ABIRIA 108 WANUSURIKA KIMIUJIZA KATIKA AJALI YA NDEGE...

Ndege hiyo baada ya kutumbukia baharini.
Zaidi ya abiria 100 wamenusurika kimiujiza jana baada ya ndege kuvuka njia ya kutua/kuruka na kwenda hadi ufukwe wa Bali na kujikita kwenye bahari.

Mashuhuda walisema abiria waliokuwa wakihofia maisha yao walipiga makelele kutokana na kuchanganyikiwa huku ndege hiyo ya Lion Air ilipovuka njia ya kutua/kuruka kwenye Uwanja wa Ndege wa Ngurah Rai, karibu na Denparsar.
Ndege hiyo, ilikuwa imebeba abiria 101 na wafanyakazi saba - kisha ikatumbukia baharini kutoka urefu wa karibu mita 50 juu.
Abiria waliojawa na hofu walipigwa picha wakitoka kwenye ndege hiyo iliyovunjika vipande, huku wengi wakisubiri juu ya mabawa yake wakati waokoaji wakifanya juhudi za aina yake za ukoaji.
Dewi, mmoja wa abiria ambaye alipata majeraha kichwani katika ajali hiyo, alianika tukio hilo la kuogofya la ndege kujikita kwenye maji: "Ndege hiyo ilikuwa kwenye harakati za kutua ndipo ghafla nikaona inakaribia kwenye bahari, na mwishowe ikajikita kwenye maji.
"Abiria wote walikuwa wakipiga mayowe ya kuchanganyikiwa kwa hofu wangezama. Niliacha vitu vyangu na kwenda kwenye mlango wa dharura. Nilitoka nje ya ndege na kuogelea kabla ya waokoaji kuchupa kwenye maji na kunisaidia."
Uwanja huo wa ndege unafahamika zaidi kutokana na njia yake ya kuruka/kutua kurefushwa hadi baharini.
Wengi wa abiria waliokoka kupitia milango ya dharura ambayo ilifunguliwa nusu sambamba na kiunzi hicho cha ndege na kufanya njia yao kuelekea ufukweni.
Baada ya kuwa wameokolewa kutoka kwenye ndege, walipelekwa kwenye uwanja wa ndege kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Maofisa wa Uwanja wa Ndege walisema kwamba watu kadhaa walijeruhiwa kwenye ajali hiyo, lakini ukubwa wa majeraha yao haukuweza kufahamika.
Lion Air kwa sasa imefungiwa kusafiri katika Umoja wa Ulaya sababu ya hofu kuhusu viwango vya usalama wake.
Picha kutoka eneo la tukio zinaonesha ndege hiyo ya abiria ikiwa na jina lake mashuhuri la red Lion ubavuni mwake ikiwa imelala kiasi ikielea kwenye maji karibu na miamba mwishoni mwa njia ya kutua/kuruka.
Mkuu wa Polisi Bali, Arif Wahyunadi alisema: "Abiria wote na wafanyakazi wameondolewa kwenye ndege hiyo huku ikiwa imelala kwenye maji.
"Wamepokelewa na kuhudumiwa kwenye uwanja wa ndege."
Abiria wote na wafanyakazi wameokolewa salama na kwamba watu 22 wamepelekwa kwenye hospitali tatu tofauti kutokana na majeraha mbalimbali.
Taarifa za awali zinaonesha kwamba kulikuwa na abiria 101 na wafanyakazi saba ndani ya ndege hiyo.
Wahyunadi alisema ndege hiyo asili yake ni mji wa Bandung, mji wa tatu kwa ukubwa nchini Indonesia - kivutio cha utalii sababu ya ujenzi wake.
KUHUSU SHIRIKA LA NDEGE LA LION AIR:
Ndege hiyo iliyoanguka ilikuwa ikimilikiwa na Lion Air, ambalo kaulimbiu yake ni: Tunawezesha Watu Kuruka.
Ni shirika la ndege binafsi la pili kwa ukubwa nchini Indonesia, likishikilia sehemu kubwa ya soko la ndani.
Mmiliki huyo kwa sasa amefungiwa kufanya safari zake katika nchi za Umoja wa Ulaya sababu ya hofu kuhusu usalama wake.
Shirika hilo hivi karibuni lilihusishwa na skendo - mnamo Januari mwaka jana Wizara ya Uchukuzi ya Indonesia ilisema kwamba wafanyakazi kadhaa wamekutwa wakiwa na mihadarati. Leseni zao zilibatilishwa.
Shirika hilo la ndege linafanya safari zake kwenda miji mikuu ya Indonesia, na pia safari nyingine Kusini Mashariki mwa Asia, ikichukua abiria kwenda Vietnam, Singapore, Malaysia na hata Saudi Arabia.
Likianzishwa mwaka 1999, shirika hilo lilianza kutumia ndege moja aina ya Boeing 737-200.
Lion Air ni ndege zinazotoza viwango vya chini vya nauli ambalo linashikilia asilimia 45 ya soko nchini Indonesia.
Lion Air limesaini mkataba wa Dola za Marekani bilioni 24 mwezi uliopita kwa ajili ya kununulia ndege 234 aina ya Airbus, oda kubwa kabisa kuwahi kupokewa katika karakana ya kuunda ndege nchini Ufaransa. Pia ilitoa oda kubwa kabisa kwa Boeing pale ilipokamisha mkataba wa kununua ndege 230 mwaka jana. Ndege hizo zitaanza kukabidhiwa kwa Lion Air kuanzia mwaka 2014 hadi 2026.

No comments: