Magereza ya jiji la Dar es Salaam yana msongamano mkubwa wa mahabusu na
wafungwa, ikilinganishwa na uwezo wake halisi, imeelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana, Mkuu wa Magereza wa jiji hilo, Joel Bukuku alisema kuna wafungwa
pamoja na mahabusu zaidi ya 4,734 kwa siku wakati uwezo wa magereza hayo ni
kuchukua watu 3,040.
Aliyataja magereza hayo kuwa ni Keko, Segerea,
Ukonga na gereza la kawaida la Wazo ambayo yalijengwa miaka mingi iliyopita na
kukadiriwa kuwa na watu wachache lakini kwa sasa watu wanaotunzwa katika
magereza hayo ni zaidi ya uwezo wake kutokana na ongezeko la watu.
“Pamoja na changamoto nyingine tulizonazo ni
pamoja na msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani jambo ambalo
linapelekea kuwa na watu wengi katika magereza yetu,” alisema Bukuku.
Alisema magereza ya jiji hilo yanachukua
asilimia 10 tu ya wahalifu waliopo magereza yote nchini na kuyataja magereza
hayo kuwa ni gereza la Ukonga ambalo ni kubwa na kongwe lilianzishwa mwaka
1952, gereza la Keko lilianzishwa mwaka 1957 na gereza la Segerea lilianzishwa
mwaka 1991.
Bukuku alisema msongamano mkubwa uliopo ni wa
mahabusu ambao hawafanyi kazi yoyote isipokuwa kula na kulala huku shughuli
zote za uzalishaji zikifanywa na wafungwa.
Alisema changamoto hiyo iko nje ya uwezo wa
magereza kwa sababu watu kurundikana magereza kunatokana na sababu nyingi,
ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa kesi ambapo inahitajika fedha pamoja na
uwajibikaji wa taasisi zingine kama mahakama na ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP).
Akizungumzia miradi ya urekebishaji
inayoendeshwa katika magereza hayo alisema kuwa ni pamoja na kiwanda cha Samani
za ndani na ofisini, kiwanda cha sabuni ambazo ni kwaajili ya matumizi ya
wafungwa, kiwanda cha nguo, kilimo cha michikichi na kiwanda cha mafuta ya
mawese na kilimo cha mihogo.
Alisema miradi hiyo husaidia wafungwa
kurekebishwa tabia zao kupitia stadi za kazi katika magereza yao, kwa kuwapatia
ufundi mbalimbali ambao utawasaidia wanapomaliza vifungo vyao na kurudi kwenye
jamii.
“Kumlinda na kumtunza mtu ambaye
hajishughulishi ni tofauti kabisa na kumlinda mtu ambaye ana shughuli za
kufanya, mtu asipokuwa na kazi za kufanya akili yake wakati wote inawaza
kufanya uhalifu na kutoroka,” alisema Bukuku.
Bukuku
alisema kwa kuwaingiza mahabusu katika kazi hizo zinazoendeshwa katika
magereza, inasaidia kujihisi kwamba ni sehemu ya jamii na kuondokana na mawazo
ya kurudi katika uhalifu ambapo wengi wamebadilika kabisa.
1 comment:
Story hii ni ya kwangu wewe umeitoa wapi? maadili ya uandishi wa habari yanatutaka ukitumia story ya mtu taja chanzo cha habari yako vinginevyo ni kinyume ni KOSA
Post a Comment