OFISA WA TAKUKURU AUA MWENZAKE KWA RISASI...

Ofisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Makao Makuu Dar es Salaam, Musa John (34), amemuua mfanyakazi mwenzake kwa bunduki wakiwa ‘beach’ katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
John amemuua mfanyakazi mwenzake Bhoke Rioba inadaiwa saa tisa usiku wa kuamkia jana katika ufukwe wa Southern ulioko Kigamboni, wilayani Temeke wakiwa katika sherehe ya kuaga wenzao waliopata uhamisho kwenda mikoani.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa John alimfyatulia risasi ya kichwa Bhoke ambaye alifia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokimbizwa kwa matibabu.
Kwa sasa kwa mujibu wa taarifa hiyo, John anashikiliwa na Polisi Chang’ombe baada ya kufanya mauaji hayo na mwili wa Bhoke umehifadhiwa Muhimbili.
Akisimulia kisa cha mauaji hayo, mtoa habari wetu alidai kuwa wafanyakazi hao wakiwa katika ufukwe huo usiku saa tisa; baadhi wamelala na wengine wamekaa katika kusheherekea  , walivamiwa na vibaka.
Mtoa taarifa huyo alidai baada ya kuvamiwa na vibaka, John alitoa bastola yake kwa nia ya kupiga juu ili kuwatawanya vibaka hao ambao haikufafanuliwa walikuwa wangapi, lakini kwa bahati mbaya Bhoke aliyekuwa amelala, aliamka ghafla na risasi ikampata kichwani.
Ofisa Habari wa Takukuru, Doreen Kapwani alithibitisha kutokea kwa kifo hicho cha Bhoke jana kwa kupigwa risasi na John na kueleza kwamba ilikuwa kati ya saa 1 na saa 2 usiku tofauti na taarifa za awali kwamba ilikuwa si saa tisa.
“Ni kweli imetokea jana usiku kati ya saa moja na saa mbili huko beach Kigamboni na wote wawili (Bhoke na Musa) ni watumishi wa Takukuru, Makao Makuu, Dar es Salaam,” alisema Kapwani.
Huku akigoma kueleza kwa undani kuhusu tukio hilo kwa madai kuwa Polisi inafanya uchunguzi, Kapwani alisema utaratibu wa mazishi ya Bhoke unafanywa na familia yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo akizungumzia tukio hilo alisema, ”Taarifa ya tukio hilo tunayo na mtuhumiwa wa mauaji alijisalimisha mwenyewe Polisi na bado tunamshikilia kwa uchunguzi.”
Kwa mujibu wa Kiondo, mauaji hayo yalitokea kati ya saa moja na saa mbili usiku katika eneo la ufukwe wa Southern, Kigamboni ambako mtuhumiwa na marehemu walishiriki na wenzao kwenye masuala ya kijamii.
”Walikuwa kwenye kufurahi kijamii, si shughuli ya kiofisi, walikwenda kwa gari ndogo binafsi ambayo bado namba za usajili hatujazipata, katika kufurahi huko ndipo John  alipiga risasi na kumpata Bhoke katika jicho la kushoto,” alisema.
Kamanda Kiondo alisema Bhoke alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili usiku huo kwa matibabu lakini baadae alifariki akiwa hospitalini hapo na mwili umehifadhiwa hapo hapo Muhimbili.
Kiondo alisema Polisi inachunguza sababu za John kupiga risasi kutokana na tukio hilo kutawaliwa na utata.
Takukuru na Polisi wamekanusha kuhusu kuwepo kwa uhusiano wa kimapenzi baina ya wahusika hao wawili.

No comments: