KUPIGA SIMU SASA SHILINGI 35 KUANZIA MACHI MOSI...

Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Barabara ya Sam Nujoma, Dar es Salaam.
Gharama ya kupiga simu kwa mteja wa kampuni moja ya simu ya mkononi kwenda mteja wa kampuni nyingine sasa zitapungua.
Mapendekezo ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kampuni za simu kushusha  gharama hizo kutoka Sh 112 hadi Sh 35 kwa dakika kuanzia Machi mosi mwaka huu, yamekubaliwa na wadau zikiwamo kampuni hizo.
TCRA ilitoa mapendekezo hayo baada ya kupata ripoti ya  Kampuni Mwelekezi Mshauri kutoka Uingereza iliyofanya utafiti kwa kuangalia mapato na faida za kampuni za simu nchini.
Mkurugenzi wa Ofisi za Kanda wa TCRA, Victor Nkya alisema jana kwamba katika mapendekezo yao gharama hiyo inatakiwa kushuka kuanzia Machi kutoka Sh 112 ya sasa mpaka Sh 34.92. Mwakani inatarajiwa kuwa Sh 32.4; 2015 Sh 30.58; 2016 Sh 28.57 na mwaka 2017 Sh 26.96.
Kutokana na mapendekezo hayo ambayo yalitokana na utafiti uliobaini kuwa gharama hizo nchini ni kubwa, wadau na kampuni zilizohudhuria kongamano la wadau la kujadili bei hizo, walikubali.
Wadau hao ni pamoja na kampuni za  Tigo, Vodacom, Airtel, Benson Online, Dovetel(Sasatel), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) , Six Telecom, Zantel, Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano, Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Tume ya Ushindani na wananchi wa kawaida.
Wadau hao walitaka ushindani ubaki katika utoaji huduma si gharama za kupiga simu kutoka kwa mteja wa kampuni moja kwenda wa kampuni nyingine.
Walisema punguzo hilo litaongeza wateja huku gharama zikipungua, jambo litakalosaidia kuongezeka kwa kampuni za utoaji huduma za simu sokoni na kuongeza ushindani.
Walisisitiza kuwa utafiti wa kina katika sekta hiyo, umeonesha kuwa Tanzania ikilinganishwa na nchi zingine Afrika, gharama zake za simu ni kubwa jambo linalofanya watumiaji kutumia asilimia 30 hadi 40 za kipato chao kwenye simu.
TTCL
Kaimu Mkurugenzi wa TTCL, Mrisho Shaban alisema kampuni hiyo inaunga mkono mapendekezo hayo na kushauri yaanze mapema zaidi kuliko Machi mosi na mlaji asibebeshwe gharama zisizo za lazima.
Pia alishauri TCRA isisubiri miaka mitano kufanya mabadiliko ya kupunguza gharama hizo bali waangalie  hali ya soko.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi  na Teknolojia, Samson Mwela alisema wamekubaliana na mapendekezo hayo, kwa kuwa sekta hiyo inaendeshwa kwa ushindani ambao unalindwa, hivyo ni lazima mtumiaji apate haki zake.
Alisema kupungua kwa gharama hizo, kutawapunguzia watumiaji mzigo wa simu ikiwa ni pamoja na kudhibiti simu bandia zinazotumiwa na wengi na kuongeza unafuu wa matumizi ya simu mpaka vijijini.
Stanley Mwabulambo wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), alibainisha kuwa waliunga mkono kwa kuwa mpango wa kibiashara wa kampuni hizo hutegemea gharama za muunganisho.
Alizitaka kampuni hizo kuwa bunifu katika ushindani huku akitaka punguzo hilo lionekane kwa mteja na TCRA ihakikishe punguzo hilo haliongezwi upande mwingine.
Mkuu wa Idara ya Ushawishi na Utetezi wa Ushindani kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Shadrack Nkelebe alisema mapendekezo hayo yataongeza ushindani kwa kuruhusu wateja kuwa na chaguo na kampuni moja.
Waziri wa zamani wa Ujenzi na Uchukuzi, Nalaila Kiula aliunga mkono mapendekezo hayo na kuitaka TCRA kuzitazama zaidi kampuni za simu kwa manufaa ya wateja kutokana na huduma wanazotoza gharama kubwa.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Airtel, Clara Mramba alisema kampuni hiyo inapendekeza gharama hizo zishuke taratibu kwa kuanzia Sh 84 Machi hadi Sh 29.26 mwaka 2017.
Alidai kuwa kushuka kwa kiwango hicho kikubwa cha Sh 34.92 Machi, kunaweza kuharibu uwekezaji wao.
Mwanasheria wa Vodacom, Walariki Ngitu alisema teknolojia mpya inaongeza gharama kwenye mawasiliano, hivyo kushuka kwa gharama hizo kutashusha uwekezaji katika mawasiliano na kusababisha washindwe kuwekeza vijijini.
Alipendekeza punguzo lianze kwa asilimia 35 na mwakani  asilimia  20  na kwenda taratibu hadi mwaka 2017 jambo litakalosaidia sekta hiyo ikue huku gharama ikipungua taratibu.
Mwakilishi wa Tigo,  Levocatus Nkata alitaka punguzo lianzie Sh 80 kwa maelezo kuwa mapendekezo ya Sh 34.92 Machi mwaka huu, litasumbua katika uwekezaji na kushusha kodi kwa Serikali. Pia alitaka soko lisiingiliwe kwa kuwa tayari limekomaa ili liendelee na ushindani.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa jopo lililoundwa kupitia punguzo hilo kwa kuzungukia wadau mbalimbali, Jaji Buxton Chipeta alisema mkutano huo wa wadau ulikuwa wa mwisho na wamepokea maoni ya wadau na watayafanyia kazi na kutoa uamuzi.

No comments: