutimuliwa kwa madaktari hao alisema kwa vile madaktari hao waliletwa na wizara hapo kwa ajili ya mafunzo kazini, wamerejeshwa huko walikotoka kwa hatua zaidi.
Madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wameingia kwenye mgomo baridi hali ambayo inasababisha wagonjwa kutopata huduma kwa wakati huku wengine wakitaka Serikali itazame hatima ya wananchi wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kwenda hospitali za kulipia.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya alisema kuwa hakuna mgomo hospitalini hapo na wanaendelea na kazi kama kawaida.
Hospitalini hapo kulikuwa na msululu mrefu  wa wagonjwa wakiwa kwenye foleni ya kumuona daktari ambapo ni daktari  moja tu alikuwa akitoa huduma huku vyumba vingine vya madaktari vikiwa havitoi huduma yoyote.
Mmoja wa wananchi hao, Zakaria Daudi ambaye ni mkazi wa Chamwino katika Manispaa ya Dodoma alisema kuwa,  hali ya huduma sio nzuri kwani wanalazimika kusubiri kuingia kwa daktari muda mrefu bila ya mafanikio.
“Nimekuwa namleta hapa mke wangu bado hajapata huduma napigwa tu kalenda bila huduma yoyote kama wamegoma waseme ukweli,” alisema.
Kwa upande wake, mkazi wa Nkuhungu, Kunze George alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa mkweli kuwa kuna mgomo na si kusema hali shwari wakati wananchi wanateseka kwa kukosa huduma.
Wakati huohuo, Chama cha Wauguzi, Tawi la MOI limeiomba Serikali kutatua haraka mgomo huo kwa kuwa wao wanabebeshwa mzigo mkubwa wa huduma na utendaji na wanalaani kitendo hicho.
Mwenyekiti wa chama hicho MOI, Prisca Tarimo alisema kazi kubwa wamekuwa wakiifanya na hivyo wanalazimika kufanya kazi zisizo kuwa zao kuokoa maisha ya watu hivyo Serikali itatue tatizo hilo kwa haraka.
Kuhusiana na afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari wanaoongoza mgomo, Dk Steven Ulimboka, Mkuu wa Jopo la Madaktari wanaomtibu daktari huyo, Profesa Joseph Kahamba alibainisha kuwa afya yake inaendelea kuimarika na wanaendelea kumtibu akiwa chini ya uangalizi wao katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

LAURYN HILL WA FUGEES KWENDA JELA MIAKA MITATU...

Lauryn Hill amekiri kwamba amekuwa akikwepa kulipa kodi makusudi kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita na sasa mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Fugees anakabiliwa na kifungo cha miaka mitatu jela.
Hill amepatikana na hatia jana katika mashitaka matatu ya kukwepa kulipa kodi kwa mwaka 2005, 2006 na 2007 pale alipojipatia zaidi ya Dola za Marekani milioni 1.8.
Pale Jaji alipouliza kama Hill "kwa kukusudia na hiari yake' alishindwa kulipa kodi, alijibu, "Ndio."
Zaidi ya miaka mitatu jela, Hill anaweza kupigwa faini ya Dola za Marekani 75,000.
Hill yuko nje kwa dhamana ya Dola za Marekani 150,000. Hukumu yake imepangwa kutolewa Novemba, mwaka huu.

ZIRO PLUS...

MJANE WA KIZUNGU AHUSISHWA NA MILIPUKO YA MOMBASA...

KUSHOTO: Jermaine Grant akipelekwa mahakamani mjini Nairobi chini ya ulinzi mkali. KULIA: Samantha akiwa na mumewe, Jermain Lindsay ambaye alihusika na milipuko ya London.
'Mjane Mzungu' wa mlipuaji bomu wa London ni mtuhumiwa nambari moja wa shambulio baya la kigaidi nchini Kenya.
Samantha Lewthwaite, ambaye mumewe Jermain Lindsay alilipua njia ya treni ya Piccadilly, amekuwa mafichoni tangu Desemba pale polisi walipofichua mpango kamambe wa kulipua hoteli za Magharibi mjini Mombasa.
Maofisa wamesema mama huyo wa watoto watatu kutoka Home Counties alionekana karibu na klabu ya usiku ambayo ni mojawapo ya sehemu zilizolengwa kwenye Hoteli ya Indian Ocean Jumapili usiku.
Bomu lilirushwa ndani ya bustani ya Jericho Beer ambamo kulikuwa na watalii wakitazama mechi kati ya England na Italia, na kuua watu watatu akiwamo kijana mdogo.
Haijafahamika kama Waingereza ni kati ya watu 25 waliojeruhiwa.
Muda mfupi kabla ya shambulio hilo, mwanamke mweupe anayefanana na taarifa za alivyo Samantha alionekana mwenye mashaka na kuuliza maswali kadhaa kuhusu baa hiyo. Alikuwa pamoja na wanaume wawili wenye asili ya Asia.
"Tunashuku Samantha Lewthwaite amehusika kwenye shambulio hili la kigaidi katika klabu," Ofisa wa Polisi wa Kenya amesema.
Mwanamke huyo mwenye miaka 28 ambaye ni mtoto wa askari kutoka Aylesbury mjini Buckinghamshire alishitakiwa Desemba mwaka jana kuandaa mpango wa kuua mamia ya watalii wa Kiingereza mjini Mombasa.
Polisi walikuta silaha na kiwanda cha kutengeneza mabomu katika nyumba yake yenye ulinzi mkali, ambamo pia hupatumia kama benki kwa ajili ya kuhifadhia fedha za magaidi wa Kisomali wa kundi la Al Shabaab.
Samantha aliachiliwa kwa sababu ambazo hazijajulikana na anasemekana aliishi Somalia kama mkimbizi kabla ya kurejea Kenya.
"Polisi wanaamini Samantha amerejea Mombasa na anashiriki kikamilifu kwenye mashambulio ya mabomu ya kutegwa kwa mkono," kilisema chanzo cha ulinzi Kenya.
"Mwanamke mweupe, mwenye kufanana kabisa na taarifa za Samantha, alionekana na wanaume wa Kiarabu wa rika la kati wakiuliza maswali kuhusu baa kabla ya shambulio.
"Hakika si hali ya kawaida kwa mwanamke Mzungu kuwapo hapa na kuvaa mavazi ya Kiislamu."
Watuhumiwa hao watatu pia walionekana jirani na makanisa Katoliki mjini Mombasa.
Samantha ambaye alitimuliwa chuo kikuu amekuwa akiwindwa na CIA, Polisi wa Kenya na Scotland Yard, ambao wametuma askari wa kutosha Nairobi kusaidia uchunguzi.
Kabla ya kukamatwa mwezi Desemba, alikuwa akisafiri Kenya kwa kutumia pasipoti bandia inayomilikiwa na Natalie Faye Webb, nesi wa Essex ambaye hana uhusiano na ugaidi na hajawahi kukanyaga nchi za Afrika Mashariki.
Samantha alizaliwa Ireland ya Kaskazini ambako baba yake, Andrew ambaye alikuwa akitumikia jeshi, alikutana na mama yake, Christine.
Wazazi hao walitengana wakati Samantha akiwa na miaka 11, tukio ambalo marafiki wanasema lilimshawishi kupenda Uislamu, na kuingia rasmi katika dini hiyo akiwa na miaka 15.
Alikutana na mlipuaji wa treni ya King's Cross, Lindsay kwenye chumba cha majadiliano ya Kiislamu wakati akisomea dini hiyo na siasa kwenye Shule ya Oriental and African Studies iliyoko katikati ya London.
Aliolewa na fundi wa kufitisha mazulia mzaliwa wa Jamaica kwenye sherehe za Kiislamu zilizofanyika Aylesbury mwaka 2004.
Wakati mume wake mwenye miaka 19 alipojilipua mwaka 2005 na kukatisha maisha ya watu 26, Samantha alikuwa na ujauzito wa miezi minane wa mtoto wake wa pili, ambaye ni msichana. Tayari alikuwa mtoto wa pili wa kiume ambaye amezaa na mwanaume asiyefahamika mwaka 2009.
Katika familia yake ya mjini Aleysbury, Samantha ni mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu, akielezea hawajaonana kwa miaka kadhaa sasa.
Mshirika wake wa tuhuma za kupanga ulipuaji bomu Desemba, Jermaine Grant mwenye miaka 29 kutoka London, yuko mahakamani mjini Mombasa.
Mji wa Bandari na Nairobi imekumbwa na mashambulio ya mabomu tangu vikosi vya Kenya vilipovamia Somalia Oktoba mwaka jana kupambana na wapiganaji wa Kiislamu.
Masaa kashaa kabla ya milipuko ya Jumapili, Ubalozi wa Marekani ulitoa tahadhari kutokea kwa mashambulio ya kujitoa muhanga ndani au kuzunguka Mombasa.
Mkuu wa Polisi, Aggrey Adoli alisema: "Mashambulio yalitokea majira ya Saa 4 usiku, bomu lilitupwa ndani ya baa, lakini wengi kati ya waliojeruhiwa walikuwa nje ya baa kwenye mlango.
"Mmoja kati ya watu waliojeruhiwa anatusaidia kwenye uchunguzi sababu anatoa taarifa za kukanganya. Amekuwa akishikiliwa kama mtuhumiwa."

JICHO LA TATU...

CHEKA TARATIBU...

Mwanasheria alikuwa akirandaranda kutafuta msalaba wa kuweka mwenye kaburi la mwenzake mmoja, ndipo fundi akamuuliza anachotaka kiandikwe katika msalaba huo.
"Hapa amezikwa Mtu mwaminifu na Wakili," alijibu yule Mwanasheria.
Fundi akajibu kwa hamaki, "Samahani, siwezi kufanya hivyo. Katika nchi hii sheria hairuhusu watu wawili kuzikwa kwenye kaburi moja."
Akaongeza, "Labda kukusaidia tu nitaandika HAPA AMEZIKWA WAKILI MWAMINIFU."
Mwanasheria akapinga kwa kusema, "Lakini hiyo itawafanya watu wasielewe huyu ni nani!"
Fundi akajibu, "Uko sahihi kabisa. Watu watasoma na kushangaa, HAIWEZEKANI!"

ZIRO PLUS...

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUFANYA NGONO NA WANAFUNZI...

Eneo la Wokingham, mjini Berkshire ambako shule hiyo iko jirani na hapa.
Mfanyakazi wa kike katika shule amefikishwa kortini akidaiwa kufanya ngono na wanafunzi.
Emma Webb anakabiliwa na mashitaka 19 ya kutumia vibaya nafasi yake ya uaminifu kwa kujiingiza katika vitendo vya ngono na wanafunzi katika sekondari iliyoko jirani na Wokingham mjini Berkshire, ambayo haikutajwa kwa sababu za kisheria.
Webb, ambaye ni msaidizi wa machapisho na mshauri wa shule, pia anakabiliwa na shitaka la kupotosha mtiririko wa haki, Korti ilielezwa.
Mwanamke huyo mwenye miaka 41, ambaye amenyimwa dhamana, alikamatwa Alhamisi iliyopita na wapelelezi wanaochunguza skendo ya vitendo vya ndono kwenye shule hiyo.
Tukio hilo linasemekana kuhusisha wanafunzi watatu wa kiume.
Mapema Msemaji wa Kituo cha Polisi cha Thames Valley alisema kwamba Webb alikuwa akituhumiwa kwa mashitaka 19 ya kutumia vibaya madaraka yake ya uaminifu, chini ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.
"Mwanamke huyo amesimamishwa kazi kupisha kufanyika uchunguzi na polisi wanaendelea kufanya kazi kwa karibu na shule pamoja na mamlaka za jamii," aliongeza msemaji.
Mwanamke huyo anatarajiwa kufikishwa tena Mahakama ya Reading keshokutwa Jumatatu.

Friday, June 29, 2012

MABAO YA BALOTELLI YAIKABIDHI ITALIA KWA HISPANIA JUMAPILI...


Mabao mawili maridadi ya kipindi cha kwanza yaliyowekwa kimiani na mshambuliaji 'mtukutu' Mario Balotelli usiku wa kuamkia leo yaliiwezesha timu yake ya taifa ya Italia "The Azzuri" kutinga fainali ya Michuano ya Ulaya "Euro 2012" kwa kuibwaga Ujerumani kwa mabao 2-1. Bao la kufutia machozi la Ujerumani katika mechi hiyo lilifungwa na Mesut Ozil kwa njia ya penalti kipindi cha pili. Kwa matokeo hayo, Italia sasa itakutana na mabingwa watetezi Hispania katika mechi ya fainali siku ya Jumapili. Pata utamu wa mabo hayo kwenye video hapo juu.

SNOOP DOGG DOGGY AKAMATWA UWANJA WA NDEGE KWA KUKUTWA NA TUMBAKU...

Snoop Dogg alishikiliwa kwenye Uwanja wa Ndege nchini Norway jana asubuhi baada ya maofisa forodha kugundua rapa huyo amebeba tumbaku.
Idara ya Polisi wa Agder imeeleza kwamba Snoop alisimamishwa lango la forodha kwenye Uwanja wa Ndege wa Kjevic mjini Kristiansand ambapo maofisa waligundua gramu 8 za tumbaku.
Kwa mujibu wa polisi, kitu chochote chenye uzito wa chini ya gramu 15 adhabu yake inaweza kuwa faini na kwa suala la Snoop, faini yake inaweza kuwa Krone za Norway 12,000 ambazo ni sawa na Dola za Marekani 1,980.13.
Imeelezwa Snoop alitoa ushirikiano wa kutosha na haraka akalipa faini sababu alikuwa amebeba fedha za nchi hiyo katika mfuko wake wa nyuma wa suruali.
Snoop yupo nchini humo kwa ajili ya maonesho kwenye Tamasha la Hove lililotarajiwa kuanza majira ya Saa 4:30 usiku wa kuamkia leo, ambalo litamuwezesha kupata muda kidogo wa kufidia tumbaku yake.

ZIRO PLUS...

MFUNGWA ATOROKA KWA KURUKA UKUTA WA GEREZA LENYE ULINZI MKALI...

Mfungwa wa mauaji ametoroka kutoka jela kwa kuruka ukuta kwa kutumia kamba kwenye gereza lenye ulinzi mkali.
John Massey mwenye miaka 64 ambaye amepachikwa jina la 'mtu hatari asiyevuma' na polisi, alifungwa miaka 37 iliyopita kwa kumpiga risasi na kumuua baunsa kwenye klabu moja mashariki mwa London.
Msako mkali umeanza leo baada ya muuaji huyo, mmoja wa wafungwa waliotumikia kifungo kwa muda mrefu nchini Uingereza, alitoroka kutoka gereza la Pentonville mjini Islington, Kaskazini mwa London usiku wa kuamkia jana.
Aliruka ukuta kwa kutumia kamba bila kuonekana na walinzi majira ya Saa 12:30 jioni.
Wizara ya Sheria imesema jana kwamba wameanzisha uchunguzi kuhusiana na utorokaji jela hiyo ambayo inashikilia wafungwa zaidi ya 1,250 wa Kundi B na C.
Polisi wa Scotland Yard wameshauri jamii kutokabiliana na Massey na badala yake wapige simu polisi kama wakimuona popote.
Aliamriwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela wakati alipofungwa kifungo cha maisha kufuatia kesi ya mauaji ya Charlie Higgins mwenye miaka 36 mjini Hackney mwaka 1975 kwa kutumia bunduki iliyokatwa kitako.
Marafiki wameelezea mauaji hayo ya kulipa kisasi baada ya 'kuwa amelewa kupita kiasi'.
Massey ambaye wakati huo alikuwa fundi seremala, alimuua mlinzi wa mlangoni sababu yeye na rafiki zake wawili walikataliwa kuingia kufuatia ugomvi.
Terence Harper mwenye miaka 29, naye pia alifungwa baada ya Baraza la Mahakama kwenye Mahakama Kuu ya Makosa ya Jinai kuwakuta wote na hatia ya mauaji.
Baada ya miaka 18 jela, muuaji alitoroka mwaka 1994 wakati alipokwenda kutembelea nyumbani kwake huku akiwa chini ya ulinzi.
Massey alitoroka na kutumia miaka mitatu akiwa nchini Hispania kabla ya kukamatwa na kurejeshwa gerezani.
Baadaye alitoka Juni 2007 na kuishi chini ya uangalizi maalumu kwenye hosteli mjini Streatham, kusini mwa London, na akapata kazi kama mhudumu wa dukani. Lakini wakati alipotakiwa kwenda kumtembelea baba yake, Jack mwenye miaka 82 aliyekuwa akiumwa mahututi mjini Kentish Town, alivunja masharti ya kuachiwa kwake mwezi Novemba ya mwaka huo.
Baada ya vikosi vya jeshi kumuwinda sana akajisalimisha mwenyewe na kufungwa tena. Maofisa wa Magereza walikataa kumpa ruhusa kuhudhuria mazishi ya baba yake siku chache baadaye.
Miaka kama mitatu hivi baadaye alihamishiwa gereza la wazi la Ford lililoko West Sussex, sambamba na dada yake, Carol aliyekuwa akiumwa sana.
Carol alifariki wiki chache baadaye, lakini badala ya kujikabidhi mwenyewe kwa polisi, akaamua kwenda kuishi na mama mkubwa wa Carol huko Camdem, London, na kukamatwa tena miezi kumi baadaye.
Kufuatia kutoroka kwamara ya pili, akahamishiwa gereza la Pentonville ambako sasa ametoroka tena kwa mara ya tatu.
Msemaji wa Magereza alisema: "Kama majira ya Saa 12:30 jioni Jumatano ya Juni 27 mfungwa huyo hakuonekana kwenye gereza la Pentonville.
"Wakati huohuo polisi wakataarifiwa na tukio hili litafuatiwa na uchunguzi."

ZIRO PLUS...

CHEKA TARATIBU...

Jamaa mmoja kaoa mwanamke mwenye wivu kupindukia kiasi cha kufuatilia kila anachofanya mumewe. Siku moja jamaa karudi nyumbani usiku ndipo mkewe akaanza kumkagua huku na kule kisha akasema, "Enhee, umeanza kutembea na wanawake mwenye kipara siyo, ndio maana sijakuta mabaki ya nywele!" Kesho yake mume aliporudi mke akaanza kumnusa-nusa kisha akasema, "Tena mwanamke mwenyewe sio kipara tu, kumbe kafulia kiasi cha kushindwa kununua hata pafyumu!" Kweli ndoa ndoana...

JICHO LA TATU...

Thursday, June 28, 2012

MADAKTARI WAIKATAA TUME YA KUCHUNGUZA KIPIGO CHA DK. ULIMBOKA...


"Dk. Ulimboka alipopata nguvu alielezea yaliyomkuta alipotekwa jana kuwa ni pamoja na kufungwa kitambaa, kamba mikononi na miguuni na kushushiwa kipigo na baadaye alitupwa porini na kufunikwa na majani. Waliompiga walidhani amekufa hivyo, walimuacha hapo baada ya kupishana wamuue kwa risasi au sindano na kuishia kumtupa porini ambako mwenyewe alijikongoja hadi alipokutana na wasamaria wema na kumuokoa."
Madaktari Tanzania wameikataa Tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuchunguza tukio la kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini,  Dk. Steven Ulimboka.
Pamoja na hayo hali ya Dk. Ulimboka inaanza kuimarika ambapo leo mchana alianza kuwatambua watu waliomtembelea na kuzungumza huku akilindwa na madaktari nje ya wodi ya wagonjwa mahututi alikolazwa katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI).
Aidha wakati daktari huyo akipatiwa huduma ya matibabu kupitia jopo la madaktari bingwa, hali ilikuwa tofauti kwa wagonjwa wa kawaida waliofika hospitalini hapo ambao waliishia nje huku wakiambia hakuna huduma kwa kuwa sasa mgomo umeshika kasi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, Katibu wa Jumuiya hiyo ya Madaktari, Edwin Chitage, alisema madaktari wote nchini wameamua kutokuwa na imani na tume iliyoundwa na Polisi kutokana na mazingira ya tukio lilimpata Dk. Ulimboka.
“Tunaomba kiundwe upya chombo huru kitachokuwa na wajumbe wanaoaminika ambao watachunguza kwa dhati tukio hili na kuja na majibu, hatuna imani na tume hii kwa kuwa mazingira ya kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka yanatufanya tusiiamini polisi,” alisisitiza. 
Aidha alidai madaktari na hospitali ya Dodoma wamekuwa wakipokea vitisho mbalimbali kwa njia ya simu na kusisitiza kuwa havisaidii kwa kuwa ndio vinazidisha mgogoro huo. “Serikali itambue hakuna njia yeyote ya kutatua mgogoro huu bali ni kwa njia ya kuzungumza kwa dhati,”
Alisema madaktari kwa sasa wamechoshwa na hali mbaya ya sekta ya afya kuanzia mlundikano wa wagonjwa, ufunyu wa vifaa tiba na dawa na kwamba mgomo wao ni ishara ya madaktari nchi nzima kujitolea kutetea sekta hiyo licha ya vitisho.
Dk. Chitage pia alisema Dk. Ulimboka alipopata nguvu alielezea yaliyomkuta alipotekwa jana kuwa ni pamoja na kufungwa kitambaa, kamba mikononi na miguuni na kushushiwa kipigo na baadaye alitupwa porini na kufunikwa na majani.
Alisema waliompiga walidhani amekufa hivyo, walimuacha hapo baada ya kupishana wamuue kwa risasi au sindano na kuishia kumtupa porini ambako mwenyewe alijikongoja hadi alipokutana na wasamaria wema na kumuokoa.
Awali akizungumza na waandishi wa habari Msemaji wa MOI Almas Jumaa, alisema hali ya Dk Ulimboka inaendelea vizuri ikilinganishwa na jana ambapo kwa sasa ameanza kuzungumza vizuri na kutambua watu.
Naye Dk Joseph Kahamba anayemtibia Dk Ulimboka alisema hali ya mgonjwa inatia matumaini na kwamba jopo la madaktari bingwa linamhudumia kuhakikisha afya yake inaimarika.
Dk Ulimboka mwenyewe aliwahakikishia watanzania kuwa anaendelea vizuri ila aliomba apatiwe muda apumzike na kuwataka wagonjwa wanaoenda kumuangalia wapungue.

DK ULIMBOKA AELEZEA AFYA YAKE AKIWA HOI KITANDANI...

                     BREAKING NEWS!!                        
  

TIBA YA KUTUAMA MAJI SOKO LA TANDALE...


Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Skol wakijenga mitaro ya Soko la Tandale lililopo katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam jana. Hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la kutuama maji ya mvua.

HARAKATI ZA KUOKOA MAISHA YA DK ULIMBOKA...

Baadhi ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo wakikokota kitanda alichobebewa Mwenyekiti wao, Dk. Steven Ulimboka kwenye Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa, Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupokea kipigo kitakatifu kutoka kwa watu wasiofahamika usiku wa kuamkia jana Dar es Salaam.
Madaktari wakimshusha mwenzao, Dk. Steven Ulimboka kutoka kwenye gari la wagonjwa la Hospitali ya AAR  nje ya Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Muhimbili (MOI) kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake.
Baadhi ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo kabla ya kurejea jana kuokoa maisha ya Mwenyekiti wao, Dk. Steven Ulimboka, wakilisukuma gari la wagonjwa lililombeba mwenzao kuelekea Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Muhimbili (MOI) kwa uchunguzi zaidi.

MADAKTARI WALIOGOMA WAREJEA KUMWOKOA DK ULIMBOKA...

Wakati madaktari wakiendelea kususia kuhudumia wagonjwa nchi nzima, Mwenyekiti wa Jukwaa la Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka (35), anayeongoza mgomo huo, amevamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa kwa kipigo usiku wa kuamkia jana. 
Dk Ulimboka ambaye anaongoza mgomo huo ingawa yeye si mwajiriwa wa Serikali, alifikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbli, Dar es Salaam jana asubuhi baada ya kuokotwa eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni  akiwa amejeruhiwa. 
Wakati Dk Ulimboka alipofikishwa nje ya Kitengo cha Mifupa (MOI), madaktari wenzake ambao wamesusa kuhudumia wagonjwa, walifurika hospitalini hapo na kuanza kusukuma gari hilo huku wakiimba nyimbo za mshikamano na wengine wakilia. 
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana ni kulipiza kisasi, madaktari hao ghafla walimgeukia mmoja wa askari Polisi aliyekuwa amevalia kiraia na kumshambulia kwa kipigo kwa madai kuwa aliwasiliana na wenzake na kuwataarifu kuwa Dk Ulimboka bado yuko hai. 
Askari huyo pia alinyang’anywa simu na redio ya mawasiliano ambavyo vyote viliharibiwa vibaya na  alionekana akiwa ameumizwa na kuvimba mwilini huku akiwa hajapatiwa huduma yoyote. 
Kutokana na majeraha hayo, askari wenziwe walimuondoa eneo hilo; na mara moja Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewataka waliomshambulia askari huyo kujisalimisha. 
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova aliwataka madaktari waliomshambulia askari huyo, wajisalimishe na kurudisha vifaa walivyomnyang’anya; simu na redio ya mawasiliano.

Kova aliyezungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, alikemea tabia ya wananchi kujichukulia hatua mkononi kwa kumshambulia askari huyo na kuongeza kuwa alikuwa kazini akichunguza tukio hilo. 
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi, alidai Dk Ulimboka alitekwa juzi usiku na watu wasiojulikana na kupigwa na kung’olewa kucha na meno na hali yake ni mahututi. 
Alidai Dk Ulimboka alizungumza kwa taabu alipofikishwa hospitalini ambapo alidai juzi jioni alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Abduel anayedaiwa kutoka Ikulu na alitaka kuzungumza naye kuhusu maendeleo ya madai ya madaktari. 
 “Alikubali kuonana na mtu huyo ambaye pia alikuwa akizungumza naye mara kwa mara na alikubaliana na wenzake asiende kuonana naye mwenyewe, aliongozana na rafiki yake Dk Deo hadi eneo walilopatana ambalo ni Kinondoni barabara ya Tunisia,” alisimulia Dk Mkopi. 
Alidai Dk Ulimboka alisimulia kuwa akiwa katika eneo hilo pamoja na Abduel na Dk Deo, walitokea watu watatu; wawili wakiwa na silaha aina ya bastola na mmoja bunduki. 
Kwa mujibu wa madai ya Dk Ulimboka, watu hao walianzisha vurugu na kuwataka wengine waondoke na kumchukua peke yake na kumuingiza kwenye gari nyeusi yenye namba zisizosajiliwa na kutokomea naye. 
Kwa mujibu wa madai hayo, Dk Deo aliamua kuwasiliana na wenzake ambao walimtafuta kwenye vituo vyote vya Polisi bila mafanikio na kuishia kuandika maelezo ya tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi. 
Dk Deo pia aliwasiliana na wanaharakati akiwamo Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) Hellen Kijo-Bisimba. Anadai alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni msamaria kwamba amemuokota Dk Ulimboka akiwa hoi eneo la Mabwepande. 
Inadaiwa Dk Deo aliwachukua wanaharakati hao hadi Kituo cha Polisi Bunju alikopelekwa Dk Ulimboka na kumchukua na kumkimbiza Muhimbili. 
Kova alisema Dk Ulimboka  alikuwa na rafiki yake aitwaye Dk. Deogratius Michael na watu wengine katika Klabu ya Leaders Kinondoni ambapo ghafla saa 5:30 usiku, walitokea watu watano wasiofahamika wakavamia klabu hiyo na kuwatishia na kuwataka walale chini.
 “Dk Ulimboka na wateja wengine walilala chini kwa kuhofia madhara kwa kuwa watu hao walikuwa na kitu wanachohisi ni silaha na hatimaye watu hao walimchukua Dk Ulimboka na kusema kwamba walikuwa wakimhitaji yeye na kumuingiza katika gari aina ya Suzuki Escudo nyeusi ambayo haikuwa na namba za usajili,” alidai Kova. 
Alidai wakati wakiwa njiani, watu hao walianza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake na bila kusema wanataka nini kutoka kwake na walipofika maeneo ya Mwenge, walimvisha fulana nyeusi usoni na hakujua tena wanaelekea wapi huku wakiendelea kumpiga na mmoja wa watu hao akasema watamuua. 
Kamanda Kova alidai ilipofika asubuhi, Dk  Ulimboka alijikuta yupo msitu wa Mambwepande na alijivuta hadi barabarani na alikutwa na msamaria akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi. 
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Dk Ulimboka alieleza kuwa gari yake aliiacha maeneo ya Leaders Club na watu hao waliuchukua ufunguo wake, nyaraka zake pamoja na fedha ambazo hakumbuki ni kiasi gani. 
Kamanda Kova alisema ameunda jopo la wapelelezi wa fani mbalimbali chini ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mlalamikaji mwenyewe na mashahidi walioona tukio hilo, ili uchunguzi wa shauri hilo ufanyike  na kuwaomba raia wema kutoa ushirikiano ili matukio ya aina hiyo yasijirudie. 
 “Naamini kwamba watu wengi watakuwa wameguswa na tukio hili ila nawasihi watuache polisi tufanye upelelezi na waachane na minong’ono kwa kuwa sisi hatukuwa na ugomvi wowote na Dk Ulimboka wala madaktari…upelelezi utafanyika kwa makini na taarifa rasmi zitatolewa baadaye.” alisema.

JICHO LA TATU...

CHEKA TARATIBU...

Paka na Panya walikufa siku moja na wote wakafika peponi. Akiwa huko Mungu akamwona Panya na kumuuliza, "Unajisikiaje kuwa hapa?" Panya akajibu, "Najisikia raha sana, lakini je, naweza kupata viatu vya kutelezea kwenye barafu?" Mungu akajibu, "Hakuna tabu, chukua hivi hapa!"
Siku iliyofuata, Mungu akamwona Paka na kumuuliza, "Unajisikiaje kuwa hapa?" Paka akajibu huku akimtazama Panya, "Najisikia raha sana, sikujua kama kuna mlo mzuri kama ule wa duniani!? Duh...

ZIRO PLUS...

MAMA AUA WANAWE 'ALIOWACHOKA' KWA KUWATUPA GHOROFANI...

Mama mmoja amekamatwa kwa tuhuma za kuwatupa watoto wake wawili na kufa kutoka kibaraza cha ghorofa ya 15 sababu alikuwa 'amewachoka'.
Galina Ryabkova mwenye miaka 30 alionekana hana hisia zozote katika video iliyopigwa kwenye jengo hilo mjini Moscow, Urusi baada ya tukio hilo.
Majirani katika jengo hilo walifahamu hilo baada ya kusikia kishindo wakati miili ya watoto hao wenye umri wa miaka 4 na 7 ilipokita kwenye ardhi.
Licha ya juhudi za majirani, watoto hao walifariki kabla wahudumu wa huduma ya kwanza kuwasili.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwanamke anasemekana kuwa 'aliwachoka watoto hao' na 'kuamua kuondokana nao'.
Mwanamke hue amble mumewe alikuwa safarini kibiashara, alikuwa akiishi ghorofa ya nane kwenye jengo hilo na inasemekana aliwapeleka watoto hao hadi ghorofa ya 15 kabla ya kuwatupa Jumapili iliyopita.
Jirani yetu kwenye jengo hili amesimulia mtiririko wa matukio ya kutisha tukio hili.
Mwanaume, ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema mkewe aliamka na kusema kwamba watoto walikuwa wakianguka kutoka kwenye jengo hili.
Wapenzi hao walikimbia kutazama watoto wawili wakiwa wamelala ardhini mbele ya lango kuu la kuingilia kwenye jengo hilo.
Mwanaume huyo aliongeza: "Muda huohuo mama yao alikuwa akiondoka kwenye jengo hilo. Tulimuuliza kama hawa walikuwa wanawe na akajibu bila wasiwasi, "Ndio, nimewatupilia mbali."
Kamera za CCTV kwenye jengo hilo zimeonesha mmoja wa watoto hao akianguka kutoka dirishani mbele ya jengo hilo.
Kisha baadaye zikamuonesha Galina akija kwenye ngazi huku akiwa amevalia suruali ya jeans na fulana nyeupe.
Kwa utulivu akaketi kwenye kibaraza cha jengo hilo na kushitushwa na majirani waliomzingira katika kujaribu kuzuia asitoroke.
Video imemalizia kwa kuonesha maofisa wa polisi wakiwasili kwenye jengo kutambua kilichojiri na kumkamata mama huyo.
Imeripotiwa kwamba Galina alijaribu kujiua siku za nyuma kwa madai kuwa mumewe hakuwa mwaminifu kwenye ndoa.
Galina anatarajiwa kupelekwa kwa daktari wa magonjwa ya akili kwa vipimo wakati uchunguzi kujua kilichotokea ukiendelea.

ZIRO PLUS...

MWANAMKE APONEA TUNDU LA SINDANO KUFA AJALINI...

Mwanamke mwenye miaka 20 amenusurika kifo kwenye tundu la sindano kwa kukata mkanda wa kiti cha gari na kubiringita nje wakati lori lilipoangukia juu gari lake.
Picha za kushangaza zimeonesha jinsi alivyokaribia kabisa kupondwa ndani ya gari lake aina ya Nissan Micra pale lilipobinywa kwenye Barabara ya A50 mjini Staffordshire.
Mwanamke huyo kijana aliyeshitushwa mno aliona trela la lori likianza kupinduka na kufanikiwa kugalagala upande mwingine.
Maamuzi yake ya haraka yaliokoa maisha yake huku Nissan yake ya rangi ya kijivu ikipondwapondwa kabisa na trela la lori hilo la rangi nyekundu lililobakia juu ya gari hilo dogo.
Alifanikiwa kutoka kishujaa kwenye gari hilo kupitia upande wa abiria, akinusurika kifo kwa kuumia kidogo mkononi.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya Saa 2:30 asubuhi mjini Uttoxeter.
Msemaji wa Huduma za Magari ya Wagonjwa wa West Midlands alisema: "Tukio limetokea baada tu ya mzunguko wa barabarani. Lori lilikuwa nje ya njia katika njia yake ya kawaida ya magari ya mizigo, huku Nissan Micra ikiwa ndani ya njia.
"Lori lilikuwa likivuta trela ambalo lilifunika kabisa gari dogo na kubinya sehemu ya juu upande wa abiria.
"Mwanamke mwenye miaka 20 aliyekuwa kwenye gari aliwaeleza wafanyakazi wa gari la wagonjwa kwamba aligundua kinachotokea na kufanikiwa kufungua mkanda wa gari na kubiringita nje kupitia upenyo mdogo.
"Hadi gari la wagonjwa linafika, alikuwa ameshafanikiwa kutoka nje kupitia upande wa abiria.
"Mtu aliyekuwa akiendesha lori hilo hakujeruhiwa ila ametishwa na tukio hilo."