WAZIRI ATAMANI ZIWEPO TANESCO NYINGINE NYINGI...


Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, ameelezea kukerwa na Shirika la Umeme (Tanesco), kwa kushindwa kufikisha umeme vijijini na kusababisha miradi ya maji kusuasua.
“Tungekuwa na mashirika mengine ya umeme tungewafungia maji haraka, lakini kwa vile ni Tanesco peke yake, sasa wananchi hawana maji … Tanesco ukiritimba umezidi,” alisema Profesa Maghembe.
Profesa Maghembe alitoa kauli hiyo juzi wakati akizindua mradi wa usambazaji majisafi katika kata ya Kiboroloni na viunga vyake, ambako huduma hiyo haikuwapo kwa muda mrefu.
Alisema Wizara yake inatambua kuwa vijiji 74 vya mkoa wa Kilimanjaro havina maji na lengo ni kuhakikisha hadi mwisho wa mwaka huu vinapata huduma hiyo.
Alisema katika vijiji hivyo 74, vijiji 28 miradi yao imekamilika na wananchi wanapata huduma hiyo na miradi ya vijiji vingine 17 iko hatua za mwisho lakini tatizo ni umeme.
“Kwa kweli tatizo tulilonalo sasa ni Tanesco… kwa muundo walionao ni lazima waongeze bidii,” alisema.
Katika vijiji vingine 26, miradi yake ya maji iko hatua mbalimbali za utekelezaji na katika bajeti ya mwaka huu, mipango ni kuvipa maji vijiji 25 kila wilaya nchini.
Alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Moshi (MUWSA), Cyprian Luhemeja, kuhakikisha hadi Juni wananchi wa Moshi wawe na maji.
Akielezea utekelezaji wa miradi mjini Moshi,  Luhemeja alisema Mamlaka imejiwekea vipaumbele vya kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 38 Juni mwaka jana.
Kutokana na malengo hayo, ilipofika Desemba mwaka jana kiwango cha upotevu wa maji kilishuka hadi asilimia 24 na lengo ni kukishusha hadi asilimia tisa  Desemba.
Vipaumbele vingine kwa mujibu wa Luhemeja, ni kuongeza wateja kutoka kaya 20,000 hadi 35,000.
Alisema wameongeza chanzo cha maji cha  Coffee Curing chenye uwezo wa kutoa lita za ujazo 1,500 kwa siku huku juhudi za kuchimba kisima katika tangi la Kilimanjaro lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 1,800 kwa siku, zikiendelea.
Alisema Mamlaka ilijipa siku 180 kutekeleza mipango yake na walikusudia kukarabati miundombinu na kuondoa mtandao wa mabomba chakavu yenye urefu wa kilometa 85 lakini hadi juzi, mchakato wa kuondoa mabomba hayo uliondoa ya kilometa 24.

No comments: