MSONGAMANO WA MAHABUSU WATISHIA AMANI MAGEREZA DAR


Magereza ya jiji la Dar es Salaam  yana msongamano mkubwa wa mahabusu na wafungwa, ikilinganishwa na uwezo wake halisi, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Magereza wa jiji hilo, Joel Bukuku alisema kuna wafungwa pamoja na mahabusu zaidi ya 4,734 kwa siku wakati uwezo wa magereza hayo ni kuchukua watu 3,040.
Aliyataja magereza hayo kuwa ni Keko, Segerea, Ukonga na gereza la kawaida la Wazo ambayo yalijengwa miaka mingi iliyopita na kukadiriwa kuwa na watu wachache lakini kwa sasa watu wanaotunzwa katika magereza hayo ni zaidi ya uwezo wake kutokana na ongezeko la watu.
“Pamoja na changamoto nyingine tulizonazo ni pamoja na msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani jambo ambalo linapelekea kuwa na watu wengi katika magereza yetu,” alisema Bukuku.
Alisema magereza ya jiji hilo yanachukua asilimia 10 tu ya wahalifu waliopo magereza yote nchini na kuyataja magereza hayo kuwa ni gereza la Ukonga ambalo ni kubwa na kongwe lilianzishwa mwaka 1952, gereza la Keko lilianzishwa mwaka 1957 na gereza la Segerea lilianzishwa mwaka 1991.
Bukuku alisema msongamano mkubwa uliopo ni wa mahabusu ambao hawafanyi kazi yoyote isipokuwa kula na kulala huku shughuli zote za uzalishaji zikifanywa na wafungwa.
Alisema changamoto hiyo iko nje ya uwezo wa magereza kwa sababu watu kurundikana magereza kunatokana na sababu nyingi, ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa kesi ambapo inahitajika fedha pamoja na uwajibikaji wa taasisi zingine kama mahakama na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Akizungumzia miradi ya urekebishaji inayoendeshwa katika magereza hayo alisema kuwa ni pamoja na kiwanda cha Samani za ndani na ofisini, kiwanda cha sabuni ambazo ni kwaajili ya matumizi ya wafungwa, kiwanda cha nguo, kilimo cha michikichi na kiwanda cha mafuta ya mawese na kilimo cha mihogo.
Alisema miradi hiyo husaidia wafungwa kurekebishwa tabia zao kupitia stadi za kazi katika magereza yao, kwa kuwapatia ufundi mbalimbali ambao utawasaidia wanapomaliza vifungo vyao na kurudi kwenye jamii.
“Kumlinda na kumtunza mtu ambaye hajishughulishi ni tofauti kabisa na kumlinda mtu ambaye ana shughuli za kufanya, mtu asipokuwa na kazi za kufanya akili yake wakati wote inawaza kufanya uhalifu na kutoroka,” alisema Bukuku.
Bukuku alisema kwa kuwaingiza mahabusu katika kazi hizo zinazoendeshwa katika magereza, inasaidia kujihisi kwamba ni sehemu ya jamii na kuondokana na mawazo ya kurudi katika uhalifu ambapo wengi wamebadilika kabisa.

1 comment:

Anonymous said...

Story hii ni ya kwangu wewe umeitoa wapi? maadili ya uandishi wa habari yanatutaka ukitumia story ya mtu taja chanzo cha habari yako vinginevyo ni kinyume ni KOSA