Uongozi wa Awamu ya Nne chini
ya Rais Benjamin Mkapa, umetajwa kwamba ndio uliojenga msingi wa uanzishwaji wa
viwanda vya ndani nchini kupitia mfumo wa kodi.
Mbunge
wa Singida Mjini, ambaye pia ni mmoja wa wafanyabiashara wenye viwanda, Mohamed
Dewji, amesema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiingia
mkataba wa ushirikiano na kampuni ya RMB.
“Katikati
ya miaka ya 1990 Rais Benjamini Mkapa aliingia madarakani akaanzisha mfumo wa
kodi ambao ulilazimisha uchumi kujenga msingi wa viwanda vya ndani,” alisema
Dewji.
Kwa
mujibu wa Dewji, kabla ya hapo wafanyabiashara wa Tanzania, walikuwa wakipata
faida kwa kuagiza kutoka nje ya nchi karibu kila kitu, kutoka karatasi za
chooni mpaka dawa za meno.
Alisema
Mkapa alipoingia madarakani, alianzisha mfumo wa kodi ambao ulimlazimisha
mfanyabiashara kuacha kununua bidhaa zilizotengenezwa viwandani nchi za nje na
kununua malighafi ili atengeneze bidhaa hapa nchini.
Mfumo
huo wa kodi kwa maelezo ya Dewji, ulimtoza mfanyabiashara anayeagiza kutoka nje
bidhaa zilizo tayari kuuzwa katika soko la ndani, asilimia 25 ya thamani ya
bidhaa hiyo.
Kwa
mfanyabiashara aliyeagiza bidhaa ambayo bado ina ughafi kidogo (semi finished),
ambayo itatakiwa kuingizwa katika viwanda vya ndani kuondolewa ughafi ndio
iuzwe katika soko la ndani, mfumo huo ulimpa unafuu kwa kumtoza kodi ya
asilimia 10 ya bidhaa hiyo.
Dewji
alisema mfanyabiashara aliyeagiza malighafi kabisa, ambayo ilipaswa kuingia
katika viwanda vya ndani ili kutengeneza bidhaa ya kuuza katika soko la ndani,
alipata nafuu kubwa kwa kuwa hakutozwa kodi ya aina yoyote.
“Nilitambua
fursa kubwa iliyokuwa hapo, baba yangu alikuwa akiagiza mafuta ya kula,
nikafikiria kwa nini nisianzishe kiwanda cha mafuta ya kula, lakini akaona ni
hatua ya hatari kibiashara.
“Nilimkopa
dola za Marekani milioni moja na kununua kiwanda cha sabuni kinachozalisha tani
24 za sabuni kwa siku, leo kinazalisha tani 500 kwa siku. Niliendelea nikanunua
kiwanda cha kwanza cha mafuta ya kula chenye uwezo wa kuzalisha tani 60 za
mafuta ya kula kwa siku,” alisema Dewji.
Kwa
mujibu wa Dewji, kwa sasa kiwanda hicho cha mafuta ya kula kinazalisha tani
2,200 kwa siku na ndio kiwanda kikubwa cha mafuta ya kula Afrika huku kampuni
ya Mohammed Enterprises Ltd (MeTL), ikitarajia kuongeza pato lake la mwaka hadi
dola bilioni tano na kutoa ajira rasmi laki moja ifikapo 2018.
Dewji
ambaye kampuni yake inafanya biashara nyingi katika Ukanda wa Afrika ya
Mashariki, Kati, Kusini mpaka nchi za Mashariki ya Kati, alisema pia aliingia
katika kilimo cha katani, ambacho zao lake sasa lina soko jipya kimataifa.
Alisema
zao hilo lilizoeleka kutengenezea kamba na kuwa malighafi katika viwanda vya
meli na mashuwa, leo linatumika
kutengeneza mabodi ya magari aina ya Mercedes Benz na ndege katika Bara la
Ulaya na katika nchi za Mashariki ya Kati, linatumika kutengeneza nyumba
zinazozuia joto kuingia ndani.
No comments:
Post a Comment