CHINA YAKUBALI KUIPANGA UPYA LINDI, MTWARA KUWA YA KISASA...

Moja ya mitaa katikati ya mji wa Mtwara.
Uchumi wa gesi unaotarajiwa kuinua maisha ya Watanzania, umesababisha Rais Jakaya Kikwete kuagiza maandalizi ya haraka ya ujenzi wa majiji ya kisasa katika miji ya Mtwara na Lindi.
Akizungumza juzi na Waziri wa Nyumba, Makazi na Maendeleo ya Miji na Vijiji wa China, Jiang Weixin Ikulu, Zanzibar, Rais Kikwete aliomba nchi hiyo kusaidia kupanga miji ya kimkakati ya Mtwara, Lindi na Kigamboni, Dar es Salaam.
Alisema pamoja na kwamba changamoto za mipangomiji ziko katika miji yote ya Tanzania, ikiwamo Dar es Salaam, lakini Serikali kwa sasa inapenda kuelekeza nguvu zake katika miji mitatu yenye uwezo mkubwa wa kuendelea kwa kasi kubwa zaidi, katika miaka michache ijayo na hivyo lazima iendelee ikiwa imepangwa vizuri.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa  pia na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Rais Kikwete alisema miji hiyo mitatu itakua kwa kasi kutokana na uvumbuzi wa gesi na uchumi utakaotokana na uvumbuzi huo, na isipopangiliwa vizuri, itaishia kupanuka kiholela.
“Chukulia mfano wa Jiji la Dar es Salaam. Mamilioni ya watu wanaishi katika Jiji hili lakini asilimia 70 ya Jiji  haikupimwa na imejengwa holela tu.
“Ni asilimia 30 ya Dar es Salaam iliyopimwa. Hatuwezi kuiruhusu miji mingine, hasa ya kimkakati, kupanuka na kukua kwa namna hii,” alisema Rais Kikwete.
Alimwelezea Weixin kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali katika upangaji miji na kuiweka miji ya Tanzania katika hali nzuri, akisisitiza kuwa Serikali inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa uwezo wa kiufundi, ukosefu wa vifaa na wa uwezo kifedha  unaohitajika kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Baada ya kumsikiliza Rais Kikwete, Waziri Weixin alisema ameelewa changamoto zinazoikabili Tanzania na kuwa Wizara yake itatuma wataalamu kuja nchini kufanya tathmini katika maeneo muhimu kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wawili hao pia walizungumzia uhusiano kati ya nchi na wananchi wa nchi hizo mbili ambao utafikisha miaka 50, Mei, kutakapofanyika kumbukumbu ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mwaka 1964.
“Tanzania imenufaika na uhusiano huu katika miaka 50 iliyopita. China imeisaidia sana katika miaka hiyo 50. Tunahitaji kuuendeleza uhusiano huu na bado tunahitaji kuendelea kuungwa mkono na China kwa sababu pamoja na yote, Tanzania bado ni nchi inayoendelea,” alisema Rais Kikwete.
Miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa nchini kwa ushirikiano na China ni pamoja na Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara); Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam; kiwanda cha nguo cha Urafiki; kiwanda cha zana za kilimo Ubungo (UFI), barabara na madaraja kadhaa.

No comments: