Mkoa wa Tanga umetenga vituo kadhaa vya afya
vitatu, ikiwa ni hatua ya maandalizi ya kudhibiti watu watakaobainika
kuambukizwa virusi vya homa ya ebola.
Vituo hivyo ni cha kwenye mpaka wa Horohoro
wilayani Mkinga, Masiwani Shamba na Maramba.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa
alibainisha hayo juzi katika mkutano na waandishi wa habari.
Alisema timu maalumu ya mkoa ya wataalamu wa
afya, tayari inakagua uwezo wa vituo vingine vilivyotengwa na halmashauri
nyingine za mkoa huo, kama vinastahili kupokea wagonjwa wa aina hiyo.
Alisema ingawa mpaka sasa hakuna mgonjwa wa
ebola nchini, serikali imechukua hadhari hiyo, kuwaondoa wasiwasi wananchi
kutokana na mwingiliano wa wageni kutoka nchi jirani kupitia mpaka wa Horohoro.
Alisema vituo hivyo vitatu vimeimarishwa kwa
kupelekewa vifaa tiba, madaktari na wauguzi wenye stadi za kutosha na vitatumika
kutoa huduma kwa wagonjwa watakaobainika.
“Kwa kuwa ebola haina chanjo wala tiba, mpango
mkakati wa mkoa sasa ni kuhakikisha wananchi wanaelimishwa kuhusu namna ya
kujikinga kuzuia maambikizi…pia tumeziagiza halmashauri zote 11
zinazounda mkoa kutenga maeneo sahihi ya kupokelea wagonjwa hao”, alisema.
Aliongeza, “wananchi ondoeni wasiwasi na tunawataka
muimarishe usafi wa mazingira, hakikisheni mnanawa vizuri mikono kwa maji safi
na sabuni…acheni kusalimia kwa kushikana mikono na watu kila mahali”, alisema.
No comments:
Post a Comment