POLISI WAKAMATWA KWA KUUA MWANAKIJIJI KIGOMA...

Kamanda Fraiser Kashai.
Jeshi la Polisi  mkoani Kigoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumpiga na kusababisha kifo cha mkazi wa kijiji cha Herushingo, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, Gasper Mussa.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Fraiser Kashai, aliwataja askari hao kwa waandishi wa habari mjini hapa kuwa ni mwenye namba NCC 8622 Koplo Peter na G.1236 Konstebo Sunday. Alisema wawili hao wanadaiwa kumpiga Mussa walipokuwa kwenye kilabu cha pombe usiku wa Sikukuu ya Krismasi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Kashai, Mussa alifariki siku moja baada ya kupata kipigo hicho alipokuwa akipelekwa hospitalini baada ya kukaa mahabusu kwa siku moja.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kashai alisema siku ya tukio, Mussa na askari hao walikuwa wakinywa pombe katika kilabu cha pombe na wakati wakinywa, ikatokea vurugu ambapo inadaiwa kusababishwa na Mussa kukataa kulipa pombe aliyokunywa.
Baada ya Mussa kukataa kulipa, Kamanda Kashai alisema askari hao ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Kasulu, walianza kumuadhibu kwa kumpiga na baadaye walienda kumlaza mahabusu.
Hata hivyo, siku iliyofuata, Kamanda Kashai alisema Mussa alizidiwa ndipo Mkuu wa Kituo cha Polisi Herushingo, alianza jitihada za kumpeleka Mussa hospitali, lakini alifariki mikononi mwa polisi kabla ya kufikishwa hospitali.
Alisema baada ya tukio hilo, alituma askari wake kufuatilia kwa undani kujua kile kilichotokea ili wachukue hatua.
Kwa sasa Kamanda Kashai alisema hatua za kijeshi kwa askari hao zinaendelea  ikiwa ni pamoja na kuwavua hadhi ya kijeshi waliyonayo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika tukio lingine Polisi mkoani Kigoma inamshikilia Hassan  Shija, mwalimu wa fani ya umeme katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) mkoani Kigoma kwa tuhuma za kumpiga mapanga na kumjeruhi mke wake sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Kashai alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Rida Mbili ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni na kwamba chanzo cha mgogoro huo ni wivu wa mapenzi.

No comments: