WANAZUONI WA KIISLAMU WAWAJIBU MAASKOFU


Taasisi ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu, imewataka maaskofu nchini wawe wavumilivu, kwani Serikali ni ya watanzania wote.

Aidha, imewasisitiza watanzania kwa ujumla, kupata elimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuisoma kwa makini na kuielewa ili wawe na uwezo na uhuru wa kuchagua kile wanachokiona kina manufaa kwao, bila kuwepo shinikizo la kiimani.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Shehe Khamis Mataka (pichani), wakati akitoa tamko la taasisi hiyo, kufuatia tamko la TCF kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na Hali ya Usalama na Amani ya Nchi.
“Tunawasihi watanzania wote kuendelea kudumisha undugu wao kama watanzania, bila kujali rangi, dini, kabila na itikadi za kisiasa na tumkemee yeyote yule anayetaka kutugawa kwa kutumia misingi ya kidini, kikabila, kisiasa na kiuchumi” alisema.
Pia, imeiomba Serikali iache kuzingatia tamko lililotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), badala yake iendelee na mchakato wa Katiba Inayopendekezwa na Mahakama ya Kadhi kwa kufuata misingi ya haki.
Shekhe Mataka aliongeza “Taasisi imezipitia kwa kina nukta zote nne za Tamko hilo pamoja na hitimisho lake na kubaini kwamba maaskofu wamejisahau kwamba wao ni viongozi wa kiimani na kiroho, ambao wanatakiwa wawe tayari kumpokea yeyote na kumpa neno la hekima lililojazwa faraja, bila hata ya kujali itikadi au chama chake cha siasa. Badala yake wameamua kutoa faraja kwa waumini wao kwa kuzingatia utashi wa kisiasa”.
“Maaskofu wameamua kuanzisha utamaduni mpya wa kuendesha mambo ya kisiasa kwa misingi ya kiimani na hivyo kutoa tishio la kuwagawa watanzania kwa misingi hiyo. Hivyo baada ya Taasisi yetu kujiridhisha na yaliyomo katika Tamko hilo la Maaskofu chini ya mwavuli wa TCF, tunashauri hatua za kuchukua,” alisema.
Alisema, “Kwa kuwa serikali ina vyombo makini vyenye wataalamu wenye uwezo wa kufahamu na kuelewa uvunjifu wa katiba na Umoja wa Kitaifa, tunaomba ipuuze tamko hilo ambalo limeisikitisha taasisi yetu na kuwadhalilisha waislamu.
 “Suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu na haliwahusu wala halihitaji ridhaa ya wasiokuwa Waislamu, kama ambavyo waislamu hawajapata kuombwa ridhaa yao katika yale ambayo Serikali imekuwa ikiwafanyia wakristo na makanisa yao,” alisema.
Shehe Mataka alisema, “Taasisi hii inapinga kwa nguvu zote madai ya Maaskofu kuwa, Waislamu kuwa na Mahakama ya Kadhi ni uvunjifu wa Katiba, kwani sheria za Kiislamu ni moja ya vyanzo vya sheria ya Tanzania. Mahakama za Tanzania zimekuwa zikitumia sheria hizo kuhukumu kesi za waislamu kuhusu ndoa, talaka, mirathi toka mwaka 1963 na kufuatiwa na sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu ya mwaka 1964 na kuhitimishwa na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971”.
Alisema, “Jambo la msingi hapa ni kuwa kesi hizo zinahukumiwa na mahakimu wasio na elimu, wala ujuzi na sifa za kuwa Makadhi, kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu na ndio msingi wa Waislamu kudai uwepo wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara”.
Alisema taasisi hiyo inawakumbusha maaskofu kuzingatia kuwa madhara ya kuwagawa watanzania kwa misingi ya kiimani, dhambi yake haitaishia kwenye kadhia ya Mahakama ya Kadhi, wala Katiba Inayopendekezwa, bali itaendelea kukita mizizi yake katika kila jambo linalowahusu watanzania.
Mataka alisema, “Jukwaa linasisitiza viongozi wa dini wabaki kuwa walezi, siyo kuwagawa watu. Mambo ya siasa tuwaachie wanasiasa, sisi tubaki na heshima yetu ya kuwa viongozi wa dini, kwa sababu hata waumini wetu wanatuamini tunapoongea jambo kwamba ni tamko la Kimungu na wanatakiwa kulifuata. Kwa hili, hata Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameona hili lina tatizo”.

No comments: