MAMA NA WATOTO WAKE SABA JELA MIAKA 15 KWA KUACHA UISLAMU...

Rais Mohammed Morsi.
Mama na watoto wake saba wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kurejea katika Ukristo kutoka Uislamu nchini Misri.
Nadia Mohamed Ali alikuwa Mkristo lakini akasilimu na kuwa Muislamu miaka 23 iliyopita wakati alipoolewa na Mohamed Abdel-Wahhab Mustafa.
Kufuatia kifo chake, alipanga kurejea kwenye imani yake ya awali, sambamba na familia yake nzima.
Lakini mahakama ya makosa ya jinai mjini Beni Suef, iliyoko katikati ya Misri, iliwahukumu kifungo cha miaka 15 jela wiki iliyopita, kwa mujibu wa taarifa mbalimbali.
Watu wengine saba, ambao walihusishwa katika kesi hiyo, nao pia walihukumiwa kifungo cha mitano jela.
Wanasheria wa haki za binadamu sasa wameonya hukumu hiyo kuwa ni ishara ya vitu vijavyo katika Misri chini ya Serikali ya Kiislamu, kwa mujibu wa Fox News.
Kubadili kwake dini kumefichuka baada ya familia kujaribu kupata vitambulisho vipya mwaka 2004.
Kwa mujibu wa taarifa, mmoja wa watoto alikamatwa miaka miwili baadaye na kukiri nyaraka zilibadilishwa kinyume cha sheria wakati polisi walipogundua kabadili jina lake na kuanza kumtilia mashaka.
Nadia, watoto wake na wafanyakazi walioshughulikia vitambulisho hivyo walikamatwa na kufunguliwa mashitaka.
Wakristo nchini humo wamesema wanakutana na ugumu kama walishasilimu kuwa Waislamu na kutaka kurejea katika imani zao za awali, jambo linalowafanya kughushi nyaraka, jambo linaloweza kuwapeleka jela.
Samuel Tadros, mmoja wa watafiti katika taasisi ya Center for Religious Freedom ya Chuo cha Hudson, amesema wakati ubadilishaji huo umekuwa maarufu, katiba mpya inayoegemea kwenye Sharia katika Misri ni 'maangamizi makubwa' kwa uhuru wa kidini, kwa mujibu wa Fox News.
Alisema: "Matukio haya yataongezeka katika siku za usoni. Itakuwa ngumu zaidi kwa watu kurejea katika Ukristo."
Katiba hiyo ililazimishwa kupita mwaka jana na Rais Mohamed Morsi, ambaye alimrithi Hosni Mubarak kufuatia uchaguzi wa mwezi Juni.
Makundi yasiyo ya kidini na yasiyoegemea upande wowote, na pia Wakristo wenye asili ya Misri, walipinga katiba hiyo na kuandamana dhidi yake mara tu ilipopitishwa.

No comments: