FAMILIA YA RAIA WA UGANDA YAVUNA MAMILIONI KITAPELI UINGEREZA...

KUTOKA JUU: Lamulah, Albert na Jordan. KULIA: Mahakama ambako kesi hiyo inasikilizwa.
Familia ya walaghai wa Kiafrika imeiba kiasi kisichopungua Pauni za Uingereza milioni 4 kutoka kwa walipakodi katika kipindi cha miaka 20.
Mmoja alitengeneza vitambulisho feki kwa watoto zaidi ya 100 ili kufaidi utaratibu wa mfumo wa mafao.
Pia alidai kuwa na virusi vya ukimwi na kuhitaji dawa za gharama kubwa mno - lakini badla yake alizisarifisha kinyemela kwenda nchini Uganda kwa ajili ya kuziuza kwa faida kubwa.
Mahakama ilielezwa kwamba usafirishaji dawa hizo kwa miaka mingi uliwagharimu walipakodi zaidi ya Pauni za Uingereza milioni 2.
Zaidi ya Pauni za Uingereza 154,000 zililipwa kwa ajili ya elimu kwa 'familia', ambapo Pauni za Uingereza 37,000 ni kwa ajili ya kozi moja tu ya elimu ya juu.
Ulaghai unaohusiana na gharama za malazi na kodi ya pango la maghorofa uligharimu Pauni za Uingereza 650,000, na kiwango kikubwa cha mafao ya familia kinachofikia Pauni za Uingereza 900,000.
Kwa kipindi cha wiki sita cha usikilizwaji kesi yao, baraza la mahakama lilielezwa jinsi kundi 'lililoungana kuandaa, kutumia na kunyonya' utambulisho feki kwa lengo la kutekeleza ulaghai wa kuduwaza.
Mchunguzi mmoja alilieleza gazeti la Daily Mail: "Balaa ni, walikuwa na vitambulisho vingi mno kwamba inaweza isifahamike hasa kiasi gani walichovuna kutoka kwenye mfumo wa mafao na nchi hii katika kipindi hicho kirefu."
Mwendesha mashitaka Paul Raudnitz alisema: "Mkono wa ulaghai huu umefika mbali na kwa mapana kwa miaka mingi sana. Kila mshitakiwa kwa mara tofauti alishiriki njama hizo."
Alisema 'mshiriki mkuu' Ruth Nabuguzi mwenye miaka 49, 'ametumia vitambulisho kadhaa ... vingi kiasi kwamba idadi ya vitambulisho haiwezi kufahamika'.
Nabuguzi, mwenye asili ya kutoka Uganda, alidai dawa za Ukimwi zilizogharimu Pauni za Uingereza 2,280,000. Pia alipokea Pauni za Uingereza 500,000 kwa ajili ya mafao ya nyumba kutoka Halmashauri ya Newham huko mashariki mwa London, Mahakama ya Croydon ilielezwa.
Nabuguzi aliingia Uingereza mwaka 1991 na kuomba hifadhi ya ukimbizi yake mwenyewe na ya watoto wanne aliowaacha nchini Uganda.
Miaka mitatu baadaye, alitumia jina la Jane Namusisi kuomba tena hifadhi ya ukimbizi sambamba na ya watoto wawili zaidi. Mwaka 1999 akitumia jina la Pauline Zalwango, aliomba tena hifadhi safari hii akiwa na watoto wengine watatu.
Anaaminika amekuwa akisafiri mara kwa mara kwenda Uganda na kuweza kununua nyumba takribani tatu ndani na maeneo mbalimbali katika mji mkuu Kampala.
Dennis Kyeyune mwenye miaka 29, anadhaniwa kuwa ni mtoto wa Nabuguzi. Polisi walikuta begi jeusi kubwa la kubebea nguo nyumbani kwake mashariki mwa London likiwa limefichwa kwenye paa na mkoba wenye nyaraka bandia, ulioelezewa kama 'hifadhi ya ulaghai wa vitambulisho'.
Wafuasi wengine wa genge hilo ni pamoja na Jordan Sebutemba mwenye miaka 26, ambaye anadhaniwa kuwa ni binti wa Nabuguzi; Albert Kaidi, mshirika wa zamani wa Sebutemba ambaye anadhaniwa kuwa na asili ya Rwanda; na Lamulah Sekiziyuvu mwenye miaka 36, mshirika wa zamani wa Kyeyune na Kaidi.
Kyeyune, Sebutemba, Kaidi na Sekiziyuvu walipatikana na hatia ya makosa mbalimbali ya ulaghai juzi.
Watahukumiwa wiki ijayo sambamba na Nabuguzi na Betty Tibakawa mwenye miaka 21, Lina Katongola mwenye miaka 29, Mathy Matumba mwenye miaka 50, na Eddie Carlos Semcenda mwenye miaka 30.

No comments: