HIKI NDIO CHANZO CHA MAUAJI YA KAMANDA WA POLISI MWANZ

Geti la kuingilia nyumbani kwa marehemu Kamanda Liberatus Barlow, Mwanza.
Kitendo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow kuhoji wanaodhaniwa kuwa majambazi kama hawakuwa wanamtambua kijeshi ndicho kilichomponza na kuuawa.
Kamanda Barlow aliuawa usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kitangiri mjini hapa, muda mfupi baada ya kutoka kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake katika hoteli ya Florida.
Mauaji hayo yamesababisha hali ya wasiwasi kiusalama jijini hapa, kutokana na mauaji hayo kufanywa dhidi ya mtu ambaye angedhaniwa kuwa katika ulinzi imara kwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani na mtu muhimu katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, tukio hilo lilitokea kati ya saa 7 na 8 katika kona ya Bwiru jirani na hoteli ya Taifive.
Akisimulia tukio hilo, Ndikilo alisema Kamanda Barlow aliuawa na kundi la watu kati ya sita na 10 baada ya kumpiga risasi kwenye bega na kupenya shingoni na kutokea kwenye taya.
Alisema mazingira ya mauaji hayo hayako wazi sana, lakini alipoteza maisha papo hapo kwenye eneo la tukio.
Ndikilo alisema awali Barlow alishiriki kikao cha harusi ya mpwa wake, Sembui Maneto katika hoteli ya Florida akiwa na ndugu zake na kikao hicho kilimalizika kati ya saa 4 na 6 usiku.
Alisema wakati akiondoka kurudi nyumbani akiwa na gari lake binafsi aina ya Toyota Hilux Double Cabin, alimsaidia usafiri mwanamke ambaye awali ilisemekana kuwa ni dada yake, lakini baadaye ikabainika kuwa si dada yake.
Alisema mwanamke huyo Doroth Moses ni mwalimu wa shule ya msingi Nyamagana.
Mkuu wa Mkoa alisema alipofika Kitangiri alisimama ili kumteremsha abiria huyo na ghafla mbele wakajitokeza watu wawili wenye tochi na kuonesha kutofurahishwa na taa za gari la Kamanda zilizowamulika.
Alisema mwanamke huyo alimwuliza Kamanda kama anawatambua, akamjibu kuwa ni Polisi Jamii walio kwenye doria kwani walikuwa wamevaa vikoti vya Polisi Jamii vinavyoakisi mwanga usiku.
Alisema akiwa ameegesha gari watu hao walisogea kwenye mlango wa abiria yule na kisha kutokea kundi la watu wengine na kwenda kwenye mlango wa Kamanda.
Wakiwa mlangoni palitokea majibizano huku Kamanda akiwauliza kama hawamjui huku akitoa redio ya mawasiliano (radio call) ili kuwasiliana na polisi wenzake ndipo mtu aliyekuwa nje ya mlango wa gari alipomfyatulia risasi.
Baada ya kufanya mauaji hayo, majambazi walichukua redio hiyo na simu mbili za mkononi. Hata hivyo katika hali ya kawaida, RPC hupaswa kuwa na mlinzi lakini siku hiyo kwa mujibu wa taarifa, hakuwa naye.
Ndikilo alisema polisi wa kituo cha Kirumba wanamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo, Ndikilo alisema Polisi imemleta hapa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba kuja kuongeza nguvu ya uchunguzi.
Alitoa rai kwa wananchi kutulia kutokana na tukio hilo na wasubiri uchunguzi wa kina unaofanywa na Jeshi la Polisi na litafanya kazi kubwa kuhakikisha waliofanya mauaji hayo wanatiwa nguvuni.
Mwandishi alifika eneo la tukio na kuzungumza na mtoto wa kaka wa Mwalimu Moses anayeitwa Kennyrogers Edwin aliyedai kuwa muda mfupi kabla ya tukio, mwalimu huyo aliwapigia simu akiwataka wamfungulie.
Alipofungua lango, aliona gari limepaki na watu wawili wakiwa upande wa abiria na wengine kwa dereva na alisikia mlio wa risasi na kushuhudia watu hao wakikimbia baada ya kuona pikipiki inakuja nyuma yao.
Mmoja wa wakazi wa Kitangiri, Edward Jackson ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu sekondari ya Kitangiri alisema akiwa mezani anajisomea usiku alisikia mlio wa risasi na alipotaka kutoka nje mama yake alimzuia ili asije akadhurika.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, licha ya kushitushwa na kuhuzunishwa na tukio hilo, alitaka wananchi kutoa ushirikiano ili kubaini wahusika. 
Mwili wa Barlow ulifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kati ya saa 8.30 na tisa alfajiri na kufanyiwa uchunguzi na madaktari na kisha kuhifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.
Mmoja wa madaktari ambao walimpokea na kumfanyia uchunguzi wa awali walisema jeraha la risasi lililosababisha kifo cha Kamanda huyo liliharibu mfumo wa mawasiliano baada ya kumvunja shingo. 
“Hakika ni moja ya vifo vya kutisha ambavyo nimewahi kuvishuhudia tangu niwe daktari, hata wenzangu tuliokuwa nao tulibaki tunashangaa kuona kiongozi mkubwa anakatishwa maisha kwa risasi,” alisema mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Baadhi ya wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti, walionesha masikitiko yao kutokana na kifo cha Kamanda Barlow.
Walisema katika kipindi alichokaa hapa alifanikiwa kudhibiti ujambazi kutokana na kusimamia doria za mara kwa mara jijini hapa na atakumbukwa kwa jinsi alivyosimamia mauaji ya majambazi watano walivamia duka katikati ya Jiji.
“Tumepoteza jembe halisi na mwana wa Tanzania, Kamanda Barlow alifanikiwa kusimamia haki na kukomesha ujambazi, tunaliomba Jeshi la Polisi mkoani hapa lihakikishe linawatia nguvuni wahusika wote,” alisema Patricia Jumbe mkazi wa hapa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Lily Matola alisema wanamshikilia mwanamke aliyekuwa na Kamanda huyo kwa mahojiano ili kujua chanzo cha mauaji hao.
“Tunamhoji mwanamke huyo na kufanya uchunguzi wa kina, tutatoa taarifa baada ya kufanya uchunguzi wa awali na suala la mazishi tunasubiri maelekezo ya kaka wa marehemu aliye Dar es Salaam,” alisema.

No comments: