WENYE MABASI WAIZIDI KETE SUMATRA KUPANDA KWA NAULI...

Lango Kuu la kuingilia katika Stendi ya Mabasi ya kwenda Mikoani iliyoko Ubungo, Dar es Salaam.
Kutokana na watu wengi kutaka kusafiri wakati huu wa msimu wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka bei za nauli kwa kwenda mikoani zimepanda zaidi huku baadhi ya abiria wakishindwa kusafiri kutokana na ongezeko la nauli na mabasi kujaa.
Pamoja na juhudi za Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuweka kambi katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) lengo likiwa ni ukaguzi wa mabasi na kudhibiti nauli, lakini wenye mabasi wamebuni njia mbalimbali za kukwepa agizo la serikali na kutopandisha nauli.
Uchunguzi uliofanywa na HabariLeo kwa takribani siku tatu zilizopita, umebaini kupanda nauli kiholela baada ya kutoza nauli tofauti na inauli halisi iliyoandikwa kwenye tiketi, huku baadhi ya mabasi husani coaster na magari binafsi aina ya Noah yakitumika kusafirisha abiria kwa bei juu.
Ikiwa tofauti na bei elekezi iliyopo kwenye ubao kituo hapo kuonyesha safari ya Dar es Salaam-Arusha yenye kilomita 616, ya mabasi ya kawaida (sh16,400), semi-Luxury (sh 25,100) na luxury(sh 28,600), lakini nauli imekuwa kati ya sh 35,000 hadi 50,000.
Imeshuhudiwa tiketi ya abiria aliyejitambulisha kwa jina la Ambha, aliyekuwa akienda Arusha ikionyesha sh 22,000, lakini bei aliyouziwa na wapigadebe ilikuwa ni sh 35,000.
“Inaonekana tiketi ziko mikononi mwa wapigadebe, nimeenda ofisi nimeambia nafasi zimejaa hadi Jumatatu(leo), lakini wapigadebe wanazo na wanazilangua,”
Hata hivyo, jana hali ilionekana kuwa mbaya zaidi, ambapo mabasi aina ya coaster yaliegezwa maeneo mbali kama vile External karibu na ofisi za EPZ wakikwepa Sumatra.
Mwandishi alishuhudia mpigadebe akiwa na abiria sita alipanda nao kwenye daladala ifanyayo safari zake Mwenge-Temeke na kuwapeleka eneo la external kwa ajili ya kupata usafiri.
Pia kituo cha Oilcom cha Ubungo kilikuwa kituo cha magari aina ya Noah ambapo wapigadebe walionekana kupigia debe usarifi wa kwenda Moshi-Arusha kwa kati ya sh 40,000 hadi 45,000.
Huko Mbezi Louis, katika Kituo kipya cha Mabasi, abiria wa mikoani walionekana kufurika juzi na jana, na walikuwa wakitozwa kati ya sh 45,000 hadi 50,000 kwenda mikoa ya Kaskazini hususani Arusha na Kilimanjaro (Moshi).
Bila woga wala wasiwasi, wakala wa mabasi ya kaskazini waliokuwa na tiketi mikononi katika eneo hilo, walisikika wakitangaza Moshi shilingi elfu hamsini na abiria kadhaa waliokuwa hawana tiketi walikubaliana na bei hiyo.
Aidha, magari binafsi yalipakia pia abiria kwa bei hiyo ikiwa ni pamoja na malori ya mizigo na mafuta yalisimama pembezoni mwa barabara ya Morogoro karibu na kituo hicho, kuchukua abiria.
Hata hivyo, baadhi ya abiria wamepeleka lawama Sumatra kuwa wameshindwa kuthibiti mfumuko wa bei pamoja na kutoa onyo hilo mapema.
Abiria aliyejitambulisha kwa jina la Mlay alisema ameamua kurudi nyumbani baada ya kushindwa kupata usafiri kutokana na bei kuwa juu.
Alipoulizwa Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Leo Ngowi alisema wamefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei za nauli baada ya kufanya ukaguzi kila siku.
Kuhusiana na ujanja wa kutoza nauli tofauti na iliyoandikwa kwenye tiketi, Ngowi alisema ofisi yake lipokea malalamiko hayo na kutuma watu ili kuwanasa wanaofanya nitendo hiyo, walibaini kuwa taarifa hizo hazikuwa za kweli.
Kuhusiana na mabasi kukwepa kituo cha ubungo na kupakia abiria kwa bei ya juu, Ngowi alisema: “ Leo (jana) kulikuwa na abiria wengi sana, tulichofanya katika kukabiliana na ujanja huo ni kuweka kambi ya ukaguzi Mbezi na Kibaha, ambako watu wengi tumewarudishia nauli walizozidishiwa.
“ Kwa sasa siwezi kukutajia ni mabasi magapi tumeyakamata, ila mengi yao ni aina ya coaster, oparesheni tuliyoifanya ni kubwa, unaweza kwenda kibaha sasa ukaoana ni jinsi gani magari yanavyoamatwa na kutozwa faini na watu kurudishiwa nauli zao.”
Ngowi aliongeza kuwa: “ Pia tulipewa taarifa kuwa kuna mengine yanapita njia ya Bagamoyo, hivyo tumeweka kambi nyingine Tanga, ili kuwakamata wale pote wanaokwepa huku na kupitia njia hiyo,” alisema.
Habari ambazo zimetufikia jana saa 9;56 zinasema abiria waliokuwa akisafiri na basi la Metro kutoka Dar-Arusha walishindwa kuendelea na safari kutokana na ubovu wa basi hilo.
Mmoja wa abiria, Mujenga Gwao alisema tangu saa 1:30 asubuhi gari hilo lilishindwa kuendelea na safari eneo la Mbezi Louis katika kituo kipya cha daladala.
“Tangu saa 1:30 asubuhi tumekwama hapa na hatujui kinachoendelea na wala hatima yetu. Trafiki na Sumatra wamefika hapa na kuondoka bila msaada wowote.
“ Watu wanateseka, akina mama na wato wanashindia biskuti na juisi, maisha yetu ni magumu na nadhani tunaweza kulala hapahapa,” alisema

No comments: