TFDA KUFUATILIA VYAKULA VYENYE VIRUTUBISHO


Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imeandaa mpango wa ufuatiliaji  wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwenye soko. 
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Habari wa TFDA, Gaudencia Simwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 
Alisema mpango huo ulianza kutekelezwa tangu Aprili mwaka huu.Alisema  kanuni za uongezwaji wa virutibisho, hairuhusu viwanda vidogo na vya kati kutokana na kutokuwepo na teknolojia muafaka ya uongezaji wa vyakula katika ngazi ya wasindikaji wadogo na wa kati. 
Aliongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya  na Ustawi wa Jamii inafanya majaribio katika halmashauri sita za mikoa ya Iringa (Kilolo, Iringa Vijijini), Njombe (Njombe Mjini) na Arusha (Karatu, Meru na Monduli) kuhusu uongezaji virutubishi kwenye unga wa mahindi unaosindikwa na wasindikaji wadogo. 
Kwa upande wa mafuta ya kula yanayozalishwa na wasindikaji wadogo, majaribio yanafanyika katika Mkoa wa Manyara (Babati) Singida na Dodoma. 
Alisema katika kufanikisha mpango wa kitaifa wa urutubishaji vyakula, TFDA pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa, kwa lengo la kulinda afya ya walaji kwa kutekeleza uratibu wa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula.

No comments: